Friday, October 21, 2016

MENEJA WA DIAMOND NA MWENZAKE WAKWAMA BAADA YA MAHAKAMA KUU KUTUPILIA MBALI MAOMBI YAO.


                                       BABU TALE.
Wakurugenzi wa Kampuni ya Tiptop Connections ya jijini Dar es Salaam,  Hamis Taletale maarufu kama Babu Tale na ndugu yake Idd Taletale wamekwama tena mahakamani katika harakati zao za kukwepa ulipaji wa fidia ya Sh250 milioni kutokana na makosa ya hakimiliki.
Badala yake hatima yao sasa itajulikana Jumanne juma lijalo wakati Mahakama itakapotoa maelekezo muhimu.
Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii maarufu nchini wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Abdul Nassib maarufu kama Diamond Platnum na nduguye leo wamekwama  baada ya Mahakama Kuu, Dar es Salaam kuwagomea na kutupilia mbali maombi yao.
Leo walipaswa waieleze Mahakama ni kwa nini wasifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama hiyo iliyowaamuru kulipa fidia hiyo baada ya kupatikana na hatia ya  ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki, au kueleza ni lini na namna gani watalipa fidia hiyo .
http://burudaninaangie.blogspot.com/

MOURINHO: POGBA APEWE MUDA MAN UNITED.

Paul Pogba

Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema hakutarajia Paul Pogba, ambaye alicheza vyema sana dhidi ya Fenerbahce katika ligi ndogo ya Ulaya, azoee soka ya England haraka.
Amesema mchezaji huyo anafaa kupewa muda kuzoea kucheza tena England badala ya kukosolewa kila mara.
Pogba, 23, aliyenunuliwa £89m mwezi Agosti na kuvunja rekodi ya dunia, alifunga mabao mawili Alhamisi wakati wa ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Fernabahce.
Hata hivyo hakung'aa Jumatatu dhidi ya Liverpool mechi waliyotoka sare 0-0.
"SIku mbili zilizopita, alitajwa kuwa mchezaji mbaya zaidi katika Lgi ya Premia na saa 48 anasifiwa sana," amesema Mourinho.
"Anahitaji muda. Naridhishwa na uchezaji wake. Ana ustadi tunaohitaji.
Mourinho amesema anaamini Pogba bado anazoa aina tofauti ya soka.
"Niliwa Italia na nafahamu sifa za soka huko, kasi yake na ukali wake," Mourinho, 53, alisema.
"Kuwa Italia kwa miaka minne au mitano na kisha urejee Ligi ya Premia, sikumtarajia aanze mara moja kung'aa."
Group A standings
Pogba kwenye Twitter

HILLARY CLINTON NA DONALD TRUMP WATANIANA.

