Tuesday, November 15, 2016

USAIN BOLT KUJIUNGA NA BORUSSIA DORTMUND.

Bingwa wa mbio za mita 100 duniani Usain Bolt
USAIN BOLT
Klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund imesema kuwa mwanariadha wa mbio fupi kutoka Jamaica Usain Bolt atashiriki mazoezi na klabu hiyo kwa siku chache.
Bolt amekuwa akisema kwamba angependa kucheza soka baada ya kustaafu katika riadha.
Mashabiki wa klabu ya Borussia Dortmund
Lakini wakimkaribisha, maafisa wa klabu hiyo wamesema kuwa hakuna hakiksho kwamba mwanariadha huyo ataichezea klabu hiyo katika siku za usoni.

TANZANIA KUSHIRIKI MISS AFRIKA.

Tanzania
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye , ameahidi kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika mashindano ya urembo hapa nchini ili kuondoa dosari zinazojitokeza katika mashindano hayo.
Nape ametoa ahadi hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akimkabidhi Bendera Mshiriki wa Tanzania katika mashindano ya urembo Bara la Afrika kwa mwaka 2016 yatakayofanyika Novemba 28 mwaka huu nchini Nigeria.
Nnauye ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mashindano kama haya yanakuwa na tija Tanzania hasa katika kuleta ajira kwa vijana pamoja na kuitangaza nchi kimataifa kupitia urembo."Serikali nia yake ni kuhakikisha kuwa jambo hili linakuwa bora, linaminiwa na kuheshimika hivyo watanzania wote watajivunia uwepo wa mashindano ya urembo nchini" alisistiza Mhe Nnauye.
Aidha Mwakilishi wa Millen Magese group Ltd Bw. Matukio Aranyande Chuma amesema kuwa shindano hili litailetea sifa Tanzania na ni kwa mara ya kwanza kufanyika hivyo wataitumia fursa hiyo kuitangaza nchi kimataifa kupitia urembo.
Kwa upande wake Mshiriki kutoka Tanzania anayekwenda kushiriki mashindano hayo Bi. Julietha Kabete ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono mashindano mbalimbali ya urembo Tanzania inaposhiriki."Naahidi kuitangaza nchi yangu vizuri katika mashindano haya na naomba watanzania waniombee na wanipigie kura ili niweze kushinda na kuitangaza Tanzania kimataifa katika urembo" Alisema Bi Julietha.
Mashindano ya Miss Afrika yameanzishwa mwaka 2016 na Prof. Bena Yage ambaye ni Gavana wa Jimbo la Cross River nchini Nigeria kwa lengo kupata mabalozi wa nchi za Afrika watakaosaidia kutangaza na kuelimsha waafrika kuhusu uchumi unaozingatia utunzaji wa mazingira.

TB JOSHUA:UTABIRI WANGU ULIFANIKIWA.

TB Joshua ana mamilioni ya wafuasi barani Afrika
MHUBIRI TB JOSHUA.
Mhubiri mashuhuri raia wa Nigeria TB Joshua amevunja kimya baada ya utabiri wake kuwa mgombea urais nchini Marekani Hillary Clinton angeshinda, kugonga mwamba.
Mhubiri huyo alikejeliwa kwenye mitandao ya kijamii wakati ujumbe wa utabiri wake, kufutwa na baadaye kurejeshwa katika akaunti yake ya Facebook kufuatia ushindi wa Donald Trump.
Hata hivyo, wafuasia wake wamekuwa wakimtetea wakisema kuwa utabiri wake ulitimia kwa sababu Bi Clinton alishinda wingi wa kura licha ya yeye kushindwa kutokana mfumo unaotumiwa kwenye uchaguzi nchini Marekani unaofahamika kama "electoral College".
Ujumbe mpya katika akaunti ya Joshua ya Facebook unaunga mkono maoni hayo,ukisema:
"Tumeona matokeo ya uchaguzi nchini Marekani. Baada ya kusoma, utaelewa kuwa hii inahusu kura nyingi, kura ya waamerika wengi"
"Kwa hali hii tunahitaji roho ya nabii kutambua au kumuelewa nabii." TB Joshua anaendelea kusema.

