Wednesday, November 9, 2016
SIMBA CHALI, WALA KICHAPO CHA 2-1 NA TANZANIA PRISON.
Timu ya Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kunyukwa na Maafande wa Tanzania Prisons goli mbili kwa moja.
MARTIN KADINDA:MIMI SIO MENEJA WA WEMA.
MARTIN KADINDA. |
Mbunifu huyo wa mavazi amesema kuwa kwa sasa yeye na Wema Sepetu ni kama kaka na dada na sio meneja wake tena. “Mimi kum-meneji Wema nimemaliza kama miaka miwili iliyopita, mkataba uliishia hapo, lakini tukasimama kama mtu na kaka yake,” alisema Martin. “Kwa hiyo umeneja ule wa ukaka na udada upo mpaka tunaingia kaburini lakini kama umeneja wa mkataba uliisha na ukabaki ule umeneja wa imani baada ya kuaminiana.”
“Tuliona hakuna umuhimu wa kuwa na mikataba kwa sababu tayari tumeshaaminiana, kwa sababu sasa hivi mimi Wema nimeshamchukulia kama ndugu yangu na yeye kama kaka yake. Kwahiyo kugombana kupo lakini baadaye mnawekana sawa na maisha yanaendelea,” Aliongeza,
“Ukaribu wa mimi na Wema umepungua kwa sababu mimi kwa sasa nafanya mambo yangu na yeye anafanya mambo yake kwa sababu zamani Wema alikuwa anafanikiwa sana nakuniacha mimi nikiwa pale pale, kwa hiyo sasa hivi kila mtu anafanya mambo yake hatuwezi kuwa tunajenga kwake halafu kwangu kunaungua,” Katika hatua nyingine mbunifu huyo wa mavazi amewataka mashabiki wake wa fashion kusubiria mambo mazuri kutoka kwake.
UTABIRI WA TB JOSHUA MASHAKANI.
MHUBIRI TB JOSHUA WA NIGERIA. |
Utabiri wa mhubiri maarufu raia wa Nigeria TB Joshua, kuwa Hillary Clinton atamshinda Donald Trump umeambulia patupu.
Aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa Bi Clinton atashinda kwa kura chache. Kwa sasa ujumbe aliouandika kwenye mtandao umefutwa na sasa watu wanaendelea kumkejeli mhubiri huyo.
TB Joshua ni mmoja wa wahubiri maarufu na wenye kukumbwa na utata barani Afrika huku wengi wa wafuasi wake wakiamini kuwa utabiri wake ni wa ukweli.
Sawa na wahubiri wengine nchini Nigeria, TB Joshua ni tajiri na mwenye ushawishi mkubwa.
Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia husafiri hadi kanisa lake nchini Nigeria kutibiwa na kushuhudia unabii wake.
Wakati ugonjwa wa Ebola ulikumba eneo la magharibi mwa Afrika, mamlaka ya mji wa Lagos ilitangaza kuwa hakuna mgonjwa wa ugonjwa wa ebola angepelekwa kanisani humo kuponywa. Hii ilikuwa ni hatua ya kuzuia maambukizi.
Baada ya kifo cha Michael Jackson, mhubiri huyo alidai kuwa hilo ni suala ambalo alikuwa amelizungumzia miezi sita kabla.
Wakosoaji wake wameutaja utabiri wake kuwa uongo. Hata hivyo hilo halijawazuia wafuasi wake kufurika kanisani mwake kutafuta mwelekeo.
ALICHOAHIDI TRUMP KUKIFANYA NDANI YA SIKU 100 MADARAKANI.
Ni kipi Donald Trump ameahidi kukifanya siku za kwanza 100 akiwa rais?
Baadhi ya ahadi zake ndani ya siku 100 za kwanza zilitolewa wakati wa hotuba yake mwezi uliopita mjini Gettysburg jimbo la Pennsylvania.
- Ameapa kujenga ukuta kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico, mradi ambao utagharamiwa na Mexico.
- Ahadi nyingine ambayo licha ya kutokuwepo kwenye hotuba ya Gettysburg ni kusaini upya mikataba ya biashara kati Marekani,Canada na Mexico.
- Anasema kuwa mikataba hii inachangia katika kuwapokonya raia ajira zao.
- Trump pia ameahidi kuboresha uhusiano na Raias wa Urusi Vladimir Putin, ambaye amemsifu na kumtaja kuwa kiongozi aliye imara.
- Aidha ameapa kuondoa Marekani kutoka kwa mkataba kuhusu mpango wa nuklia wa Iran.
