|
BARAKA NA NAJ |
Mtoto wa miaka miwili badala ya kusema kikombe akatoa tusi, hufai kumpiga wala kumgombeza. Unachotakiwa kufanya ni kumtia nguvu katika juhudi zake za kujifunza na kumwambia kwa usahihi neno kikombe linavyotamkwa. Hivyo ndivyo hata kwa mtu mgeni katika miji mikubwa.
Mshamba akitoa huko mashambani na kukutana na lifti katika majengo makubwa na kutaka kuvua viatu kisha ndio aingie, ukimcheka utakuwa juha.
Sasa unamcheka nini na hayo mambo kwao hakuna? Unashanga kitu gani yeye kuvua viatu na kutaka kuingia katika lifti wakati huko kwao kafundishwa ni ustaarabu ukikuta maeneo nadhifu uvue viatu?
Nimetoa mifano hiyo nikikumbuka tabia ya msanii Baraka Da Prince. Kwa siku za hivi karibuni bwana mdogo amekuwa na matukio na kauli za ajabu na cha kushangaza watu wanamshangaa na wengine kumtolea maneno makali.
Ni kweli Baraka anafanya mambo ya kijinga, yasiyofaa kufanywa na mtu anayejitambua. Ila mimi sishangai hayo mambo kufanywa na mtu aina ya Baraka.
Yangefanywa na Diamond, Ali Kiba na akina Chegge ningeshangaa mno. Nishangae vipi Baraka kuposti nyumba ya mama yake Naj na kusema ni yake wakati najua kijana wetu huyu bado hajatokwa matongotongo machoni?
Katu siwezi kushangaa na yeyote atakayemshangaa, nitamshangaa yeye. Ni jambo linalotarajiwa kabisa kwa kijana ambaye miaka mitatu nyuma alikuwa akishindia kababu na mihogo huku akiwa ndani ya kaptura chafu isiyojulikana rangi yake, viatu vilivyotoboka na akiwa anadhihakiwa na kila msichana anayejaribu kumchombeza, kuwafanyia unyama ndugu zake kisa kuwa na msanii Naj katika mapenzi.
Baraka ni kwanini asitokwe na akili kwa Naj wakati miaka mitatu iliyopita alikuwa akimuona bibie katika magazeti na majarida akiwa kakumbatiwa na Mr Blue, msanii ambaye Baraka huyu amekuwa akimuona toka kipindi anaomba Shilingi ishirini akanunue ice cream kwa mama John?
Siwezi kumlaumu Baraka. Kumlaumu Baraka kwa ujinga anaoufanya ni sawa na kulaumu mtoto mdogo anapotukana kipindi akijifunza kuongea.
Siku moja katika mitandao ya kijamii Baraka baada ya kuposti picha ya mpenzi wake, Najma Dustan, msanii mwenzake, mtoto wa mjini Msami akamtania kwa kujifanya anamtamani Naj.
Kilichotokea kiliniacha hoi kwa kicheko. Baraka akatokwa na matusi kwa Msami na kumwambia akamtamani dada yake.
Baraka anatupa maneno haya kwa mtu ambaye amekuwa akionekana katika video na magazeti kwa zaidi ya miaka sita sasa.
Anatokwa povu la kijinga kwa Msami kwa kudhani kuwa eti ni kweli anamtamani mpenzi wake huku akiwa amesahau ni Msami huyu ambaye aliwahi kudaiwa kutoka na mastaa wengine wakubwa wa Bongo.
Msami ni mtoto wa mjini sana kuliko Baraka. Msami kaona mengi ya kimjini kuliko yeye. Kutoka dansa hadi kuwa msanii mwenye kueleweka, Baraka anatakiwa ajue uzito wa Msami.
Yeye bado ni mgeni katika jumba la mastaa, anayofanya ni sehemu ya ulimbukeni wa kawaida kwa mgeni. Kumlaumu au kumkosoa sana ni kumkosea.
Anayofanya Baraka ni sawa na mtu ambaye hajawahi kumiliki au kuendesha gari zuri la thamani. Atatembea kila eneo kutaka kuonesha kuwa anaendesha gari zuri. Huu ni ulimbukeni.