Hillary Clinton na Kadinali Tim Dolan na Donald Trump - 20 Oktoba 2016

Wagombea wakuu wa urais nchini Marekani Hillary Clinton na Donald Trump walirushiana vijembe kwa utani katika dhifa ya jioni iliyoandaliwa kuchangisha pesa za hisani.
Walishiriki kwenye dhifa hiyo siku moja baada ya kushambuliana vikali kwenye mdahalo wa mwisho wa runinga.
Bi Clinton alicheka sana Bw Trump alipomtania kuhusu hotuba za kulipwa na pia uchunguzi wa FBI kuhusu tuhuma kwamba alitumia barua pepe ya kibinafsi kwa shughuli rasmi.
Lakini Bw Trump alizomewa alipofanya mzaha kwamba mpinzani huyo wake huwachukia Wakatoliki.
Dhifa hiyo ya Wakfu wa Ukumbusho wa Alfred E Smith mjini New York hufanyika kila baada ya miaka minne na kuwashirikisha wagombea urais.
Kuna desturi kwamba wagombea husimama na kutaniana, lakini mwana huu imeandaliwa wakati kumekuwa na uhasama mkubwa sana kwenye kampeni.
Jumatano jioni mjini Las Vegas wakati wa mdahalo wa mwisho, Bw Trump alimweleza mpinzani wake wa chama cha Democtaric kama "mwanamke mbaya", na wote na kila mmoja alikuwa anamkatiza mwenzake akiongea wakati wa mdahalo huo.
Mwishowe, walikataa kupatiana mikono kuagana.
Bw Trump amembandika "Crooked Hillary" (Hillary Mwovu) na ametishia kumteua mwendesha mashtaka maalum wa kumshtaki na kuhakikisha amefungwa jela iwapo atashinda.
Bi Clinton naye amesema mpinzani huyo wake wa chama cha Republican anaendesha "kampeni ya chuki na kuwagawanya watu" na kwamba hafai kuwa rais wa Marekani.
Lakini kwenye dhifa hiyo ya New York, walionekana kuweka kando tofauti zao kwa muda. Waliketi wakikaribiana sana, wakitenganishwa tu na KadinaliTimothy Dolan.
Walipoingia na kuketi, hawakusalimiana wala kuangaliana kwa macho. Lakini Bw Trump aliposimama kuhutubu, alimgusa begani kwa urafiki.
Alitania kwamba hadhira hiyo ya watu 1,500, ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu aliohutubia kufikia sasa.
Na akimshambulia Bi Clinton kwa uhusiano wake na matajiri wa Wall Sreet, akasema litakuwa jambo la ajabu sana kwa Bi Clinton kuwa na viongozi wengi hivyo wa mashirika na kampuni na awe hajalipwa.
Lakini aliposema mpinzani wake ni mfisadi kiasi kwamba alitupwa kutoka tume ya Watergate, alizomewa.
Na alizomewa tena aliosema Bi Clinton amekuwa "akijifanya kwamba hawachukii Wakatoliki". Matukio hayo mawili yalionekana kumfanya Bi Clinton kutabasamu.
Hillary Clinton na Kadinali Tim Dolan na Donald Trump - 20 Oktoba 2016
Bw Trump pia alijitania kwa kugusia hotuba ya mkewe Melania aliyoitoa Julai, ambapo alidaiwa kukopa sana maneno kutoka kwa Mama Taifa Michelle Obama.
Kisha, Bi Clinton alisimama kuhutubu. "Tutakuwa na mwanamke wa kwanza rais au rais wa kwanza aliyeanzisha vita kwenye Twitter na Cher," alisema.
Badala ya kutazama Sanamu ya Liberty kama mnara wa matumaini, Bw Trump amekuwa akigeza urembo wa sanamu hiyo. Alama "nne" au "tano labda" iwapo sanamu hiyo itapoteza mnara wake na tablet na kubadilisha nywele, Bi Clinton alitania. (Bw Trump wakati aliendesha shindano la urembo na ametuhumiwa kuwadhalilisha wanawake).

Vichekesho vya Clinton...
"Nimelazimika kumsikiliza Donald Trump kwa midahalo mitatu ... Sasa nimeketi karibu na Donald Trump muda mrefu kuliko maafisa wake wa kampeni."
"Baada ya kusikiliza hotuba yako, nitafurahia sana kumsikiliza (mgombea mwenza wake) Mike Pence akikanusha kwamba hukuitoa."
"Nimefurahia sana kusikia Donald alidhani nilitumia dawa za kuchangamsha mwili (kabla ya mdahalo). Ni kweli nilitumia. Kunaitwa kujiandaa."
Vichekesho vya Trump...
"Usiku wa kuamkia leo, nilimwita Hillary mwanamke mbaya, lakini mambo haya yote yanategemea. Baada ya kumsikiliza Hillary akiongea na kuongea, sidhani Rosie O'Donnell ni mbaya tena."
"Sasa ninaambiwa Hillary alienda kuungama dhambi kabla ya hafla ya leo, lakini kasisi alikuwa na wakati mgumu alipomwuliza dhambi zake, na alisema hawezi kukumbuka mara 39."

NGULI WA MZIKI WA AFRO JAZZ KENYA ACHIENG ABURA AFARIKI DUNIA.