UTAFITI:24% YA WANAWAKE HUFARIKI DUNIA WAKATI WA KUJIFUNGUA.

dk-nguke-mwakatundu
DK.NGUKE MWAKATUNDU.
Wanawake 8,000 nchini   (wastani wa wanawake 24 kwa siku), hufariki dunia wakati wakijifungua, kwa mwaka.
Idadi hiyo inaifanya Tanzania kushika nafasi ya nne Afrika na ya sita duniani kwa vifo vya wajawazito na watoto, kwa mujibu wa utafiti mbalimbali duniani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Shirika la Thamini Uhai, Dk.Nguke Mwakatundu alisema katika kuthamini uhai wa binadamu, shirika limesaidia kuboresha vituo vya afya vijijini na kuwasaidia wanaojifungua kuepuka hatari wakati wa kujifungua.
Alisema nchi nyingine zinazoongoza kwa tatizo hilo ni India, Ethiopia na Pakistan hivyo ni vema serikali ikaendelea kuiangalia kwa karibu sekta hiyo muhimu ya afya na kuipa kipaumbele.
“Kwa kubaini tatizo hilo shirika letu liliona haja ya kuokoa, kuhifadhi na kuboresha maisha ya wanawake na watoto wachanga katika mikoa ya Kigoma, Morogoro na Pwani likishirikiana na serikali tangu mwaka 2008.
“Kwa kushirikiana na wadau tumejitahidi kuboresha upatikanaji wa huduma za dharura za uzazi katika vituo vya afya 19 vijijini,” alisema Dk. Mwakatundu.
Alisema mwaka 2014 shirika lilianza kampeni  ya kuhamasisha jamii mambo mbalimbali ya uzazi yanayolenga kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Mambo hayo ni pamoja na  kuhamasisha kujifungulia kwenye vituo vya afya, kufanya matayarisho ya kujifungua na kuwahi kwenye kituo mara wanapokuwa na dalili za hatari.
“Serikali ina mikakati mingi ya kukabiliana na tatizo la vifo vya wanawake na watoto ila utendaji bado ni mdogo.
“Hiyo ni  kwa sababu ya changamoto mbalimbali zinazovikabili vituo vya afya ikiwamo uchache wa watoa huduma na vifaa tiba hivyo ni vema kuwekwa mikakati thabiti ya kumaliza tatizo hilo.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kitengo cha afya ya mama na mtoto, Dk. Koheleth Winani, alisema kila mwananchi ajitahidi kuwa  na ushirikiano kupunguza vifo vya wanawake na watoto.
“Twakwimu zinaonyesha kuwa asilimia 85 ya wanawake wanaofika vituo vya afya hujifungua bila matatizo na asilimia 15 hupata matatizo kwa sababu mbalimbali zikiwamo upungufu wa damu, shinikizo la damu, malaria, ukosefu wa dawa na vifaa tiba na mengineyo,” alisema.
Alisema wanawake wakipatiwa huduma muhimu wana uwezo wa kujifungua salama hivyo iko haja kwa jamii kushirikiana na serikali kuboresha huduma hizo na kila mmoja kwa upande wake aone ana wajibu wa kuokoa vifo vya wanawake na watoto.

SAMSUNG YANUNUA KAMPUNI YA KUTENGENEZA MAGARI.

Kampuni ya kilelektroniki ya Samsung

Kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Samsung imeinunua kampuni ya kutengeza magari ya Harman International Industries kwa kitita cha dola bilioni 8 pesa taslimu ikitaka kujikita katika safu ya utengenezaji wa magari ya kiteknolojia.
Samsung imesema kuwa utengezaji wa magari ya kielektroniki ni ''kipaumbele muhimu sana''.
Soko la magari ya kiteknolojia linatarajiwa kuimarika na kufikia dola bilioni 100 kufikia 2025.
''Magari ya kesho yatabadilishwa na teknolojia mpya kama vie simu zilivyobadilika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita," alisema Young Sohn, Samsung's ambaye ni rais na afisa mkuu wa mipango katika taarifa yake.
Ununuzi huo unajiri wakati wa kashfa ya simu ya Galaxy Note 7 ambayo iliifanya kampuni hiyo na faida yake kuanguka kabla ya kuzirudisha simu hizo, na kusitisha utengezaji wake baada ya kubainika kuwa zimekuwa zikilipuka.
Samsung inajipatia mapato yake makubwa kutoka kwa biashara ya simu aina ya smartphone lakini sasa inatafuta maeneo mengine yanayoendelea.

