Jeshi la polisi mkoani Dodoma limepiga marufuku na kuwataka wananchi wasishiriki katika maandamano yatakayofanyika Septemba mosi.
Limesema maandamano hayo ya ukuta ambayo yameandaliwa na Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA si halali na yana nia ya kupotosha na kuvuruga amani ya nchi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa amesema kwa muda mrefu kumekuwa na makundi ya wafuasi wa Chadema kuhamasishana ili kufanya vurugu kupitia hoja ya maandamano waliyoyapa jina la UKUTA.
"Wapo watu wanaosambaza machapisho mbalimbali yenye kauli za uchochezi katika fulana, mabango na katika mitandao ya kijamii na pia wapo wanaofanya kampeni zisizo halali nyumba kwa nyumba kuwashawishi watu kufanya uhalifu huo" alisema kamanda.
Tuesday, August 30, 2016
MAANDAMANO YA UKUTA MARUFUKU KUFANYIKA DODOMA.
WALIOJIHUSISHA NA WATUMISHI HEWA MATATANI.
Serikali imeanza kuwashughulikia wale wote waliojihusisha na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa na polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, serikali unatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kuwaondoa wafanyakazi hewa.
Waziri wa nchi, ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora), Angellah Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya Wizara yake katika kipindi cha "tunatekeleza" kinachorushwa na televisheni ya TBC1.
"Kwa sasa wapo watumishi wanahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua za kisheria" alisema.
LEMA AWAGOMEA POLISI.
Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema, amezua tafrani kwenye mahakama ya hakimu mkazi Arusha baada ya askari polisi waliomleta awali kutaka apande gari kwenda mahabusu kwa sababu ya kutokidhi masharti ya dhamana. Awali Lema, alisomewa makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Desdery Kamugisha na Wakili wa serikali Innocent Njau. Katika mashtaka ya kwanza ni la kutuma ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwake kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Mashtaka ya pili kutumia Whatsapp kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wa jiji la Arusha kuandamana Septemba Mosi. Baada ya Lema kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Kamugisha alimuuliza kama ni kweli au la, na Lema alikana baada ya kukana Wakili Njau aliomba Lema asipewe dhamana kwa sababu wana taarifa za kiintelijensia kuwa, endapo atapewa dhamana maisha yake yatakuwa matatani. Hoja ya Wakili huyo wa serikali, ilipingwa na wakili wa utetezi John Mallya. Baada ya mabishano hayo Hakimu Kamugisha alitupilia mbali pingamizi la Wakili Njau la Lema kunyimwa dhamana. Baada ya sharti la dhamana kutolewa, wadhamini wawili walijitokeza ambao ni madiwani wa jiji la Arusha, lakini hali tofauti ilijitokeza baada ya wakili wa serikali Njau kukagua barua ya kumdhamini Lema na kugundua kuna kasoro za matumizi ya majina. Kutokana na sintofahamu hiyo wakili alikubaliana na hoja ya Njau na kusema kuwa Lema atafute wadhamini wengine na kuahirisha kesi hiyo kwa muda hadi Septemba 19 mwaka huu. Baada ya kusomewa kesi hiyo, ikasomwa kesi ya pili ambayo inadaiwa ya kutoa lugha ya uchochezi kati ya Agosti mosi hadi 26 mwaka huu kwa njia ya kurekodi kwa sauti "audio clip" na kurusha kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuhamasisha maandamano Septemba mosi mwaka huu. Saa 8:20 mchana mapolisi walimtoa mahabusu na kumpandisha kwenye gari wakitaka kumpeleka mahabusu Kisongo. Kutokana na sintofahamu hiyo Lema alibishana na polisi hao huku akiwa na Mawakili wake, Mallya na James Lyatuu walihoji kuwa wanampeleka wapi wakati muda wa mahakama haujafika. "Muda wa mahakama haujafika mnanipeleka wapi, nasema nitafia hapa mahakamani muda huu ni saa nane, muda wa mahakama haujaisha mnanipeleka wapi, siendi, mniue, siendi popote mniue hapahapa, muda wa mahakama haujaisha bro, mnanipeleka wapi na kwanini mnanifanyia hivyo, nasema siendi kokote bora kufa, sikubali" alisema Lema.