Wednesday, October 19, 2016

FAHAMU NCHI ZENYE WANAFUNZI BORA DUNIANI.

University of Sydney
Shirika la Kimataifa la Uchumi na Maendeleo (OECD) limefanya wazi matokeo ya mtihani wa kupima uwezo wa wanafunzi wanaohitimu kutoka nchi mbalimbali.

Orodha ya ubora wa vyuo vikuu hutawaliwa na vyuo vikuu kutoka Marekani na Uingereza kama vile Harvard, MIT, Stanford, Oxford, Cambridge na UCL.
Lakini baada ya OECD kuchunguza uwezo wa kusoma na kuandika miongoni mwa wahitimu kutoka vyuo vikuu, wanafunzi walio bora zaidi ilibainika wanatoka Japan na Finland na wala si Marekani na Uingereza..
Nchi zenye wanafunzi bora zaidi wanaohitimu kwa mujibu wa OECD
  1. Japan
  2. Finland
  3. Uholanzi
  4. Australia
  5. Norway
  6. Ubelgiji
  7. New Zealand
  8. England
  9. Marekani
  10. Jamhuri ya Czech
Nchi hizi zote huwa mara nyingi hazina chuo haka kimoja kinachokuwa kwenye orodha ya vyuo vikuu 10 bora duniani.
Badala ya vyuo vikuu vya Marekani kufana, yamkini vyuo vikuu vya Norway na Australia vina wanafunzi bora wanaohitimu.
Kwa mujibu wa orodha ya ubora wa vyuo ya QS World University Rankings, kulikuwa na vyuo 32 vya Marekani katika 100 bora, na chuo kikuu kimoja pekee kutoka New Zealand.
Lakini ripoti ya OECD inaonesha wanafunzi wa New Zealand wanafanya vyema kushinda wenzao Marekani.
Orodha ya ubora wa vyuo vikuu ya QS 2016-17
  1. Massachusetts Institute of Technology (MIT)
  2. Stanford University
  3. Harvard University
  4. University of Cambridge
  5. California Institute of Technology (Caltech)
  6. University of Oxford
  7. University College London
  8. ETH Zurich
  9. Imperial College London
  10. University of Chicago

MKURUGENZI WA MASHTAKA AFUTA KESI YA SCORPION.

Dar Es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala,  imemfutia shtaka linalomkabili mshtakiwa Salumu Njwete baada ya upande wa mashtaka kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani kwa sababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kutokana na maombi hayo,  Hakimu Adelf Sachore amekubaliana na ombi hilo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ambacho kinampa Mamlaka Mkurugenzi Wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa shtaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu.
Lakini kifungu hicho kinampa Mamlaka DPP kumshtaki mshtakiwa huyo endapo kama ana nia ya kuendesha shtaka hilo.
Njwete anakabiliwa na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Saidi Mrisho.
Lakini shtaka hili limefutwa  hata hivyo anaweza kufunguliwa shtaka lingine.
Tutaendele kukupa taarifa zaidi kuhusu tukio hili.

KIJANA WA KUNDI LA PANYA ROAD AZINDUKA MOCHWARI.

