Thursday, October 20, 2016

TCU KUANZA KUSAJILI WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KWA AWAMU YA PILI NA YA MWISHO.

Image result for tcu image tanzania
Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU), imefungua awamu nyingine ya udahili ili kuwapa nafasi wanafunzi ambao hawakuchaguliwa katika awamu zilizopita kutuma maombi upya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka TCU Dk. Kokuberwa Mollel amesema awamu hiyo ya mwisho itakayodumu kwa siku tatu itaanza Oktoba 24 hadi 26.

Amesema udahili huo utahusisha waombaji waliokwisha tuma maombi yao lakini walishindwa kuchaguliwa kutokana na kukosa sifa za kuingia katika kozi walizoomba.

''Awamu hii itawahusisha wahitimu wa kidato cha sita, stashahada na sifa linganishi, wengi wao walishindwa kuchaguliwa kutokana na ushindani mkubwa katika programu walizoomba, kushindwa kukamilisha taratibu za uombaji na waombaji kukosa sifa kwa kozi walizoomba'' Alisema.

Hadi sasa wanafunzi 61590 wameshachaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali na wanafunzi 17717 wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu bado wapo kwenye mfumo wa uchakataji.

MGAO WA MKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUPITIWA UPYA.


Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu Tanzania (TAHLISO), imekubaliana na Wizara ya Elimu kupitia upya mchakato wa mgao uliofanyika kwa mara ya kwanza ili kuondoa kasoro zilizojitokeza mara ya kwanza.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Stanslaus Kadugazile amesema makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kukutana leo Alhamisi na viongozi wa Wizara hiyo pamoja na wahusika wanaopokea, kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

''Tumejadiliana juu ya changamoto zote zilizojitokeza kwenye mgao uliokwenda vyuoni pamoja na viwango vidogo vya fedha walizopangiwa wanafunzi kwa ajili ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa pamoja na ada na kuona ipo haja ya kufanya marekebisho ya viwango hivyo vilivyopangwa kwa wanafunzi hao ili kuweza kukidhi mahitaji halisi kwa kila mwanafunzi anayestahili kupata mkopo na kutoa mgao mpya tofauti na wa kwanza''. Alisema.

MSAMI AELEZA SABABU ZA KUACHANA NA UWOYA.

 MSAMI
Mtu wangu kama wewe utakuwa ni mpenzi wa kufuatilia mahusiano ya mastaa basi penzi la Mrembo kutoka Bongomovie (Irene Uwoya) na Mkali kutoka Bongoflevani (Msami)  litakuwa sio penzi geni kwenye macho yako leo  October 19 2016 Msami ameweka wazi sababu za kuachana na Ireen Uwoya
kuachana kama kuachana mimi sioni kama tumeacha kwasababu mimi na Ireen bado tunawasiliana sema tu mimi niliona kuna vitu haviendi sawa nikaamua kukaa pembeni yaani sina sababu maalumu ila niliamua tu mwenyewe

WANAVYUO 66,000 WAKOSA MIKOPO.

Dar es Salaam. Ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni mwaka jana kwamba katika Serikali yake hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo wa masomo ya elimu ya juu imekuwa ngumu kutekelezeka.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wengi hawatapata.
Uwezo wa bodi hiyo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa na asilimia 24 na waliopatiwa hadi sasa ni wanafunzi 11,000 sawa na asilimia 12.
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

MTANZANIA KUIWAKILISHA AFRIKA KWENYE SHINDANO LA MAPISHI.

Mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Fred Uisso anatarajiwa kuiwakilisha Afrika kwenye fainali za mashindano ya upishi duniani zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8 hadi 15, mwaka huu huko Alabama, Marekani baada ya kufanya vizuri katika upishi wa nyama na mkate wa kuchanganya.
Uisso, Mtanzania anayefanya kazi katika mgahawa wa Afrikando uliopo Kinondoni, atakuwa Mwafrika wa kwanza kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo. Akizungumza jana wakati wa kukabidhiwa Bendera ya Taifa, Uisso alisema alipata nafasi hiyo baada ya kushiriki katika mchakato kupitia mitandao ya kijamii.
“Walinitambua kupitia kazi zangu ambazo nilizifanya mtandaoni katika dunia nzima tulikuwa zaidi ya watu 3,700 na kila mmoja alionesha uwezo wake wa kupika vyakula mbalimbali, tukachujwa tukabaki 100 na baadaye hadi 21,” alisema.
Alisema kushiriki mashindano hayo ni moja ya mwanga wa ndoto zake. Anatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 28, baada ya kupata udhamini na ubalozi kupitia Kampuni ya usindikaji matunda na mboga ya Redgold.
Mshindi wa jumla kwenye mashindano hayo atajinyakulia dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 210) na mshindi wa kila kipengele atajishindia dola 10,000 (Sh milioni 21).
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Geofrey Tengeneza alisema ni jambo la kujivunia kwa Mtanzania huyo kuwakilisha Afrika na kumtaka kutumia fursa hiyo kwenda kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Uisso atachuana na wapishi kutoka mataifa mengine ikiwemo Haiti, Ukraine, Marekani, Canada na Puerto Rico.

SCORPION AFUNGULIWA MASHTAKA MENGINE.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam jana imefuta na kumsomea upya mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, mshitakiwa Salum Njwete (34) maarufu kama Scorpion anayedaiwa kumtoboa macho Said Mrisho.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana kuitwa Scorpion na kuieleza mahakama kuwa anaitwa Salum Njwete Salum.
Awali, saa 3:30 asubuhi, mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore ambapo Wakili wa Serikali, Munde Kalombola aliiomba mahakama hiyo kuondoa mashitaka hayo kwa sababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kalombola alidai kuwa wameomba kufuta mashitaka hayo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria ya Makosa ya Jinai.
Katika kifungu hicho, kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa mashitaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu lakini pia kinampa mamlaka DPP kumshitaki mshitakiwa endapo kama ana nia ya kuendesha mashitaka hayo. Kutokana na maombi hayo, Hakimu Sachore alikubaliana na maombi hayo na mshitakiwa alirudishwa mahabusu.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alitolewa mahabusu akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi huku akiwa amevalia kanzu na baraghashia na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule na kusomewa mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 (a) cha Sheria ya kanuni ya adhabu.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole alidai mshitakiwa alitenda makosa hayo Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala. Alidai kuwa mshitakiwa aliiba cheni ya silver yenye gramu 38 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi, fedha taslimu Sh 331,000 pamoja na pochi vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.
Pia alidai kabla na wizi huo alimtishia mlalamikaji (Mrisho) na kisha kumchoma kisu machoni, tumboni na mabegani ili kujipatia vitu hivyo.
Wakili Gavyole, alidai kuwa upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mshitakiwa huyo pia alikana mashitaka hayo na Hakimu Haule aliiambia mahakama kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 148 kifungu kidogo cha 5 (a) mashitaka hayo hayana dhamana, hivyo mshitakiwa alitakiwa kurudi rumande na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2, mwaka huu itakapotajwa.

WANAOANZA DARASA LA KWANZA MWAKA 2017 KWENDA NA MCHE MMOJA WA MTI

Serikali imeagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha kuanzia mwakani kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na binafsi afike shuleni kwake na mche mmoja wa mti.
Aidha, imebainisha kuwa kwa upande wa shule za sekondari kila mwanafunzi atapaswa kwenda na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakati akishiriki katika upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambako aliongozana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wa Iringa jana.
Alisema agizo hilo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na linapaswa kutekelezwa mara moja; na kwamba maelekezo ya agizo hilo yatapelekwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. “...Kuanzia mwakani kila mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake,” alisisitiza January.
Alisema katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa kwenye maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa.
“Kuanzia Novemba 5 hadi 6 tumewaita wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti na mameya wote Arusha, kwa ajili ya kuwapa mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusu suala la hifadhi ya mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji,” alisema.
Waziri huyo alisema lengo la kushiriki katika upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kwamba uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.

