Thursday, October 6, 2016

MAAMUZI YA MWIGULU NCHEMBA KUHUSIANA NA VIDEO ILIYOSAMBAA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII IKIMUONESHA MWANAFUNZI AKIPIGWA NA WALIMU.

Ni tukio la kusikitishwa lililotokea mkoani Mbeya katika shule ya sekondari ya Mbeya Day, ambapo mwanafunzi alipigwa na kundi la walimu ambao inasemekana wapo katika mafunzo (Field).

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani Mwigulu Nchemba amesikitishwa na jambo hilo na hivyo ametoa agizo kukamatwa kwa wahusika mara moja iwezekanavyo.

Kwa sasa huyo mwanafunzi aliyepigwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Mbeya kwa matibabu ya majeraha aliyoyapata sana sana kichwani.

ITAZAME HIYO VIDEO UJIONEE KILICHOTOKEA

HANS VAN PLUIJM-YANGA HAIJASHUKA KIWANGO


Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema timu yake haijashuka kiwango kama ambavyo baadhi ya wadau wa soka wanavyodai na kuongeza kuwa muda si mrefu watarudi katika ubora wao.
Baadhi ya wadau na wachambuzi wa soka kwa siku za karibuni wamekuwa wakitoa maoni yao kuwa Yanga imekwisha na wengine wakidai imechoka kutokana na wachezaji wengi kutopata muda wa kupumzika baada ya kutoka kwenye mashindano ya kimataifa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema muda sio mrefu watarudi tena na itadhihirika kama kweli wamechoka ama la.
“Sio kweli kama tumekwisha, tuko vizuri na muda sio mrefu mtaona mambo mazuri, tunaendelea kujipanga na kurekebisha mapungufu yetu kuhakikisha tunafanya vizuri,”alisema.
Yanga imetoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Matokeo hayo yameishusha kutoka nafasi ya tatu hadi ya tano ikiwa na pointi 11 sawa na Azam FC ambao wanashika nafasi ya sita, lakini Yanga ikiwa nyuma mchezo mmoja.
Timu zinazoongoza nne bora ni Simba yenye pointi 17, Stand United 15, Mtibwa Sugar 13 na Kagera Sugar yenye pointi 12.
Kikosi hicho kilianza mazoezi juzi jioni kwenye uwanja wa Polisi Kurasini kujiwinda katika mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting.
Bado timu hiyo na Simba zimekuwa zikihangaika kutafuta viwanja vyao vya nyumbani, baada ya ule wa taifa kuzuiwa kuutumia kufuatia vurugu zilizojitokeza katika mchezo wao uliopita.

NAHODHA WA SIMBA MKUDE AFUTIWA ADHABU YA KADI NYEKUNDU.


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyooneshwa nahodha wa Simba, Jonas Mkude katika mechi ya timu hiyo dhidi ya Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kama angekutwa na hatia na kadi hiyo kubaki, Mkude angekosa mechi tatu na kamati ingemhukumu kifungo cha kuanzia miezi mitatu adhabu ambayo hupewa mchezaji aliyeoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na kumshambulia mtu ambaye hakuwa na mpira.
Kuondolewa kwa adhabu hiyo kumemwepusha Mkude na kifungo cha kukosa mechi tatu, na adhabu ya kufungiwa si chini ya miezi mitatu.
Hiyo ni kutokana na aina ya kosa hilo kwamba mbali na kufuta kadi hiyo, kamati ya bodi ya ligi ya uendeshaji na usimamizi wa ligi imewaweka kiporo waamuzi wawili wa mechi hiyo Martin Saanya (katikati) na Samwel Mpenzu (pembeni) wakichunguzwa kuhusu uchezeshaji wao wa mechi hiyo.
Mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 ilitawaliwa na vurugu iliyosababisha kuharibika kwa miundombinu ya Uwanja wa Taifa, ikiwa ni pamoja na kuvunjwa mageti na kung’olewa viti.
Mwamuzi wa mechi hiyo, Martin Saanya alimwonesha Mkude kadi nyekundu ikidaiwa kuwa nahodha huyo alimpiga baada ya kukubali bao la kuongoza la Yanga lililofungwa na Amisi Tambwe ambaye kabla ya kufanya hivyo alishika mpira na mkono na ndipo kilipozuka kizaazaa.
Lakini taarifa ya TFF kwa vyombo vya habari jana ilisema kamati ya bodi ya ligi ya uendeshaji na usimamizi wa ligi iliyokutana juzi iliifuta adhabu hiyo ya Mkude baada ya kuthibitika pasi na shaka kuwa nahodha huyo hakustahili adhabu hiyo.
“Mbali na ripoti ya kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyooneshwa ‘live’ kama inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo habari za uhakika zilizopatikana juzi kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kamati iliwafungia miaka miwili Saanya na Mpenzu. Aidha, kamati hiyo imeipiga faini ya Sh milioni tano klabu ya Simba kwa kitendo cha mashabiki wake kung’oa viti katika mechi hiyo na kuiagiza ilipe gharama za uharibifu zilizofanywa siku hiyo.
“Kamati hiyo katika kikao chake imekilaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali ikiwemo kucheza bila mashabiki, adhabu hii ya Simba imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu,” ilisema taarifa hiyo.

