Saturday, October 29, 2016

MTANGAZAJI WA CLOUDS MILLARD AYO APEWA TUZO.

Taasisi ya Great Hope Foundation (GHF) leo imemtunukia tuzo ya kuwa mfano wa kuigwa Mtangazaji maarufu wa kituo cha Radio cha Clouds Fm Millard Ayo.

Mgeni katika tuzo hizo zilizokwenda kwa jina la ‘Onesha uwezo’ Mkurugenzi mkazi wa Trademark East Afrika John Ulanga alisema Mtangazaji huyo alipambana na kufanikiwa kuonesha uwezo wake ambao sasa umekuwa na mafanikio makubwa kwake na taifa kwa ujumla.

"Millard aliweza kufanya kazi ya utangazaji katika changamoto nyingi ikiwemo kukatishwa tamaa na wazazi wake, kufanya kazi bila malipo kwa muda mrefu lakini leo uwezo unadhihirika,"alisema Ulanga.

HONGERA MILLARD.


MISS TANZANIA LEO KUONDOKA NA GARI.

Hashim Lundenga

Mshindi wa shindano la Miss Tanzania litakalofanyika leo jijini hapa, ataondoka na zawadi ya gari na fedha taslimu, imeelezwa.

Akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema mshindi atapewa zawadi ya gari na Sh milioni 4,huku mshindi wa pili atachukua Sh mil 3, nafasi ya tatu Sh mil 2 huku wa nne na tano kila mmoja atondoka na Sh mil 1.

Washiriki wengine waliobaki ambao hawatakuwemo katika tano bora kila mmoja ataondoka na Sh 500,000.

Lundenga alisema mashindano hayo ya warembo yanafanyika leo hii katika ukumbi wa Rock City Mall na shoo hiyo itakuwa ni ya saa mbili na nusu itakayotumbuizwa na Christian Bella.

Mshindi wa mashindano hayo atawakilisha nchi katika mashindano ya kumtafuta mrembo wa dunia mwaka huu yatakayofanyika katika jiji la Washington DC, Marekani, Desemba 18. Viingilio ni Sh 20,000, Sh 50,000 kwa viti vya dhahabu na viti maalumu ni Sh 100,000.

Warembo 30 watakaochuana ni Julitha Kabethe, Nuru Kondo, Grace Malikita, Spora Luhende (Ilala), Diana Edward, Regina Ndimbo, Ndeonansia Pius, Hafsa Abdul (Kinondoni), Upendo Dickson, Abella John, Elineema Chagula, Irene Ndibalema ( Mashariki), Anna Nitwa, Lisa Mdolo, Irene Masawe (Kanda ya Kati), Laura Kway (Kanda ya Elimu ya Juu).


PLUIJM:KWELI SHUKRANI YA PUNDA NI MATEKE.

KATIKA dunia ya soka inafahamika kazi ya kocha ni kuajiriwa na kutimuliwa.

Lakini wengi wanaoondoka kwenye timu hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya vibaya, kustaafu na wengine wakisaka changamoto kwingine. Hivi karibuni kocha wa Yanga, Hans van Pluijm aliandika barua ya kujiuzulu kuifundisha timu hiyo baada ya kubaini mabosi wake walifanya mazungumzo na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina pasipo kumshirikisha. Alikuwa akiona taarifa kwenye vyombo vya habari juu ya mabadiliko mapya kwenye benchi la ufundi, lakini hakuelezwa kinachoendelea.

Awali, taarifa hizo zilikuwa zikionesha kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi na baadaye zikawepo taarifa kuwa Pluijm huenda akawa Mkurugenzi wa Ufundi na nafasi yake kuchukuliwa na kocha huyo wa Zesco. Mabadiliko hayo ya ghafla yalipokewa kwa mitizamo tofauti wengine wakiona ni sawa, wengine wakihuzunika na mwisho wa siku kocha huyo kipenzi cha Wanayanga anaondoka.

Pluijm kama kocha aliyeleta mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi ndani ya timu hiyo hakupaswa kufanyiwa alivyofanyiwa, kusoma taarifa za kutemwa kwake kwenye vyombo vya habari, kwani timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri chini yake kwa muda mrefu. Lakini Yanga ndio yenye uamuzi kwa kuwa ndiyo inayomlipa mshahara kwa hivyo pengine kuna kitu ambacho imedhamiria kukifanya katika kuboresha zaidi benchi lake la ufundi.

Au pengine kuna mambo ambayo yapo nyuma ya pazia yasiyojulikana kuhusu Pluijm ndio maana hata uongozi wa klabu hiyo umeona kuna haja ya kuachana naye kutafuta wengine ambao ni wazuri zaidi yake. Inadaiwa pia sababu ya kumuondoa kocha huyo ni timu kushindwa kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo Yanga iliishia kwenye hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa na Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa.