BEI YA UNGA WA SEMBE HATARINI KUPANDA.


Bei ya unga wa sembe huenda ikapanda kutoka Sh1,200 hadi Sh2,000 kwa kilo kwenye maduka ya rejareja baada ya bei ya mahindi kupanda mara mbili ya bei ya awali.
Kwa sasa mahindi yanauzwa Sh760 kwa kilo kutoka Sh350 za awali.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki na Wazalishaji sembe na dona (Uwawase), Oscar Munisi alisema jana kuwa kupanda kwa bei ya mahindi kumetokana na kuadimika kwa nafaka hiyo nchini, hususani inayotoka Dodoma na Ruvuma, mikoa ambayo alisema imekumbwa na ukame. “Bei ya kununulia mahindi imepanda mara mbili ya awali. Tunaiomba Serikali itusaidie tupate mahindi, hali ikizidi kuwa kama hivi sasa atakayeumia ni mwananchi wa kawaida,” alisema Munisi.
Munisi alisema umoja huo ndiyo unaosambaza unga kwa asilimia kubwa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tanga na Zanzibar hivyo kuiomba Serikali iingilie kati kuimarisha hali ya upatikanaji wa mahindi ili kusitokee mfumuko wa bei. Alisema sababu zinazosababisha uhaba wa mahindi mwaka huu ni Serikali kuchelewa kuzuia bidhaa hiyo kusafirishwa nje kwa kuwa mahindi yalikuwa yameshasafirishwa. Pia alisema migogoro baina ya wakulima na wafugaji ulisababisha mimea kukatwa au kuliwa na mifugo.
Munisi alisema tatizo hilo lilijitokeza pia mwaka jana ila hali haikuwa kama ya mwaka huu baada ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoa mahindi na kuwauzia kwa bei ya Sh480 mpaka 500 kwa kilo.
Msimamizi wa Kampuni ya Msouth Extra Power Sembe, Evod Sanga alisema wameanza kuuza kiroba mara mbili ya bei ya awali ili kupata faida ya shughuli wanazofanya kuzalisha sembe.
“Tangu kuanza kwa hili tatizo, hata bei zetu tumepandisha. Kwa sasa, awali bei ya kiroba cha kilo tano ilikuwa Sh3,000 lakini sasa tunauza Sh6,000, cha kilo kumi kilikuwa kinauzwa Sh7,000 sasa Sh11,000 pia cha kilo 25 tulikuwa tunauza Sh17,000, lakini sasa ni Sh26,000 na cha kilo 50 ilikuwa Sh30,000 sasa imefikia Sh 53,000 na bado hatupati faida,” alisema Sanga.
Mshauri wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Revelian Ngaiza alisema wafanyabiashara na wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani msimu mpya utaanza Februari mwakani hivyo upatikanaji wa mahindi utakuwa wa kawaida. “Mikoa ambayo wanaegemea kupata mahindi ni ile inayotegemea msimu mmoja kwa mwaka tofauti na Kanda ya Ziwa wanaotegemea misimu miwili. Pia hali hiyo inachangiwa na mahitaji na usambazaji wa mahindi maana watu ni wengi na hiki si kipindi cha mavuno,” alisema Ngaiza
Ngaiza aliongeza kuwa endapo hali itazidi kuwa mbaya, Serikali itaingilia kwa kuuza kwa wafanyabiashara mahindi yanayohifadhiwa na NFRA ili kukabiliana na hali hiyo.

UTAFITI:TANZANIA INA JUMLA YA WAGONJWA 822,880 WA KISUKARI.

