Saturday, September 3, 2016

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMTUSI RAIS MAGUFULI KWENYE MTANDAO WA WHATSAPP.

Mhasibu wa shule ya Sekondari ya Mtakatifu Josefu, Elizabeth Asenga (40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kumkashifu Rais John Magufuli kwenye mtandao wa Whatsapp.

Elizabeth alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa serikali Leonard Chalo, mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili Chalo alidai kuwa, Agosti 6 mwaka huu, huku akijua Elizabeth alituma ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya WhatsApp kwenye kundi la kijamii liitwalo STJ Staff Social Group. Inadaiwa aliandika ujumbe unaosema;

"Good morning humu, hakuna rais kilaza kama  huyu wetu duniani, angalia anavyompa Lissu umashuhuri fala lile, picha yake ukiiweka ofisini ni nuksi tupu, ukiamka asubuhi, ukikutana na picha yake kwanza, siku inakuwa mkosi mwanzo mwisho".

Baada ya mshitakiwa kusomewa mashtaka alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kesi hiyo ihairishwe hadi tarehe nyingine.

Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaotakiwa kusaini dhamana ya shilingi milioni mbili. Kesi itatajwa tena Septemba 22.

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara Juma Shabani (31) amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kesi Sita likiwemo la kutakatisha dola za Marekani 340,000 sawa na shilingi milioni 680.


MUFTI MKUU ATANGAZA EID TAREHE 12.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakary Zubery ametangaza Septemba 12 mwaka huu kuwa ndio siku ya sikukuu ya Eid Alhaj itakayoswaliwa kitaifa katika makao makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Kauli hiyo ya Mufti Zubery imetangazwa leo na Sheikh mkuu wa Dar es salaam, Alhad Mussa Salum wakati kikao cha kuwatambulisha safu ya viongozi wapya wa Baraza la Vijana la Jumuiya ya Waislamu wa Dar es salaam.


ASKOFU NCHINI ENGLAND ATANGAZA KUSHIRIKI MAPENZI YA JINSIA MOJA.

Askofu Nicholas Chamberlain

Askofu mmoja wa kanisa la Kianglikana nchini Uingereza amekuwa wa kwanza kutangaza hadharani kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja na sasa yupo kwenye uhusiano.

Kasisi Nicholas Chamberlain amesema kuwa walioshiriki katika mchakato wa kumteua mwaka uliopita walielewa fika mwelekeo wake wa jinsia moja.

"Watu wanajua nashiriki mapenzi ya jinsia moja, lakini si kitu cha kawaida kumwambia yeyote. Jinsia ni sehemu ya yule niliye, lakini ni kazi yangu ya kitume ambayo ninataka kuiangazia".

Chamberlain anasema hata hivyo anafuata kanuni za kanisa zinazosema kuwa haruhusiwi kuoa.

Msemaji wa kanisa la England amesema Nicholas hajamkera mtu yoyote na amekuwa wazi na mkweli ukiuliza. Suala lake si la siri, ingawa ni la kibinafsi kama ilivyo kwa wale walio katika mahusiano ya kimapenzi.

Inadhaniwa kuwa hakuna askofu yeyote anayehudumia aliyewahi kutangaza hadharani msimamo wake wa kingono.

Kanisa la Kianglikana kote duniani limegawanyika sana miaka ya hivi karibuni kuhusu masuala yanayohusu mwelekeo wa kijinsia na kutawazwa kwa makasisi hao wanaojihusisha na ndoa moja.


BODI YA MIKOPO YAAHIDI KUTOA MIKOPO KWA WATU WOTE WATAKAOKIDHI VIGEZO.

Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) imesema wale wote walioomba mkopo mwaka huu na kukidhi vigezo watapatiwa.

Mkurugenzi mtendaji wa HESLB Abdul Razaq Badru alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa hafla ya kukabithi vyeti kwa watu watano waliorejesha mkopo wa elimu ya juu kwa mkupuo na kwa hiari.

Badru alisema idadi ya watu walioomba mkopo mwaka huu ni wanafunzi 88,000 ambao bodi itahakikisha wale wote waliokidhi vigezo wanapatiwa fedha kwa ajili ya elimu ya juu.