Pluijm anaondoka lakini atakumbukwa kwa mambo mengi ndani ya Ligi Kuu soka Tanzania bara, lakini pia hata kwa vyombo vya habari kutokana na jinsi alivyoishi nao kwa muda mrefu. Kwa upande wa vyombo vya habari. Pluijm atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa makocha wa kigeni walioonyesha ushirikiano wa hali ya juu pindi zilipokuwa zikihitajika taarifa mbalimbali kuhusu timu au yeye mwenyewe.

Wakati wowote akitafutwa Kocha huyo iwe kwenye mitandao ya kijamii, au amepigiwa simu au amekutana na waandishi na akaulizwa maswali basi amekuwa akionesha ushirikiano katika kujibu. Tofauti na makocha wengine baadhi ambao timu zao zinapofanya vibaya hutawaona kwenye mkutano na waandishi wa habari wamekuwa na jazba ya kufungwa. Pluijm ni aina ya Kocha mwenye weledi wa hali ya juu na mwenye uvumilivu hata kama timu yake imepoteza ni lazima atajitokeza kwa vyombo vya habari kujibu maswali yao.

Mbali na ushirikiano huo kwa vyombo vya habari, atakumbukwa kwa kuleta changamoto kwenye ligi na kuifanya Yanga leo inaitwa wa kimataifa kutokana na rekodi bora aliyoiweka. Pluijm alijiunga na Yanga mwaka 2014 akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts aliyetimulia baada ya kushindwa kufanya vizuri mechi ya mtani jembe dhidi ya Simba. Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazili, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.

Anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22. Pluijm anaondoka baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC). Aliifikisha Yanga hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria.

Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Mara nyingi Yanga ilikuwa ikishiriki michuano hiyo ya kimataifa lakini iliishia kwenye hatua ya makundi. Ni dhahiri kuwa alipoifikisha timu hiyo, anaiacha ikiwa inajivunia mafanikio yake. Kutokana na mafanikio hayo, Pluijm alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita.

Chini yake, kuna wachezaji walionekana kung’ara akiwemo Juma Abdul aliyeibuka mchezaji bora msimu uliopita, Simon Msuva msimu wa mwaka juzi alikuwa mfungaji bora, Amis Tambwe msimu uliopita alikuwa mfungaji bora, Thaban Kamusoko alikuwa mchezaji bora wa kigeni. Hiyo yote ni kwa sababu aliwaamini na kuwapa kazi chini ya mfumo wake na wakaweza kutekeleza. Mfumo wake pia ulileta changamoto kwa timu pinzani ambazo zilishindwa kutamba mbele yake.

Kocha huyo alikuwa akipenda kutumia mbinu za kushambulia na kasi ambayo iliwawezesha kupata magoli mengi katika baadhi ya mechi kadhaa na hatimaye kuchukua mataji. Pluijm hakuwa rafiki upande wa vyombo vya habari pekee, bali hata mashabiki wa klabu hiyo walionesha wazi kumkubali na ndio maana amekuwa akiwasiliana nao kwenye mtandao wa kijamii wa facebook mara kwa mara. Historia Pluijm alizaliwa miaka 67 iliyopita Uholanzi. Enzi zake alicheza soka katika nafasi ya mlinda mlango.

Aliwahi kudakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na baadaye alistaafu baada ya kuumia goti. Alianza kazi ya ukocha kwenye timu hiyo na kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu ya nchini humo. Aprili mwaka 1995, alisaini mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na msaidizi wake, John Metgod.

Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima. Baada ya kufanya vibaya Ulaya, alihamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana. Pia, aliwahi kuifundisha Saint-George ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-Juniors Feyenoord ya Ghana. Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa na kuhamia Medeama ya Ghana, nako hakudumu baada ya kufanya vibaya pia. Nenda Pluijm na kila la heri katika safari nyingine!


KIKWETE:NAOMBA NIACHWE NIPUMZIKE.

Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete amelalamika kutokana na kile alichosema ni kutumiwa vibaya kwa picha zake mtandaoni na 'kulishwa maneno'.

Takriban mwaka mmoja tangu astaafu, Bw Kikwete, rais wa awamu ya nne, amesema anafaa kuruhusiwa apumzike.

Aidha, amesema anamuunga mkono Rais wa sasa Dkt John Pombe Magufuli, pamoja na serikali yake.

"Nimestaafu naomba niachwe nipumzike. Nisingependwa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali. Namuunga mkono Rais na Serikali yake," ameandika kwenye Twitter.

