Thursday, November 24, 2016

BIFU LA OMMY DIMPOZ NA DIAMOND LAPAMBA MOTO.

Image result for ommy dimpoz NA DIAMOND
OMMY DIMPOZ NA DIAMOND.
Wiki hii kumekuwa na majibizano kati ya wasanii wakubwa wawili hapa Bongo, nawazungumzia OMMY DIMPOZ na DIAMOND PLATNUMZ.

Hayo majibizano yamekuja baada ya Ommy Dimpoz kupost ujumbe Instagram uliokuwa ukisema kuwa kuna baadhi ya wasanii wamekuwa wakinunua viewers youtube ili video zao zionekane kuwa zinaangaliwa na watu wengi.

Kutokana na ujumbe huo, mashabiki wa Diamond walikuja juu na kuanza kumtukana Ommy, kitu ambacho kilipelekea Diamond naye kujibu ujumbe huo kwenye akaunti yake Instagram.

Hatimaye Diamond akafanya interview na XXL Clouds FM na kutokwa na mapovu juu ya Ommy. Na Ommy pia akatuma ujumbe kuomba kufanya interview XXL naye ili aeleze ya moyoni baada ya Diamond kusema anapumuliwa.

Hili bifu kati ya hawa wasanii wawili linapamba moto na hakuna dalili ya kulizima kiurahisi.

MAAJABU:MWANAMKE AWAPIGA RISASI WAGENI WALIOMTEMBELEA KWA SABABU YA KUPIGA KELELE.

Alana Annette Savell
Mwanamke mmoja katika jimbo la Florida nchini Marekani, aliwafyatulia risasi wageni waliokuwa wamemtembelea kwa sababu walikuwa wamekaa sana na walikuwa wanapiga kelele, polisi wanasema.
Alana Annette Savell, 32, alikuwa mwenyeji wa wageni hao wawili, wapenzi, katika jiji la Panama pale walipoanza kupiga kelele sana.
Polisi wanasema aliwaamrisha kuondoka kutoka nyumbani kwake, kabla ya kuwapiga risasi miguuni.
Walijipeleka hospitalini wakiwa na majeraha, ambayo hayakuwa mabaya sana.
Bi Savell ameshtakwia kwa kuwashambulia watu akitumia bunduki.
Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa wilaya ya Bay iliambia BBC kwamba mwanamke huyo kwa jina Kristy Jo Mohr alikuwa amefika na mpenzi wake, ambaye walikuwa wamekutana kwenye baa, nyumbani kwa mshtakiwa mwendo wa saa saba usiku Jumatatu.
Bi Savell aliambia polisi alianza kukerwa na wageni hao baada yao kuanza kunywa pombe na kuzungumza kwa sauti ya juu.
Badala ya kuwadokezea kwamba alikuwa amechoshwa nao kwa kula miayo au kuweka vyombo vya jikoni kwenye mashine ya kuosha vyombo, alichomoa bunduki yake na kuwafyatulia risasi miguuni.
Bi Mohr aliumizwa miguu yote miwili naye mpenzi wake, aliyetambuliwa tu kwa jina Cowboy akaumia mguu mmoja.
Bi Mohr ameambia polisi anakadiria kwamba kwa jumla Bi Savell alifyatua risasi nane au tisa.
Aliposhtukia amepigwa risasi mguuni, anasema alikimbia na kuingia kwenye gari.
Mpenzi wa washukiwa ameambia maafisa wanaochunguza kisa hicho kwamba alikuwa amemshauri kwamba mgeni akikatalia nyumbani baada ya kumwambia mara tatu, achukue bunduki na kufyatua risasi sakafuni.
"Hilo lisipofanya kazi, basi awafyatulie risasi miguuni," maafisa wa mashtaka wamesema.
Bi Savell kwa sasa bado anazuiliwa uchunguzi zaidi ukiendelea.

INSTAGRAM YAZINDUA VIDEO YA MATANGAZO YA MOJA KWA MOJA.

