Thursday, November 17, 2016

AKOSA MATIBABU MUHIMBILI KISA UREFU.

BARAKA ELIAS

Urefu usio wa kawaida umeikwamisha Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) kumfanyia upasuaji kurekebisha nyonga Baraka Elias baada ya kukosekana kwa vifaatiba vinavyokidhi maumbile yake.

Baraka mwenye urefu wa futi 7.4 alikwenda hospitalini hapo baada ya kupata rufaa kutoka Hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma.

Meneja uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi alisema matibabu ya Baraka yameshindikana kutokana na mifupa yake kuwa mirefu kupita kiasi, hivyo kukosekana kwa vifaa vya kuunganishia.

“Siyo kwamba tumeshindwa kumtibu kwa kukosekana wataalamu. Wataalamu hao tunao wengi wa kutosha, tatizo ni vifaa vinavyolingana na mifupa yake.

Hivyo vifaa labda viagizwe kwa kutolewa oda kiwandani, kinyume na hapo ni kwenda nje ya nchi kwa ajili ya upasuaji huo,” alisema.

Changamoto nyingine aliyoianisha Almasi ni urefu wa vitanda hospitalini hapo kushindwa kumtosheleza mgonjwa huyo.

“Kwa mujibu wa madaktari mtu anapofanyiwa upasuaji kuna namna anatakiwa alale kwenye kitanda, sasa huyu urefu wake ni futi 7.4 na vitanda ni futi 6,” alisema.

Baada ya kushindwa kupata tiba hospitalini hapo, Baraka anasubiri hatima ya matibabu yake nje ya nchi akiwa Majohe alikofikia.

Alisema bado anasumbuliwa na maumivu makali na hafahamu lini atapata matibabu.

“Nimeambiwa natakiwa nikatibiwe nje ya nchi kwa sababu hapa hakuna vifaa vinavyokidhi mifupa yangu. Bado sijajua ni nchi gani, lini nitaenda na gharama zikoje, nasubiri kauli ya madaktari, wao ndiyo wanajua mambo yao ya kitaalamu,” alisema.

Baraka ambaye ni mhubiri wa injili, alisema haoni kama yeye ni mtu wa ajabu na maisha yake yamekuwa ya kawaida kwa kuwa ameridhika jinsi alivyo.

Alisema nyonga zake zilivunjika alipoteleza na kuanguka akiwa nyumbani kwake Mbinga, Aprili mwaka huu na kuanza matibabu katika Hospitali ya Peramiho.

“Nilitumia gharama kubwa hadi kufika Muhimbili kwa kuwa nilikuwa siwezi kutembea. Ninachoweza kusema ni kuwa familia yangu haitaweza kugharamia matibabu nje ya nchi, nategemea sana wahisani wajitokeze,” alisema huku akikataa kuelezea kwa undani namna alivyofika Dar es Salaam.

MAISHA YA KAWAIDA.

Baraka anasema anajitambua umbile lake lilivyo, hivyo anaishi kulingana na jinsi alivyo.

“Siwezi kutamani vitu ambavyo siwezi kuvipata kutokana na maumbile yangu, mfano nguo navaa zile zinazonifaa, sina wigo mpana inapofika kwenye uchaguzi wa vitu.”

Akizungumzia nguo, Baraka alisema hununua vitambaa na kushona suruali wakati mwingine huagiza kutoka nje ya nchi.

“Kuna jamaa yangu alikuwa Marekani, ndiye nilikuwa namuagizia vitu vyangu vidogovidogo kama nguo na viatu ambavyo navaa namba 20.

“Kwenye mitumba ukizunguka unaweza kupata ila vinavyonitosha navipata kwa gharama kubwa,” alisema.

Inapotokea amepanda kwenye daladala anachagua kukaa kwenye siti ya nyuma katikati ili aweze kuweka vizuri miguu yake.

ASILI YA UREFU.

“Kwenye familia yetu hakuna mtu mrefu, hata wazazi wangu ni wa kawaida kabisa isipokuwa nasikia walikuwepo watu warefu katika vizazi vilivyopita. Haya ni mambo ya kurithi ukiwaona wazazi wangu unaweza usiamini kama ndiyo wamenizaa tulivyo tofauti kwa kimo,” alisema.

Baraka ambaye hakutaka kutaja umri wala uzito wake, hajaoa wala hana mtoto ila nje ya uhubiri alikuwa anajihusisha na kilimo cha jembe la mkono.

Kuhusu kitanda, alisema nyumbani kwake amechonga kinacholingana na urefu wake lakini anakuwa safarini, inambidi atumie kilichopo kwa shida.