"Nasikitishwa sana na matumizi mabaya ya picha zangu mtandaoni hususan watu kunilisha maneno kwa kutaka kutimiza malengo yao ya kisiasa."

Bw Kikwete aliondoka madarakani mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuongoza taifa hilo kwa miaka kumi.

Tangu aondoke madarakani, ameonekana kujiepusha na masuala ya kisiasa.

Ni nadra sana kwa rais mstaafu Jakaya Kikwete kujibu shutuma ambazo zinahusanishwa naye.

Hivi karibuni watu wamekuwa wakitumia sehemu ya hotuba anazozitoa kumhusisha na ukosoaji wa serikali utendaji kazi wa serikali ya Rais Magufuli.

Siku chache zilizopita Kikwete alikuwa anahutubia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na katika hotuba yake alitamka haya: "Unapokuwa mpya watu wanataka mambo mapya pia, lakini yawe mapya ya maendeleo na siyo (mapya) ya kuharibu kule tulikotoka." Sasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakiitumia nukuu hii kuashiria Bw Kikwete alikuwa akiukosoa utawala wa Rais Magufuli


JINSI MTOTO KUTOKA GHANA ALIVYOPATA UMAARUFU MITANDAONI.

Mtoto mmoja wa kiume ambaye picha yake ilipata umaarufu kwenye mitandao huenda ikasababisha kijiji kizima kupata elimu.

Jake amekuwa mmoja wa wanafunzi maarufu zaidfi nchini Afrika Kusini tangua watu waanze kusambaza picha yake huku wakiifanyia utani picha hiyo

Hata hivyo Jake anaishi umbali wa kilomita kadha kaskazini, katika kijiji kimoja kilicho mashariki mwa Ghana bila ya kufahamu umaarufu alioupata.

Ukweli ni kwamba hadi siku ya Jumatano hata mtu ambaye aliipiga picha hiyo hakuwa na habari kuwa imepata umaarufu.

Mpiga picha Carlos Cortes alisafiri kwenda nchini Ghana mwaka 2015 na kufanya makala kuhusu Solomon Adufah, ambaye ni msanii aliyekuwa akirejea nyumbani kutoka Marekani.

Picha ya Jake ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka minne, ni kati ya mamia ya picha zilizopigwa wakaati Adufah alikuwa akiwafunza watoto sanaa.

Lakini picha hiyo ya Jade ilianza kusambaa mitandaoni baada ya Adufah kuituma kwa akaunti yake ya mtandao wa Instagram.

Wakati aligundua kuwa picha hiyo imeanza kupata umaarufu hakujua cha kufanya.

Hapo ndipo sasa Adufah ambaye ameishi Marekani tangu umri wa miaka 16 alianzisha mchango akiwa na matumaini kuwa Jake atasababisha watu kudhamini elimu yake na ya watoto wengine kijijini.

Ndani ya saa 24 kampeni hiyo ilichangisha dola 2000. Adufa anasema kwa pesa hizo zitatatumiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa watoto wa eneo hilo.


UBAROZI WA MAREKANI NCHINI KENYA UMEFUNGWA.

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umefungwa kwa muda leo Ijumaa kufuatia kisa ambapo mwanamume aliyekuwa na kisu alijaribu kumshambulia afisa wa usalama karibu na ubalozi huo Alhamisi.

Mwanamume huyo aliuawa kwa kupigwa risasi.

Hakuna afisa yeyote wa ubalozi huo aliyeathiriwa na kisa hicho.

"Ubalozi utafungwa Oktoba 28. Huduma zote za kibalozi zimesitishwa, lakini huduma za kibalozi za dharura kwa raia wa Marekani zitaendelea kutolewa," taarifa kwenye tovuti ya ubalozi huo imesema.

Maafisa wa ubalozi huo wametoa wito kwa raia na wafanyakazi wake kuwa makini kuhusu usalama wao.

Polisi nchini Kenya wanachunguza kubaini iwapo mwanamume huyo aliyepigwa risasi alikuwa na washirika, afisa mmoja mkuu wa polisi Vitalis Otieno aliambia shirika la habari la AFP.

Bw Otieno alisema mwanamume huyo alimdunga kisu afisa mmoja wa polisi lakini akapigwa risasi na kichwani na kuuawa na afisa aliyekuwa karibu.

Maafisa watano wa idara ya uchunguzi wa jinai ya Marekani (FBI) walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye pamoja na polisi wa Kenya kufanya uchunguzi.

Msemaji wa polisi Kenya George Kinoti alisema mwanamume huyo wa miaka 24 alikuwa "mhalifu wa kuendesha shughuli zake kivyake", kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Hata hivyo, alisema uchunguzi unaendelea.