Video ya matangazo ya moja kwa moja ya Instagram
Mtandao wa Instagram ndio mtandao wa huduma ya kijamii wa hivi karibuni kuzindua video za matangazo ya moja kwa moja.
Ukifuata nyayo za mtandao wa facebook,unaomiliki Instagram,You Tube pamoja na programu ya moja kwa moja ya Twitter ya Periscope ,Instagram imezindua programu mpya inayoruhusu wateja wake kuweka matangazo ya moja kwa moja wakati wowote.
Mtu yeyote anayetazama anaweza kutoa maoni yake kwa kuweka emoji ambazo hujitokeza katika video hiyo ya moja kwa moja.
Inaonekana kuwa ya kawaida,lakini kuna tofauti kubwa.Mara tu unapomaliza kuweka matangazo yako hupotea kabisa.
Hiyo inamaanisha hutaweza tena kusambaza link ya video yako kwa wanaotazama na hawataweza kuiona tena baada ya matangazo hayo.
Katika taarifa, msemaji wa Instagram alisema kuwa hiyo inalenga kuwafanya wateja kuhisi faraja na kuweza kusambaza chochote wanachotaka kusambaza.
Programu hiyo itasambazwa kwa kundi la wateja wa mtandao huo kabla ya kutumika na kila mtu katika kipindi cha wiki chache zijazo.

JUSTIN BIEBER AONEKANA AKIMPIGA NGUMI SHABIKI.

Image result for JUSTIN BIEBER
JUSTIN BIEBER.
Bado mwanamziki Bieber anaendelea na mikasa yake ya kupigana hadharani. Kanda ya video inayomuonesha Justin Bieber akimpiga ngumi shabiki wake usoni imetolewa.
Mtu huyo anaonekana kupeleka mkono wake katika dirisha la gari ya Bieber ambapo anapigwa ngumi na kuachwa akitoka damu mdomoni.
Kanda hiyo inaonekana kurekodiwa mjini Barcelona,ambapo msanii huyo alikuwa akitumbuiza ikiwa ni miongoni mwa ziara yake ya muziki.
Gari moja linaendeshwa polepole katika umati wa watu na msani huyo wa miaka 22 anaonekana kuwa katika kiti cha nyuma huku kioo chake cha dirisha la gari kikiwa wazi.
Shabiki huyo anaonekana kuingiza mkono katika dirisha la gari hilo na kujaribu kumshika Bieber.Wakati gari linapoondoka mkono unaonekana ukitoka katika dirisha hilo.
Shabiki huyo baadaye anarudi nyuma na kuisogelea kamera akiwa na damu katika meno yake na midomo.
Newsbeat imewasiliana na wawakilishi wa msanii huyo lakini haijapata tamko lolote kutoka kwao.
Mapema siku hiyo msanii huyo alipigwa picha akifanya zoezi na wachezaji wa Barcelona.

AL QAEDA YATHIBITISHA KUUAWA KWA KIONGOZI WAO MKUBWA.

Ndege za kivita za Marekani zilimlenga al-Qahtani katika mji wa Kunar
Kundi la kigaidi la Al-Qaeda limethibitisha kuuawa kwa kiongozi wao mkubwa Farouq al-Qahtani huko kaskazini Mashariki mwa Afghanistan katika mapigano na vikosi vya marekani mwezi mmoja uliopita.
Huko mjini Washington wamethibitisha kifo hicho kutokea November 15 yalikuwa ni makabiliano adhimu.
Lakini Al-Qaeda wamesema kuwa mkewe na watoto waliuwawa pia japo hawakujulikana kijeshi.
Vikosi vya Marekani vimeiweka Al-Qahtani mzaliwa wa Saudi huko Quatar kama mtu wanayemtafuta sana kwao akituhumiwa kuhusika na mipango ya mashambulizi huko Marekani na Ulaya.

MATUKIO KATIKA TUZO ZA AMAs HUKO MAREKANI.

rihanna
RIHANNA.
Wavunja rekodi
Wakali wa muziki wa Pop kutoka Canada, Aubrey Drake na Justine Bieber wamevunja rekodi ya aliyekuwa mfalme wa muziki wa pop duniani, Michael Jackson, baada ya kunyakua tuzo nne kila mmoja katika tuzo hizo.
Drake amenyakua tuzo ya msanii bora wa mwaka, msanii wa hip hop anayependwa, albamu ya hip hop inayopendwa ‘Views’, wimbo wa hip hop unaopendwa ‘Hotline bling’.
Beiber amenyakua tuzo ya video bora ya mwaka ‘Sorry’, msanii wa kiume wa muziki wa Pop anayependwa, albamu inayopendwa zaidi ya Pop ‘Purpose’ na wimbo unaopendwa wa Pop ‘Love Yourself’.
Licha ya kunyakua tuzo hizo nne, jina la Drake kwa mara ya kwanza lilikuwa katika vipengele 13, lakini akanyakua tuzo nne na Bieber naye alikuwa akiwania tuzo sita akanyakua nne.
Tangu tuzo hizo zilipoanza mwaka 1972, Michael Jackson ndiye msanii pekee aliyeweka historia ya jina lake kuwa katika vipengele 11 mwaka 1984 hadi Drake alipoivunja rekodi hiyo mwaka huu kwa kuwa katika vipengele 13.
Hata hivyo, Drake aliwataka mashabiki wake kutumia jina lake vizuri, huku akijinadi kuwapoteza kimuziki wasanii wenye majina makubwa zaidi yake.
Rihanna
Mkali wa muziki wa RnB, Robyn Rihanna Fenty ‘Rihanna’ alifuata kwa idadi kubwa ya tuzo baada ya kujinyakulia tuzo tatu, huku Twenty One Pilots nao wakinyakua tuzo mbili.
Rihanna amenyakua tuzo ya wimbo bora unaopendwa wa RnB ‘Work’, albamu ya RnB inayopendwa ‘Anti’ na msanii wa kike wa RnB anayependwa.
Walionogesha
Wasanii wengine ambao waliwagusa mashabiki kutokana na shoo kali ni pamoja na John Legend kutokana na wimbo wake wa ‘Love Me Now’, wengine ni Ariana Grande na Nicki Minaj, ambao walipiga shoo ya kuvutia.

MENEJA WA LADY JAYDEE AZUNGUMZIA KUHUSU TETESI ZA NDOA ZA JIDE.

jde
LADY JAYDEE NA MUMEWE.
Kufuatia sintofahamu kwa mashabiki wake kuhusiana na tetesi za kufunga ndoa na kwenda mapumziko visiwani Zanzibar, mwanamuziki, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ anatarajia kuweka wazi suala hilo hivi karibuni.
Akizungumza jana, Meneja wa mwanamuziki huyo, Seven Mosha, hakutaka kuzungumzia suala hilo, huku akisisitiza kwamba Lady Jaydee mwenyewe ataliweka wazi suala hilo hivi karibuni.
“Habari hizo zipo kwenye mitandao, lakini suala hili anatakiwa kuliongelea mhusika mwenyewe, mimi sina la kuzungumza, ni mapenzi yake ila naamini ataliweka wazi mwenyewe suala hilo hivi karibuni,’’ alieleza Seven.

PANYA BUKU KUPIMA SAMPULI ZA UGONJWA WA KIFUA KIKUU (TB).

Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mohamed Ally Mohamed (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha ugunduzi wa Kifua Kikuu kwa kupitia panya buku (Apopo) kilichopo Dar es Salaam. Wengine ni Mwalimu wa panya, Ezekiel Mwakyonde (aliyemshika panya) na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dk Abdu Hayghaimo. Sherehe hizo zilifanyika jana. (Picha na Yusuf Badi).
Maabara ya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa kutumia panya buku wa Mradi wa Apopo ulio chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), imezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku ikielezwa kuwa panya mmoja ana uwezo wa kupima sampuli 100 ndani ya dakika 20.
Uzinduzi wa maabara hiyo ulifanywa jana na Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya wa Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mohamed Mohamed kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo na uzinduzi ulioshuhudiwa na wadau mbalimbali pamoja na wananchi.
Akielezea mradi huo wa kupima vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia panya waliofunzwa, Meneja Mradi, Dk Georgies Mgode alisema panya hao wana uwezo wa kubaini harufu ya vimelea vya ugonjwa huo ndani ya sekunde.
Aidha, alisema kwa dakika 20 panya anaweza kupima sampuli 100 wakati sampuli kama hizo zingepimwa kawaida kwenye maabara zinazotumia hadubini kwa siku nne, hivyo majibu hadi yafike kwa mgonjwa yanaweza kuchukua siku saba ili hali kwa kutumia panya mgonjwa ndani ya siku moja anapata majibu na kuanza tiba.
“Ni kweli hawa panya wana faida kubwa kwenye ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB, kwa sababu wana uwezo ndani ya sekunde wakabaini maambukizi ya kwa mgonjwa wakati mtu wa maabara anatumia zaidi ya siku moja kupata majibu,” alisema Dk Mgode.
Alisema kwa kuzinduliwa kwa maabara hiyo itakayokuwa na panya buku 10 jijini Dar es Salaam ni hatua ya mafanikio ya harakati za vita dhidi ya ugonjwa huo hasa kwa kuwa jiji hilo ndilo linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, kuliko maeneo mengine na pia ni moja la miji yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kikua kikuu.

WIMBO WA RICH MAVOKO NA DIAMOND "KOKORO" KUCHUNGUZWA.

screenshot-from-2016-07-01-134855
DIAMOND PLATNUMZ.
Video ya wimbo mpya wa ‘Kokoro’ ulioimbwa na wasanii wa Bongo Fleva kutoka kundi la Wasafi, Richard Martin (Rich Mavoko) na Nassib Abdul (Diamond Platnumz), unachunguzwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Bodi ya Filamu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama video hiyo ina udhalilishaji wa mwanamke au la.
Mkuu wa matukio wa Baraza hilo, Kurwijira Maregesi, amesema kwamba wanafanyia uhakiki wa video hiyo kutokana na baadhi ya vipande katika video hiyo kuonyesha udhalilishaji wa mwanamke, tabia ambayo inapingwa vikali na jamii.
“Katika kusimamia maadili ya sanaa na udhalilishaji wa wanawake, tuko thabiti kuhakikisha hakuna msanii anayepotosha taifa wala kumdhalilisha mtu,” alisema Maregesi
Maregesi aliongeza kwamba kumekuwa na tabia kwa wasanii wa Bongo fleva kutoa nyimbo zenye kupotosha Taifa.

POLISI MBARONI KWA KUMVUA NGUO MCHUNGAJI NA KUMPIGA PICHA ZA UTUPU.


Polisi wanne wametiwa mbaroni mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumvua nguo mchungaji mmoja na kumpiga picha za utupu na mtu mwingine ili wamtuhumu kwamba anafanya mapenzi ya jinsia moja.
Katika mkasa huo uliotokea ndani ya chumba cha hoteli moja wilayani Hai, polisi hao wanaidaiwa kumpiga picha na kisha kumtaka atoe Sh10 milioni ili kumaliza suala hilo. Alitoa Sh5.4 milioni na kuachiwa huru.
Ilivyokuwa
Katika tukio hilo linaloaminika kuwa lilitengenezwa na polisi hao kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa mchungaji huyo ambaye jina lake na kanisa analohudumu tunalihifadhi kwa sasa, baada ya kuwakuta wawili hao ndani ya chumba, waliwaamuru wavue nguo wakiwatuhumu kufanya mapenzi ya jinsia moja na kuwapiga picha kwa kutumia simu zao.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mchungaji huyo alilazimika kupigana na polisi hao kupinga kitendo hicho lakini alizidiwa nguvu na kuvuliwa nguo zote na kubaki na bukta tu.
Taarifa za awali zinasema, siku moja kabla ya tukio hilo, mchungaji huyo alikutana na dereva mmoja wa malori eneo la Njiapanda ya Himo ambaye alisema anafanya biashara ya pumba.
“Kwa maelezo ya mchungaji ni kuwa walipeana simu ili pumba hizo zikipatikana apigiwe. Siku iliyofuata kweli huyo mtu akampigia akisema amepata magunia 150,” mtoa habari wetu alidokeza.
Alisema mtu huyo alimtaka mchungaji afike Bomang’ombe ambako angempeleka kuziona pumba hizo ili kama akiridhika wafanye biashara.
“Yule bwana aliyejifanya ana pumba alimuomba mchungaji amsindikize ili achukue chumba kwa vile siku hiyo angelala hapo Bomang’ombe kusubiri wenzake kutoka Segera.”
Mchungaji na mtu huyo walifuatana hadi katika hoteli moja (jina tunalo) na mtu huyo anayetuhumiwa kupangwa alichukua chumba na mchungaji akaingia kukiona.
“Huyo bwana akaomba akanunue sigara ili akirudi ndiyo waende kuangalia mzigo lakini aliporudi tu, ndipo wakaingia na watu wengine kama watano au sita hivi,” alidokeza mtoa habari wetu.
Watu hao ambao baadaye wanne walibainika kuwa ni polisi, wanadaiwa kuwalazimisha mchungaji na mtu huyo kuvua nguo na kuwarekodi kwa picha wakiwatuhumu kufanya ushoga.
Inadaiwa kwamba walimchukua mchungaji na mtu huyo aliyekuwa naye, wote wakiwa nusu uchi hadi kituo cha Polisi cha Bomang’ombe.
Hata hivyo, badala ya kufungua jalada la uchunguzi, polisi hao wanadaiwa kuwahifadhi watuhumiwa upande wa nyuma ya kituo wakimtaka mchungaji awape fedha.
Inadaiwa kuwa walitaka wapewe Sh10 milioni lakini mchungaji aliwasihi kwamba alikuwa na Sh5 milioni, ambazo aliwapa lakini wakamtaka aongeze zifike Sh6 milioni.
Mchungaji huyo akiwa chini ya ulinzi kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa tatu usiku, aliwapigia simu marafiki zake ambao baadaye walimtumia Sh400,000 kwa njia ya simu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, polisi hao walimchukua mchungaji akiwa na bukta hadi kwa wakala na kumshurutisha awape namba za siri ambazo aliwapa na wao kutoa pesa.
Baada ya kuwapa fedha hizo, walimrudisha hadi nyumbani kwa mmoja wa polisi hao na kumpa nguo zake lakini wakashikilia simu yake kwa sharti la kumrudishia kama tu angewaongezea Sh100,000.
“Baada ya kuachiwa ndiyo siku iliyofuata alitoa taarifa Takukuru ambao walichukua maelezo yake na viongozi wa juu wa Polisi wakajulishwa.”
Katika uchunguzi wa awali uliofanywa siku hiyo kati ya maofisa wa Polisi na Takukuru, ilithibitika kuwa hakuna jalada lolote lililokuwa limefunguliwa dhidi ya mchungaji wala mtu waliyekuwa naye.
Mbali na kutofunguliwa kwa jalada hilo, uchunguzi ulibaini kuwa ni kweli mchungaji huyo alikutwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kuchukuliwa na polisi na pia muamala wa fedha kwenye mtandao wa simu ulipatikana.
“Wale polisi walikamatwa na kuwekwa mahabusu hadi leo (jana) walikuwa hawajatoka na tayari walishamrejeshea yule mchungaji pesa zake zote Sh5.4 milioni,” mtoa habari adokeza.
Pia, alidokeza kuwa simu yake ambayo polisi waliishikilia hadi atakapokamilisha malipo ya Sh100,000 amerudishiwa kimyakimya ili suala hilo lisije kuwagharimu.
Hata hivyo, mtu aliyekutwa akiwa na mchungaji huyo hajafahamika wala aliko huku taarifa nyingine zikidai huenda naye ni polisi.
Kaimu Kamanda Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema askari hao wanne wanashikiliwa kwa madai ya kumkamata mtu anayedaiwa kuwa mchungaji na kumtengenezea mazingira hayo.
“Ni kweli tumepata taarifa na tumezifanyia kazi haraka, kinachofuata sasa ni kumpata huyo anayedaiwa kuwa ni mchungaji ili tuweze kumuhoji athibitishe,” alisema.
Inadaiwa kuwa askari hao wamemshawishi mchungaji huyo akubali kuwasamehe na asiandike maelezo ya uhalisia wa tukio, jambo linaloelezwa kwamba amelikubali.