CHELSEA, LIVERPOOL, ARSENAL ZASHIKA ALAMA ZA JUU EPL.
Wakati klabu ya Liverpool ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England (EPL), ushindani wa timu gani itaibuka bingwa mpya ifikapo Mei mwakani umeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka jana.
Kipigo cha mabao 6-1 ilichokitoa kwa Watford, Jumapili kilitosha kuiweka kileleni Liverpool ikiwa na pointi 26 na kufuatiwa na Chelsea yenye pointi 25 baada ya Jumamosi kuiadhibu Everton 5-0. Hizo, zinafuatiwa na Manchester City, Arsenal, zenye pointi 24, timu mbili zilizozuiwa na wapinzani wao, Middlesbrough na na Tottenham kwa sare ya bao 1-1, zinafuatiwa na Spurs yenye pointi 21.
Ligi hiyo itasimama mwishoni mwa wiki ili kupisha michezo ya kimataifa, imeshuhudia mabadilio ya uongozi wake wa juu baada ya Manchester City iliyoanza vyema kwa ushindi wa mechi saba kupoteza mwelekeo kwenye mechi kadhaa zilizopita.
Chelsea yenye kiwango bora kwa sasa ikiwa chini ya kocha Antonio Conte imerejesha ushindani ilioupoteza msimu uliopita.
Ndani ya saaa 24, siku za Jumamosi na Jumapili zilishuhudia uongozi wa ligi hiyo ukihama kutoka City, Chelsea, hadi Liverpool. Lakini, vijana wa kocha Jurgen Klopp, Liverpool wanaocheza vizuri msimu huu wataiongoza ligi hiyo hadi Novemba 19.
Klopp alihitimisha mafanikio ya klabu yake akiesema: “Tuliwaangalia Chelsea, walicheza vizuri. Manchester City walicheza vizuri dhidi ya Barcelona. Tusiwadharau Manchester United. Tottenham ni timu nzuri. Kwa jumla, ligi ina timu nzuri.”
Tofauti ya pointi mbili kati ya Liverpool, Chelsea, City na Arsenal kileleni mwa ligi inatosha kuwa ushahidi mwingine wa ushindani ambao umeshika kasi mapema, ingawa Spurs na United, pia zinanyemelea, endapo timu yoyote iliyoko juu ikiteleza, zenyewe zitapanda juu.
Ni nafasi gani timu yako inapewa kutwaa ubingwa EPL?
Liverpool
Kwa sasa ndiyo vinara wa EPL, wana kasi inayobebwa na washambuliaji wakali walioiangamiza Watford Jumapili.
Tangu Agosti mwaka jana, Klopp hajaonja uchungu, anaiongoza timu inayofunga mabao mengi itakavyo ana imani ya mashabiki kuendelea kutamba msimu huu.
Sare dhidi ya Manchester United mwezi uliopita ilitibua ushindi wake wa asilimia 100, ingawa klabu hiyo ya Anfield inajiamini kuwa itaendeleza makali.
Inakabiliwa na mechi zijazo: Southampton (ugenini), Novemba 19; Sunderland (nyumbani), Novemba 26; Bournemouth (ugenini), Desemba 4; West Ham (nyumbani), Desemba 11; Middlesbrough (ugenini), Desemba 14; Everton (ugenini), Desemba 19.
Alama: 8/10
Chelsea
Kocha Conte ameibadili klabu hiyo ya Stamford Bridge kuwa mshindani wa kweli kwa kuondoa udhaifu wa msimu uliopita na kuwa moto wa kuotea mbali, ikitumia mfumo mpya wa 3-4-3.
Tangu ianze kutumia mfumo huo, Chelsea haijapoteza mchezo, kufungwa bao, imefunga mabao 16 kwenye mechi tano, ambako kiungo Eden Hazard na mshambuliaji Diego Costa wanatisha.
Mechi zijazo zitakuwa baina ya Middlesbrough (ugenini), Novemba 20; Tottenham (nyumbani), Novemba 26; Manchester City (ugenini), Desemba 3; West Brom (nyumbani), Desemba 11; Sunderland (ugenini), Desemba 14; Crystal Palace (ugenini), Desemba 17.
Alama: 8.5/10
Manchester City
Baada ya kuilaza Barcelona 3-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ilidhaniwa kuwa Manchester City imeimarika, lakini Jumamosi ilizuiwa na Middlesbrough kwa bao la dakika za majeruhi.