Mkurugenzi huyo ambaye amehimiza walionufaika na mkopo kulipa madeni yao, alisema mwaka jana wanafunzi waliokopeshwa ni 55,000.

Kuhusu waliopewa vyeti ikiwa ni hatua ya kuwatambua, ni pamoja na mfanyakazi wa VETA Shinyanga, Richard Jafu aliyerejesha kwa mkupuo sh.14,749,950 na Francis Mwilafi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo aliyelipa sh.15,115,200.

Wengine ni mbunge wa VWAWA, Japhet Hasunga aliyerejesha sh.255,000, Profesa Peter Msoffe ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo cha Dodoma (UDOM) aliyerejesha sh. 1,430,749.

Mwingine ni Mbunge wa Biharamulo, Oscar Mukasa ingawa kiasi alichorejesha hakikutajwa ingawa mkurugenzi mtendaji wa HESLB, alisema amerejesha kiasi kikubwa kwa mkupuo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisisitiza umuhimu wa manufaiko ya mikopo kuirejesha kwa hiari ili kuiwezesha bodi hiyo kukopesha wanafunzi wengine.

Mbunge wa Biharamulo, Mukasa alisema alishauri bodi hiyo kuangalia uwezekano wa kurekebisha vigezo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi watokao maeneo ya pembezoni kunufaika na mikopo hiyo ya elimu.


KIJANA NCHINI NIGERIA ATOLEWA MACHO.

Kijana mwenye umri wa miaka 19, mkazi wa jimbo la Bauchi Kaskazini magharibi mwa Nigeria anasema kuwa macho yake yalitolewa na watu waliotaka kuyatumia kwa ajili ya sababu za kishirikina.

Viungo vya mwili wa binadamu ambavyo hutumiwa katika imani za uchawi ama kwa ajili ya mazingaombwe hutolewa kutoka kwa watoto nchini humo, na Mara nyingi watu wazima huwa hawaathiriki.

Hussain Emmanuel, ambaye kwa sasa anatibiwa katika hospitali ya mji wa Bauchi, alisema shambulio lililomuacha bila ya uwezo wa kutoona tena, lilitokea wiki mbili zilizopita katika kijiji kilicho eneo lisiloweza kufikiwa kwa urahisi la Tafawa Balewa.

Anasema alirubuniwa na watu wawili katika kijiji cha Marti kilichopo karibu na mto waliomshawishi waende kuogelea.

Emmanuel ambaye hufanya kazi yake binafsi kama fundi magari, anasema alikuwa pamoja na watu hao wawili kwa sababu mmoja wao alimuahidi kumpa kazi kusini mwa Nigeria.

Lakini walipokwenda mtoni walimshambulia, wakataka kumnyonga na mnyororo shingoni na baadae wakaamua kumgonga na kiasi cha kupoteza fahamu.

Alipoamka hakuweza kuona ndipo alipopiga mayowe hadi alipookolewa na wapita njia ambao walibaini kuwa macho yake mawili yalikuwa yameondolewa.

Polisi wanasema wanachunguza kisa hicho na hawakutoa kauli yoyote kuhusiana na sababu ya washtakiwa hao kutekeleza kitendo hicho.


UMESIKIA ALICHOSEMA NAY WA MITEGO BAADA YA SHAMSA FORD KUOLEWA?

Inajulikana kuwa Shamsa Ford aliwahi kuwa na mahusiano na Nay wa Mitego kipindi cha hivi karibuni, lakini wakaachana na kubaki kuwa marafiki tu.

Siku ya Jana watangazaji wa kipindi cha The Weekend chat show, Qwhisar na Soudy brown waliamua kumpigia simu Nay, na hiki ndicho alichosema Nay wa Mitego;

"Namtakia kila la kheri, lakini wakiachana atarudi tu. Hatuombi waachane lakini kuna hapa na pale inaweza kutokea endapo wakishindwana mimi nitampokea kwa mikono miwili".

DJ MAPHORISA KASHATUA BONGO KWA AJILI YA TAMASHA LA NYAMACHOMA.

Tamasha la Nyama Choma linafanyika leo katika viwanja vya Leaders Club kuanzia saa Sita mchana, kwa kiingilio cha shilingi 10,000 huku msanii wa Afrika Kusini DJ Maphorisa ataburudisha katika tamasha hilo.

