Friday, October 28, 2016

SUMAYE APEWA NOTISI YA SIKU 90 KUENDELEZA MASHAMBA.

Serikali imemtaka Frederick Sumaye kuendeleza mashamba yake mawili ndani ya siku 90, la sivyo itafuta hati ya umiliki wake, lakini waziri mkuu huyo mstaafu amesema notisi hiyo ni matokeo ya chuki ya Serikali dhidi yake baada ya kuhama CCM na kujiunga Chadema.

Sumaye, ambaye alikuwa mmoja wa wasemaji tegemeo kwenye mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anamiliki shamba lililoko mkoani Morogoro na jingine lililoko Mabwepande jijini Dar es Salaam, ambalo limevamiwa na wananchi.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alisema hati ya shamba la Sumaye iko katika hatua ya kufutwa na kwamba Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni, Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi.


MAOFISA 10 WA POLISI MBARONI.

Moshi. Jeshi la Polisi limetikiswa baada ya maofisa wake 10 kutiwa mbaroni wilayani Siha mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kuwaachia watuhumiwa wa shehena ya bangi.

Tukio hilo ambalo limekuwa gumzo, lilitokea Jumanne iliyopita kwenye Kijiji cha Olmolok baada ya maofisa hao kudaiwa kukamata magunia manane yaliyosheheni bangi yakisafirishwa kwenda nchini Kenya.

Ofisa Mnadhimu wa jeshi hilo Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.


MUUGUZI KIZIMBANI KWA KUIBA MTOTO WA SIKU NNE.

MUUGUZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Scolastica Leoni (43) ambaye ni mkazi wa kata ya Sanawari amepandishwa kizimbani kujibu shitaka moja la kuiba mtoto mchanga wa kiume wa siku nne.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda, ilidaiwa mshtakiwa alifanya kosa hilo Aprili 15, mwaka huu majira ya usiku wa manane akiwa kazini.

Mwendesha Mashitaka alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa kazini katika Hospitali ya Mount Meru wakati akifahamu wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria na ni kinyume cha sheria na kanuni na taratibu za kazi. Alidai muuguzi huyo akiwa mtumishi wa umma katika hospitali hiyo aliiba mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu 169 kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.

Mshtakiwa alikana shitaka na hakimu alisema dhamana ni haki ya mtu kwa mujibu wa sheria hivyo anatakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili wenye mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20.


NDEGE YA MGOMBEA MWENZA WA TRUMP YAPATA AJALI.



Mgombea mwenza wa chama cha Republican katika kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani Mike Pence amenusurika baada ya ndege iliyombeba kuteleza uwanja wa ndege.

Ndege hiyo iliteleza na kuvuka barabara inayotumiwa na ndege kupaa na kutua katika uwanja wa LaGuardia jijini New York.

Gavana huyo wa Indiana amewaambia wanahabari kwamba yuko salama baada ya kisa hicho.

Hakuna aliyejeruhiwa.

Bw Pence na abiria wengine takriban 30 waliokolewa kupitia mlango wa dharura wa ndege upande wa nyuma.

Alikuwa anatoka mkutano wa kampeni Fort Dodge, Iowa.

Uwanja wa ndege wa LaGuardia kwa muda usiojulikana, maafisa wamesema.

Rubani anadaiwa kukanyaga breki na abiria wanasema walinusa harufu ya raba ikiungua.

Kanda za video za runinga zimemuonesha Bw Pence baadaye akiwa amesimama kwenye mvua karbu na magari ya huduma za dharura, akizungumza na baadhi ya maafisa.

Baadaye aliandika kwenye Twitter: "Nashukuru sana kwamba kila mtu aliyekuwa kwenye ndege yetu yuko salama. Nashukuru maafisa wa dharura na wote waliotuombea. Tutarejea kwenye kampeni kesho!"

Amesema matope yaliruka na kujaa kwenye kioo cha sehemu ya mbele ya ndege.

Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump alimpigia simu Bw Pence kumjulia hali baada ya kisa hicho, maafisa wa kampeni wamesema.

Msemaji wa Trumo Stephanie Grisham alisema mgombea huyo alikuwa kwenye msafara wa kampeni akielekea Geneva, Ohio.

Bw Trump alizungumzia ajali hiyo kwenye mkutano wake wa kampeni baadaye akisema: "Mnajua, kulitokea ajali kubwa ya ndege.

"Ndege imeteleza kutoka barabara uwanja wa ndege na ilikaribia sana kuwa mbaya, kuwa mbaya sana, nimezungumza na Mike sasa hivi na yuko salama. Alitoka. Kila mtu yuko salama

Bw Pence aliahirisha hafla ya kuchangisha pesa ambayo ilifaa kuandaliwa katika jumba la Trump Tower eneo la Manhattan, na akaelekea moja kwa moja hadi hotelini.

Haijakuwa wiki njema kwa gavana huyo wa Indiana.

Jumatano, alitangaza kwenye Twitter kwamba mbwa wake kwa jina Maverick, alikuwa amefariki akiwa na miaka 13.


MOYES ASHITAKIWA NA FA.

Meneja wa klabu ya Sunderland ya Uingereza David Moyes ameshtakiwa na chama cha soka cha Uingereza kwa utovu wa nidhamu wakati wa mechi dhidi ya Southampton Jumatano.

Southampton walishinda mechi hiyo ya Kombe EFL Cup uwanjani St Mary's kupitia bao la Sofiane Boufal

Chama cha Soka cha Uingereza (FA) kimesema inadaiwa "Moyes alitumia lugha ya kutusi au maneno ya kuudhi akiyaelekeza kwa mwamuzi wa mechi."

Kisa hicho kilitokea dakika ya 90 refa Chris Kavanagh alipokataa kuwapa Sunderland penalti baada ya mshambuliaji wa Sunderland Victor Anichebe kuonekana kuchezewa visivyo eneo la hatari.

Sunderland walilazwa 1-0.

Moyes, aliyeteuliwa meneja wa Paka Weusi Julai, ameshinda alama mbili pekee kutoka kwa mechi tisa ligini.

Amepewa hadi saa tisa alasiri saa za Afrika Mashariki Jumanne kujibu tuhuma hizo.