FAHAMU KUHUSU UGONJWA WA MAPUNYE.

Mapunye ni kuvu inayoshambulia kichwa ambayo kitaalamu huitwa tinea capitis. Ugonjwa huu hushambulia watu wengi ingawa huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Daktari wa magonjwa ya ngozi, Dk Flemming Andersen anasema kuvu hawa huweza kushambulia eneo lote au sehemu ya kichwa.

Anasema eneo la ngozi ambalo lina mashambulizi ya mapunye huwa na umbo linalofanana na sarafu na kama eneo hilo lina nywele basi nywele hizo hunyonyoka. Andersen anaelezea dalili za ugonjwa wa mapunye ni kuwashwa na kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi.

“Ukitazama kwa makini eneo ambalo lina mashambulizi ya maradhi haya utagundua kuwapo kwa vidoti vyeusi ambavyo vinaonesha eneo ambalo nywele imeng'oka kutokana na maradhi,” anasema.

Anasema dalili nyingine ni kubanduka na kukauka kwa ngozi katika eneo lenye maambukizi na wakati mwingine eneo hilo huweza kuwa na usaha.

Maradhi haya yakikaa bila kutibiwa kwa muda mrefu husababisha dalili nyingine ambayo ni kuonekana kama kutoka majimaji kwenye eneo la ngozi lililoathirika pamoja na kutoa harufu mbaya kwenye eneo hilo lililoathiriwa na vimelea hivi vya fangasi. Andersen anasema kuna njia nyingi zinazoweza kufanya maambukizi ya mapunye. Hata hivyo ili uambukizaji ufanyike lazima kuwe na mazingira yanayofaa kuishi na kuhama kirahisi vimelea vya fangasi.

“Mazingira ambayo yanaweza kuruhusu vimelea wa fangasi (kuvu) hao wa mapunye kuhama kutoka kichwa cha mtu mmoja au mwingine ni uwepo wa hali ya joto na majimaji au unyevunyevu,” anasema.

Anasema watu ambao wako katika hatari ya kupata maambukizi ya mapunye ni wale wanaoshirikiana na wenzao vifaa vya kunyolea bila kuvisafisha vizuri, vifaa vya kufanya usafi wa mwili zikiwamo taulo.

“Pia watu wanaotoka jasho sana hasa kichwani huweza kuweka mazingira ya kuruhusu maambukizi ya ugonjwa huo yatokee kirahisi au kama mtu atafanya usafi wa mwili na maji yaliyobeba vimelea vya fangasi wa mapunye na kama mtu hatajikausha kichwa baada ya kuoga,” anasema.

Anasema pia matumizi ya vifaa vya nywele kama chanuo la kuchania nywele kwa zaidi ya mtu mmoja hususan pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi ya vimelea vya kuvu, kugusana na mtu aliye na maambukizi na pia kushirikiana mavazi kama kofia na mtu aliyekwisha pata maambukizi hayo.

Andersen anasema watu wengine ambao wanaweza kukumbwa na ugonjwa huo ni wale wenye maradhi yanayosababisha kushuka kwa kinga ya mwili kikiwemo kisukari na wale wanautumia kwa muda mrefu dawa za kuua vimelea (antibiotic).

Mara nyingi mapunye hutibika kwa dawa za kutibu kuvu, ambazo ni za kupaka na huyaponesha bila kuhitaji kutumia dawa za kumeza. Hii ni kwa kuwa ni rahisi kwa dawa ya kupaka kupenya kwenye ngozi na kusababisha matokeo yanayohitajika.

Matibabu ya mapunye huchukua muda mfupi lakini huwa ni rahisi kwa maradhi hayo kurudi baada ya kumaliza matibabu kama hatua madhubuti za kujikinga na maradhi haya hazitochukuliwa.

Namna ya kujikinga Magonjwa mengi ya kuvu hujirudia kwa waathirika hata baada ya matibabu iwapo hawatozingatia njia sahihi za kujikinga na maradhi hayo. Zipo njia mbalimbali za kujilinda usipatwe na mapunye na kuvu kwa ujumla ikiwamo kuhakikisha mwili wako hasa kichwani kinakuwa kikavu muda wote.

“Kwa sababu kuvu hupenda kumea katika sehemu yenye unyevunyevu, hivyo ni vema kuhakikisha kichwa chako kinakuwa kikavu,” anashauri mtaalamu huyu.