Achieng Abura
                 
MAREHEMU ACHIENG ABURA
Mwanamuziki nguli wa nyimbo za mtindo wa Afro Jazz kutoka Kenya Achieng Abura amefariki dunia.
Mwanamuziki huyo aliaga dunia akipokea matibabu katika hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta (KNH) jijini Nairobi.
Lydia Achieng Abura, alipata umaarufu miaka ya 1990 kwa wimbo wa injili kwa jina I Believe.
Baadaye, alianza kukumbatia mitindo mingine ya uimbaji kama vile jazz.
Kwenye ujumbe katika ukurasa wa Facebook mapema mwezi huu, alikuwa amedokeza kwamba hakuwa buheri wa afya.
Alisema alikuwa amepoteza uzani wa kilo 50 katika kipindi cha miaka mitatu pekee, na madaktari walikuwa wamemshauri kuongeza uzani.
"Kutembea ni shida na ninaumwa kila pahali," aliandika.
 Achieng Abura
Kwenye mahojiano na gazeti la Business Daily mwezi Julai, alikuwa amesema alikabiliwa na matatizo ya kifedha kutokana na afya ya mwanawe wa kiume aliyehitaji kufanyiwa matibabu ambayo yangegharimu Sh4 milioni (dola 400,000 za Marekani).
"Niliandaa mchango lakini waliohudhuria walikuwa chini ya 10," aliambia gazeti hilo.
Abura alishinda tuzo ya muziki ya Kora mwaka 2004.
Alikuwa pia jaji katika shindano la kuwatafuta wanamuziki wenye vipaji la Tusker Project Fame ambalo liliwashirikisha vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Wanamuziki wenzake, viongozi na mashabiki wameeleza kushangazwa kwao na kifo hicho na wamekuwa wakituma salamu za rambirambi mtandaoni.
Suzanna Owiyo
Sauti Sol

AFRIKA KUSINI WAJITOA KATIKA MAHAKAMA YA ICC.

Omar al Bashir
Afrika Kusini imeanzisha mchakato wa kujiondoa kutoka uanachama wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita.
Wanadiplomasia wa Afrika kusini wamearifu umoja wa mataifa juu ya uamuzi huo na kuilaumu ICC kwa kuzilenga zaidi nchi za Afrika.
Uamuzi wa Afrika kusini kujiondoa ulitokana na shinikizo ilikumbana nazo mwaka uliopita za kuitaka imkamate rais wa Sudan Omar al Bashir wakati wa mkutano wa muungano wa nchi za Afrika mjini Johannesburg.
Septemba mwaka jana, mahakama nchini nchini Afrika Kusini iliinyima serikali ya nchi hiyo ruhusa ya kukata rufaa uamuzi ulioishutumu kwa kukosa kumkamata Bw Bashir alipohudhuria kongamano hilo mwezi Juni mwaka 2015.
Serikali ilitaka kukata rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu ikisema Bashir alikuwa na kinga ya urais kwa sababu yeye ni kiongozi wa taifa.
Lakini Jaji Hans Fabricius alisema rufaa hiyo haiwezi kufanikisha chochote.


Aliongeza kuwa Afrika Kusini ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo, na kwamba mkataba huo unabatilisha sheria zozote ambazo huenda zingempa kinga Bashir asikamatwe na kushtakiwa.
Jeneza ICC
Kiongozi huyo wa Sudan amekuwa akisakwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na makosa ya uhalifu wa kivita Darfur.
Kiongozi huyo aliyechukua mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 amekanusha madai hayo.

MAKONDA KUPAMBANA NA WAHALIFU WALIOIBUKA HIVI KARIBUNI.

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM, PAUL MAKONDA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ofisi yake inaanziasha operesheni maalum kwa ajili ya kupambana na magenge ya wahalifu ambayo yaibuka hivi  karibuni.
Akizungumza leo (Ijumaa) kabla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Makonda amesema hiyo ndiyo changamoto inayoikabili jiji la hili.
Makonda ambaye amesema hayo wakati akitoa salamu kwa Rais John Magufuli anayetarajia kuweka jiwe hilo muda mfupi kuanzia sasa amesema operesheni hiyo inalenga kushughulikia magenge ya wahalifu hao ambao wamekuwa wakidhuru wananchi na kupora mali zao.