UMMY MWALIMU.
Tanzania ina wagonjwa wa kisukari wapatao 822,880 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, huku ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yakiwamo kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kansa na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa yakiongezeka kwa kasi zaidi nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema jana kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini, ulionesha kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64 wana ugonjwa wa kisukari.
Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.
Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulini. Insulini husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe.
Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.
Akitoa tamko la Siku ya Kisukari Duniani inayoadhimishwa duniani kote kila Novemba 14, Waziri Ummy alisema takwimu za watoto wenye kisukari mwaka 2015 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wote wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye kliniki nchini.
“Lakini wapo wengine wengi hawajitokezi kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali zikiwemo imani potofu, gharama pamoja na umbali wa huduma za afya zilipo pamoja na ukosefu wa elimu juu ya tatizo hili,” alieleza Ummy.
Akifafanua zaidi takwimu, Ummy alisema asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa milioni 246 duniani. Takwimu za mwaka 2015 kutoka kwenye Atlas ya kimataifa ya kisukari zinaonesha kuwa kulikuwa na wagonjwa milioni 415 duniani kote. Ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa na wagonjwa milioni 642,” alieleza Ummy na kuongeza:
“Katika Bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 14.2 mwaka 2015 na idadi hii itaongezeka na kufikia milioni 34.2, na kwa Tanzania mpaka mwaka 2015 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 822,880 wa kisukari.”
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani mwaka huu ni “Macho yote kwenye Kisukari” na waziri huyo alisema kaulimbiu hiyo inalenga katika kuwafumbua macho zaidi wananchi kwamba kisukari ni tatizo linalopamba moto siku hata siku, hivyo nguvu ziongezwe kuhakikisha wanajikinga na tabia zinazosababisha upatikanaji wa tatizo hilo.
Alisema macho hayo yaangalie zaidi katika tabia za ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku.
Alifafanua kuwa ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko cha kutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
“Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, matunda, mboga, vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa,” alieleza Ummy.
Alisema ili kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.
Alitaja madhara za ugonjwa wa kisukari kuwa ni upofu, mtoto wa jicho, shinikizo la damu kuwa juu, kiharusi, ugonjwa wa figo, kupungua nguvu za kiume, upungufu wa kinga mwilini, kuwa na vidonda hasa miguuni visivyopona pamoja na ganzi ya miguu au mikono.

MASHINDANO YA MISS TANZANIA KUBORESHWA.

Image result for MISS TANZANIA
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha mashindano ya ulimbwende yanakuwa na thamani na yenye faida.
Nape aliyasema hayo wakati akimkabidhi bendera ya Taifa, Miss Ilala 2016, Julitha Kabete ambaye pia ni mshiriki wa mashindano ya Miss Tanzania 2016, ambaye anakwenda kushiriki mashindano ya urembo Afrika yatakayofanyika Novemba 26 katika kitongoji cha Calabar nchini Nigeria.
“Tunataka mashindano ya Miss Tanzania ambaye anafaidika sio mshindi peke yake tumeona hapa huyu alikuwa mshindi wa nne na amepata nafasi ya kuwakilisha nchi, tunafahamu mashindano ya Miss Tanzania yalikuwa yamefungiwa kufanyika ila sasa yamerudi vizuri, tutaendelea kuyaimarisha yawe bora na matarajio ya serikali ni kuona tunakuwa tunafanya vizuri na siku moja hata mshindi wa Miss World atoke Tanzania,” alisema Nape.
Pia Nape alisema serikali inamtakia safari njema na ipo nyuma yake kumpa msaada pindi unapohitajika.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa Miss Julitha Kabete amesema amejiandaa kwa ajili ya mashindano hayo na anaamini atafanya vizuri kwenye mashindano hayo ambayo ndio kwanza yanaanza.
“Naomba Watanzania wanisapoti ili nifanikiwe kushinda Miss Africa ambayo inafanyika Nigeria, ni nafasi ya kipekee ambayo nimepata na nikipata ushindi ni wetu sote,” alisema Julitha.
Mashindano hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza Afrika katika kitongoji cha Calabar kilichopo Nigeria. Naye mrembo huyo akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa amejiandaa vizuri kwa ajili ya shindano hilo la kwanza kufanyika.

WAHITIMU WA ELIMU YA JUU KUBANWA.

