Huo ndio mwonekano mpya wa mwanadada Ray C aliyekuwa akisumbuliwa na madawa ya kulevya.
Alituma picha yeye mwenyewe kwenye akaunti yake ya Instagram. Inasemekana pia Ray C ameondoka kwenye kituo cha sober kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam bila kutoa taarifa yoyote.
Wednesday, September 7, 2016
MUONEKANO MPYA WA RAY C.
UTAFITI: VITAMIN D HUPUNGUZA PUMU.
Matumizi ya virutubisho vya Vitamin D pamoja na dawa za pumu hupunguza hatari ya shambulio la ugonjwa wa pumu.
Utafiti uliofanywa na watafiti wa Cochrane umebaini kwamba vinapunguza shambulio la wagonjwa wanaotumia steroids.
Lakini watafiti wanasema kuwa haijulikani iwapo inawasaidia wagonjwa walio na upungufu wa Vitamin D.
Wanasema utafiti zaidi unahitajika kabla ya kuwapa wagonjwa ushauri rasmi.
Walipendekeza kuzungumza na wauza dawa ili kupata ushauri kabla ya kutumia virutubisho vya Vitamin D.
Kiongozi wa watafiti hao Profesa Adrian Martineau anasema kuwa walibaini kwamba Vitamin D inapunguza makali ya Ugonjwa wa Asthma, bila kusababisha athari zozote.
MRISHO MPOTO: MR.BLUE NDIO MSANII BORA TANZANIA.
Mwanamziki wa nyimbo za asili Tanzania, Mrisho Mpoto siku ya jana aliongea mkoani Tabora katika semina ya fursa ya Fiesta na kukiri kuwa Mr.Blue ndiye msanii bora Tanzania kwa sasa.
Mrisho aliyasema hayo maneno wakati anawaelimisha wakazi wa Tabora kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika nchi yetu.
"Nilikuwa sijui kama Mr.Blue ni yule kijana ambaye niliyekuwa namsikiaga enzi zile lakini Leo nimeuliza baada ya kuona akitumbuiza kwenye jukwaa la Fiesta nikaambiwa ni yeye" alisema Mpoto.
"Nabadilisha kauli zangu zote nilizowahi kusema nyuma, tena naangalia na Kamera kabisa na kusema Mr.Blue ndiye msanii bora Tanzania kwa sababu mpaka sasa ameweza kudumu kwenye tasnia hii ya mziki kwa muda mrefu bila kuacha" alimaliza kwa kusema hivyo.
Mr.Blue ni moja kati ya wasanii wachache waliotumbuiza Fiesta zote zilizoanza jijini Mwanza mpaka wiki hii ndani ya Tabora na Singida.
WANAODAIWA NHC KUPEWA SIKU SABA NA MAGUFULI.
Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa malimbikizo ya kodi na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha zinalipa madeni yao, vinginevyo mali zao zitatolewa nje.
Dk. Magufuli amemtaka mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu kutomuogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, CCM, Chadema au kiongozi yeyote wa serikali endapo hajalipa pango lake la nyumba, atolewe nje mali zake.
Pamoja na hayo mkuu wa nchi amewaahidi makazi wakazi 644 wa Magomeni kota wilaya ya Kinondoni kuwa ndani ya miezi miwili ujenzi wa nyumba za kisasa zitaanza katika eneo hilo na ndani ya mwaka mmoja zikishakamilika wakazi hao watakuwa wa kwanza kupatiwa nyumba hizo.
Akizungumza na wazee waliokuwa eneo hilo, Rais alisema tayari ameshatoa maagizo kwa taasisi zote za serikali zikiwemo Wizara zinazodaiwa na NHC kuhakikisha zinakamilisha madeni yao ndani ya siku saba.
"Wasipolipa nakuagiza Msechu watolee nje vitu vyao kama ulivyomtolea nje yule jamaa. Usiogope mtoe mtu yeyote asiyelipa pango. Lazima watu hawa wakulipe ili uweze kupata fedha za kuendeleza shirika hilo"alisema Magufuli.
"Nashangaa eti hawa wa serikalini wanashindwa kulipa pango la nyumba kwa NHC, lakini pesa za safari ya nje wanazo kila kukicha wanaomba vibali vya kusafiri na kupeana posho" alisema na kuongeza pia endapo shirika hilo litazitolea nje baadhi ya taasisi na Wizara za serikali kwa kushindwa kulipa kodi, itakuwa ni vyema kwakuwa sasa taasisi hizo zitaenda moja kwa moja Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Miongoni mwa taasisi zinazoongoza kudaiwa ni Ofisi ya Rais ml10, Wizara ya ujenzi na uchukuzi bilioni 2, Wizara ya Habari, tamaduni, Sanaa na michezo bilioni 1, Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto bilioni 1, Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ml 613, Tume ya haki za binadamu na utawala bora ml 360.