Rekodi ya ushindi wa mechi sita za kwanza imeanza kupotea, kocha Pep Guardiola amepata ushindi mmoja pekee kwenye mechi tano zilizopita. Ni wazi kuwa Manchester City bado inao uwezo wa kushinda taji, lakini lazima ipigane
Mechi zijazo: Crystal Palace (ugenini), Novemba 19; Burnley (ugenini), Novemba 26; Chelsea (nyumbani), Desemba 3; Leicester City (ugenini), Desemba 10; Watford (nyumbani), Desemba 14; Arsenal (nyumbani), Desemba 18.
Alama: 6.5/10
Arsenal
Sare ya 1-1 dhidi ya Tottenham Jumapili ulimwacha kocha Arsene Wenger akiwa mwenye hasira na kukosa nafasi ya kukaa kileleni, ikiwa imepata sare mbili kwenye mechi mbili kati ya tano.
Inao Alexis Sanchez na Mesut Ozil ambao wanang’ara msimu huu, imempata tena Olivier Giroud akiwa na kiwango kizuri, kiasi cha kuongeza chachu kwenye safu yao ya ushambuliaji. Msimu huu, Arsenal imeimarika zaidi kwenye ulinzi.
Safari ya kwenda Old Trafford ambako Wenger atakutana na mbabe wake, Jose Mourinho ni kipimo kingine cha ukakamavu wa Arsenal msimu huu. Pia, lazima Arsenal iweke kando matokeo mabaya ya mwezi Novemba, ambao umekuwa mbaya kwake kwa miaka mingi.
Mechi zijazo: Manchester United (ugenini), Novemba 19; Bournemouth (nyumbani), Novemba 27; West Ham (ugenini), Desemba 3; Stoke (nyumbani), Desemba 10; Everton (ugenini), Desemba 13; Manchester City (ugenini), Desemba 18.
Alama: 7/10
Tottenham
Hadi sasa, Spurs ndiyo pekee haijapoteza mechi EPL, lakini inakwenda mapumziko ya mechi za kimataifa ikiwa na ndoto ya kuifikia Liverpool ambayo imeipita kwa pointi tano.
Kocha Mauricio Pochettino hawezi kubadili sare ambazo Spurs imekuwa ikipata katika mechi zake za karibuni kuwa ushindi ili kuzikamata timu zilizo juu yake.
Kurejea uwanjani kwa Harry Kane, anayekaribia kuwa fiti na pengine atakuwa tayari kuiongoza safu ya ushambuliaji dhidi ya West Ham wiki mbili zijazo, Spurs inataka mageuzi.
Mechi zijazo: West Ham (nyumbani), Novemba 19; Chelsea (ugenini), Novemba 26; Swansea (nyumbani), Desemba 3; Manchester United (ugenini), Desemba 11; Hull (nyumbani), Desemba 14; Burnley (nyumbani ), Desemba 14.
Alama: 6/10
Manchester United
Ushindi wa kwanza katika mechi tano kwa kuilaza Swansee City mabao 3-1 Jumapili ulipoza vidonda ya mashabiki ambao hata hivyo hawana imani na kocha Jose Mourinho, bosi ambaye bado anauguza kidonda.
Alikuwa na wakati mgumu dhidi ya mabeki wake, Chris Smalling na Luke Shaw ambao aliwaeleza kuwa waoga wanapokaribia mechi. Pia, kiwango cha mshambuliaji wake mkongwe, Zlatan Ibrahimovic na kiungo Paul Pogba waliofunga mabao dhidi ya Swansea kinamfariji, ingawa lazima wakaze buti kwenye mchezo ujao dhidi ya Arsenal.
Mechi zinazofuata: Arsenal (nyumbani), Novemba 19; West Ham (nyumbani), Novemba 27; Everton (ugenini), Desemba 4; Tottenham (nyumbani ), Desemba 11; Crystal Palace (ugenini), Desemba 14; West Brom (ugenini), Desemba 17.
MASTAA WALIOSEMA TRUMP AKISHINDA WATAHAMA MAREKANI.
Kuna ule msemo maarufu siku hizi, ‘Usiempenda kaja’ ndiyo tunaweza kusema sasa unatumika kwa watu waliompinga Trump na huku akiwa ameshinda kiti cha Urais Marekani.
Waliotamka maneno hayo walijiapiza kuwa akishinda watachukua uamuzi mgumu, je, watafanya kama walivyoahidi?
Mwandishi wa Vitabu na mtunga mashairi, wa Nigeria, anayeishi Marekani, Wole Soyinka, alijiapiza kuwa Trump akishinda atachana kibali maalum cha kuishi Marekani.
Nyota wa Hollywood Samuel L Jackson alisema atahamia Afrika Kusini iwapo Donald Trump atashinda uchaguzi wa urais Marekani, tovuti ya News 24 iliripoti.
Mastaa wengine walioahidi kuhama Marekani endapo Trump atashinda ni pamoja na Miley Cyrus ambaye ni muigizaji. Moja ya muvi alizoigiza ni Hanna Montana na pia ni Mwanamuziki pia. kupitia ukurasa wake wa Instagram Cyrus alisema Trump akishinda yeye atahamia Canada.
Muigizaji Neve Campbell na mtunzi wa Filamu Lena Dunham walisema watahamia Canada.
KUTANA NA HISTORIA YA MAISHA YA CLINTON NA TRUMP.
Hillary Clinton alizaliwa na kukulia katika eneo la Chicago; Donald Trump alikulia Queens, New York |
Alikuwa katika kilabu cha kikundi cha mdahalo katika shule ya sekondari ya manispaa huku Trump akisoma katika shule ya wanajeshi (military academy ) mjini New York, ambako alianza kuwa kuwa becoming captain katika shule hiyo |
Mnamo mwaka 1995, Clinton akitoa hotuba kuhusu haki za wanawake kama mke wa rais mjini Beijing . Katika mwaka huo huo, Trump alikuwa katika ofisi ya soko la hisa la New York linalofahamika kama Trump Plaza Casino lililofahamika |
Clinton akigombea kwa mara ya kwanza mwaka 2008 - lakini alishindwa na Barack Obama katika uchaguzi wa awali wa Democratic : Donald Trump akiongoza kupindi cha televisheni - The Apprentice alichokiendesha kwa zaidi ya miaka 10 |
Mnamo mwaka 2011, Waziri wa Mashauri ya Kigeni akisoma ujumbe katika ndege alipokuwa akielekea Libya, picha iliyopata umaarufu , Trump akisikiliza watu mashuhuri wakimkejeli katika tukio la kukusanya misaada ya kijamii |
Wakati wa majira ya joto 2016: Clinton na Trumpwakikubali uteuzi wa vyama vyao kuwa rais. |
POLISI WATIMULIWA BAADA YA KUWACHARAZA WANAFUNZI WA KIKE KWA KOSA LA KUKATAA KUTOKA NAO KIMAPENZI.
Polisi wawili wanaodaiwa kuwapiga na kuwadhalilisha wanafunzi wa Sekondari ya Isuto mkoani Mbeya, wamefukuzwa kazi.
Askari hao ni wale waliokuwa wakisimamia mitihani ya kidato cha nne katika shule hiyo ambao inaelezwa kuwa waliwashambulia wanafunzi wa kike kwa bakora na adhabu nyingine.
Waliofukuzwa kazi kutokana na tuhuma hizo ni Konstebo Petro Magana wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya na Konstebo Lukas Ng’weina wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari amesema kuwa licha ya askari hao kufukuzwa kazi, watafikishwa mahakamani wakati wowote ili sheria ichukue mkondo wake.
Polisi hao wamekumbwa na kashfa ya kuwacharaza bakora na kuwapa adhabu nyingine wanafunzi wa kike wa shule hiyo, baada ya jaribio lao la kutaka kufanya ngono na mabinti wawili wa shule hiyo kushindikana.
Kidavashari amedai kuwa Novemba 4, saa 5:00 usiku, askari hao walituhumiwa kuwafanyia vitendo vibaya kinyume cha maadili wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
“Inadaiwa kuwa, askari hao kwa pamoja wakiwa kwenye ulinzi wa mitihani ya Taifa ya kidato cha nne waliwatoa kwenye hosteli wanafunzi wa kike kwa kile walichodai kupiga kelele, baada ya kuwatoa waliwapeleka eneo la kufoleni na kuanza kuwapa adhabu mbalimbali,” amedai kamanda huyo.
VYAMA VITATU VYA SIASA VYAFUTWA.
JAJI FRANCIS MUTUNGI |
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amevifutia usajili wa kudumu vyama vitatu vya siasa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutowasilisha ripoti za ukaguzi wa hesabu za fedha.
Sababu nyingine ni kutokuwa na ofisi na kushindwa kuthibitisha kuwa na wanachama Zanzibar
Amevitaja vyama hivyo ni Chama cha Haki na Ustawi (Chausta) kilichokuwa kinaongozwa na James Mapalala na The Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) kilichokuwa kinaongozwa na Peter Mziray kama Rais Mtendaji.
