Mwanamume mmoja amekiri kujaribu kuingia ndani ya nyumba ya Wayne Rooney wakati mchezaji soka huyo alipokuwa katika mechi uwanjani Old Trafford.
Mwanajeshi wa zamani, Robert McNamara, mwenye umri wa miaka 24, kutoka Scarborough, amekiri makosa katika mahakama ya Chester Crown kwa kujaribu kuingia katika nyumba hiyo pasi idhini akiwa na nia ya kuiba.
Mnamo Agosti 3 King'ora kililia katika nyumba hiyo yenye thamani ya pauni milioni 6 huko Prestbury, Cheshire.
McNamara atahukumiwa Desemba 21.
Jaji Nicholas Woodward amesema kulikuwa na mambo ya kutia wasiwasi katika kesi hiyo na kuagiza kitengo cha dhamana mahakamani kukusanya ripoti ya kabla hukumu kutolewa.
Rooney, mkewe Coleen, na watoto wao watatu, Kai, Klay na Kit, walikuwa wamehudhuria mechi ya kuchangisha fedha za misaada dhidi ya timu alioichezea kwanza Rooney, Everton, wakati jaribio hilo la wizi lilipotokea.
McNamara alikamtwa siku sita baadaye.
Upande wa mashtaka haukueleza upande wake wa kesi hiyo lakini mahakama ilielezewa kuwa hivi karibuni McNamara amegunduliwa kuugua matatizo ya akili na kuwa familia yake ilitafuta usaidizi kutoka taasisi inayotoa huduma ya afya kwa magonjwa ya akili, mapema mwaka huu.
Thursday, October 27, 2016
JAMAA AKIRI KUTAKA KUIBA KWENYE NYUMBA YA MWANASOKA ROONEY.
HAKIMU AMWAMBIA MWIZI AMUIGE 50 CENT.
Hakimu mmoja nchini Australia amemtaka kijana mmoja kumuiga mwanamuziki 50 Cent ili kuepuka maisha ya uhalifu.
Hakimu Deen Potter alitoa matamshi hayo wakati alipokuwa akimhukumu kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 kutokana na shtaka la wizi.
''Kama wewe alikuja hapa kutokana na hali ya kutisha na yenye kiwewe'',alisema hakimu,''lakini sasa ameweza kuepuka''.
Nyota huyo wa mziki wa Hip Hop kwa jina Curtis Jackson anayezingirwa na utata aliipata umaarufu baada ya kuwa katika maisha ya uhalifu ,dawa za kulevya na ghasia.
Kijana huyo alikuwa anakabiliwa na mashataka 49 baada ya kuiba mali yenmye zaidi ya thamnai ya dola 7,000.
''Katika kipindi cha miaka 10 ijayo nataka kukuangalia na kuona mafanikio yako''.
WATAHINIWA 238 WAFUTIWA MATOKEO YA DARASA LA SABA.
UFAULU mtihani wa Darasa la Saba umeongezeka kwa asilimia 2.52 kutoka asilimia 67.84 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.36 mwaka 2016.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Dk Charles Msonde ameyasema hayo leo wakati anatangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa Darasa la Saba mwaka 2016.
Amesema, watahiniwa 555,291 kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo mwaka huu wamefaulu na watajiunga na kidato cha kwanza 2017.
"Idadi hii ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36, kati ya hao wasichana ni 283,751 na wavulana 271540. Mwaka 2015 watahiniwa waliofaulu ulikuwa ni asilimia 67.84 kuwa kuwapo ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.52,” amesema Dk Msonde.
Amesema, watahiniwa 16,929 wamepata daraja A, 141,616 wamepata daraja B, watahiniwa 396,746 wamepata daraja C, watahiniwa 212,072 wakipata daraja D na 21,872 wakipata daraja E .
Kwa mujibu wa Msonde, watahiniwa 238 wamefutiwa matokeo ya mtihani huo kutokana na udanganyifu.
Amesema shule 6, waalimu, wamiliki wa shule na wasimamizi wa mitihani wamebainika kufanya udanganyifu na kuwafanyia mtihani wanafunzi.
GALAXY NOTE 7 YAATHIRI FAIDA YA KAMPUNI YA SAMSUNG.
Faida ya Kampuni ya teknolojia kutoka Korea Kusini Samsung imepungua baada ya kurudishwa kwa simu aina ya Galaxy Note 7.
Faida ya operesheni kati ya mwezi Julai na Septemba ilishuka kwa asilimia 30 na kufikia dola bilioni 4.6,ikiwa ni kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka miwili.
Kampuni hiyo kubwa ya utengenezaji simu ilisitisha utengenezaji wake wa simu aina ya Note 7 baada ya ripoti kwamba zilikuwa zinashika moto.
Baada ya kutaka simu aina ya Galaxy Note 7 iliokuwa ikishindana na iPhone kurudishwa,hatua hiyo imeonekana kuwa pigo kwa sifa ya kampuni hiyo kwa ubora na utegemezi.
Samsung imesema kuwa kitengo chake cha simu sasa kitalenga kuimarisha mauzo ya biadhaa zake mpya mbali na kurudisha imani ya wateja wake.
Hatahivyo simu yake nyengine Galaxy 8 huenda ikazinduliwa mwaka ujao.
WEMA ADHIHIRISHIA WATU KUWA HANA SHIDA NA AUNTY EZEKIEL.
Baada ya bifu la mda mrefu kati ya Wema Sepetu na Aunty Ezekiel, sasa Wema aonyesha hadharani kuwa hana shida na Aunty baada ya kupost picha ya Aunty na kuandika maneno kama unavyoona hapo juu.
WAUAJI ALBINO WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA.
Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imewahukumu kunyongwa hadi kufa watuhumiwa wawili, Pankras Minago na Lameck Bazil kwa kumuua mlemavu wa ngozi, Magdarena Andrea.
Jaji Firmin Matogolo ametoa hukumu hiyo leo baada ya kuridhika na ushahidi kuwa ndio walimuua mlemavu huyo mkazi wa Wilaya ya Biharamulo mwaka 2008.
MATOKEO YA DARASA LA SABA.
Baraza la Mitihani la Taifa limetangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi (PSLE) ambayo yameonyesha ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.
Akitangaza matokeo hayo leo (Alhamisi), Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema jumla wa watahiniwa 555,291 kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 70.3 ya ufaulu tofauti na ufaulu wa mwaka jana ambao ulikuwa ni asilimia 67.8
"Hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.52," amesema Dk Msonde.
Pia amezitaja shule 10 bora kuwa ni Shule ya Msingi Kwema (Shinyanga), Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy ( Dar es Salaam), Tusiime (Dar), Mudio Islamic (Kilimanjaro), Atlas (Dar), St Achileus (Kagera), GiftSkillfull (Dar) na Carmel (Morogoro)
JACOB ZUMA ASINZIA BUNGENI.
Macho ya wengi nchini Afrika Kusini jana yalikuwa kwenye Waziri wa Fedha Pravin Gordhan ambaye alikuwa akihutubu bungeni.
Uchumi wa Afrika Kusini umekuwa ukikabiliwa na matatizo na kumekuwa na maswali mengi kuhusu ufadhili wa elimu.
Wanafunzi katika vyuo vikuu vingi wamekuwa wakiandamana na kuzua vurugu kulalamikia viwango vya karo.
Bw Gordhan mwenyewe amejipata kwenye mzozo wa kisiasa na hivyo basi taarifa yake ya bajeti ya muda ilisubiriwa kwa hamu na ghamu.
Lakini asubuhi hii, habari zimeanza kuenea mtandaoni kwamba Rais Jacob Zuma huenda alisinzia (au kupumzisha macho kama wasemavyo Kenya) wakati wa hotuba ndefu ya waziri huyo.
Tovuti ya habari ya Times Live imesema alikuwa anasinzia.
Baadhi wamejaribu kutoa ufafanuzi, kwa njia ya ucheshi kuhusu alichokuwa akifanya rais huyo.
Tovuti ya habari ya Rand Daily Mail imeeleza mambo matano ambayo huenda yalikuwa yakitokea, na ambayo huenda Rais Zuma akatumia kujieleza:
Nilikuwa naangalia ujumbe kwenye TwitterSikio langu lilikuwa na mwasho kidogo, nilikuwa najikuna kwa kutumia begaNilikuwa najaribu kusikia kiranja wa ANC bungeni Jackson Mthembu alikuwa anasema nini nyuma yanguHuwa nakuwa makini zaidi nikiwa nimefunga macho.Kulala ni hali mbadala ya kuwa macho
Afisi ya Rais Zuma bado haijazungumzia habari hizo.
Kiongozi huyo si wa kwanza Afrika kupatikana hadharani akiwa amefunga macho.
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye ameongoza tangu 1980, amepatikana mara kadha.
Aprili mwaka huu, alionekana kana kwamba anasinzia wakati wa kikao cha wanahabari alipokuwa na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe:
Septemba 2012, alipigwa picha akiwa amesinzia katika mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York.
Mwaka 2014, runinga ya NTV nchini Uganda iliashiria kwamba huenda Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza tangu 1986, alisinzia bungeni.
Kituo hicho cha runinga kilisema alikuwa amefunga macho.
Msemaji wa serikali alisema kiongozi huyo alikuwa anatafakari wakati huo. Kituo cha NTV kilipigwa marufuku kuripoti kuhusu hafla za rais kwa muda.
MWANAMKE MWENYE MACHO YA KUSHANGAZA AKAMATWA.
Mhamiaji kutoka Afghanistan, ambaye alipata umaarufu picha yake ilipochapishwa kwenye ukurasa wa kwanza wa jarida la National Geographic miaka thelathini iliyopita, amekamatwa.
Maafisa wanasema amekamatwa kwa kuwa na nyaraka bandia za utambulisho.
Sharbat Gula alipata umaarufu mwaka 1985 kutokana na picha hiy aliyopigwa akiwa na umri wa miaka 12.
Macho yake yalikuwa na rangi ya kijani, jambo lililomfanya kufahamika kwa jina 'Green-eyed Girl'.
Maafisa wanasema alikamatwa na Idara ya Uchunguzi ya Pakistan (FIA) baada ya uchunguzi wa miaka miwili Peshawar, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan.
Pakistan ilianza kuwasaka watu wenye vitambulisho bandia majuzi.
Bi Gula aliwasilisha ombi la kutaka kitambulisho Aprili 2014 akitumia jina Sharbat Bibi.
Iwapo madai hayo yatathibitishwa, basi atakuwa mmoja wa maelfu ya wakimbizi kutoka Afghanistan ambao wamejaribu kukwepa mfumo wa usajili wa watu unaotumia kompyuta nchini Pakistan.
Afisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usajili wa Watu (Nadra) amesema maafisa wa FIA pia wanawatafuta wafanyakazi watatu ambao wanadaiwa kumpa kitambulisho Bi Gula.
Gazeti la Dawn la Pakistan limesema Bi Gula alipewa vitambulisho pamoja na wanaume wengine wawili waliodai kuwa wanawe wa kime.
Picha maarufu ya Bi Gula ilipigwa 1984 alipokuwa kambi ya wakimbizi kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Wakati huo wanajeshi wa Muungano wa Usovieti walikuwa wameingia Afghanistan.
Mwaka 2002, mpiga picha Steve McCurry alimtafuta na kumpiga picha. Wakati huo alikuwa anaishi kijiji kimoja Afghanistan akiwa na mumewe na binti zao watatu.
Baada ya kutokea kwa habari za kukamatwa kwa Bi Gula, Bw McCurry amesema atafanya kila juhudi kumsaidia kifedha na kisheria.
"Nimejitolea kufanya kila niwezalo kutoa msaada wa kifedha na kisheria kwake na familia yake," aliandika kwenye Instagram.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha Pakistan inatoa hifadhi kwa wakimbizi 1.4 milioni kutoka Afghanistan ambao wamesajiliwa. Inakadiriwa kwamba wengine milioni moja wanaishi humo lakini hawajasajiliwa.
CHELSEA WATOLEWA NA WESTHAM KATIKA KOMBE LA EFL.
West Ham wamefika hatua ya robo fainali Kombe la EFL baada ya kudhihirisha ubabe wao na kuwalaza Chelsea kwenye mechi iliyochezewa uwanja wa London, zamani ukijulikana kama uwanja wa Olimpiki.
Mechi hiyo hata hivyo ilikumbwa na vurugu za mashabiki.
Chupa za plastiki na viti vilirushwa mamia ya mashabiki walipokabiliana karibu na mwisho wa mechi.
Cheikhou Kouyate alifunga bao la kichwa kabla ya muda mapumziko, naye Edimilson Fernandes akaongeza la pili dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Gary Cahill alikomboa bao moja dakika za mwisho mwisho lakini lilikuwa tu la kufutia machozi.
West Ham watakutana na Manchester United ambao walilaza Manchester City 1-0 kwenye mechi nyingine iliyochezwa usiku wa Jumatano.
Southampton nao walilaza Sunderland 1-0.
West Ham mechi yao ijao itakuwa dhidi ya Everton uwanjani Goodison Park ligini tarehe 30 Oktoba nao Chelsea siku hiyo wame ugenini St Marys dhidi ya Southampton.
MTU ALIYEVALIA KAMA MTI AKAMATWA MAREKANI.
Mwanamume mmoja nchini Marekani, ambaye ameanza kufahamika kama "binadamu mti", alikamatwa baada yake kuvuka barabara akiwa amevalia kama mti.
Asher Woodworth, kutoka jimbo la Maine nchini Marekani, alijifunika kwa matawi na kuvuka barabara polepole.
Polisi walimsindikiza hadi kando mwa barabara kabla ya kumuweka kizuizini.
Asher baadaye aliachiliwa huru na polisi.
Aliambia BBC kwamba alikuwa akivuka barabara mara ya tatu pale alipokabiliwa na maafisa wa polisi.
Yeye ni mwigizaji mjini Portland, Maine.
Anasema: "Nilipata wazo hili nilipokuwa natafakari sana siku moja."
Anasema alikuwa anataka tu kuwashangaza watu kwa mavazi yake na kuwafanya "watafakari upya kuhusu matarajio yao".
Alikuwa ametumia matawi ya miti ya aina mbalimbali na anasema ilimchukua yeye na rafiki yake saa kadha kukamilisha vazi hilo.
Anasema matawi ya miti aliyokuwa amevalia yalikuwa "yananukia".
Lakini mbona akaamua kuvalia matawi ya miti?
"Huwa nahisi nina uhusiano wa karibu na miti, naipenda sana," aliambia.
Alikuwa pia ametiwa moyo na mpiga picha Charles Freger, aliyepiga picha hii iliyo hapa chini.
Baada yake kukamatwa, Asher Woodworth anasema alikaa saa sita kizuizini kabla ya kuachiliwa huru Jumatatu.
BINTI YAKE OBAMA NA VITUKO VYA SNAPCHAT KWA BABA YAKE.
Rais wa Marekani Barack Obama amesema bintiye wa miaka 15, Sasha, alimcheka kwenye ujumbe aliowatumia marafiki zake kupitia mtandao wa kijamii wa Snapchat.
Kiongozi huyo wa Marekani amesema Sasha alimpiga video akijadili mtandao huo wa kijamii kwenye dhifa ya familia na kisha, kisiri akawatumia marafiki zake akiwa ametoa maoni yake.
Hii si mara ya kwanza kwa rais huyo kujadili shughuli za mtandaoni za bintiye huyo.
Mwezi Julai, alisema kwamba Sasha hutumia Twitter na kusababisha baadhi ya vyombo vya habari kujaribu kutambua akaunti ya Sasha kwenye Twitter.
Hadi wa leo imesalia kuwa siri.
Maneno hasa aliyoandika Sasha kwenye Snapchat hayajafanywa wazi.
Ujumbe unaopakiwa kwenye mtandao huo wa kijamii huwa unatoweka baada ya kutazamwa na anayelengwa au baada ya kipindi kifupi, lakini kuna njia za kukwepa hilo.
Picha ya upweke
Rais Obama alisimulia kuhusu kisa hicho cha Snapchat kwenye mahojiano katika kipindi cha runinga cha Jimmy Kimmel Jumatatu.
Sasha alinipa maagizo Snapchat," alisema.
"Jioni moja wakati wa dhifa ya jioni ya familia tumeketi hapo, na nilikuwa nimesoka kuhusu jinsi Snapchat imekuwa maarufu kwa watu wa rika lake. Kwa hivyo nikamwambia: 'Sasa, niambie kuhusu Snapchat.'
"Hivyo, anaanza kunifafanulia - unaweza kubadilisha sura yako, na hili na lile.
"Na mwishowe, Michelle na mimi tumeketi hapo. Na nikasema: 'Si inafurahisha sana?'
"Na nikaanza kumwambia Michelle kuhusu athari za mitandao ya kijamii.
"Na kisha nikagundua kwamba alikuwa anatunakili kwenye video wakati wote, na kisha akawatumia marafiki zake baadaye: 'Huyu ni babangu akitufundisha kuhusu mitandao ya kijamii.'
"Na akajipiga picha yake mwenye akionekana mwenye upweke."
Rais aliongeza kwamba mkewe alijiunga na Snapchat mwezi Juni, na bintiye mkubwa alikuwa "amependa" ujumbe huo.
Jimmy Kimmel, alifanya mzaha kwamba kisa hicho kilikuwa sawa na ukiukaji wa masharti ya kiusalama.
Kufichuliwa kwa barua pepe
Rais pia alisema simu yake ya iPhone amekuwa tu akiitumia kupokea barua pepe na kuchakura mtandaoni na kwamba hawezi kupiga picha, kucheza muziki au kupiga simu.
"Kanuni yangu kipindi changu cha uongozi imekuwa, nachukulia kuwa siku moja, wakati mmoja, kuna mtu atasoma barua pepe hii," amesema.
"Hivyo, huwa situmi barua pepe yoyote ambayo siwezi nikafurahia ikigonga vichwa vya magazeti."
MATETEMEKO YATOKEA TENA NCHINI ITALIA.
Matetemeko makubwa mawili yamepiga katikati ya Italia kwa muda wa saa mbili, karibu na eneo ambapo tetemeko jingine lililoua karibu watu mia tatu mwezi Agosti. Matetemeko yote mawili yametokea mashariki mwa jiji la Perugia, likiwa na ukubwa wa kipimo cha Ritcher 5.4 na 6.
Nguzo za umeme zimearifiwa kudondoka na baadhi ya majengo yamebomolewa. Lakini Meya wa karibu na eneo hilo amesema kuwa tayari ameshatoa taarifa kuhusu uharibifu uliotokea kijijini hapo, na kuna taarifa za majeruhi na kusema kuwa picha yote haiwezi kuchukuliwa mpaka mchana.
Watu wengi wameenda nje ya eneo hatari kabla ya tetemeko la pili na nguvu yake kutokea.
WATU WANNE WAKAMATWA MTANDAONI KWA WIZI WA MAGARI.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za wizi wa magari kwa kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema jana Dar es Salaam kuwa askari waliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Watuhumiwa hawa wanajihusisha na wizi wa magari kwa mbinu ya kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima, pamoja na kukata vibali vya namba ya ‘chassis’ ya magari hayo kisha kuweka kwenye magari waliyoyaiba,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema baada ya askari kupata taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji eneo la Tandale na kukamata mtuhumiwa Dennis Gasper (25), mfanyabiashara wa Manzese Uzuri akiwa na mabaki ya gari namba T 290 DDM Toyota ALPHAD.
Alisema katika mahojiano mtuhumiwa alitaja watuhumiwa wengine na kuwaongoza askari hadi Magomeni Mikumi maeneo ya kituo cha daladala na kuwakamata watuhumiwa wengine watatu ambao ni Alfred Ditrick (33), mkazi wa Sinza, Venance Bureta (24) wa Mbezi na Dickson Valentino (23) mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na mkazi wa Kimara, wote katika Jiji la Dar es Salaam.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikutwa na gari la wizi namba T 368 CES Toyota Passo na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya wizi wa magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuyauza nje ya mkoa huo.
Katika tukio lingine, askari wamekamata magari mengine matatu ya wizi yaliyoibwa mkoani Dar es Salaam na kupelekwa mafichoni Arusha yakiwemo Toyota Vitz T 262 CTF, Suzuki Carry lenye namba za usajili T 935 CPC, Toyota Passo lenye namba za usajili T 368 CES na Toyota Landcruiser Prado lenye namba za usajili T 735 BLZ.
Alisema watuhumiwa wa mtandao huo wanashikiliwa mkoani Arusha na juhudi za kuwafuata zinafanyika ili kuja kuwaleta Dar es Salaam kujibu mashitaka yanayowakabili.
WACHINA WAWILI WAKAMATWA KWA KUMTEKA MWENZAO.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia raia wawili wa China kwa tuhuma za kumteka nyara Mchina mwenzao, Liu Hong (48) ambaye ni mfanyakazi wa Le Grande Cassino, wakidai kulipwa Dola za Marekani 19,000 (zaidi ya Sh milioni 38).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema walipokea taarifa kwamba raia huyo wa China alitekwa nyara na watu wasiofahamika.
Alisema taarifa hizo zilieleza kwamba Liu alitekwa nyara Oktoba 23, mwaka huu saa moja asubuhi na ndipo polisi wakaunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini watekaji walikuwa wakidai Yen 100,000 (fedha za China) ambazo ni sawa na Dola za Marekani 19,000.