mtz1
Sheria mpya ya kulipa mikopo kwa wahitimu wa elimu ya juu iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, itazidisha machungu kwa waajiriwa wapya na wale wa zamani.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wakopaji hao wataanza kukatwa deni hilo moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao baada ya mwaka miaka miwili tangu walipomaliza masomo yao.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wakopaji ambao tayari wamehitimu na kuajiriwa watakutana na kibano katika kulipa deni hilo kwa kukatwa asilimia 15 ya mshahara wao.
Mbali ya makato hayo, mtumishi mpya ambaye ataajiriwa baada ya kumaliza masomo yake,   mshahara wake pia itabidi ukatwe kodi ya mapato (Payee) pamoja na makato mengine yakiwamo ya mifuko ya jamii, chama cha wafanyakazi na bima ya afya.
Mathalani, muhitimu wa Shahada ya kwanza ya udaktari ambaye kwa mujibu wa sheria anapokea mshahara wa Sh 1,480,000, baada ya makato atabakiwa na wastani wa Sh 754,300.
Katika mchanganuo huo, mwajiriwa  atakatwa asilimia 15 kodi ya mapato, sawa na Sh 326,000, Sh 148,000 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), deni la mkopo  wa HESLB Sh 222,000.
Katika orodha hiyo, pia kuna makato ya    Sh 29,600 ya chama cha wafanyakazi mbali na makato ya Bima ya Afya ambayo mfanyakazi hukatwa kulingana na mshahara wake.
Watumishi wengine watakaokumbana na panga hilo la makato ni   walimu na wauguzi ambao wamenufaika au watanufaika na mkopo huo wa Serikali.
Kwa mwalimu mwenye Shahada ambaye mshahara wake unaanzia Sh 716,000 atalazimika kubaki na Sh 565,500 huku mwenye Stashahada   ambaye mshahara wake wa kuanzia ni Sh 530,000 atabakiwa na wastani wa Sh 440,000 baada ya makato yote, kwa mujibu wa sheria.
Wakati huohuo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jana ilitangaza kuwasaka kwa udi na uvumba wadaiwa wote sugu 142,470 ili wafikishwe mahakamani.
Wadaiwa hao ni walionufaika na mkopo  tangu mwaka 1994-1995 hadi Juni mwaka huu na kufikisha deni la zaidi ya Sh 239,353,750,176. 27.
Ili kuhakikisha fedha hizo za mikopo zinapatikana, HESLB itawasilisha majina ya wadaiwa hao kwenye taasisi za fedha ili kutathmni tabia zao kabla ya kukopeshwa au kuwadhamini.
Akizungumza   Dar es Saalam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru alisema kuanzia sasa wadaiwa hao na wadhamini wao wanapaswa wajisalimishe kwa bodi hiyo vinginevyo watafikishwa mahakamani.
“HESLB inatoa notisi ya siku 30 kwa wadaiwa hao  walipe kiasi chote cha madeni yao baada hapo watafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, alisema Sh 51,103,685,914 ni deni lililorithiwa kutoka kwa iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambazo zilizokopeshwa kwa wanafunzi 48,378 tangu mwaka 1994 hadi Juni mwaka 2005.
Badru alisema kuanzia Julai, mwaka 2005 hadi Juni 30, mwaka huu Bodi imetoa Sh 2,544,829,218,662.50 kwa wanafunzi 330,801.
Hali hiyo inafanya  jumla ya fedha zilizokopeshwa tangu mwaka 1994/95 hadi 2015/2016 kufikia Sh 2,595,932,575.56 ambako wanafunzi 379, 179 wamenufaika nazo.
Badru alisema kati ya mikopo yote iliyotolewa kuanzia mwaka 1994/95 mpaka Juni mwaka huu, mikopo iliyoiva ni Sh 1,425,782,250,734.31 ambayo ilitolewa kwa wanufaika 238,430.
Mkurugenzi Msaadizi wa Mikopo kutoka HESLB, Dk. Abdul Mussa Ally alisema hali ya urejeshaji wa mikopo ni nzuri.
Alisema  katika   mwaka wa fedha uliopita, Sh bilioni 36 zimekusanywa na Julai hadi Oktoba mwaka huu zimekusanya Sh bilioni 25,000.
Ally alisema ukusanyaji wa fedha hizo  umezidi kuongezeka  kutoka  Sh bilioni mbili  kwa mwezi hadi Sh bilioni sita hadi saba kwa mwezi hivi sasa.

WANAOSHINDANIA TUZO YA BBC YA MWANAKANDANDA BORA AFRIKA 2016.

