Friday, November 11, 2016

MKE WA RAIS MAGUFULI ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI.


Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameruhusiwa na kurejea nyumbani leo (Ijumaa), baada ya afya yake kuimarika.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa imesema kuwa kabla ya kuondoka katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa Mama Janeth Magufuli amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa matibabu mazuri aliyoyapata na pia amewashukuru Watanzania wote kwa kumuombea afya njema.
"Namshukuru sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru madaktari na wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara.
"Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishie kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako nitamalizia matibabu yangu" amesema Mama Janeth.
Mama Janeth alilazwa MNH tangu juzi  baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.

BONGO FLEVA: THAMANI MAPENZI BY RWEGA DA ONE.

Kutoka kwenye miamba iliyopangana ikapangika, sio pengine tunazungumzia Rock City (Mwanza). Yule kijana machachali RWEGA DA ONE aliyeimba Isabela na Nakudeku anakuja tena na video mpya inayokwenda kwa jina la THAMANI MAPENZI.
Video inatoka siku ya Jumapili 13Nov.
Video directed by Blaki Bryan kutoka ROCK GOLD ENTERTAINMENT.



MWANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE ASHINDWA KUFANYA MTIHANI BAADA YA KUPIGWA NA MWALIMU MKUU.

Image result for beaten students
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ridhwaa Seminary iliyopo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Yusuph Kivugo, amemshambulia mwanafunzi wake, Mbaraka Mwalimu, kwa kumpiga ngumi usoni na kumsababishia maumivu makali.
Mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha nne katika shule hiyo iliyopo Kinondoni Mkwajuni, alikutwa na mkasa huo Novemba 3, mwaka huu wakati akijiandaa na mtihani wa Historia.
Kwa mujibu wa ratiba ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne inayoendelea nchini, mtihani huo ulikuwa unafanyika mchana, lakini hata hivyo hakufanya kutokana na maumivu aliyokuwa nayo.
“Tulikuwa msikitini na wenzangu tunasoma, ilikuwa ni saa mbili asubuhi kabla ya mtihani wa Historia kuanza, mwalimu alikuja akauliza kwanini tunapiga kelele na kuanza kutupiga.
“Upande wa pili kulikuwa na wanafunzi wa pre-form one ndio waliokuwa wakipiga kelele, nilishangaa kamkunja mwenzangu anaitwa Mohamed akawa anampiga mangumi, mimi nilijua labda kuna kosa amefanya.
“Katika kujitetea akina Mudy walikimbia, mara akaja kwangu akanishika akaanza kunishambulia, amenipiga ngumi nyingi za usoni, kwenye taya na nyingine jichoni kiasi kwamba sikuweza kufanya mtihani kwani jicho lilivimba sana,” alisema.
Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Omary Ikome, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema jukumu lake ni kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kwamba suala hilo lipo juu ya uwezo wake.
“Nilimkuta Mbaraka analia na jicho la kushoto limevimba, nilimuuliza akasema amepigwa na mkuu. Mimi nasimamia nidhamu kwa wanafunzi, lakini kwa kuwa kitendo hiki kimefanywa na bosi wangu, siwezi kuzungumzia zaidi kwani lipo juu ya uwezo wangu,” alisema.
Mwalimu mkuu huyo alipoulizwa kiini cha tatizo, hakuweza kutoa ushirikiano na kumfukuza mwandishi ofisini kwake.

TB JOSHUA AREJESHA UJUMBE ALIOFUTA FACEBOOK.

index
TB JOSHUA
Utabiri kutoka kwa mhubiri raia wa Nigeria TB Joshua kuwa Hillary Clinton angeshinda urais wa Marekani, umerejeshwa tena baada ujumbe huo kufutwa kutoka mtandao wa Facebook.
Kulingana na barua pepe iliyotumwa kwa BBC na idara ya mitandao ya kanisa la TBJMinistries ilisema kuwa , “ujumbe huo uliondolewa kimakosa na sasa umerejeshwa kwa kuwa hiyo si sera yetu.”
“Siku kumi zilizopita nilimuona rais wa Marekani akishinda kwa kura chache, yule niliyemuona ni mwanamke,” ujumbe huo ulisema.
TB Joshua alikejeliwa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii wakati watu walitambua kuwa ujumbe huo ulikuwa umefutwa, licha ya wafuasi wake wengi katika mitandao ya kijamii bado kumtaja kuwa nabii.