TAZAMA ALIVYOWASILI AIRPORT.

TAZAMA MJENGO WA YA MOTO BAND.

Kiongozi wa kundi la Mkubwa na wanawe, Mkubwa Fella siku ya jana aliwaita vyombo mbalimbali vya habari kuonyesha nyumba wanayoishi vijana wa kundi la YA MOTO BAND .

Mkubwa Fella amechukua hatua hiyo kwa sababu watu walikuwa wakisema Ya Moto wanaishi kwenye vibanda, sasa ameamua kuwaonyesha na kudhihirisha kuwa yasemwayo siyo ya kweli.

TAZAMA PICHA ZA NYUMBA YA "YA MOTO BAND" HAPA CHINI.

HAYAWI HAYAWI YAMEKUWA: SHAMSA FORD KAOLEWA.

Muigizaji katika tasnia ya Bongo Movie Shamsa Ford (Chausiku), hatimaye adhihirisha watu na wasanii wenzake kwa kufunga pingu za maisha na mfanyabiashara maarufu mjini anayejulikana kama Chiddy Mapenzi.

TAZAMA PICHA ZAO ZA HARUSI.

RAIS MAGUFULI ASISITIZA KUWA SHEIN NDIO RAIS HALALI WA ZANZIBAR.

Rais Magufuli akihutubia huko Visiwani Pemba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amewataka wananchi wa Pemba wasibabaishwe na wanasiasa waliofilisika, wanaowadanganya watu na kusisitiza kuwa uchaguzi mkuu umekwisha na hautafanyika mwingine hadi 2020 na Ali Mohammed Shein ndio Rais halali wa Zanzibar.

Amewakemea wanasiasa wanaopita kila kona na wakitembea Ulaya, amesema safari zao hizo zitaishia vichochoroni kwani Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk.Shein.

"Nataka niwaambie hao wanaokwenda nje kwa kujitangaza na kujitapa, kwamba Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk. Shein...uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo 2020" alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema hayo wakati akihutubia wananchi wa mikoa miwili, kisiwa cha Pemba ya kaskazini na kusini katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Gombani ya kale, uliokuwa na lengo la kutoa shukrani kwa wananchi wa Pemba kwa kumpigia kura katika uchaguzi wa Oktoba mwaka Jana.

Alisema anakerwa na matukio ya vitendo vya chuki na uhasama ikiwemo watu kuchomeana mali zao ikiwemo mikarafuu, neema ambayo wananchi wamepewa na Mungu.

Alisema matukio hayo yanafanywa kwa lengo la kujenga chuki na uhasama huku baadhi ya watu wakiathirika vibaya baada ya kuharibiwa mazao yao.

Aliongeza kuwa, wakati akila kiapo cha utii na uaminifu aliahidi kulinda Muungano pamoja na amani na utulivu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwaonya viongozi wanaopandikiza chuki na uhasama kwamba atapambana nao kwa nguvu zote.

Aliviagiza vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinawasaka watu wote wanaofanya vurugu kiasi kuhatarisha amani na utulivu.

"Mimi nawashangaa sana watu wa Pemba, mmepata Rais mpole sana ambaye anatoka Pemba, sasa sijui mnataka nini jamani" alihoji Magufuli.

Dk.Magufuli alisema tangu kumalizika kwa marudio ya uchaguzi mkuu Machi mwaka huu, viongozi wa vyama vya upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) waliosusia uchaguzi huo ambao Dk. Shein alishinda kwa kishindo kwa asilimia 91.4 wamekuwa wakipita ndani na nje ya nchi wakidai uchaguzi huo haukua halali.


BENKI NCHINI ZIWE NA DIRISHA LA WAJASIRIAMALI WADOGO WADOGO.

Mhe.Waziri Jenista Mhagama.

Taasisi za fedha na benki zimeombwa kuwa na dirisha la wajasiriamali wadogo, badala ya kuwajumuisha na wajasiriamali wakubwa.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Jenista Muhagama alisema hatua hiyo itasaidia wajasiriamali wadogo kujikomboa kiuchumi na kupata mikopo yenye masharti nafuu ili kuendeleza biashara zao.

