Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam imetuma askari zaidi ya 80 kwenda katika misitu ya vikindu, Mkuranga na maeneo ya jirani kufanya operesheni maalumu ya kuwasaka majambazi.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro amesema kikosi cha askari hao kimeondoka mchana huu kwenda kwenye operesheni hiyo.
Kuhusu mapambano ya jana katika eneo la vikindu mashariki, wilayani mkuranga alisema kuna watu kadhaa waliuawa na wengine kadhaa wamekamatwa bila kutaja idadi kwa kile alichoeleza kuwa kinaweza kuvuruga upelelezi.
Wakati huo huo kamishna Sirro amesema bado jeshi hilo linaendelea kusisitiza kutokufanya maandamano Septemba 1 na tayari limepata taarifa kuwa kuna vijana wamelipwa fedha kufanya hivyo.
"Kuna vijana tunajua wamelipwa fedha kufanya maandamano Septemba 1 sisi tumekataza ila kama wao wanaona ni vyema kuandamana tunawakaribisha" alisema kamanda Sirro.
Saturday, August 27, 2016
POLISI WAANZA MSAKO MAALUMU WA MAJAMBAZI.
MKAPA ATIMIZA MIAKA 50 YA NDOA.
Rais John Pombe Magufuli na mkewe Janeth Magufuli ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria ibada ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa na mkewe Anna Mkapa.
Misa ya maadhimisho hayo yalifanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro Oysterbay imeongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa katoliki jimbo kuu la Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo na kuhudhuriwa na maaskofu na viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi ya umma.
Wageni maarufu waliohudhuria maadhimisho hayo pamoja na mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania, Cleopa Msuya, Edward Lowasa na mkewe, Dk.Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na mjane wa baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere.
LEMA AKAMATWA ARUSHA KWA KOSA LA UCHOCHEZI.
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema amesekwa rumande na jeshi la polisi mkoani Arusha kwa kosa la kusambaza maneno ya uchochezi katika mitandao ya kijamii, usiku wa kuamkia jana.
Lema alikamatwa na polisi, alfajiri nyumbani kwake kata ya Engutoto, Njiro ndani ya jiji la Arusha akiwa bado hajaamka.
Kamanda wa polisi wa mkoa, Charles Mkumbo alikiri Polisi kumsweka rumande mbunge huyo na kusema kuwa inamhoji na kufahamu ni kwa nini alisambaza maneno ya kichochezi yenye lengo la kuvunja amani ya nchi. Alisema Lema alikamatwa nyumbani kwake Alfajiri akiwa amelala.
Alisema baadhi ya maneno hayo ni "kama mauti imepoteza utukufu wake hakuna statement ya kurudisha nyuma Arusha kuandamana".
Kwa mujibu wa kamanda, maneno hayo aliyoyatoa Lema ni ya uchochezi na kuvuruga amani ya nchi na ndiyo maana wanamshikiria kwa mahojiano juu ya kauli zake hizo.
Alisema Watanzania wanatambua umuhimu wa amani na hakuna mtu aliye juu ya sheria, hivyo ni vyema wakaheshimu utulivu uliopo.
POLISI NA MAJAMBAZI WAJIBISHANA KWA RISASI HUKO MKURANGA.
Majibizano ya risasi baina ya polisi na majambazi yaliyodumu kwa takribani saa saba kuanzia saa 8:20 usiku wa kuamkia jana mtaa wa Vikindu Mashariki, Mkuranga mkoani pwani, yamesababisha vifo vya watu wawili akiwemo askari polisi na mtu mwingine anayedhaniwa kuwa ni miongoni mwa majambazi.
Mbali ya milio ya risasi, mtaa huo pia ulitanda moshi kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa mfululizo na kuibua taharuki kubwa kwa wakazi wake. Mmoja wa majirani katika nyumba iliyozingiwa waliyoishi watuhumiwa, Mjenge Faki alisema walishtuka usingizini na kuanza kusikia milipuko ya risasi na ghafla wakaanza kutokwa na machozi kufuatia hewa hiyo ya machozi kuanza kusambaa.
Katika majibizano hayo, askari aliyekuwa katika majibizano na mtuhumiwa walikufa hapo hapo. Hata hivyo kamanda wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi, licha la kuwepo eneo la tukio, hakuwa tayari kuzungumzia lolote, akisema mwenye jukumu la kuzungumzia tukio hilo ni Kamanda wa polisi kanda ya Dar es salaam, Simon Sirro.
Naye Kamanda Sirro akizungumzia hilo alisema, taarifa rasmi ya tukio hilo zitatokewa leo kwani bado wanakusanya taarifa kuhusiana na tukio hilo. Lakini Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema katika mapambano hayo, Jeshi la polisi limepoteza askari mmoja, lakini bado lipo imara na litaendelea kuwasaka wahalifu popote watakapokuwepo.
"Askari wetu katika shughuri zake za kupambana na majambazi ameuawa hapa leo (Jana) usiku, ni tukio baya katika mkoa wetu, wilaya yetu na nchi yetu kwa ujumla. Hawa ni wahalifu, lakini mbaya zaidi hata watoto na familia zao zinaaminika wana mafunzo maalumu ya kulinda wazazi wao ambao ni wahalifu" alisema Ndikilo.
Aliongeza kuwa, kama waalifu hao walidhani kwa kuua askari watakuwa wametimiza malengo yao, basi wamechelewa kwani watawawinda popote pale watakapokwenda. Kwa mujibu wa Faki milio ya risasi na mabomu ilisikika katika nyumba inayosadikiwa kumilikiwa na mkazi wa Temeke, aliyetajwa kuwa ni Salum Kingungo.
"Tulianza kusikia kama watu wanakimbizana kutoka eneo la juu barabarani na kelele hizo zikaja kuishia ndani ya nyumba hii walianza kusikia majibizano baina ya watu waliokuwa nje na mingine kutoka ndani, lakini hatukuweza kujua kinachoendelea kwani tulijawa na hofu kubwa", alisema Faki.
Alisema alishindwa kutoka nje na hata walipobaini kuwa ni askari, hawakuruhusiwa kutoka nje hadi ilipohitimu saa tano asubuhi.
Katika majibizano hayo ya risasi na mabomu, nyumba inayodaiwa yalikuwa makazi ya watuhumiwa hao, iliharibiwa vibaya. Baada ya hali kutulia, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo akiwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, alipata fursa ya kuzungumza na wananchi.
Baada ya kutembelea nyumba hiyo na kujionea hali halisi, waliwataka wananchi wa Mkulanga na mkoa wa Pwani kwa ujumla kuwa watulivu kwani serikali imejipanga na kupambana na watu wachache ambao sio waaminifu.