BEYONCE NA JAY Z WAMTAKA MICHELLE OBAMA KUGOMBEA URAIS 2020.

beyonce-jay-z
BEYONCE NA MUMEWE JAY Z.
Baada ya Hillary Clinton kushindwa katika uchaguzi mkuu nchini Marekani dhidi ya Donald Trump, nyota wa muziki nchini humo, Jay Z na mke wake, Beyonce, wamemtaka mke wa Barack Obama, Michelle Obama, awanie kiti hicho 2020.
Wasanii hao walikuwa wanamsapoti Hillary katika uchaguzi huo na walikuwa wanaungana baadhi ya sehemu kwa ajili kumnadi, lakini hajafanikiwa kushinda, hivyo wawili hao wameamua kuangukia kwa mke wa Obama, Michelle, kuwa awanie nafasi hiyo mwaka 2020 wataungana pamoja kwenye kampeni.
Michelle na mume wake, Obama, ni miongoni mwa watu ambao walikuwa wanampigia debe Hillary, lakini hawakufanikiwa.
Novemba 7 mwaka huu, Jay Z aliachia wimbo mpya ambapo ndani yake kuna mistari inasema kuwa anataka mtoto wake akue huku akiwa anaongozwa na rais mwanamke na hivyo walitamani kuona Hillary kupata nafasi hiyo.
“Nilitamani kuona mtoto wangu akiwa anakua chini ya rais mwanamke, Hillary hajapata nafasi hiyo, lakini ninaamini bado kuna nafasi nyingine baada ya miaka minne ijayo, nimekuwa nikiongea na Michelle mara kwa mara na ninaamini atafanya hivyo,” alisema Jay Z.
Wasanii mbalimbali wameonesha kuguswa na uchaguzi huo, huku wengine wakionesha kuwa tofauti na matokeo hayo.
Lady Gaga
Image result for LADY GAGA
LADY GAGA.
Nyota huyo wa muziki nchini Marekani, juzi alionekana mtaani akiwa amevaa T-shirt ambayo inaonesha kumpenda Rais Mteule, Donald Trump.
Msanii huyo alionekana katika mitaa ya jiji la New York akiwa amevaa T-Shirt nyeupe yenye maandishi mekundu ambayo yanasema ‘Nakupenda Trump’.
T.I
Image result for T.I
T.I
Rapa T.I kwa upande wake amempa pole rais ambaye anamaliza muda wake, Barack Obama, kwa mteja wake kushindwa katika uchaguzi huo.
“Pole kwa matokeo ambayo kuna baadhi ya watu hawakuyatarajia, lakini tunafurahi tulikuwa na wewe kwa kipindi chote, lakini sasa tunasubiri kinachofuata,” alisema T.I.
Snoop Dogg
Image result for snoop doggy
SNOOP DOGG.
Rapa huyo ameonekana kumshambulia Hillary kwa kushindwa uchaguzi huo. Snoop amedai kuwa Hillary ameshindwa mbele ya mtu dhaifu.
Hata hivyo, rapa huyo alionekana kutumia maneno makali kwa Hillary na pia amedai kuwa Obama hakuwa na timu nzuri ya kuweza kuwashawishi watu.

TUZO YA SOKA YA BBC KUFANYIKA NOVEMBA 28.

Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka 2016
Wachezaji watano nyota Afrika ambao watapigania tuzo ya BBC inayotolewa kwa Mwanakandanda Bora Afrika wa mwaka watatangazwa Jumamosi na upigaji kura kuanza.
Majina ya wachezaji hao watakaoshindania tuzo ya mwaka 2016 watatangazwa kwenye kipindi cha moja kwa moja BBC World TV na kwenye redio ya BBC World Service kuanzia saa 18:00 GMT.
Mashabiki wa soka ya Afrika kote duniani watapata fursa ya kupiga kura kwenye tovuti ya BBC African football kuanzia saa 18:50.
Upigaji kura utafungwa saa 18:00 Mnamo Jumatatu, 28 Novemba na mshindi atatangazwa moja kwa moja kupitia runinga ya Focus on Africa TV na pia kwenye redio Jumatatu 12 Desemba saa 17:35.
Wachezaji nyota wa zamani Afrika pamoja na wataalamu wa soka watahudhuria kipindi hicho maalum siku ya Jumamosi.
Wanaotumia mitandao ya kijamii wanaweza kufuatilia matukio kupitia kitambulisha mada #BBCAFOTY.
Mshindi wa mwaka jana alikuwa Yaya Toure.

Washindi wa zamani wa Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka:

2015: Yaya Toure (Manchester City & Ivory Coast
2014: Yacine Brahimi (Porto & Algeria)
2013: Yaya Toure (Manchester City & Ivory Coast)
2012: Chris Katongo (Henan Construction & Zambia)
2011: Andre Ayew (Marseille & Ghana)
2010: Asamoah Gyan (Sunderland & Ghana)
2009: Didier Drogba (Chelsea & Ivory Coast)
2008: Mohamed Aboutrika (Al Ahly & Egypt)
2007: Emmanuel Adebayor (Arsenal & Togo)
2006: Michael Essien (Chelsea & Ghana)
2005: Mohamed Barakat (Al Ahly & Egypt)
2004: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2003: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2002: El Hadji Diouf (Liverpool & Senegal)
2001: Sammy Kuffour (Bayern Munich & Ghana)
2000: Patrick Mboma (Parma & Cameroon)

BAADA YA SAKATA LA SCORPION, SASA NI RAMBO MKATA MAPANGA AWA TISHIO.


