Friday, September 9, 2016

MREMBO MWENYE NDEVU ALIYEVUNJA REKODI DUNIANI.

Mwanamitindo mwenye ndevu za urefu wa inchi Sita ametambuliwa na Guinness World Record kuwa mwanamke wa umri mdogo zaidi  duniani kuwa na ndevu zilizokomaa.

Harnaam Kaur, 24 ambaye ni mwanamke mtetezi wa kutambuliwa na kukubalika kwa hali ya mwili wa binadamu ulivyo bila ubaguzi. Anatokea Slough, Berkshire nchini Uingereza.

Ameeleza ndevu hizo ndefu kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na watu wengi waliomkejeli kutokana na muonekano wake.

Kaur ana tatizo la homoni lifahamikalo kwa kiingereza kama Polycystic ovary syndrome, ambalo humfanya mwanamke kuwa na nywele zaidi kuliko kawaida usoni.

Machi 2016 Harnaam Kaur alikuwa mwanamke wa kwanza kushiriki maonyesho ya mitindo ya London Fashion week akiwa na ndevu.


WANAHABARI NCHINI KENYA WAANDAMANA.

Waandishi wa habari nchini Kenya wameandamana Nairobi na miji mingine kupinga kile wanachosema ni kuongezeka kwa visa vya wanahabari kutishiwa na hata kuuawa.

Maandamano yaliitishwa na chama cha waandishi wa habari ambacho kinasema wanahabari watano wamefariki katika hali ya kutatanisha katika kipindi cha mwaka mmoja.

Maandamano yamefanyika siku kadhaa baada ya mwandishi wa habari za kisiasa kufariki katika mazingira ya kutatanisha eneo la Kilifi, pwani ya Kenya.

Katika waraka wao waliotuma kwa bunge waandishi hao walilalamika kuhusu namna watakavyoshambuliwa na kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa wanasiasa na umma.

Wamesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wa serikali kuu, kaunti pamoja na raia wamekuwa wakijiamulia wenyewe kuchukua sheria mkononi na kuwashambulia waandishi wa habari kwa kuwapiga na kuwatusi kwenye mitandao ya kijamii na baadhi yao kuwatishia mauaji endapo hawatotoa taarifa zinazowapendelea.

Wamesisitiza kuwa wanayo haki ya kikatiba ya kutangaza taarifa.


KAMANDA SIMON SIRRO AKANUSHA UVUMI WA KUKAMATA WANAOPUMZIKA GUEST MCHANA.

Kamanda Simon Sirro

Kamanda wa polisi kanda kuu ya Dar es salaam, Simon Sirro ametoa rai kwa wakazi wa jiji hilo na wageni wanaoingia jijini humo kutoka mikoa mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa katika mitandao ya jamii kuwa polisi wanawakamata ovyo wanaolala mchana kwenye nyumba za wageni.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Sirro leo, habari zinazosambazwa katika mitandao ya Whatsapp na Telegram pamoja na zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti kuwa polisi wanawakamata watu hao kwa madai ya uzururaji na uzembe ni uvumi.

Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu, taarifa hizo zimedai kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli la "Hapa kazi tu" jambo ambalo si la kweli.

"Ninawatoa hofu raia wema kuwa tunaendeleza operesheni kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria kwa kuendesha guest bubu" alisema.

Amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa nyumba za wageni zinazoendesha biashara kiholela kwa kuhifadhi wahalifu wakiwemo wanawake na wanaume wanaouza miili yao (dada na kaka poa).

Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi Mara kwa Mara kwenye nyumba za wageni, hotelini, migahawani, vilabu vya vileo na kumbi za starehe zinazokesha, alisema na kuongezea kuwa watakaobainika watakamatwa.

Sirro amewataka wafanyabiashara wa nyumba za wageni kufuata taratibu za kuandikisha wageni majina yao kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanazotoka na watakapomtilia mashaka mteja yoyote watoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi.


KOCHA WA ZAMANI WA TIMU YA TAIFA AFARIKI.

Kocha wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars) na timu kadhaa za ligi kuu katika miaka ya nyuma, Mohammed Msomali amefariki dunia ghafla jana alasiri akiwa amejipumzisha chumbani kwake.

Msomali pia aliwahi kushika nyadhifa za kuwa mwenyekiti wa makocha wa mkoa wa Morogoro kwa kipindi kirefu kabla ya kustaafu na nafasi yake ikanyakuliwa na kocha mkongwe John Simkoko.

Chama cha makocha mkoa wa Morogoro kupitia mwenyekiti wake Simkoko kilithibitisha  kupokea taarifa ya kifo cha nguli huyo ambaye pia aliwahi kuifundisha Moro United mwanzoni mwa miaka 2000.