BEYONCE ASHAURIWA NA MADAKTARI KUPUMZISHA SAUTI.
Mwanamziki Beyonce amehairisha tamasha lake la New Jersey kwa jina la World Tour baada ya madaktari kumshauri kupumzisha sauti yake.
Msanii huyo ambaye alisherehekea siku yake ya 35 ya kuzaliwa siku ya jumapili alitoa taarifa akisema tamasha hilo halitafanyika mnamo tarehe 7 Octoba.
Hata hivyo ataendelea na tamasha nyingine katika miji ya Los Angeles, Houston, New Orleans na Atlanta kama ilivyopangwa.
Ziara hiyo ambayo inalenga kuuza album yake mpya ya Lemonade ilianza mjini Miami mnamo tarehe 27 mwezi April.
Ilitarajiwa kukamilika Nashvile mnamo tarehe 2 mwezi Oktoba, lakini sasa inaonekana kwamba New Jersey itaandaa tamasha lake la mwisho
MWANAMKE AKAMATWA AKIUZA MABINTI.
Jeshi la polisi katika mkoa wa Mara linamshikiria Juritha Lucas (60) mkazi wa kijiji cha Masinki Wilaya ya Serengeti mkoani humo, kwa tuhuma ya kufanya biashara haramu ya binadamu kinyume cha sheria.
Kamanda wa polisi mkoani Mara, kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi Ramadhani Ng'azi alisema mwanamke huyo alikamatwa na polisi akiwa na mabinti watano wenye umri kati ya miaka 15 na 23 alokuwa anataka kuwauza.
Kamanda Ng'azi alisema mabinti hao ni wakazi wa kijiji cha Muruvyagiza, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ambako ndiko mwanamke huyo aliwatoa na kuwasafirisha hadi katika kijiji cha Masinki Wilayani Serengeti, kwa nia ya kuwauza kwa kuwaozesha kwa wanaume kwa bei kati ya 150,000 hadi 300,000 kila mmoja kulingana na umri, uzuri na tabia ya binti husika.
Polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema kuhusu biashara hiyo, waliweka mtego na ndipo Septemba 4 mwaka huu walimkamata mwanamke huyo na kumhoji na akakiri kuwachukua mabinti hao kutoka mkoani Kagera kwa ajili ya kuwauza.
Jitihada zinafanyika ili kuwasiliana na wazazi wa mabinti hao ili kuwachukua.
Kamanda Ng'azi hakuwataja majina kwa ajili ya usalama, lakini walisema wanaendelea na uchunguzi wa kina na kuwa baada ya upelelezi kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya kufanya biashara ya binadamu kinyume cha sheria.
AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMTUSI MAGUFULI.
Mfanyabiashara Leonard Materu (31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kutuma ujumbe wa kumtishia Rais John Pombe Magufuli kwenye mtandao wa Whatsapp.
Materu ambaye ni mkazi wa Moshi bar kwa diwani, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo mbele ya hakimu mkazi Magreth Bankika.
Akisoma mashtaka wakili Diana alidai mshtakiwa huyo amefunguliwa kesi hiyo kwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Whatsapp chini ya sheria ya mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa kuwa Julai 17 mwaka huu jijini Dar es salaam Materu aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma kupitia Whatsapp ukisomeka; Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.
Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais Magufuli. Baada ya kusomewa mashtaka, mshitakiwa alikana kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kuombwa tarehe nyingine kutajwa.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati ya sh. Milioni 5. Kesi itatajwa tena Septemba 20 mwaka huu.
WANAFUNZI WA DARASA LA SABA WAANZA MITIHANI LEO.
Watahiniwa 795,761 wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) unaofanyika leo na kesho nchini kote.
Akizungumza Dar es salaam jana katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 372,883 ambao ni sawa na asilimia 46.86 ni wavulana na 422,878 ni wasichana sawa na asilimia 53.14.
Mwaka 2015 watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 775,729 huku 763,602 ndio waliofanya mtihani huo na wanafunzi 518,034 walifaulu.
Msonde alisema watahiniwa 765,097 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili na watahiniwa 30,664 watafanya mtihani kwa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia wakati wa kufundishwa. Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Sayansi, Hisabati na Maarifa.
Amesema watahiniwa wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 95 wakiwemo wavulana 57 na wasichana 38 wakati wale wenye huoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa ni 810 ambao kati yao wavulana ni 402 na wasichana 408.
"Wasimamizi wanatakiwa kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Nawaasa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya Taifa" alisema Msonde.