Rais wa Marekani Barack Obama amemwalika Rais mteule wa Marekani Donald Trump katika White House, huku maandamano ya kupinga ushindi wa Trump yakifanyika miji mingi Marekani.
Rais Obama amesema lengo la mkutano wao litakuwa kujadiliana kuhusu shughuli ya mpito na kupokezana madaraka.
Amesma anataka shughuli hiyo iwe laini na bila matatizo.
Bw Trump wa Republican atakuwa rais wa 45 wa Marekani baada ya kupata ushindi wa kushangaza dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic, chake Rais Obama.
Bw Obama alifanya kampeni kali kumzuia Bw Trump kushinda, na alisema hafai kuongoza. Wakati mmoja alisema hata hafai kuwa mwuzaji dukani.
Lakini rais huyo sasa amewahimiza Wamarekani wote kukubali matokeo ya uchaguzi wa Jumanne.
"Sasa tunatafuta ufanisi wake katika kuunganisha na kuongoza nchi hii," Bw Obama alisema kuhusu Trump.
Licha ya Rais Obama kuhimiza umoja na Bi Clinton kuwaambia wafuasi wake kwamba Bw Trump anafaa kupewa "nafasi ya kuongoza", ushindi wake umezua maandamano katika miji na majimbo kadha Marekani.
Mamia ya waandamanaji wanaompinga Trump walikusanyika nje ya jumba kuu la Bw Trump, Trump Tower eneo la Manhattan jijini New York Jumatano jioni, wakibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe "Not my president" (Si Rais wangu), pamoja na mabango mengine.
Polisi hapo awali waliweka vizuizi vya saruji pamoja na kuchukua hatua nyingine za kiusalama nje ya jumba hilo refu linalopatikana barabara ya 5th Avenue, jumba ambalo huenda likawa makao makuu ya Bw Trump wakati wa kipindi cha mpito kabla yake kuingia White House.
Kuliripotiwa pia taarifa za waandamanaji kuziba lango la kuingia jumba la Trump Tower mjini Chicago Jumatano jioni, wakiimba: "No Trump, No KKK, No Fascists USA" (Hatumtaki Trump, Hatutaki KKK, Hatutaki Wafashi Marekani) na "Not my president!" (Si Rais wangu).
Mjini Oakland, California, na Portland, Oregon, waandamanaji waliteketeza bendera za Marekani.
Wakati wa hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi mapema Jumatano, Bw Trump aliahidi kuponya vidonda vya migawanyiko, baada ya uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, na kuahidi kwamba atakuwa "rais wa Wamarekani wote".
Msemaji wa White House Josh Earnest amesisitiza kwamba Bw Obama atakuwa na uwazi kuhusu kuhakikisha shughuli laini ya mpito atakapokutana na Bw Trump, ingawa aliongeza kwamba: "Sijasema kwamba utakuwa mkutano rahisi."
Rais huyo mteule atasindikizwa kwenda White House Alhamisi na mkewe, Melania, ambaye atakutana na Mke wa Obama, Michelle.
Bw Obama, aliyempongeza mrithi huyo wake kwa njia ya simu mapema Jumatano, alisema si siri kwamba yeye na Bw Trump wana tofauti nyingi.
Lakini aliongeza kwamba wanataka kuhakikisha wanalinda maslahi ya taifa na kwamba alitiwa moyo na yale Bw Trump alikuwa amesema usiku uliotangulia.
Kundi la kushughulikia shughuli ya mpito la Bw Trump litaongozwa na Chris Christie, gavana wa New Jersey, na lina wiki 10 kukamilisha maandalizi hayo.
Rais huyo mteule, ambaye hajawahi kuhudumu katika wadhifa wowote wa kuchaguliwa au kuteuliwa serikalini, amesema kipaumbele chake kitakuwa kufufua na kuimarisha miundo mbinu ya nchi hiyo pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa hilo maradufu.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Republican Reince Priebus alisema: "Donald Trump anachukulia hili kwa uzito sana," na kuongeza kwamba mfanya biashara huyo tajiri atatumia uwezo wake wa kutetea na kufanikisha mikataba ya kibiashara kuhakikisha mambo mema "yanatendeka kwa Wamarekani" haraka iwezekanavyo.
Kama Rais mteule, Bw Trump ana haki ya kupokea taarifa za kila siku za ujasusi sawa na Rais Obama, ambazo ni pamoja na habari kuhusu operesheni za kisiri za Marekani pamoja na habari za kijasusi zinazokusanywa na mawakala 17 wa ujasusi za Marekani.
Bw Trump na kundi lake wanaaminika kuwa tayari kujaza nafasi kuu za usalama wa taifa haraka iwezekanavyo watakapoingia madarakani.
Lakini haijabainika nani atakuwa kwenye baraza lake la mawaziri au atakayejaza nyadhifa kuu wakati wa utawala wake kama vile mkuu wa majeshi.
Kunao wanaotarajiwa kupewa nyadhifa kuu wakiwemo Christie, spika wa zamani wa bunge Newt Gingrich na meya wa zamani wa New York Rudy Giuliani, mmoja wa washauri wakuu wa Bw Trump ambaye wengi wanasema huenda akafanywa mwanasheria mkuu au mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa taifa.
Baada ya kupata hasara kubwa kutokana na ushindi wa kushangaza wa Bw Trump, masoko ya hisa yameanza kuimarika.