Mwingine aliyepitiwa na ‘rungu’ la adhabu katika mechi hiyo ni Ofisa habari wa Simba Haji Manara aliyetozwa faini ya Sh 200,000 kwa kitendo chake cha kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maofisa wa mechi waliotakiwa kuingia katika eneo hilo.
Aidha, Azam imepigwa faini ya Sh milioni tatu kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu mkono mmoja badala ya miwili, jambo ambalo ni kinyume na kanuni ya 13 (1) na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 13 (6).
Nayo JKT Ruvu imepewa onyo na kutozwa faini ya Sh 500,000 baada ya msimamizi wa kituo na ofisa wa bodi ya ligi kushambuliwa na mashabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani.
Shabiki huyo amefungiwa miezi 12 na iwapo vitendo hivyo vitaendelea uwanja huo utafungiwa kutumika kwa mechi za Ligi Kuu.
Aidha Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi ya African Lyon dhidi ya Mbao FC, ikiwemo kutoa penalti isiyostahili. Mwamuzi huyo pia alipata alama za chini ambazo hazikumruhusu kucheza Ligi Kuu.
“Pia makamisaa David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi za raundi ya tano na saba walizozisimamia,” ilisomeka taraifa hiyo.

HABARI NJEMA KWA WAKAZI WA DAR ES SALAAM KUWEKEWA HUDUMA YA BURE YA WIFI.


Makamu wa rais nchini Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza mpango wa kuzindua mradi ambao utapelekea kuwekwa kwa huduma ya mtandao wa WI-FI katika maeneo ya umma na yale ya burudani mjini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa mradi huo wa kampuni ya mawasiliano nchini humo utapanua huduma za mawasiliano ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo basi kuimarisha uchumi.
''Tunawapongeza kwa kutekeleza mradi huu na tunatumai upandaji wa miti katika maeneo tofauti mjini ikiwemo maeneo ya burudani, watu wataweza kupata huduma ya mtandao ''.
Kwa upande wake Kamishna wa Jimbo la Dar es Salaam, Paul Mkonda amesema kuwa mradi huo ni mmoja wa awamu tano za juhudi za serikali kuimarisha huduma kadhaa hususani mawasiliano na huduma za mtandao kwa wote.

Utekelezaji wa mradi huo ndio mwanzo wa safari ya kujenga miji na miji mikuu katika kiwango cha Smart City nchini Tanzania.

TYSON AKILI KUTUMIA COCAINE ILI KUKABILIANA NA UGONJWA WA KIAKILI.


Bingwa wa ndondi katika uzani mzito duniani, Tyson Fury amesema amekuwa akitumia Cocaine ili kumsaidia kuyakabili matatizo ya kiakili.

Bondia huyo wa Uingereza amesema kuwa amekuwa akiugua ugonjwa wa kiakili kwa miaka kadhaa na hajafanya mazoezi tangu mwezi Mei. Nimekuwa nje nikilewa, Jumatatu hadi Jumapili na kutumia Cocaine, Fury aliliambia jarida la Rolling Stones.

Hatua hiyo inajiri siku mbili baada ya Fury kudai katika mitandao ya kijamii kwamba amejiuzulu, kabla ya kukana madai hayo saa tatu baadaye akisema alikuwa akifanya utani.

Akizungumza kuhusu maswala ya afya yake Fury aliongezea ''siwezi kukabiliana na matatizo haya na kitu kinachonisaidia ni wakati ninapokunywa ili nitoe matatizo hayo akilini, wanasema nina ugonjwa wa kiakili, nahisi huzuni, ningependa mtu aniue kabla ya kujiua.


SAMSUNG GALAXY NOTE 7 YALIPUKA NDANI YA NDEGE.


Simu ya kampuni ya Samsung aina ya Galaxy Note 7, ambayo ilikuwa imethibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, imeshika moto kwenye ndege nchini Marekani.

Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa na abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines. Shirika hilo limesema abiria waliokuwa kwenye ndege moja yake, iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky hadi Baltimore, Maryland waliondolewa kwenye ndege kwa dharura kabla ya ndege hiyo kupaa Jumatano.

Kampuni ya Samsung iliwashauri watu waliokuwa wamenunua simu za Note 7 kuzirejesha kwa kampuni hiyo baada ya kugunduliwa zilikuwa na tatizo kwenye betri zake. Samsung inasema bado inachunguza kisa hicho cha Jumatano.

''Tunashirikiana na maafisa wa serikali na maafisa wa shirika la Southwest kupata simu hiyo na kuthibitisha chanzo cha moto huo'' kampuni hiyo imesema kupitia taarifa.
Msemaji mmoja wa shirika la Southwest amesema '' abiria mmoja alitufahamisha kuhusu moto uliokuwa unafuka kutoka kwa simu. Abiria wote na wahudumu wa ndege waliondolewa salama kutoka kwenye ndege''.

Mmiliki wa simu hiyo Brian Green akizungumza na Jordan Golson wa shirika la The Verge, amesema alinunua simu hiyo tarehe 21 Septemba.

Amesema simu hiyo ilikuwa na alama ya mraba ya rangi nyeusi kwenye pakiti yake, alama ambayo iliongezwa na kampuni ya Samsung kutofautisha kati ya simu zilizokuwa zimeuzwa awali ambazo zilidaiwa kutokuwa salama na simu mpya zilizokuwa zimechunguzwa.

WATU SITA WAUAWA NA AL-SHABAB NCHINI KENYA.


Watu sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia eneo lenye nyumba za makazi Bulla usiku wa manane.

Gavana wa jimbo la Mandera, Ali Roba ameandika kwenye twitter kwamba watu sita wameuawa na mmoja kujeruhiwa, amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye plot hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.

kituo kimoja cha redio kinachojihusisha na kundi la Al-shabab kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo. Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu walioshambulia walikuwa watu kutoka maeneo mengine.

Gazeti la Standard nalo linasema kuwa walioshambuliwa walirusha guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.

Roba alisema dalili zote zinaashiria wavamizi hao walikuwa wa kundi la Al-shabab. Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa Al-shabab kutoka Somalia.

Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na umoja wa mataifa.