Monday, September 12, 2016

WAFUASI WA DINI YA KIISLAMU WASHEREHEKEA SIKUKUU YA EID EL HAJJ.

Leo ni sikukuu ya Eid El Hajj ambapo Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limewataka waislamu wote nchini kusherehekea kwa amani, huku wakiwakumbuka wenye matatizo, kuwa wepesi wa kutoa sadaka na isiwe siku ya kutenda maovu.

Katibu mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila alitangaza jana kuwa leo ni sikukuu ya Eid el hajj na kuongeza kuwa kitaifa sherehe hizo zitafanyika katika makao makuu ya Bakwata yaliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam.

Alisema mgeni rasmi katika sherehe hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo sala itaanza mapema saa moja asubuhi na Baraza la idd kuanza 2:30 hadi saa 4:00 asubuhi.

Idd El Hajj inahitimisha ibada ya hija kwa waumini mbalimbali wa dini ya kiislamu huko Makka nchini Saud Arabia, ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za dini ya kiislamu ambayo hutakiwa kutekelezwa mara moja kwa watu wenye fedha.

Angie Blog na uongozi mzima unawatakia sikukuu njema.


HILLARY CLINTON AUGUA KATIKA KUMBUKUMBU YA WAHANGA WA SHAMBULIO LA SEPTEMBA 11.

Clinton akisaidiwa kuingia kwenye gari.

Mgombea uraisi kupitia chama cha Demokratic Hillary Clinton amegundulika kuwa na ugonjwa wa homa ya mapafu baada ya kuugua katika maadhimisho ya kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Septemba 11.

Daktari wake Lisa Bardack amesema kuwa Clinton amekutwa na ugonjwa huo toka ijumaa.

Amesema pia Clinton aliongezeka joto na kuishiwa na maji mwilini katika maadhimisho hayo.

Clinton aliondoka mapema, picha zilizowekwa mtandaoni zinamuonesha akisaidiwa na msaidizi wake huku akitaka kuanguka alipokaribia kwenye gari. Lakini kwa sasa anaendelea vizuri.


WALIOKUFA NA TETEMEKO WAZIKWA JANA.

Maafa zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi mkoani Kagera ambapo imeripotiwa idadi ya vifo kuongezeka na kufikia 16 huku wengine 253 wakijeruhiwa na kusababisha simanzi na masikitiko kwa familia nyingi.

Pia nyumba 840 za makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.

Tukio hilo limemfanya Waziri mkuu Kassim Majaliwa kulazimika kufanya ziara ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tukio hilo na kuhudhuria ibada ya mazishi iliyofanyika siku ya jana.


AKAMATWA KWA KOSA LA KUTOA MIMBA NA KUFUKIA MWILI WA MTOTO.

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga linamshikilia msichana, Elizabeth Benjamin (20) anayedaiwa kutoa mimba ya miezi nane na kisha kufukia mwili wa mtoto. Viungo vya mwili wa mtoto huyo vilizagaa hovyo mtaani huku mbwa wakifanya kitoweo.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, Elias Mwita amethibitisha leo kukamatwa kwa msichana huyo Septemba 9, mwaka huu.

Alidakwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema. Polisi walimkamata nyumbani kwake mtaa wa Butengwa kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga.

Mwita amesema katika mahojiano msichana huyo alikiri kufanya kitendo hicho na kueleza kuwa katika maelezo ya awali msichana huyo alieleza kuwa yeye ni mfanyakazi wa bar iliyopo manispaa ya Shinyanga.

Alisema bado wanaendelea na mahojiano na baada ya kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Wakazi wa mtaa huo Tuma Masanja na Monica Hassan walipozungumza na mwandishi wa habari walisema kuwa baada ya tukio kutokea hawakufahamu aliyehusika na unyama huo.

Lakini baada ya siku moja walishangaa kuona askari wakifika kwenye nyumba aliyokuwa anaishi mwanamke huyo, aliyefika hapo kumtembelea dada yake, ambapo alikiri kutoa mimba ya miezi sita na kufukia mwili wa mtoto nje ya nyumba.

"Sisi tulishangaa kuona msichana huyo anaongoza moja kwa moja akiwa na askari kwenye eneo ambalo anadai alimfukia mtoto, wakajidhihirisha na kumuona hali yake ilivyo kisha wakaondoka naye kwenda kituoni lakini dada yake alikuwa akikataa kuwa ndugu yake si mhusika wa tukio hilo" alisema Monica.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Derefa alisema kuwa msichana aliyetupa mtoto na viungo vyake kuzagaa ovyo mitaani amepatikana na tayari ameshikiliwa na jeshi la polisi, ambapo lilibaini kuwa alikuwa mjamzito.