Wakazi wa kata ya Kipawa jijini Dar es Salaam wameingiwa na hofu baada ya kuibuka kijana anayejiita ‘Rambo mkata mapanga’ anayedaiwa kufanya uhalifu kwa kujeruhi watu kwa kuwakata mapanga kisha kuwapora fedha na mali zao.
Kijana huyo ambaye jina lake halisi ni Abdul Chata ameibuka ikiwa ni wiki kadhaa zimepita tangu kuibuka kwa sakata la ‘Scorpion’ aliyeshtakiwa kwa tuhuma za uporaji na kujeruhi ikiwamo kutoboa macho.
Miongoni mwa watu waliovamiwa, kukatwa mapanga na kuporwa na anayedaiwa kuwa Rambo mkata mapanga ni walimu watatu wa Shule ya Msingi Mogo, iliyopo kata ya Kipawa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo hilo walisema tangu kuibuka kwa mkata mapanga wiki mbili zilizopita, hali ya amani ya eneo hilo imekuwa mbaya kiasi cha kushindwa kutembea usiku kuanzia saa moja.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Karakata, Kata ya Kipawa Andrew Olutu alisema hadi sasa ofisi yake imethibitisha zaidi ya matukio manne ya watu kuporwa kisha kujeruhiwa kwa mapanga.
“Ni mtu hatari na amewapa hofu kubwa wananchi kwa sababu hawezi kupora kitu chochote bila kukukata mapanga, tumekumbwa na taharuki,” alisema Olutu.
Alisema kijana huyo hutembea na mapanga mawili ambayo huyaficha mgongoni na kwamba huwa haijalishi muda gani anaweza kufanya tukio japo, matukio mengi yamefanyika usiku.
Akisimulia zaidi, mwenyekiti huyo alisema tukio jingine lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 3, ambapo kijana huyo aliteka bodaboda kisha kumjeruhi dereva kwa panga usoni akimlazimisha ampakie na kumpeleka eneo analotaka. “Inavyoonekana kulikuwa na mvutano baina ya Rambo na dereva wa bodaboda, kwa sababu tulikuwa tunalinda sungusungu tukasikia kelele na kwenda haraka na kumkuta bodaboda akivuja damu. Alikuwa amecharangwa mapanga usoni,” alisema.
Hata hivyo, alisema hawakufanikiwa kumkamata ‘Rambo’ ambaye alikimbia baada ya kuona sungusungu lakini walitoa taarifa za tukio hilo polisi na kumpeleka majeruhi hospitali.
Olutu alisema kutokana na hali kuwa mbaya zaidi, wamelazimika kuunda vikosi vya sungusungu viwili vikiongozwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa ili kuwanusuru watu wanaovamiwa.
Baadhi ya wananchi walisema kutokana na hali hiyo wanalazimika kurejea majumbani mapema ili kukwepa mapanga ya Rambo anayeonekana kuwa tishio.
Mkazi wa Mtaa wa Mkarakata, Sam Aidan alisema alinusurika kucharangwa mapanga ya ‘Rambo’ mwishoni mwa wiki iliyopita na kilichomuokoa siku hiyo ni gari lililotokea mbele yao.
“Ilikuwa saa mbili maeneo ya mji mpya nikakutana na ‘Rambo’, nashukuru Mungu muda huo huo lilitokezea gari akakimbia na kuniacha salama. Tangu hapo ni bora nilale huko huko au nikodi teksi ili nirejee nyumbani, kama nikiona giza limeingia,” alisema.
Aliliomba jeshi la Polisi lisaidie kumkamata mhalifu huyo ili wapate amani.
Diwani wa Kata ya Kipawa, Kennedy Simon alisema kijana huyo alianza kufanya matukio ya uhalifu mwaka jana akiwajeruhi wananchi na kuwapora mali zao.
Alidai hali hiyo iliwafanya kumvizia siku moja na kumkamata kisha kumpiga kabla hajaokolewa na polisi.
Simon alisema alifikishwa kituoni, kisha mahakamani ambako alihukumiwa kifungo jela.
“Wiki mbili zilizopita tumeshangaa amerejea mtaani kwa kasi kubwa, safari hii anaitwa ‘Rambo mkata mapanga’ na ukikutana naye, ni bora ujaliwe kutimua mbio kwa sababu hawezi kukuibia bila kukuachia alama ya panga,” alisema.
Alisema taarifa za matukio hayo zimeripotiwa polisi na wanaendelea kumtafuta japo hadi sasa hajakamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alithibitisha kuwapo kwa kijana huyo anayejiita ‘Rambo mkata mapanga’ na kusema tukio linalofahamika hadi sasa ni lile la uvamizi wa shule.
Aliwataka wananchi kusaidia kutoa taarifa za eneo analopatikana mtuhumiwa huyo ili wamkamate.
“Taarifa za ‘Rambo mkata mapanga’ ninazo, tumeshaweka mitego mbalimbali ili kumkamata na niwasihi wananchi wakimuona tu watoe taarifa ili adhibitiwe,” alisema.
Tukio shuleni
Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mobo, jijini Dar es Salaam walisema wanasoma kwa hofu tangu walimu wao walipovamiwa, kuporwa na kuibiwa.
“Alikuja kama saa 10:00 jioni, akaenda moja kwa moja kwenye eneo walikokuwa walimu akawaumiza na kuwapokonya vitu vyao zikiwamo simu, tunaogopa kwa sababu anaweza kuja tena,” alisema.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Magreth Fredrick alithibitisha kutokea kwa tukio la kujeruhiwa walimu watatu na kwamba taarifa zaidi zimefikishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

TAMTHILIA YA JUMBA LA DHAHABU KURUDI TENA TBC1.

