Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameitaja Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa ndio inayoongoza kwa vitendo vya rushwa kisekta nchini, kutokana na kuwa na majalada mengi ya kesi za rushwa zinazoendelea mahakamani.
Aidha, amebainisha kuwa Mahakama ya Ufisadi iko mbioni kuanza kazi, baada ya Jaji Mkuu kukamilisha kutengeneza kanuni za uendeshaji pamoja na mafunzo kwa majaji.
Akizungumza katika kikao kati ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali ya Mtaa mjini Dodoma jana, Kairuki alisema kwa mujibu wa mchanganuo wa kesi zilizopo mahakamani kisekta kuanzia Juni mwaka huu, zinaonesha mamlaka hiyo na sekta ya afya ndio zinaongoza kwa kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
Alisema mchanganuo huo unaonesha kuwa hadi Juni mwaka huu, kesi zilizopo mahakamani za kisekta ni 509 na kati ya hizo kesi 209 sawa na asilimia 41 zinaihusu Serikali za Mitaa na kufuatiwa na sekta ya afya ambayo ina kesi 63 sawa na asilimia 12.
“Sekta hii pia kwa mwaka 2015/16 imeonekana kuongoza kwa kuwa na majalada mengi yanayohusu tuhuma za rushwa. Kati ya majalada 3,082 yanayoendelea na uchunguzi, majalada 1,357 sawa na asilimia 44 yanahusu mamlaka hii,” alisisitiza.
Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuzuia na kupambana na rushwa katika eneo hilo hilo la mamlaka ya serikali za mitaa kutokana na kuongoza kwa kuwa na tuhuma na kesi nyingi za rushwa zinazoendelea mahakamani.
Kuhusu hatua za kuanzishwa kwa Mahakama ya Ufisadi zilipofikia, Kairuki alisema mahakama hiyo ipo mbioni kuanza kazi na mashauri yake yatachukua muda wa miezi tisa kusikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Jaji Mkuu ameshamaliza kuandaa kanuni na majaji wameshapewa mafunzo na maelekezo kwamba ndani ya miezi tisa shauri ziwe zimekamilika,” alisema.
Kuhusu utendaji wa taasisi ya Takukuru, waziri huyo alisema kwa kipindi cha mwaka 2015/16 kesi mpya 424 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini ikiwa ni ongezeko la kesi 110 ikilinganishwa na mwaka 2014/15.
Pia alifafanua kuwa kati ya kesi hizo, kesi 177 zilihusu kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 na kesi 247 zilihusu vifungu vingine, ambavyo mashitaka dhidi ya watuhumiwa mahakamani yanahitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma na katika kesi hizo kesi kubwa zilizokuwa 15. Pia alisema Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh 43.78 ikiwa ni ongezeko la Sh 36.78 bilioni ziliozookolewa mwaka 2014/15.
Alisema fedha hizo zilitokana na kitendo cha taasisi hiyo kuanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa fedha na mali za watuhumiwa zilizopatikana kwa njia ya rushwa kwa kutaifishwa kwa mali za watuhumiwa.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati hiyo walibainisha kuwa adhabu inayotolewa kwa watu wanaotiwa hatiani kwa vitendo vya rushwa haiendani na kosa wanalolitenda.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza aliishauri serikali kuchukua hatua za kudhibiti tatizo la rushwa kwa kuwaboreshea maslahi watendaji wadogo ili kuondokana na rushwa ndogondogo.
Alisema serikali inatakiwa iweke mikakati ya kudhibiti rushwa kuanzia ngazi za chini ikiwemo kuingiza somo la rushwa katika mitaala ya shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Takukuru, Alex Mfungo alifafanua kuwa upelelezi wa kesi za rushwa, umekuwa ukichelewa kwa sababu wanataka kujiridhisha kwanza kabla ya kupeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).