Chama kingine kilichofutiwa usajili ni Jahazi Asilia kilichokuwa kinaongozwa na Kassim Bakari kama Mwenyekiti taifa.
JOSEPH MUNGAI AFARIKI DUNIA.
MAREHEMU JOSEPH MUNGAI. |
Waziri na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa, Joseph Mungai (73) amefariki dunia baada ya kuugua ghafla.
Taarifa za kifo cha Mungai, zilianza kusambaa jana jioni majira ya saa 12 na baadaye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa kiongozi huyo wa zamani.
Aligaesha alisema Mungai hakuwa amelazwa hospitalini hapo, ila mwili wake ulipokelewa Idara ya Magonjwa ya Dharura na kuthibitishwa kuwa alifariki saa 11:20 jioni.
“Ni kweli tumepokea mwili wa Joseph Mungai katika idara yetu ya magonjwa ya dharura na kuthibitisha kifo saa 11:20jioni,” alisema Aligaesha. Aligaesha alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti Hospitali ya Taifa Muhimbili. Taarifa zaidi za chanzo cha kifo chake na mambo mengine, zitatolewa kesho.
Mungai alipata kuwa Waziri wa Kilimo katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na Waziri wa Elimu kwa vipindi viwili vya mwaka 1972-1975 na 1980-1982. Mungai pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa mwaka 1976-1980. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ambalo sasa ni ATCL.
Katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Joseph Mungai alipata kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni. Mungai alishiriki kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Mufindi, ambao umefanikiwa kusomesha watoto wengi wa wilaya ya Mufindi na hivi sasa vijana hao wanashika nyadhifa za juu serikalini, mashirika ya kimataifa na nje ya nchi.
Pia, Mungai alikuwa mstari wa mbele katika kuboresha kilimo na kuanzisha viwanda katika wilaya ya Mufindi, hatua ambayo imetatua tatizo la ajira kwa vijana wengi. Pia Mungai alishiriki kuanzisha Benki ya Wananchi wa Mufindi.
Kwa sasa Mufindi ni moja ya wilaya chache nchini, zilizopiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wa elimu, Mungai alisoma katika Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa, kisha kwenda Chuo cha Colorado na baadaye Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani kwa masomo zaidi. Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa. Jina la Bwana Lihimidiwe.
BALE MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA WALES.
BALE NA JOE ALLEN |
Winga wa timu ya taifa ya Wales ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Wales kwa mara ya nne mfululizo.
Bale mwenye umri wa miaka 27 kwa ujumla ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa nchi yake kwa mara sita.
Kiungo wa Stoke City Joe Allen ametwaa tuzo mbili tuzo ya wachezaji na tuzo ya washabiki, huku mchezaji wa timu ya Exeter City, Ethan Ampadu mwenye umri wa miaka 16 akitwaa tuzo ya chipukizi bora
ETHAN AMPADU, MCHEZAJI BORA CHIPUKIZI. |
Wachezaji wengine waliopata tuzo hizo ni kiungo Aaron Ramsey aliyepata tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya ulaya ya mwaka 2016.
Mshambuliaji Robson-Kanu akipata tuzo ya goli bora la michuano ya ulaya ya mwaka 2016, goli lililompa tuzo ni la mchezo wa robo fainali dhidi ya Ubelgiji.
Natasha Harding,amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwa upande wa Wanawake.
ALICHO TWEET RAIS MAGUFULI BAADA YA TRUMP KUTANGAZWA MSHINDI.
RAIS MAGUFULI |
''Congratulation President-Elect and people of America for a democratic election, I assure and people of Tanzania for a continued friendship''
TRUMP ASHINDA UCHAGUZI WA URAIS MAREKANI.
Donald Trump amemshinda Hillary Clinton katika matokeo ya uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkali.
Bi Clinton amempigia simu Bw Trump kumpongeza kwa ushindi wake.
Bw Trump alikuwa ameshinda majimbo mengi muhimu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda.
Alikuwa ameshinda Ohio, Florida, na North Carolina, ingawa Bi Clinton alishinda Virginia.
Kwa sasa Trump ana kura 265 za wajumbe na Clinton 218 kwa mujibu wa makadirio ya ABC News. Mshindi anahitaji kura 270 za wajumbe.
Lakini mgombea wa Republican Bw Trump ameshinda majimbo mengi ya kusini mwa Marekani naye Bi Clinton akashinda majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la ABC News.