RAIS MAGUFULI HAKUMNG'OA GAMBO UKUU WA MKOA WA ARUSHA, NI TETESI TU ZA UONGO.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
               MKUU WA MKOA WA ARUSHA MRISHO GAMBO.
Rais John Magufuli amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwa taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa amemuengua ukuu wa mkoa wa Arusha, sio za kweli, kwani ni uzushi unaopaswa kupuuzwa.
Hayo yalisemwa na Gambo, wakati akitoa maelezo ya mwisho katika kikao cha wafanyabiashara wakubwa wa mkoani Arusha, aliokutana nao kusikiliza changamoto, zinazowakabili na kuzifanyia kazi ili waweze kufanya kazi bila wasiwasi.
Gambo aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa Rais amempigia simu na kumhakikishia kuwa yeye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Arusha; na hakuna mabadiliko yoyote kwa sasa, labda afikirie kumpandisha cheo zaidi; na sio kumuengua katika nafasi hiyo.
Mkuu huyo alisema baada ya kuzungumza kwa simu na Rais, Rais aliomba kuongea na kiongozi wa chama cha wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na akamkabidhi simu Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Arusha, Wolter Maeda.
Maeda alikiri kuongea na Rais Magufuli na kusema kuwa Rais amemwambia kuwa Arusha, inatakiwa kuwa ya amani na utulivu na aliwaasa kufanya biashara bila ya wasiwasi na kulipa kodi inayostahili.
Alisema pia kuwa wafanyabiashara, wasiogope chochote na iwapo watendaji wa serikali yake, watakuwa wakifanya kazi kwa vitisho, wanapaswa kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa juu wa mkoa, kwani wanapaswa kulipa kodi inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Gambo aliwataka wafanyabiashara Arusha, kushirikiana na kufanya kazi kwa malengo ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha na sio vinginevyo na aliwaahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali. Alisema kila mkazi wa Mkoa wa Arusha, anapaswa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria ;na hakuna aliye juu ya sheria.
Aliwataka wananchi wa Arusha, kufuata kazi na kuacha siasa kwenye mambo ya msingi ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha.
‘’Mimi ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha na ninafanya kazi kwa mujibu wa sheria na wenye kufanya kazi ya siasa, wafanye siasa na sio kuingilia utendaji kazi wa kila siku wa watendaji wa serikali,’’alisema.
Kusamba kwa nakala ya barua ya Ikulu, kulizua mtafaruku katika Jiji la Arusha mchana kutwa wa jana, kwani baadhi walionesha kufurahishwa, lakini wengine walionekana kusikitishwa na utenguzi huo.

MBWANA SAMATTA AFURAHIA KUWANIA TUZO YA MWANASOKA BORA AFRIKA.

Mwanasoka wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji amesema kwamba kuingizwa kwenye kinyang'aniyo cha tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika ni heshima kuu kwa nchi yake.
Samatta, amesema amefurahi sana juu ya uteuzi huo, kwani anajiona anaendelea kuiwakilisha vyema nchi yake katika soka.
Mwanasoka Bora wa Afrika pamoja na kipa Mganda, Dennis Onyango anayechezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kiungo Mkenya, Victor Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur ya England.
Orodha hiyo ina Waalgeria watatu; mshambuliaji wa mabingwa wa England, Riyad Mahrez, Islam Slimani wa Leicester City na El Arabi Hillel Soudani wa Dinamo Zagreb.
Mkongwe Samuel Eto'o anayechezea Antalyaspor ya Uturuki naye yumo kwenye orodha, pamoja na Mcameroon mwenzake, Benjamin Mounkandjo wa Lorient.
Wamo pia Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon na Dortmund), Andre Ayew (Ghana na West Ham), William Jebor (Liberia na Wydad Athletic Club), Mehdi Benatia (Morocco na Juventus), Hakim Ziyech (Morocco na Ajax), John Mikel Obi (Nigeria na Chelsea), Kelechi Iheanacho (Nigeria na Manchester City).
Samatta akicheza dhidi ya Sho Sasaki wa Sanfrecce Hiroshima ya Japan Desemba 13, 2015
Kuna pia Cedric Bakambu (DR Congo na Villareal), Yannick Bolasie (DRC na Everton), Sadio Mane (Senegal na Liverpool) na Kalidou Koulibaly (Senegal na Napoli).
Samatta ndiye anashikilia tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika aliyotwaa Januari mwaka huu kufuatia kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe ya DRC mwaka jana na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.