Mhagama alisema hayo alipofunga kongamano la huduma za kifedha na uwezeshaji, jijini Dar es salaam.

"Taasisi za fedha na mabenki muwe na dirisha la wajasiriamali wadogo ili kuwasaidia kujikomboa kiuchumi na kupata mikopo yenye masharti nafuu ili kuendeleza biashara zao. Msiwajumuishe wajasiriamali wadogo na wakubwa" alisema Mhagama kwenye kongamano hilo ambapo wajasiriamali walipata mafunzo na jinsi ya kupata huduma za kifedha kutoka kwenye benki na taasisi za kifedha.

"Mliosimamia kongamano hili muanzishe kanzidata ili iwe rahisi kuwapata wajasiriamali pale walipo. Tuanzishe ushirikiano kati ya New brand, Vicoba na serikali na vyombo vya fedha. Zipo fursa za kupata mikopo mfano, kanzidata itawawezesha wale waliopata elimu ya ujasiriamali kuongeza uchumi wao na kuongeza nafasi za ajira" alisema Mhagama.


MAJALIWA KUHAMIA DODOMA BAADA YA VIKAO VYA BUNGE KUMALIZIKA.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana.

Serikali Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi mkoa huo baada ya vikao vya Bunge kumalizika vinavyoanza wiki ijayo Septemba 6.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana, alisema baada ya kufika Dodoma ataanza kuratibu utaratibu wa Wizara mbalimbali kuanza kuhamia Makao Makuu hayo ya nchi.

Pamoja na hiyo jeshi la polisi limejipanga kuongeza vituo vya polisi ili kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi atakayenyang'anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa walishauri ujio huo ufanyike Mara baada ya vikao vya Bunge na Waziri Mkuu ameridhia swala hilo.

Alisema Waziri Mkuu atakuwa mratibu wa Wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.

Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri umefikia asilimia 90.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.

"Awali tulisema atakuja Septemba mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70" alisema Christine.


JACKIE CHAN KUPEWA TUZO YA STAHA YA OSCAR.

Achilia mbali umaarufu wake lakini Jackie Chan hajawahi kushinda tuzo za Oscar.

Mwelekezi na mwigizaji mashuhuri wa filamu Jackie Chan atapokea tuzo ya staha ya Oscar kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu.

Jopo linalotoa tuzo za Oscar pia limeidhinisha kutunzwa kwa mhariri Anne Coates, mwelekezi Lynn Stalmaster na mwandalizi wa filamu za makala Frederick Wiseman.

Rais wa jopo hilo Cherly Boone Isaacs amewataja wanne hao kama waasisi halisi na stadi katika kazi walioifanya.

Chan (62), alikuwa muigizaji nyota katika filamu nyingi za Kung fu zilizoandaliwa katika nchi yake ya kuzaliwa Hong Kong.

Alivuma kimataifa kwa filamu kama vile Rumble in the bronx, Rush hour na filamu ya vibonzo ya Kung fu panda.


KAMPUNI YA SAMSUNG YASITISHA KUUZA GALAXY NOTE 7.

Simu ya Samsung Galaxy Note 7 ikiwa imeungua baada ya kutoka kwenye chaja.

Kampuni ya kuunda simu ya Samsung imesema inasitisha uuzaji wa simu maarufu ya Galaxy Note 7 kutokana na matatizo ya betri.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutokea ripoti Marekani na Korea kusini kwamba simu hizo zilikuwa zinalipuka wakati au baada ya kuwekwa chaja.

Hilo limejiri wiki moja tu kabla ya mshindani wake mkuu Apple kuzindua simu mpya zaidi ya iPhone.

Jumatano kampuni ya Samsung ilisema imesitisha usafirishaji wa simu hizo kwa kampuni tatu kuu zinazosafirisha simu hizo maeneo mbalimbali duniani ili kufanya uchunguzi zaidi.

Mtu mmoja katika YouTube anayesema anaishi Marekani aliweka mtandaoni video inayoonesha Galaxy Note 7 ikiwa imeungua na skirini yake kuharibika.

Ariel Gonzalez kwenye video hiyo aliyoweka 29 Agosti, anasema simu yake ilishika moto baada ya kuitoa kwenye chaja rasmi ya Samsung.