Chama cha Republican pia kimehifadhi wingi wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.
Kama ilivyotarajiwa, Bw Trump ameshinda katika ngome za Republican katika majimbo ya Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana, West Virginia, Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas, ABC News wanakadiria.
Bw Trump pia anakadiriwa kushinda Arkansas, Kansas, North Dakota, South Dakota, Montana na Wyoming.
Shirika hilo linakadiria Bi Clinton atashinda ngome za Democratic majimbo ya New York, New Jersey, Connecticut, Massachusetts, Maryland, Vermont, Delaware, Illinois, Rhode Island na District of Columbia.
Mshindi anahitaji kupata kura 270 kati ya jumla ya kura 538 za wajumbe ndipo atangazwe mshindi.
Upigaji kura umemalizika katika majimbo 39 na matokeo kamili yalitarajiwa mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT Jumatano - Saa moja asubuhi Afrika Mashariki), upigaji kura utakaomalizika Pwani ya Magharibi.
Matukio mengine makuu:
- Bodi ya Uchaguzi Carolina Kaskazini imekubali kuongeza muda wa kupiga kura maeneo manane wilaya ya Durham ambapo kuna milolongo mirefu ya wapiga kura.
- Mgombea wa Republican aliyeshindwa kwenye mchujo Marco Rubio amehifadhi kiti chake cha useneta Florida
- Thamani ya pesa za Mexico, peso, imeshuka sana baada ya Trump kuonekana akiongoza Florida
- Mtu mmoja alifariki kwenye ufyatulianaji wa risasi karibu na kituo cha kupigia kura jimbo la Azusa, California. Watu watatu walijeruhiwa.
Bw Trump, tajiri kutoka Manhattan, na Bi Clinton, anayetaka kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani, walipiga kura mapema Jumanne katika jiji la New York.
Bw Trump alizomewa alipofika kupiga kura yake Manhattan, akiandamana na mkewe, Melania, na bintiye, Ivanka.
Wawili hao wamekuwa wakifuatilia matokeo kutoka jiji la New York.
Bi Clinton atahutubia wafuasi Javits Centre, Manhattan naye Bw Trump atahutubu katika hoteli ya Hilton Midtown.
Maafisa wa polisi zaidi ya 5,000 wametumwa jijini New York kuimarisha usalama.
Utafiti wa maoni wa baada ya upigaji kura, uliofanywa na ABC News, unaonyesha wapiga kura 61% hawampendi Bw Trump nao 54% ndio hawampendi Bi Clinton.
Mapema Jumanne, Bw Trump kwa mara nyingine alikataa kusema iwapo atakubali matokeo.
"Tutaangalia tuone vile mambo yatakuwa," aliambia Fox News, huku akidai kwamba kumekuwa na kasoro hapa na pale kwenye uchaguzi.
"Ninataka kila kitu kiwe wazi."
Katika baadhi ya vituo, mitambo ya kupigia kura ilifeli na kwingine kukawa na milolongo mirefu, lakini yalionekana kuwa matatizo ya kawaida.
Bw Trump, aliyezua utata kuhusu kuaminika kwa shughuli ya uchaguzi kwa kudai kura "zitaibwa" mapema, pia amewasilisha kesi ya dharura Nevada.
Maafisa wa Republican wamemshtaki msajili wa wapiga kura wilaya ya Clark, wakidai jimbo hilo lilifungua vituo vya kupigia kura muda mrefu kuliko inavyofaa.
Lakini jaji ameitupilia mbali kesi hiyo.
Kando na kura za urais, Wamarekani wamekuwa pia wakipiga kura za Maseneta, wabunge wa Bunge la Wawakilishi na Magavana.
Viti vyote 435 Bunge la Wawakilishi vilikuwa vinashindaniwa, na ABC News wanakadiria kwamba bunge hilo litabaki chini ya udhibiti wa Republican.
Lakini theluthi moja ya viti Seneti, ambao Republican wamekuwa wanaongoza, pia vinashindaniwa, na Democratic wanatumai wanaweza kudhibiti bunge hilo.
Jumla ya Wamarekani 45 milioni, idadi kubwa zaidi kuliko awali, walijitokeza kupiga kura mapema.
Bw Trump na Bi Clinton wanapigania kumrithi Barack Obama wa Democratic.
Rais Obama haruhusiwi kuwania kikatiba baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka minne.
Rais mpya ataapishwa tarehe 20 Januari 2017.
Subscribe to:
Posts (Atom)