Anashauri ufuaji vizuri na mara kwa mara kwa nguo kama vile taulo na mashuka ili kuhakikisha kuvu wanaondolewa.

Njia nyingine ni kuepuka kushirikiana vifaa vya kunyolea nywele hasa kama hakuna namna ya kuvisafisha na dawa maalumu ya kuua vimelea kabla hujatumia kifaa hicho. Njia nyingine ya kujikinga na maambukizi ni kuepuka kushirikiana katika utumiaji wa vifaa vya kufanya usafi wa mwili kama mataulo.

“Kama kazi yako inahusisha ukaaji wa muda mrefu kwenye maji basi hakikisha kwamba unakausha mwili hasa sehemu za kichwa au unaweka dawa ya kuzuia fangasi kwenye maji hayo unayotumia,” ni ushauri mwingine wa kitaalamu.


WANAFUNZI WA SEKONDARI MKOANI KILIMANJARO WANAONGOZA KWA KUPATA MIMBA.

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, SAID MECKY SADIKI.

Wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Kilimanjaro wanaongoza kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito, baada ya takwimu kuonesha kuwa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wanafunzi 216 wamepewa ujauzito.

Wakati hiyo ikitishia mustakabali wa maisha yao ya baadaye, kwa wenzao wa shule za msingi ni tisa tu waliopewa ujauzito katika kipindi hicho kufanya jumla iwe 225.

Mkuu wa mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) ambacho kimelenga kujadili masuala ya maendeleo ya mkoa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, uchumi na kilimo.

“Nimelileta kwenu hili suala la ubakaji na ulawiti hususani kwa wanafunzi wetu wanaopewa mimba za utotoni ili tujadiliane na tuweke azimio madhubuti...hali ni mbaya na tukikaa kimya tutasababisha balaa kubwa na kuathiri hali ya taaluma,” alisema mkuu wa mkoa.

Pamoja na tatizo la mimba, lakini pia mkoa una upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa 1,875 ambavyo kwa shule za msingi ni vyumba 1,531 na vyumba 344 kwa sekondari.


WANAWAKE NA WATOTO WAHUSISHWA NA UGAIDI.

Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kupitia kikosi kazi kinachopambana na uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi, kimewakamata wanawake wanne na watoto wanne kwa tuhuma za kujihusisha na mafunzo ya ugaidi katika maeneo ya Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema watoto hao wanne walikuwa wametoroshwa kutoka familia ya Shabani Abdala Maleck ambaye ni mkazi wa Kitunda.

Kamanda Sirro alisema polisi ilipokea taarifa kutoka kwa mzazi mmoja wa kiume aitwaye Maleck, kuwa ametoroshewa watoto wanne na mtalaka wake aitwaye Salma Mohamed aliyeingizwa kwenye harakati za kigaidi.

Alisema wawili hao walitengana Februari mwaka huu na Juni mwaka huu, mwanamke huyo ndiyo alikwenda Kitunda na kuwatorosha watoto hao.

Alisema kati ya watoto hao waliokamatwa mmoja imebainika kuwa ni wa Maleck.

“Jitihada za pamoja kati ya mtoa taarifa na Polisi zilifanikisha kuwakamata wanawake wanne na watoto wanne katika eneo la Kilongoni Vikindu mkoani Pwani wakiwa wamekusanywa kwenye nyumba ya mtu mmoja anayeitwa Suleiman, wakiwa wanafundishwa mambo ya dini na harakati za kigaidi,” alisema Kamanda Sirro.

Alisema baada ya mahojiano zaidi na watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, imejidhihirisha kuwa baadhi ya watoto hao wameachishwa masomo katika shule mbalimbali nchini.

“Baadhi ya watoto wameachishwa na wazazi na walezi wao na kuingizwa katika madrasa ambazo ndizo kambi walikokamatiwa chini ya uangalizi wa wanawake waliokamatwa pamoja nao,” alifafanua.

Alisema sanjari na mafunzo ya madrasa, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu ikiwemo karate, kung-fu na judo na kufundishwa jinsi ya kutumia silaha aina ya SMG na bastola.

Pia alisema wanafundishwa kupiga maeneo tete ya kummaliza mtu pumzi na kufariki haraka wakati wa mapigano (pressure point) ili kumdhibiti adui, kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe.

“Watoto hao wamefundishwa kuwa adui yao mkubwa ni Polisi, walinzi katika taasisi za fedha na makafiri katika kujipatia kipato, wamefunzwa kupora au kunyang’anya kwa kutumia silaha na kutumia viungo vyao,” aliongeza.