MWANAFUNZI AKAMATWA KWA KOSA LA KUTOA MIMBA.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Matala wilayani hapa amekamatwa na polisi kwa madai ya kutoa mimba.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amesema jana kuwa mwanafunzi huyo na mshirika wake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.
“Tunamsaka kijana aliyempa mimba na atakapopatikana sheria itafuata mkondo kwa kumfikisha mahakamani,” amesema.
Mbali na mwanafunzi huyo aliyelazwa Hospitali ya Kilema, pia jeshi hilo linamshikilia mama yake mdogo kwa madai ya kumsaidia kutekeleza kitendo hicho.
Babu wa mwanafunzi aliyetoa mimba, Henry Kaale amelalamika kushikiliwa kwa wanafamilia wakati mtuhumiwa muhimu hajakamatwa. 

WATU SITA WAKAMATWA NA SILAHA MKOANI MWANZA.

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
    KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA, AHMED MSANGI
Polisi mkoani Mwanza imewakamata watu sita wakiwa na silaha mbili zilizotengenezwa kienyeji, walizokuwa wakizitumia kwenye matukio ya unyang’anyi na uporaji wa mali, zikiwa zimehifadhiwa kwa mganga wa kienyeji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa watu hao wamekamatwa Oktoba 18, mwaka huu saa saba mchana, baada ya polisi wakiwa kwenye doria Buswelu, kata ya Buswelu, Manispaa ya Ilemela, waliwakamata watu hao baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa wahalifu hao.
Katika hatua za awali, polisi walimkamata Jeremia Mkumbo (25) mkazi wa Malega mkoani Singida.
“Alipohojiwa alikiri kuhusika kwenye matukio ya uhalifu na kuwataja watu wengine waliokuwa wakishirikiana.Alisema silaha ambazo hutumia kwenye uhalifu waliziacha kwa mganga wa kienyeji aitwaye Leonard Litta mkazi wa mtaa wa Kagida- Buswelu”, alifafanua Kamanda Msangi.
Alisema polisi walikwenda nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji, Leonard Litta (39) na baada ya kufanya upekuzi nyumbani hapo, walikamata risasi 22 zinazotumiwa na bunduki aina ya short gun.
Alisema baada ya kuhojiwa na polisi, watuhumiwa hao waliwataja watu wengine wanne waliokuwa wakishirikiana katika kufanya uhalifu ambao nao wamekamatwa.
Aliwataja watu waliokamatwa kuwa ni Kamugisha Jovin (40) mlinzi na mkazi wa Iloganzala, Juma Yusuph (35) mkazi wa Bwani –Kinondoni, Samwel Peter (36) mkazi wa Buswelu na Shaban Hussein (26) fundi viatu na mkazi wa Nyasaka Msumbiji katika Manispaa ya Ilemela.
“Watuhumiwa wote walipofanyiwa mahojiano walikiri kuwa walizitumia silaha hizi katika unyang’anyi wa mali na uporaji katika maeneo ya jiji na mkoa wetu wa Mwanza”, alieleza na kuongeza kuwa Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na mengine waliyoyafanya na pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Katika tukio lingine, Kamanda Msangi alisema Polisi imewakamata wakazi wawili wa Dar es Salaam waliokutwa na gari la wizi.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 18, mwaka huu saa nane mchana eneo la Ilemela Manispaa ya Ilemela, wakiwa kwenye harakati za kuuza gari lenye namba za usajili T.778 AZV aina ya Toyota Land Cruiser, walilokuwa wameliiba kwa mfanyabiashara wa Kiasia, Ilala jijini Dar es Salaam.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Rahim Feka (28) mkazi wa Ilala na Ally Kawale (32) mkazi wa Jet Lumo- Airport.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao, walikamatwa baada ya Polisi kupokea taarifa za kuibwa kwa gari hilo kutoka jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kupata taarifa kutoka Dar es Salaam, tulihisi kuna uwezekano wa mtandao huu wa wizi wa magari kuwepo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na baada ya kufanya uchunguzi tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao,” alisema Kamanda Msangi na kuongeza kuwa watuhumiwa wote wako chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano zaidi.
Alisema Polisi mkoani Mwanza inawasiliana na wenzao wa Dar es Salaam, kufanya taratibu za kuwasafirisha watuhumiwa hao.