Friday, September 9, 2016

KAMANDA SIMON SIRRO AKANUSHA UVUMI WA KUKAMATA WANAOPUMZIKA GUEST MCHANA.

Kamanda Simon Sirro

Kamanda wa polisi kanda kuu ya Dar es salaam, Simon Sirro ametoa rai kwa wakazi wa jiji hilo na wageni wanaoingia jijini humo kutoka mikoa mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa katika mitandao ya jamii kuwa polisi wanawakamata ovyo wanaolala mchana kwenye nyumba za wageni.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Sirro leo, habari zinazosambazwa katika mitandao ya Whatsapp na Telegram pamoja na zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti kuwa polisi wanawakamata watu hao kwa madai ya uzururaji na uzembe ni uvumi.

Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu, taarifa hizo zimedai kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli la "Hapa kazi tu" jambo ambalo si la kweli.

"Ninawatoa hofu raia wema kuwa tunaendeleza operesheni kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria kwa kuendesha guest bubu" alisema.

Amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa nyumba za wageni zinazoendesha biashara kiholela kwa kuhifadhi wahalifu wakiwemo wanawake na wanaume wanaouza miili yao (dada na kaka poa).

Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi Mara kwa Mara kwenye nyumba za wageni, hotelini, migahawani, vilabu vya vileo na kumbi za starehe zinazokesha, alisema na kuongezea kuwa watakaobainika watakamatwa.

Sirro amewataka wafanyabiashara wa nyumba za wageni kufuata taratibu za kuandikisha wageni majina yao kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanazotoka na watakapomtilia mashaka mteja yoyote watoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi.


No comments: