Thursday, August 25, 2016

AKATA MKONO NA MGUU ILI APATE MALIPO YA BIMA.

Mwanamke mmoja nchini Vietnam amekiri kutoa mguu na sehemu ya mkono wake vikatwe ili aweze kudai malipo ya bima.

Mwezi Mei mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 anayetambuliwa kama Ly Thi N, alidanganya kuwa aligongwa na treni.

Lakini kwa sasa umeripotiwa kukiri kwamba alimlipa rafiki yake dola $2200 akate viungo vyake.

Lengo lake ni kudai dola zaidi ya $150,000 kutoka kwa kampuni ya bima yake.

Mtu aliyejifanya kuwa mpita njia aliyemuokoa kwa jina la Doan Van D, ambaye ndiye aliyemkata viungo, aliita gari la kubebea wagonjwa baada ya kumpata mwanamke aliyeumia katika barabara ya Hanoi.

Picha zilizochapishwa na gazeti rasmi la polisi  zilionyesha mwanamke huyo miezi mitatu badae akiwa amepona majeraha yake.

Anaaminiwa kuendesha biashara yake kwa shida, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.

Tukio hilo lisilo la kawaida limezua mjadara mkali katika mitandao ya kijamii nchini Vietnam huku wengi wakilaani tukio hilo.


MWANAUME INDIA ABEBA MAITI YA MKE WAKE 12km.

Mwanaume mmoja maskini nchini India alibeba maiti ya mkewe kwa zaidi ya kilomita 12 baada ya hospitali alimofariki kushindwa kumsafirisha kwa gari la kubebea wagonjwa hadi kijijini mwake.

Mke wa Dana Mjhi, Amang mwenye umri wa miaka 42, alifariki dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu katika hospitali ya Ulaya, mji wa Bhawanipatna jimbo la Orissa.

Bwana Mahji alisema kijiji chake kilikuwa umbali wa kilomita 60 na hakuwa na uwezo wa kulipa gharama ya usafiri wa gari la kuwabebea wagonjwa.

Mwanamke huyo alilazwa hospitalini hapo siku ya jumanne na kufariki usiku huo huo.

Mume wake alichukua maiti hiyo bila ya kuwafahamisha wahudumu wa hospitali hiyo, Afisa mkuu wa afya Bi Brahma alisema.

Majhi anadai mkewe alifariki siku ya jumanne usiku na kuamua kubeba mwili wake siku ya jumatano baada ya wahudumu wa hospitali hiyo kumsihi kutoa mwili huo.

"Nilikuwa nikiwaomba wahudumu wa hospitali hiyo wanisaidie gari nimbebe mke wangu lakini tukaambulia patupu".

Kwa sababu mimi ni maskini na nisingeweza kukodisha gari la kibinafsi, sikuwa na njia nyingine ila kumbeba mke wangu mabegani.

Mapema jumatano alisema, alifunga mwili wa mkewe na nguo na kuanza safari hiyo ndefu ya kuelekea kijijini huko Melghar kwa mila na tamaduni za mwisho akiungana na mwanae Chaula mwenye umri wa miaka 12.

Alitembea kwa takribani kilomita 12 ndipo watu walipoingilia kati na kuamua kumsaidia kwa gari la kubebea wagonjwa wakamfikisha hadi mwisho wa safari yake.

Shughuli ya kuchoma mwili wa mkewe ilifanyia jumatano usiku.


KAMATI YA OLIMPIKI YA KENYA YAVUNJWA.

Waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario ametangaza kuvunjwa kwa kamati ya maandalizi ya olimpiki, kuhusiana na maandalizi ya timu hiyo kwa michezo ya olimpiki iliyomalizika juzi mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.

Waziri ametangaza habari hiyo kwenye kikao na wanahabari huku ikibainika kwamba bado kuna wachezaji ambao hawajaondoka Rio.

Miongoni mwao ni mbunge Wesley Korir, aliyeshiriki mbio za Marathon ambaye anasema wanaishi maisha duni.

Wario amesema majukumu ya kamati hiyo, maarufu kama NOCK yatatekelezwa na Sports Kenya.

Waziri huyo pia ameunda kamati ya kuchunguza yaliyojiri wakati wa maandalizi ya michezo hiyo na wakati wa michezo yenyewe.


UTEUZI MWINGINE UMEFANYWA NA RAIS MAGUFULI.

Rais Magufuli amemteua Andrew Massawe kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA.

Kabla alikuwa Mkurugenzi wa mifumo ya kompyuta BOT.

Anachukua nafasi ya Modestus Kipilimbi ambaye aliteuliwa siku ya jana kuwa Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa.


MWANAFUNZI AFUKUZWA SHULE KISA USHIRIKINA.

Uongozi wa shule ya Sekondari Mwatisi wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya umemfukuza mwanafunzi mmoja (jina kapuni) kwa madai ya ushirikina.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuhusika na kitendo cha baadhi ya wanafunzi shuleni hapo kukumbwa na matatizo ya kuanguka na mapepo kwa muda wa miezi miwili mfululizo.

Mwanafunzi huyo pia amehusishwa na mzuka wa ajabu uliotokea hivi karibuni ambapo ulikuwa ukianua vyakula vya watu wakati wakianika nje, huku ukiwakumba wanafunzi wa kike waliokuwa wakikimbia porini na kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Hali hiyo ilisababisha uongozi wa shule hiyo kuhitisha mkutano wa hadhara ulioshirikisha viongozi wa dini, machifu na watu wengine, lengo likiwa ni kufikia muafaka wa sakata hilo.

Furaha Mwakalundwa mwinjilisti wa kanisa la kiinjili kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Konde jimbo la Mwakaleli, alisema kufukuzwa kwa mwanafunzi huyo hakuwezi kuleta tija kutokana na masuala ya ushirikina hayana uthibitisho ni vyema hiyo kazi wangetuachia watumishi wa Mungu ili tuendelee kutatua kwa nguvu za Mungu.

Baadhi ya wanafunzi wamesema kuondolewa kwa mwanafunzi huyo kumeleta unafuu kwa 90% kulinganisha na awali.

"Alikuwa akiingia tu darasani au kukutana na mwanafunzi yoyote walikuwa wakianguka na kupata kama kichaa na kuanguka na kusababisha walimu na wanafunzi kumchukia" alisema mmoja wa wanafunzi.

Walimu na wanafunzi walikuwa wakimwogopa na kumkimbia kila anapoonekana, na walimu kuogopa kumpa adhabu.


IDADI YA WATU WALIOFARIKI KATIKA TETEMEKO NCHINI ITALIA YAONGEZEKA.

Manusura wakiwa katika mahema

Idadi ya watu hao imefika 247, huku manusura wakiendelea kutafutwa. Maafisa uokoaji wanaendelea na juhudi za kutafuta manusura na miili kwenye vifusi.

Tetemeko hilo la nguvu ya 6.2 katika vipimo vya Richter liliharibu vibaya mji wa Amatrice, Accumoli na Pescara del Tronto ambapo watu wengi walifariki.

Maafisa wa uokoaji waliendelea na shughuli za kuwatafuta manusura usiku, lakini wakati mmoja walikatizwa na mitetemeko mingine iliyotokea na kutikisa majumba yaliyosalia yakiwa bado wima.

Mahema yamewekwa kuwasaidia watu walioachwa bila makao.


KESI YA BABU TALE KUHAIRISHWA TENA.

Hukumu ya kesi inayomkabili meneja wa staa wa bongo flava Diamond Platnumz, Babu Tale ya kusambaza na kuuza DVD za mawaidha ya Shehe Hamis Mbonde bila ridhaa yake imehairishwa tena siku ya jana katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam mpaka September 12, mwaka huu.

Kwa mujibu wa msajili wa Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam Mustapha Sian alisema sababu kubwa ya kuhairishwa kwa kesi hiyo ni kwamba aliyetakiwa kuitolea hukumu ambaye ni msajili Projest Kahyoza hayupo mahakamani kikazi.

Katika kesi hii Babu Tale pamoja na mdogo wake anayeunda kundi la tip top connection wanatakiwa kuieleza mahakama kwa nini wasifungwe jera ama kumlipa shehe kiasi cha sh. Milioni 250.


KIONGOZI WA BREXIT NIGEL FARAGE AHUTUBIA KATIKA MKUTANO WA DONALD TRUMP.

Donald Trump na Nigel Farage.

Mwanasiasa mmoja wa Uingereza aliyeongoza kampeni ya kujiondoa kutoka ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) Nigel Farage, amehutubia katika mkutano mmoja wa kampeni za uraisi za chama cha Republican nchini Marekani.

Huku mgombea wa urais chama cha Republican, Donald Trump akisimama naye, kinara huyo anayeondoka katika chama cha UK Independence Party (UKIP) amewaambia wafuasi wa Republican kuwa mambo mengi yanawezekana watu wema wakisimama kidete kupinga uongozi wowote ule.

Mkutano huo ulifanyika Jackson, Mississippi umehudhuriwa na jumla ya wanaharakati 15,000 wa chama cha Republican.

Wakati wa kampeni ya kutetea kujiondoa kwa Uingereza kutoka UE, Trump alitangaza uungaji mkono wake.

Farage alipokuwa akihutubia alisema kampeni inayoendeshwa kwa sasa na chama cha Republican inatoa fursa nzuri sana.

"Mnaweza kuwashinda watu wanaofanya kura za maoni, mnaweza kuwashinda wachanganuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi, mnaweza kuwashinda watu wanaodhibiti Washington" Alisema Farage.

Kiongozi huyo wa UKIP pia alihudhuria mkutano mkuu wa kuidhinisha mgombea urais wa Republican jijini Cleveland, mwezi uliopita.

Lakini alisema pia angekuwa Mmarekeni asingethubutu kumpigia kura mpinzani mkuu wa Trump, mwanamama Hillary Clinton wa chama cha Democratic hata akilipwa.

Trump alihutubia katika mkutano huo akimsifu Farage na kusema aliwezesha Uingereza kuchukua tena udhibiti wa mipaka yake wakati wa kura ya kujiondoa kutoka UE.


NDEGE NDEFU ZAIDI DUNIANI IMEANGUKA.

Airlander ilivyoanguka

Ndege ndefu zaidi duniani - Airlander 10 imeharibika baada ya kuanguka wakati ikitua katika safari yake ya pili ya kufanyiwa majaribio.

Ndege hiyo ya urefu wa 302ft (92m) ambayo kwa kiasi fulani ni ndege na pia kwa kiasi fulani ni puto. Iliharibika ikiwa katika uwanja wa Cardington, Bedfordshire nchini Uingereza.

Ndege hiyo ya thamani ya £25m imeharibika eneo wanaloketi marubani baada ya kuanguka kwa pua mwendo wa saa tano za Uingereza.

Msemaji wa HAV kampuni iliyounda ndege hiyo amesema marubani na wahudumu wengine wote wapo salama.

Kampuni hiyo imekanusha madai kwamba waya uliokuwa umening'inia kutoka kwenye ndege hiyo ulikwama kwenye kigingi cha nyaya za simu na kusababisha ajali hiyo.

Ndege hiyo ilifanya safari yake ya kwanza 17 Agosti. Kampuni ya HAV inapanga kuunda ndege 10 aina ya Airlander kufikia 2021.


ASKARI POLISI WANNE WAUAWA JIJINI DAR ES SALAAM.

Kamishina Nsato Marijani akitoa ufafanuzi.

Polisi wanne wameuawa na raia wawili kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha ambapo pia walipokonya bunduki mbili na risasi kadhaa, jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa bado haijajulikana chanzo cha mauaji japo polisi wanasema wanahisi tukio ni la ulipizaji kisasi dhidi ya polisi.

Jeshi la polisi chini ya kamishna wa operesheni na mafunzo, Nsato Marijani limethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilikuwa la uvamizi wa moja ya benki jijini humo huku wakiwa na ulakini wa mazingira ya uharifu huo.

Anasema inaonekana kuwa tukio hilo halikulenga kuivamia benki bali lililenga kuua askari ili kulipiza kisasi kwakuwa hakuna kitu chochote kilichopotea au kuharibika katika benki hiyo.

Aidha jeshi hilo limesema kuwa kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kushabikia mauaji ya askari hao na kukejeri mazoezi walokuwa wakifanya, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa kusikika katika majukwaa yao wakiwahamasisha wafuasi wao kuwashambulia polisi.

Hatua hiyo imepelekea jeshi la polisi kutoa onyo kwa kukemea tabia hiyo na kuahidi kuwafatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliofanya uchochezi wa tukio hilo kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na hayo jeshi la polisi pia limesitisha mikutano ya ndani yenye wasiwasi wa kuchochea uhalifu kwa kuwa wamebaini mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuhamasisha uhalifu.