“Oktoba 24, mwaka huu saa 11 jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha Polisi Kanda Maalumu walibaini kuwa wateka nyara hao wapo katika Hoteli ya Palm Beach Upanga na walipofika hapo wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema polisi walipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua mlango ndipo polisi waligundua wateka nyara hao kuwepo katika chumba hicho.
Alisema wakiwa wanajiandaa kuvunja mlango, mara mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing (37) raia wa China aliamua kufungua mlango na kumkamata akiwa na Liu ambaye ni mtekwa nyara.
“Askari walipoingia ndani walimkuta aliyetekwa nyara akiwa hajitambui akiwa na majeraha usoni. Pia katika tukio hili, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine aitwaye Chen Chung Bao (35) raia wa China ambaye ndiye aliyekodi chumba hicho,” alieleza kamanda.
Alisema ndani ya chumba hicho kulikutwa vipande viwili vya taulo walivyotumia kumfunga mikono, kamba za plastiki na bomba la sindano. Alisema majeruhi alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa. Upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, Polisi ilifanya operesheni katika maeneo ya katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam na kuwakamata watuhumiwa 57 kwa makosa mbalimbali ya uhalifu.
Kamanda Sirro alisema Mkoa wa Temeke walikamatwa watuhumiwa 21, Ilala watuhumiwa 19 na Kinondoni watuhumiwa 17.
“Baadhi ya watuhumiwa hao ni vikundi mbalimbali wanaojiita majina tofauti ikiwemo ‘Panya road’, ‘Black American’, Taifa jipya na Kumi ndani na kumi nje,” alieleza na kuongeza kuwa watuhumiwa walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kivule, Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Kawe na Keko.
Alisema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvuta na kuuza bangi, kuuza na kunywa gongo na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
MAN U WAWAONDOA MAN CITY KATIKA KOMBE LA EFL.
Manchester United walifika hatua ya robo fainali katika Kombe la EFL baada ya kuwalaza mabingwa watetezi Manchester City kwenye debi iliyochezewa uwanja wa Old Trafford.
Juan Mata alifunga bao la pekee mechi hiyo baada ya kupata mpira kutoka kwa mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic.
Paul Pogba alikuwa amegonga mlingoti kwa kombora kali awali na kusisimua mechi hiyo kipindi cha pili.
Kipindi cha kwanza kilikuwa kikavu bila upande wowote kupata kombora la kulenga goli.
Manchester United sasa watakutana na West Ham ambao waliwalaza Chelsea 2-1.
Ushindi huo wa United ulikuwa wao wa pili katika mechi tano, na wa nne kwa Jose Mourinho katika mechi 18 alizokutana na Pep Guardiola.
SERIKALI YAZIPIGA STOP YANGA NA SIMBA.
Serikali imezipiga stop klabu za Yanga na Simba kuendelea na michakato yao ya kubadili umiliki wake hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya katiba zao.
Hayo yalitangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni klabu hizo kongwe ziliazimia kuingia kwenye mabadiliko, Yanga ikikodishwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji na Simba ikitaka kuuza hisa asilimia 51 kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
Kiganja alisema Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji katika klabu hizo pamoja na nyingine za wanachama, ila inachotaka kwanza kufanyike marekebisho ya katiba zao kwani za sasa haziruhusu mabadiliko hayo.
Alisema kuwa BMT inapenda kuona wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Hivi karibuni kumeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…,” alisema.
Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua nyingi za wanachama wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 Ibara ya 56 inaeleza kuhusu kampuni ya umma: Inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young African Sports Corporation Limited ambayo itasajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama kampuni ya umma yenye hisa.
Sehemu ya pili ya ibara hiyo inasema wanachama wote katika klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2007 wako hai kwa nguvu ya uanachama wao watakuwa wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakapopata kwa mujibu wa muafaka wa Yanga uliofikiwa na wana Yanga Juni 22, 2006.
Klabu itamiliki hisa zilizosawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika klabu hiyo. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili, ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.
Tayari Yanga iko chini ya Kampuni ya Yanga Yetu ambayo ni mali ya mwenyekiti wa klabu hiyo Manji, ikiwa ni kinyume na katiba yao wenyewe.
Kiganja alisisitiza kuwa klabu zisitishe mipango ya kubadilisha uendeshaji na ziendelee kuwa mali ya wanachama. Wakati Yanga walikuwa tayari wameishaingia mkataba wa miaka 10 wa kuikodisha klabu yao, wenzao wa Simba walijipa miezi sita kukamilisha taratibu za kuuza hiza.