Piga kura sasa
Wachezaji watano watakaoshindania Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka 2016 wametangazwa.
Wachezaji hao ni;
Pierre-Emerick Aubameyang
Andre Ayew
Riyad Mahrez
Sadio Mane
Yaya Toure.
Wachezaji hao watano walitangazwa wakati wa kipindi maalum cha moja kwa moja runingani Jumamosi.
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Mshindi atachaguliwa na mashabiki wa soka ya Afrika kutoka kila kona ya dunia. Mashabiki wana hadi saa 18:00 GMT tarehe 28 Novemba kumpigia kura mchezaji wanayempenda.
Mnamo Jumatatu, 12 Desemba, mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa moja kwa moja kwenye runinga ya BBC Focus on Africa pamoja na redio, kuanzia saa 17:35.
Tovuti za BBC SwahiliBBC Sport na BBC Africa pia zitachapisha habari za mshindi.
Aubameyang ameorodheshwa kwa mwaka wanne mtawalia, mshindi wa mwaka 2011 pia ameorodheshwa kwa mwaka wa nne, Mahrez ndiye mchezaji pekee ambaye hajawahi kuorodheshwa kushindania, Mane alishindania mara ya kwanza mwaka jana naye mshindi mara mbili. Toure ameorodheshwa kwa mwaka wa nane mtawalia.

WANANCHI WAIPINGA SERIKALI KUTUMIA FEDHA ZA MAAFA YA TETEMEKO.


Msimamo wa Serikali wa kutumia michango iliyotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera kujengea miundombinu umeendelea kupingwa, huku baadhi ya wananchi na wanasiasa wakitaka suala hilo liangaliwe upya.
Diwani wa Kashai (Chadema), Nuruhulda Kabaju akizungumza kwa kile alichodai kuwa ndiyo maoni ya wananchi, alisema wahisani waliotoa misaada walilenga kuwasaidia kwanza wananchi na suala la kujenga majengo ya Serikali lingefuata baadaye.
Kwa mujibu wa diwani huyo, kata hiyo imesajili nyumba 636 zilizobomoka na kaya 2,556 kukosa makazi na kati ya hizo, Shirika la World Vision Tanzania limetoa mifuko 212 ya saruji na nyumba 1,300 ni hatari kuishi.

KIDATO CHA PILI WAANZA MITIHANI YA TAIFA.

CHARLES MSONDE.
Jumla ya watahiniwa 435,221 wamesajiliwa kufanya upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili huku watahiniwa 1,045,999 wakisajiliwa kwa ajili ya Darasa la Nne kwa mwaka huu.
Upimaji wa Kidato cha Pili umeanza jana hadi Novemba 25 katika shule za sekondari 4,669 wakati ule wa Darasa la Nne utafanyika Novemba 23 na 24 katika shule za msingi 17,032 Tanzania Bara.
Akizungumzia upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema idadi hiyo ni ongezeko la watahiniwa 38,451 ambayo ni asilimia 9.7 ya watahiniwa 396,770 waliosajiliwa mwaka 2015.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wavulana ni 214,013 sawa na asilimia 49.17 na wasichana ni 221,208 ambao ni asilimia 50.83 huku watahiniwa 67 ni wasioona na 306 wenye uoni hafifu.
Matokeo ya Kidato cha Pili mwaka 2015, yanaonesha kuwa wanafunzi 324,068 ambao ni sawa na asilimia 89 kati ya wanafunzi 363,666 waliofanya mtihani walifaulu na kuendelea na kidato cha tatu.
Kwa upande wa upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, Dk Msonde alisema kati ya waliosajiliwa wavulana ni 507,732 sawa na asilimia 48.54 na wasichana ni 538,267 ambao ni asilimia 51.46 huku watahiniwa 76 ni wasioona na 483 kwenye uoni hafifu.
“Katika upimaji wa kitaifa wa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 8,694 ambao ni asilimia 0.8 ukilinganisha na watahiniwa 1,037,305 waliosajiliwa mwaka 2015,” alisema.
Matokeo ya Upimaji wa Darasa la Nne 2015 yanaonesha kuwa wanafunzi 869,057 kati ya wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 88.87 waliofanya upimaji wamepata alama katika madaraja ya A,B,C na D huku wanafunzi 108,829 sawa na asilimia 11.13 wamepata alama za ufaulu usioridhisha.
“Maandalizi yote kwa ajili ya upimaji huo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani na nyaraka zote muhimu katika mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara,” alisema na kuongeza kuwa upimaji wa Kidato cha Pili ni muhimu kwa wanafunzi ili kupima uwezo wa uelewa wa wanafunzi katika yale waliyojifunza kwa kipindi cha miaka mwili ya masomo na kwa Darasa la Nne ni kujua kiwango cha wanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha, Msonde amezitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na halmashauri au manispaa kuhakikisha kuwa taratibu za upimaji zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu na kwamba Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa upimaji wa Kitaifa.