TRUMP AMEKATAA KUAHIDI KUKUBALI MATOKEO YA UCHAGUZI AKISHINDWA.

Trump na Clinton Mgombea urais Marekani wa chama cha Republican Donald Trump amekataa kuahidi kukubali matokeo ya uchaguzi iwapo atashindwa, katika mjadala wa mwisho wa urais dhidi ya Hillary Clinton.
"Nitakuambia wakati huo" alimwambia muendesha mjadala Chris Wallace. Kwa siku kadhaa amedai kuwa kuna 'udanganyifu' katika uchaguzi huo.
Mjadala huo wa televisheni Las Vegas uliendeleza uhasama katika kampeni huku Trump akimuita Bo Clinton "mwanamke muovu".
Kura za kutafuta maoni zinaonyesha Trump poteza umaarufu katika majimbo makuu baada ya kukabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kingono.
Mjadala huo wa mwisho wa umefanyika wiki tatu kabla ya siku ya uchaguzi Novemba 8.
Wagombea hao walikataa kusalimiana kwa mikono kabla na baada ya majibizano hayo ya kisiasa, hatua iliyofungua kile ambacho baadaye kiligeuka kuwa mjadala wa kelele na kukatizana kauli.
Trump alitoa ahadi kwa wanachama wa Republican kuwateua majaji wa mahakama ya juu zaidi wanaoegemea 'mrengo wa kihafidhina' watakaogeuza sheria kuu inayohalalisha uavyaji mimba Marekani na kulinda haki za kumiliki bunduki.

Image copyright

Alisisitiza ahadi yake ya kuwarudisha nyumbani wahamiaji ambao hawakusajiliwa na kudhibiti mipaka ya Marekani.
Wakati huo huo, Bi Clinton ametangaza wazi kuwa atawatetea wapenzi wa jinsia moja, atalinda haki za kuavya mimba, atalenga kuinusha watu wa kipato cha wastani na kushinikiza kulipwa sawa kwa wanawake.
"Serikali haina shughuli yoyote katika maamuzi wanayofanya wanawake," alisema.
Katika mojawapo ya nyakati zilizokuwa na mvuto, Trump alikataa mara mbili kusema iwapo atakubali matokeo ya uchaguzi, hatua iliyobadili utamaduni wa muda mrefu wa wagombea wanaoshindwa kukubali matokeo baadaya kura kuhesabiwa.
"Hilo ni jambo la kuogofya," Clinton akajibu kwa ukali.
"Anaponda na kudharau demokrasia yetu. Na mimi kivyangu, nimeshangazwa kuwa mtu ambaye ni mgombea mteule wa mojawapo wa vyama viwili vikuu anaweza kuchukua msimamo wa aina hiyo."

Image copyright

Majibu ya Trump yamezusha shutuma kali kutoka kwa seneta wa Republican Lindsey Graham, aliyesema mgombea huyo "hawajibi ipasavyo kwa chama chake na taifa kwa kuendelea kuashiria kuwa anafanyiwa udanganyifu katika uchaguzi ujao," kwa mujibu wa taarifa.
Kauli nyingine kuu katika mjadala katika chuo kikuu cha Nevada ni :
  • Bi Clinton anasema Putin anataka Trump achaguliwe kwasababu anataka kinyago awe rais wa Marekani.
  • "Tuna watu wabaya na tuta watoa," amesema Trump, aliposhinikiza ahadi yake ya kujenga ukuta mpakani.
  • Bi Clinton amesema ataidhinisha mpango mkubwa wa ajira kuwahi kushuhudiwa tangu vita vya pili vya dunia.
  • Trump ameashiria bi Clinto na rais Barack Obama walipanga ghasia katika mkutano wake wa kisiasa Chicago mapema mwaka huu.