Monday, January 2, 2017

DARASA AFUNGA MWAKA KWA KISHINDO NA MUZIKI.

Tumezoea kusikia nyimbo za mapenzi zikipendwa zaidi kuliko zile zenye ujumbe wa masuala mengine muhimu kwa jamii. Mara nyingi ngoma zenye meseji ni zile zinazohusisha mtindo wa kofokafoka yaani Rap.
Kwenye historia ya Bongo Fleva, nyimbo za Rap hazikuwahi kuzizidi zile za mapenzi. Ngoma zenye jumbe za mapenzi zinapendwa zaidi sokoni na ndiyo  zinazochezwa zaidi.
Sasa inakuwaje pale ambapo rapa anavunja rekodi nyingi kwa wakati mmoja ambazo kwa miaka mingi marapa wengine wameshindwa kuzivunja?
Hapo ndipo Swaggaz linapomkumbuka Ramadhan Sharif  ‘Darassa’ ambaye ni bosi wa Lebo ya Classic Music Group (CMG), ambaye anafunga mwaka kwa historia ya aina yake akiwa na ‘Wimbo wa Taifa’ Muziki.
Mwaka ulipoanza Darassa alitupa karata yake ya kwanza kupitia Kama Utanipenda, aliyomshirikisha Rich Mavoko.
Juni 30, akakutana na waandishi wa habari kutambulisha lebo yake ya CMG, staili yake ya kucheza anayoiita Zombie Walk na kuwaweka tayari mashabiki kwa Too Much, wimbo uliotoka Julai 12.
Grafu ya muziki wa Darassa ilizidi kupanda Novemba 23, alipotambulisha ngoma yake mpya, Muziki. Wimbo unaokua siku baada ya siku – wimbo ulioibua vituko mtaani na kupenya mpaka kwa viongozi wakubwa wa Serikali.
Hii ndiyo ngoma yenye mzunguko mkubwa kwa sasa kwenye redio, runinga mpaka kitaa. Usipousikia kwenye nyumba/chumba cha jirani yako basi utausikia kwenye baa iliyo karibu na wewe.
Ni ngumu kuukwepa labla uwe na matatizo ya usikivu ingawa utauona kwenye runinga hata ukiwa una uono hafifu basi utausikia kwenye Bajaj na bodaboda hapo mtaani.