Mtoto aliyetambuliwa kwa jina la Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi cha uhalifu cha ‘panya road’ amezinduka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Ernest, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na mkazi wa Buza, anayedaiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi hicho, alidhaniwa amekufa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuwaibia mali zao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna vijana watatu wamekufa katika eneo la Mbagala na baada ya kufika eneo la tukio waliwakuta vijana hao wakiwa na hali mbaya.
Vijana wanaodaiwa kuwa kundi la panya road liinalojiita taifa jipya wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi baada ya kukamatwa katika msako uliofanyika Mbagala Temeke, Dar es Salaam jana. (Picha na Yusuf Badi).
Kamanda Muroto alimtaja mmoja aliyejulikana kwa jina la Kelvin Nyambocha (14) kuwa alikufa baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi na kwamba kabla ya mauti kumkuta alifuatana na wenzake kwa ajili ya kwenda kuangalia tamasha la muziki wa Singeli lililofanyika Mbagala Zakhem.
Kijana mwingine Selemani Hamis (16), mkazi wa Kilingule, alifariki akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali ya wilaya Temeke.
“Wakati watu wanarudi kutoka katika tamasha hilo, kundi la vijana hao walianza kuwavamia watembea kwa miguu na kuanza kuwaibia mali zao na ndipo wananchi waliwakamata hao watatu na kuanza kuwapiga,” alisema Kamanda Muroto.
Alifafanua kuwa Ernest alipigwa hadi kuzimia na wananchi hao walijua kuwa amekufa ambapo alipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo kuwekewa namba na kuingizwa kwenye jokofu.
“Wakati mwili wake umewekwa chini kabla ya kuingizwa kwenye jokofu, alipumua na kuzinduka na kuonekana kuwa bado yupo hai hali iliyosababisha kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu wa madaktari,” alisema.
Kamishna Muroto alisema baada ya kupata fahamu na afya yake kutengemaa alihojiwa na kuwataja wenzake 10 ambao yuko nao katika kundi moja.
Alisema kijana mwingine fundi magari aitwaye Faraji Suleiman (19) mkazi wa Buza Kwa Rulenge, hali yake ni mbaya na amelazwa katika Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Alisema Polisi kupitia Sheria ya Watoto ya Mwaka 2009 kifungu 7/9, wazazi wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anakuwa chini ya uangalizi wao, hawawekwi kwenye mazingira yatakayowasababishia madhara ya kimwili pamoja na kisaikolojia.
Alisema kuwa jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anakua kwenye malezi bora na sio kumuacha kwa walimwengu.
Aidha, alitoa mwito kwa mzazi yeyote kumsimamia vyema mtoto wake na kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 14 na kwamba atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atafungwa miezi 6 au kulipa faini ya Sh milioni tano.
Alisema kwa mazingira waliyokutwa watoto hao, wazazi wao ni watuhumiwa kwa kukiuka sheria hiyo ya watoto.
Awali taarifa ya Polisi, Temeke ilieleza kuwa inawashikilia vijana 16 wanaodaiwa ni wa kundi la uhalifu la ‘panya road’ liitwalo ‘taifa jipya’ kwa kuhusika kuwavamia watu kwenye tamasha la kuinua vipaji, la Oktoba 15 mwaka huu.

BEI YA VIFURUSHI VYA DSTV VIMEPUNGUA.

Meneja Muendeshaji wa MultiChoice- Tanzania, Baraka Shelukindo
Meneja Muendeshaji wa MultiChoice- Tanzania, Baraka Shelukindo
         
Wapenzi wa michezo na burudani za aina mbalimbali kupitia king'amuzi cha DStv kuanzia Novemba mosi watafaidi uhondo huo kwa gharama nafuu, imeelezwa.
Kwa mujibu wa Meneja Muendeshaji wa MultiChoice- Tanzania, Baraka Shelukindo, hatua hiyo imechukuliwa ili kuwapunguzia gharama wateja na kwa uhondo zaidi.
Shelukindo alisema kuwa wameamua kunufaisha wateja wake kwa kufanya mapinduzi makubwa kupitia punguzo la bei na kuongeza chaneli 8 kupitia huduma yake ya DStv.
Huduma hizo mpya za punguzo la bei zitaanza rasmi kufanya kazi kuanzia tarehe Novemba mosi, ambavyo ni DStv Premium, Compact Plus, Compact, Family na Access.
DStv Premium imefanya punguzo la asilimia 16, ambapo bei mpya sasa itakuwa Sh 184,000 wakati bei ya zamani ni Sh 219,000 wakati DStv Compact Plus, imepunguzwa kwa asilimia 17 na sasa itakuwa sh 122,500 (zamani Sh 147,000) Compact ya kawaida sasa ni Sh 82,250 wakati zamani ni Sh 84,500.
Alisema sasa kifurushi cha familia, ambacho sasa kitakuwa Sh 42,900 badala ya bei ya awali ya Sh 51,000 kwa mwezi.

SHINDANO LA MISS TANZANIA KUFANYIKA JIJINI MWANZA OKTOBA 29.