Image result for TBC1
Mkurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Ayub Rioba amesema anatarajia kuanza kurudia kuonesha tena tamthiliya ya Jumba la Dhahabu iliyopata umaarufu mkubwa chini ya Kundi la Fukuto Arts.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa TBC maeneo ya Mikocheni, alisema wameamua kuirudisha tena tamthiliya hiyo kutokana na maombi ya watazamaji wengi.
Alisema mchezo huo ambao unatarajiwa kuanza kuoneshwa wiki ijayo, ambao utakuwa ukioneshwa mara tano kwa wiki ili kuwapa nafasi watazamaji ambao kipindi cha nyuma hawakubahatika kuuona.
Rioba pia alizindua muswada mpya wa tamthiliya ya Ukurasa Uliofungwa ‘Closed Chapter’ ambayo, inatarajiwa kuoneshwa katika kituo hicho baada ya kufanyika usaili.
Kiongozi na mtunzi wa filamu ya Jumba la Dhahabu na Kurasa Uliofungwa ‘Closed Chapter’, Tuesday Kiangala, alisema amekubali kuirudisha tamthiliya hiyo kwakuwa alikuwa akiulizwa maswali mengi juu ya tamthiliya hiyo.
“Jumba la Dhahabu inarudi na sasa mashabiki watapata muda mwingi wa kuiangalia, kwa wale ambao waliitazama na ambao hawakupata nafasi ya kuitazama,” alisema.
Katika tamthiliya ya Jumba la Dhahabu kuna waigizaji waliofanya vizuri kama, Mzee Chilo, Joan, Badboy, Tuesday Kiangala, Capto Rado, Niva na wengine.

RAIS MAGUFULI ATOKWA NA MACHOZI WAKATI ANAAGA MWILI WA MUNGAI.

Rais John Magufuli akiwaongoza viongozi mbalimbali na wananchi wa Dar es Salaam kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Marehemu Joseph Mungai katika shughuli ya kumuaga iliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini jana. (Picha na Fadhili Akida).
RAIS MAGUFULI AKIONGOZA MAMIA YA WATU KUMUAGA MUNGAI.
Rais John Magufuli amebubujikwa na machozi hadharani wakati akiongoza mamia ya waombolezaji jijini Dar es Salaam, kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri katika awamu nne za uongozi wa nchi na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, aliyefariki ghafla Novemba 8, mwaka huu.
Mbali na Dk Magufuli, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mke wa Rais mstaafu Mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva, mawaziri na viongozi wengine mbalimbali walitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mungai, katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana.
Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Mungai ulipelekwa nyumbani kwake Osterbay kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kwa maziko, yatakayofanyika kesho.
Kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga, alimwelezea Mungai kuwa alikuwa na kipaji cha tofauti cha uongozi tangu akiwa mdogo.
“Uongozi pekee ni tunu. Mungai alikuwa na sifa ya uongozi. Lakini kipindi cha uongozi ni jinsi unavyotafsiri uongozi wako kwa wale unaowaongoza. Alitumia kipaji chake cha uongozi kwa jamii,” alisema Balozi Mahiga na kubainisha kuwa baba mzazi wa marehemu alitokea Kenya na mama yake mzazi alitoka katika ukoo wa Chifu Mkwawa.
Naye mtoto wa marehemu, Jim Mungai, alisema baba yake alikuwa Mbunge kwa miaka 35 katika Jimbo la Mufindi na baadaye baada ya kugawanywa Mufindi Kaskazini.
Alisema katika miaka yake hiyo kwa awamu nne alikuwa Waziri wa Kilimo, Elimu, Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM. Alisema ameacha mke na watoto saba.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Sumaye alimwelezea Mungai na kusema kuwa katika kipindi chake cha uwaziri, alikuwa waziri wa elimu mchapakazi, mwadilifu na kwamba aliongoza wizara hiyo vizuri hadi viwango vya elimu viliongezeka.
“Tumempoteza mtu muhimu sana katika nchi,” alisema Sumaye.
Aliyekuwa Waziri katika Awamu ya Nne, Steven Wassira alisema alifanya kazi na Mungai katika wizara moja ya kilimo, akiwa Naibu Waziri wake wa Kilimo.
Aliongeza kuwa Mungai alipenda kuona mabadiliko ya kilimo katika sekta zote ndio maana karibu awamu zote nne aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru alimwelezea Mungai kuwa alikuwa mtu aliyekuwa na kichwa kizuri katika utendaji kwa kuwa katika nafasi zote alizopewa alikuwa mchapakazi.
“Alikuwa akitoa mchango bungeni alioufanyia utafiti wa kina na unakuwa ni wa kujenga,” alisema. Serikali imemteua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuiwakilisha kwenye maziko yatakayofanyika kesho.