Alisema wanawake hao na watoto wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao mzima katika suala hilo ili kutokomeza tabia hiyo ya kuwaachisha watoto wadogo shule na kuwaingiza katika vitendo vya uhalifu.


MPEMBA ALIYETAJWA NA RAIS MAGUFULI AFIKISHWA KIZIMBANI.

Watu sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Yusuf (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kwa jina la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, huku baadhi wakiwa hawajavaa viatu, wakitembea kwa kuchechemea.

Baada ya kusomewa mashtaka, upande wa Jamhuri ulidai unatarajia kuwapeleka washtakiwa hao katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama “Mahakama ya Mafisadi” kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa hao watapelekwa katika mahakama hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuandaa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.

Yusuf pamoja na wenzake Charles Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46) walisomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Paul Kadushi alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Aliendelea kudai kuwa katika shtaka la pili kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.

Katika mashtaka mengine, inadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.7.

Aidha, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori. Hakimu Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu mashtaka yao kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliiahirisha hadi Desemba mosi mwaka huu.

Kabla ya kutoka kwenye chumba cha mahakama, washtakiwa walimuomba hakimu awape muda waeleze jinsi walivyokamatwa kwa kuwa walipigwa sana. Mpemba alidai siku aliyokamatwa, alipigwa sana hadi sasa hawezi kusikia vizuri na viungo vyake vya mwili havina nguvu hivyo aliomba PF3 ili akatibiwe.

Mrutu alidai kuwa alipigwa hadi wakamng’oa kidole kimoja cha mkononi na washtakiwa wengine walidai walipigwa mpaka sasa wanashindwa kutembea vizuri hivyo waliomba wapewe msaada wa kutibiwa.

Hakimu Simba alisema hawezi kutoa amri ya kutolewa kwa PF3 kwa sababu Magereza wana zahanati zao na kuna taratibu wanazifuata hivyo wasiwe na wasiwasi na kama watashindwa kuwatibia, watatafuta utaratibu mwingine wa kuwapeleka katika hospitali za nje ya Magereza.

Baadhi ya washtakiwa, waliingia mahakamani hapo wakiwa wanachechemea huku wakificha sura zao kukwepa kupigwa picha. Washtakiwa wawili hawakuwa na viatu.


WAZIRI MKUU AMTIA KITANZI CHA SHISHA MAKONDA.

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atamwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha.

Hatua hiyo inatokana na kauli ya Makonda kuwatuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda, kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa na watu waliotaka kumhonga lakini akakataa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema katika udhibiti wa suala la shisha, mkuu huyo wa mkoa amefanya kazi nzuri, na kwamba kwa kuwa ameshatoa maelekezo, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makonda hana budi kuyatekeleza.

Alisema alivyosikia anawaagiza wakuu wake wa wilaya wote kusimamia maagizo yake na kama hawakusimamia atachukua hatua, basi naye atachukua hatua kwake (Makonda) asipotekeleza suala hilo ambalo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni tatizo kubwa.

“Sasa mimi nasema nakuagiza wewe usimamie na kama hutasimamia suala hilo nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na shisha kwa wanaopuliza wakiwa wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya kusalimia wananchi katika hafla hiyo.

Katika salamu zake, Makonda alisema Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya shisha, hivyo alimwagiza Kamanda Sirro kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa kiwango kikubwa.

“Lakini Waziri Mkuu nimeshangaa kupita katika baadhi ya maeneo na kuona watu wameanza tena kuvuta shisha na nilipouliza wakasema wewe ndiyo umetoa kibali cha shisha,” alieleza Makonda na kuongeza alishangaa Waziri Mkuu alipiga marufuku shisha, ni lini ametoa kibali kuanza kutumika.

Lakini mkuu huyo wa mkoa alienda mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha watu 10 waliokwenda kwake ambao anawatambua kama “maajenti wa shetani” ambao wanapata faida kati ya Sh milioni 35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi kutokana na dawa hizo za kulevya.

Alidai watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele kuhusu shisha na wao waendelee kupata faida. “Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nimeshamuagiza Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana kigugumizi… lakini sijajua kama hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC wa Kinondoni nimemuona hapa, lakini hawa wana kigugumizi sijui kama hizi tano tano zimepita kwao,” alisema Makonda.

Alisema aliamua kufanya ziara mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo wanavuta shisha, hivyo uwezekano miaka 10 ijayo vijana wengi kuwa matatizo ya afya, hivyo kumwomba Waziri Mkuu kutochoka kusimamia suala hilo na taasisi zote ili likome katika mikoa yote.