Thursday, September 15, 2016

TRUMP AKATISHWA KUTOA HOTUBA NA MCHUNGAJI BAADA YA KUANZA KUMKASHIFU MGOMBEA MWENZAKE CLINTON.

Mchungaji wa kanisa moja la watu weusi katika jimbo la Michigan, Marekani amemkatisha Donald Trump akihutubia alipoanza kumshutumu mpinzani wake Hillary Clinton.

Mchungaji Faith Green Timmons alimkatisha Trump alipomshutumu mgombea huyo wa chama cha Democratic kuhusu mikataba ya kibiashara.

"Trump nilikualika hapa uje utushukuru kwa juhudi ambazo tumefanya Flint, si kutoa hotuba ya kisiasa" alisema mchungaji huyo wa kanisa la Bethel United Methodist.

Trump aliendelea na kuzungumza kwa kifupi kuhusu kutatua tatizo la maji safi Flint, lakini baadhi ya watu kwenye umati wakaanza kumzomea.

Mwanamke mmoja alisema kwa sauti kwamba mfanyabiashara huyo tajiri alitumia njia za kibaguzi katika kampeni yake.

Mfanyabiashara huyo alimjibu "haiwezekani umekosea, nisingeweza kufanya hivyo".

Mchungaji huyo aliingia tena na kuwashutumu waliokuwa wanamzomea Trump na kusema "yeye ni mgeni katika kanisa langu na inabidi mumuheshimu".

Trump mwishowe alilazimika kukatiza ghafla hotuba yake ambayo ilidumu kwa dakika sita hivi.


MWANAMKE AKAMATWA KWA KUIBA MTOTO MWENYE SIKU 10.

Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi wa Kipawa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za wizi wa mtoto Angel Meck mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo Maimuna Mohammed mkazi wa Chamwino katika manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea Septemba 13, saa tano asubuhi katika mtaa wa Kilimahewa manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka kituo cha Afya Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera kisha wagawane.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mama mtoto baada ya kugundua kuwa ameibiwa alienda kutoa taarifa kituo cha polisi. Ndipo polisi walipoanza kufanya msako kwenye mabasi yote ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani akienda mkoani Dar es salaam.

Mtuhumiwa alikiri na kusema hakuwa na nia mbaya bali alitaka kwenda kumlea huyo mtoto.


LOWASA AMKOSOA RAIS MAGUFULI.

Lowassa

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowasa amemkosoa mpinzani wake rais Magufuli kwa kile alichokitaja ni udikteta nchini humo.

Akizungumza na mwandishi wa BBC nchini Kenya, alisema kuwa alitarajia kwamba Magufuli angeondoa urasimu serikalini lakini kuna mambo mengi hayajakwenda sawa, japokuwa alikataa kutoa mifano alipotakiwa kufanya hivyo.

Lowasa alikuwa katika chama tawala alipokuwa Waziri Mkuu, lakini mwaka uliopita alijiunga na upinzani wa CHADEMA ambapo alishindwa na Rais Magufuli wakati wa uchaguzi.

Magufuli alipewa jina tinga (Bulldozer) anajulikana kufanya maamuzi yanayopendwa tangu achukue madaraka mwaka uliopita, kama vile kufutilia mbali sherehe za Uhuru ili kuhifadhi pesa.