WAHITIMU WA KIDATO CHA SITA MWAKA HUU KURIPOTI JKT DESEMBA MOSI.

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA, DK. HUSSEIN MWINYI.
Serikali amewaagiza wote waliohitimu kidato cha sita Mei mwaka huu na ambao hawajajiunga na vyuo vya elimu ya juu, wakaripoti katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Desemba Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ametoa agizo hilo mjini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari wa Bunge.
Dk Mwinyi alisema Mei na Juni mwaka huu, JKT iliwafanyia usaili vijana wa kujiunga na JKT kwa kujitolea. Alisema usaili huo ulifanyika kwa kushirikiana na kamati za ulinzi za wilaya na mikoa.
"Wizara ya Ulinzi na JKT inapenda kuwatangazia vijana wote waliosailiwa Juni mwaka huu, kujiunga na JKT kwa kujitolea, waripoti kwenye kambi walizopangiwa ifikapo Desemba Mosi mwaka huu kwa nauli zao," amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema mafunzo hayo ni ya miezi mitatu kwa mafunzo yenye utaratibu wa kawaida na miaka miwili kwa wa kujitolea.
Ili kufanikisha hilo, Wizara ilimuagiza Mkuu wa JKT kufufua kambi ya Makuyuni JKT iwe miongoni mwa kambi kuanzia Desemba mwaka huu.
Aliagiza kambi za Luwa na Milundikwa za mkoani Rukwa, zirejeshwe kwa shughuli za JKT za kilimo na ufugaji.
Dk Mwinyi alimuagiza Mkuu huyo wa JKT pia kambi ya Mpwapwa irejeshwe kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kilimo na ufugaji ndani ya JKT.
Juni mwaka huu, vijana 14,000 waliohitimu kidato cha sita mwaka huu, walijiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Vijana hao walimaliza mkataba wa miezi mitatu mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu.

