Tuesday, September 6, 2016

KOFI ANNAN AZOMEWA NCHINI MYANMAR.

Kofi Annan

Wanaharakati wa kibudha nchini Myanmar wamemzomea na kumkemea katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan.

Annan alizomewa baada ya kuwasili katika jimbo la Rakhine kuchunguza mzozo wa kidini katika eneo hilo.

Mamia ya maelfu ya waislamu wa jamii ya Rohingya wameharibu makao kwenye mashambulio yaliyotekelezwa na Wabudha wengi.

Wengi wamenyimwa uraia na kulazimika kukimbia nchi hiyo.

Mashambulio hayo yamepelekea baadhi ya watu kutilia shaka kujitolea kwa kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi kutetea haki za kibinadamu.

Suu Kyi alimwita Annan kuchunguza na kupendekeza njia za kupunguza uhasama baina ya jamii zinazoishi eneo hilo.


MISS ILALA KUFANYIKA SEPTEMBA 9.

Washiriki na waratibu wa Miss Ilala.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye shindano la Miss Ilala Ijumaa, Septemba 9 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mwandaaji wa shindano hilo kutoka kampuni ya Gogetime enterprises iliyopo jijini Dar es salaam, Tickey Kitundu amesema maandalizi ya shindano hilo yanaenda vizuri.

Kitundu amesema warembo 12 watapanda jukwaani kuwania taji hilo la tiketi ya kushiriki shindano la Miss Tanzania mwaka huu pamoja na zawadi mbalimbali nyingine.

"Shindano letu linatarajiwa kufanyika ijumaa hii katika Hoteli ya Hyatt Regency - Kilimanjaro na mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema" alisema Kitundu.

Kiingilio ni Tsh50,000 kawaida na V.I.P Tsh100,000. Shindano hilo litasindikizwa na burudani kutoka kwa Mwanamziki Ruby.


HELIKOPTA KUHUDUMIA WATU KAMA TEKSI NCHINI KENYA.

Baada ya uzinduzi wa safari ya teksi kupitia mtandao wa uber, sasa uber wamekuja  kudokeza kuanzisha njia ya usafiri kupitia ndege maarufu Uber Chopper nchini Kenya.

Kampuni hiyo inalenga kushirikiana na Corporate Helicopters katika uanzilishi wa safari ya kwanza ya Uber Chopper.

Ingawa huduma ya chopper inapatikana katika nchi ya Marekani na mji wa Dubai. Wakenya walipata kionjo cha safari hiyo mjini Nairobi.


MKUTANO WA BUNGE LA 11 UMEANZA.

Mkutano wa nne wa Bunge la 11 umeanza mjini Dodoma, huku miswada Sita ukiwemo wa Sheria ya upatikanaji wa habari ukitarajiwa kuchukua nafasi kubwa.

Katika mkutano huo wajumbe wa kambi ya upinzani ambao walisusia siku kadhaa za mkutano uliopita, wamesema kwamba watahudhuria.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-MAGEUZI) alithibitisha jana kwamba wapinzani watakuwepo na kuingia bungeni.

Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha habari, Elimu na Mawasiliano ya Bunge kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, jumla ya maswali 110 yanatarajiwa kuulizwa na wabunge na kujibiwa na serikali.

Aidha Waziri Mkuu anatarajiwa kuulizwa maswali 16 ya papo kwa papo. Taarifa hiyo ilisema miswada Sita ya sheria iliyosomwa kwa Mara ya kwanza katika mkutano wa tatu wa bunge na badae kupelekwa katika kamati husika ili ifanyiwe kazi itaendelea, kushughulikiwa katika hatua zinazofuata ikiwa ni pamoja na kusoma kwa mara ya pili, kamati ya bunge zima na kusomwa kwa mara ya tatu.

Miswada hiyo ni pamoja na ule wa sheria ya upatikanaji ya habari ya mwaka 2015, Muswada wa sheria ya utathimini na usajili wa wadhamini wa mwaka 2016, Muswada wa sheria ya Mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali wa mwaka 2016.

Pia utakuwepo Muswada wa sheria ya usimamizi wa wataalamu wa kemia mwaka 2016, Muswada wa sheria ya taasisi ya utalii wa kilimo mwaka 2016 na Muswada wa sheria taasisi ya utafiti wa uvuvi mwaka 2016.

Kufikia Jana mji wa Dodoma ulikuwa umefurika wageni mbalimbali wakiwemo wabunge na maofisa wa serikali wanaohamia tayari kuanza kuendesha shughuli zao katika makao makuu mapya ya serikali.


MAJAMBAZI WAMALIZANA WENYEWE KWA WENYEWE.

Kamanda Simon Sirro akionesha silaha walizokamata.

Watu watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi wa kutumia silaha ambao wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu katika Mkoa wa Dar es salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo la Vikindu Wilaya Mkuranga Mkoani Pwani.

Licha ya kuuawa kwa majambazi hao, jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam, limefanikiwa kuwakamata watu zaidi ya saba wanaohusika katika tukio la majibizano ya risasi na polisi, lililotokea Vikindu na kusababisha kifo cha polisi mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa polisi kanda ya Dar es salaam, Simon Sirro alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.

Alisema watu hao walikamatwa kufuatia tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29, mwaka huu katika jengo la Sophia House maeneo ya Veta Chang'ombe ambapo majambazi hao walipora milioni 35 na kutoweka kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah lenye namba bandia T 549 BPK.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo uliendelea kufanyika, Septemba 3 kundi la upelelezi kutoka kanda maalumu ya Dar es salaam iliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata majambazi hao watatu na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi ya kutumia silaha na kuweza kutaja silaha mbalimbali walizonazo.