Waandaaji wa shindano la Miss Tanzania wametangaza viingilio kwa shindano hilo ambapo cha chini ni Sh 20,000.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mmoja wa waratibu wa shindano hilo Pamela Irengo alisema kiingilio cha kati kitakuwa Sh 50,000 na kile cha viti maalumu kitakuwa Sh 100,000 kwa shindano hilo lililopangwa kufanyika mjini hapa Oktoba 29.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya shindano hilo kufanyika mkoani, mara zote ilikuwa ikifanyika Dar es Salaam. Waratibu wa shindano hilo mjini hapa ni Flora and Pamela production. Tayari warembo wapo kambini kwa ajili ya shindano hilo lililopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Rock City Mall.
Pamela alisema shindano hili litafanyika mkoani hapa kwa miaka mitatu mfululizo kabla waratibu wakuu, Kampuni ya Lino Agency kuamua pa kulipeleka.
Warembo 30 watapanda jukwaani siku hiyo wakiwa kwenye vazi la ubunifu, ofisini na ufukweni. Mshindi atawakilisha nchi kwenye shindano la kumsaka mrembo wa dunia litakalofanyika Marekani Desemba.
Warembo wanaotarajiwa kuwania taji ni Julitha Kabethe, Nuru Kondo, Grace Malikita, Spora Luhende (Ilala), Diana Edward, Regina Ndimbo, Ndeonansia Pius, Hafsa Abdul (Kinondoni), Upendo Dickson, Abella John, Elineema Chagula, Irene Ndibalema (Mashariki), Anna Nitwa, Lisa Mdolo, Irene Masawe (Kanda ya Kati), Laura Kway (Kanda ya Elimu ya Juu).
Wengine ni Iluminatha Dominic, Maria Peter, Lucky Michael (Kanda ya Ziwa), Maurine Ayoub, Glory Stephano, Elgiver Mwasha, Bahati Mfinanga (Kanda ya Kaskazini), Maourine Komanya, Anitha Mlay, Irene Msabaha, Eunice Robert (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini)na Mwantumu Ally, Ester Mnahi, Anitha Kisima (Kanda ya Temeke).

FA KUMWADHIBU MOURNHO

Jose Mourinho

Shirikisho la Soka England (FA) limemwandikia barua Meneja wa Manchester United Jose Mourinho likimtaka ajieleze kuhusu matamshi yake juu ya mwamuzi Anthony Taylor ambaye Jumatatu alichezesha pambano la Liverpool na Man United huko Anfield.
Mechi hiyo iliisha kwa sare 0-0.
FA imempa Mourinho muda hadi Ijumaa kujieleza.
Uamuzi huo wa FA umekuja baada ya shirikisho hilo kuona amevunja Sheria kwa kuongea kuhusu waamuzi kabla ya mechi wanayopangiwa.
Mara baada yamwamuzi Taylor, 37, kuteuliwa kuchezesha pambano hio kuliibuka malalamiko, na hasa Mashabiki wa Liverpool, ambao walilivalia njuga suala hilo kupitia kwenye Mitandao ya Kijamii.
Akiongea na Wanahabari kabla ya Mechi hiyo, Mourinho aliulizwa kuhusu uteuzi wa Refa huyo na yeye kujibu kwamba "Nadhani Bwana Taylor ni Refa mzuri sana lakini anapewa presha kubwa na itakuwa ngumu kwake kuwa na kiwango kizuri cha kuchezesha."
FA sasa inataka maelezo kutoka kwa Mourinho kwa kuvunja Sheria iliyotungwa Mwaka 2009 inayokataza mameneja kuongea lolote kuhusu marefa kabla ya Mechi.
Meneja wa kwanza kabisa kuadhibiwa na Sheria hiyo alikuwa ni meneja wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson, ambaye alishitakiwa Mei 2011 kwa kutoa kauli kuhusu Refa Howard Webb ambayo haikuwa mbaya bali ilikuwa ya kumsifia pale aliposema alikuwa ni refa bora zaidi huko England.

KAKA WA KAMBO WA RAIS OBAMA KUHUDHURIA MKUTANO WA TRUMP.

Malik Obama

Maafisa wa kampeni wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump wamepanga kumwalika kaka wa kambo wa Rais Barack Obama kuhudhuria mdahalo wa mwisho wa urais nchini Marekani.
Maafisa hao wamesema Malik Obama, ambaye alizaliwa Kenya, atakuwa miongozi mwa hadhira itakayofuatilia mdahalo huo wa runinga, Bw Trump alikabiliana na mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Malik, aliambia gazeti la New York Post kwamba ana furaha isiyo na kifani kwamba atahudhuria mdahalo huo.
"Trump anaweza kuirejeshea Marekani fahari yake tena," amesema, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.
Wagombea wamekuwa wakitumia wageni kwenye midahalo kama njia ya kuwakabili wapinzani wao.
Bi Clinton amekuwa akiwaalika wakosoaji wakuu wa Bw Trump, bilionea Mark Cuban na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Hewlett Packard Enterprise Meg Whitman.
Katika mdahalo wa pili, Bw Trump alialika wanawake watatu amabao walimtuhumu rais wa zamani Bill Clinton kwa kuwadhalilisha kingono miaka ya nyuma.
Malik Obama amekuwa akikosoa utawala wa kakake Rais Barack Obama.