MWILI WA ALIYEKUWA SPIKA WA BUNGE SITTA LEO UTAAGWA BUNGENI DODOMA

Maofisa wa Polisi wakiwa wamebeba jeneza lililohifadhi mwili wa aliyekuwa Spika wa zamani wa Bunge na Waziri katika serikali zilizopita, Samuel Sitta baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyrerere jijini Dar res Salaam jana, ukitokea nchini Ujerumani. (Picha na Mroki Mroki).
Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta (73) leo ataagwa ndani ya Bunge la Tanzania mjini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa maziko, ikiwa ni historia kwa kiongozi kuagwa ndani ya Bunge hilo.
Jana, Bunge lililazimika kutengua kanuni kuwezesha kumpa heshima za kipekee Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 ambaye leo mwili wake utaingizwa ndani ya Ukumbi wa Bunge kuagwa kwa heshima na wabunge ambao baadhi yao alikuwa nao katika Bunge hilo la Tanzania.
Sitta aliyewahi kuwa pia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu katika Hospitali ya Technical University ya mjini Munich, Ujerumani ambako alikuwa amelazwa akitibiwa saratani ya tezi dume. Alizaliwa Desemba 18, 1942 mjini Urambo.
Mwili wa Sitta uliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jana saa tisa alasiri ukitokea nchini Ujerumani ambako alienda kwa matibabu. Ulipokewa na baadhi ya viongozi wa serikali, viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa pamoja wananchi waliofika uwanjani hapo.
Kwa hatua hiyo ya kutengua kanuni, Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 utakuwa umetengua kanuni zake kwa mara ya pili; awali kanuni zilitenguliwa juzi Jumanne ili kusitisha shughuli za Bunge baada ya kifo cha Sitta kutangazwa.
Spika wa Bunge, Job Ndugai jana kwa mujibu wa utaratibu na kanuni za Bunge, alimuomba Waziri, Ofisi ya Rais, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kutengua kanuni ili kuruhusu shughuli za kumuaga Sitta zifanyike ndani ya Ukumbi wa Bunge kwa heshima ya kiongozi huyo.
“Nitaomba Waziri wa Nchi asimame ili kutengua baadhi ya kanuni ili haya yawezekane,” alisema Ndugai baada ya kuwaeleza wabunge kitakachofanyika leo. Jenista alisimama na kabla ya kutengua kanuni alisema hatua hiyo inafanyika ili kuruhusu shughuli za leo zifanyike kwa matakwa ya kikanuni. “Kwa kuwa Bunge limepata msiba na kwa kuwa Bunge limepanga kumuenzi na kumuaga katika ukumbi wa Bunge, kuna kanuni zitapaswa kutenguliwa,” alisema Jenista.
Kanuni zilizotenguliwa ni ya 139 (1) inayohusu wageni wanaoingia Ukumbi wa Bunge kwamba wataketi maeneo maalumu ya wageni na si katika ukumbi wenyewe na kanuni ya 143 (e)-(f) kuhusu mpangilio wa Bunge wa kukaa, uliowekwa kwa namna ya baadhi ya watu.
“Kanuni hizo zitenguliwe ili kuruhusu ndugu wa karibu wasiozidi 12 waingie kushiriki tukio hilo na kuhusu kanuni ya 143 mpangilio wa ukaaji bungeni utenguliwe ili jeneza liingizwe ndani ya ukumbi na kuwekwa sehemu iliyoandaliwa mbele,” alitoa hoja na wabunge wote kuiunga mkono.
Ndugai alimwelezea Sitta ambaye akiongoza Bunge alijipambanua kwa falsafa yake ya Kasi na Viwango, aliyeanzisha matangazo ya mubashara (live) katika Bunge la 10 na kuwaeleza wabunge kuwa, leo shughuli ya kumuaga itakuwa mubashara.
Akielezea utaratibu wa leo, Ndugai alisema wataupokea mwili wa Sitta saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
“Kutakuwa na kikao maalumu cha Bunge saa 8:30 mchana tuwe tumekaa kwa kikao hicho maalumu cha Bunge ambacho hakijawahi kutokea,” alisema Spika Ndugai na kuongeza kuwa wabunge watapata nafasi ya kutoa salamu za rambirambi na heshima za mwisho ingawa jeneza halitafunuliwa.
Alisema baada ya shughuli hizo bungeni, mwili utasafirishwa kwenda Urambo kwa maziko na wabunge 10 akiwemo Spika watakwenda katika maziko na wataondoka Jumamosi. Alisema Tume ya Huduma za Bunge itateua wabunge kwa uwakilishi wa vyama.
“Tunampa heshima za kipekee sana mzee wetu, tutaupokea mwili na tutauingiza ndani ya ukumbi hapo mbele ya kiti, baada ya hapo kutakuwa na ratiba. Baadhi watatoa maneno mafupi kwa uwiano kama ilivyo kawaida ya Bunge letu. Tutaongozwa na Waziri Mkuu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,” alisema.
Akielezea zaidi alisema baada ya hapo wabunge watatoka nje ya lango kuu, watakakokaa kwa muda mfupi.
“Tutabeba jeneza kwa kushirikiana. Tumepewa saa mbili tu. Tutafanya kumpa heshima kubwa Mzee Sitta. Viongozi wetu wa kitaifa watapewa heshima zote hizo kwa kuletwa bungeni ambako ndiko nyumba ya Watanzania wote ilipo,” alisema Ndugai.
Alisema kabla ya kutoka nje, Waziri Mkuu atatoa hotuba ya kuahirisha Bunge, lakini Spika hatawahoji wabunge mpaka shughuli ya kumuaga Sitta iishe na wakiutoa mwili nje na kumaliza, ndipo atawahoji.
“Tunataka hii shughuli iingie kwenye shughuli za Bunge,” alisema Ndugai.
Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana amewaongoza baadhi ya wakazi wa jiji hilo kupokea mwili wa Sitta na kueleza kuwa taifa limempoteza mshauri muhimu. Samia alisema Sitta alikuwa kiongozi mahiri ambaye alikuwa haamini kwenye kushindwa.
Makamu huyo wa Rais ambaye alifanya kazi na Sitta kwenye Bunge Maalumu la Katiba, alisema Bunge hilo lilikuwa na changamoto nyingi, lakini siku zote Sitta alimtia moyo kwamba hawatashindwa.
“Taifa tumempoteza mshauri, ni mtu ambaye hakuamini kushindwa, kwake yeye nilijifunza uvumilivu na kusimamia mambo kwa kiwango cha juu,” alisema Samia na kuongeza kuwa kuwa Sitta alikuwa kaka kwake, mshauri na kwamba hakuchoka kutoa ushauri katika mambo ambayo yeye aliona hayana ufumbuzi. “
Aliniamini akiwa ananiachia niongoze Bunge nyakati za jioni na yeye akawa anampumzika nyumbani kwake, kulipotokea changamoto nilipoenda kumweleza, kwa ushauri wake nilijikuta naona kwamba jambo hilo sio changamoto tena,” alisema Samia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta akiwa Mwenyekiti.
Mwili wa marehemu uliwasili uwanjani hapo huku ukiwa unasindikizwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Philip Marmo pamoja na mke wa marehemu, Margaret Sitta.
Baadhi ya viongozi waliofika uwanja wa ndege kupokea mwili huo pamoja na Samia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika mstaafu Pius Msekwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Shughuli ya kupokea mwili wa Sitta ilifanyika katika uwanja wa ndege wa zamani ambako ulibebwa kwa gari la Jeshi na baadaye askari wa Polisi walibeba jeneza lake na kulipitisha mbele ya Makamu wa Rais kama ishara ya kupokewa kwa mwili huo kwa taratibu zote za serikali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, jana mwili huo ulipelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam na leo asubuhi utapelekwa Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuwapa nafasi wananchi na viongozi wa serikali kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa 1.30 asubuhi.
Mchana utapelekwa JNIA kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea mkoani Dodoma na utawasili mkoani humo saa 8 mchana. Utapelekwa katika Viwanja vya Bunge ambapo salamu mbalimbali zitatolewa na Spika, Waziri Mkuu, Kambi Rasmi ya Upinzani na viongozi wa Mkoa wa Dodoma. Kisha wabunge watatoa heshima za mwisho.
Jioni mwili wa Sitta utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa ajili ya maziko. Utawasili Uwanja wa Ndege wa Tabora saa 10 jioni na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Urambo ambako utawasili saa 12 jioni.
Waombolezaji wilayani Urambo na maeneo mengine watatoa heshima za mwisho kesho kuanzia asubuhi na maziko yanatarajia kufanyika saa tisa alasiri kuhitimisha miaka 73 na ushee ya maisha ya mmoja wa wanasiasa waadilifu na wazalendo nchini Tanzania aliyeifanyia mengi mema ya kukumbukwa.

NUH MZIWANDA AFUNGA NDOA TAZAMA PICHA.


s14
s13
Mwanamziki wa bongo flava anayesumbua na wimbo wa JIKE SHUPA, Nuh Mziwanda hatimaye amefunga pingu za maisha na mpenzi wake Nawal baada ya kuachana na Shilole.