Mwaka 1996, Melanija Knavs akiwa na miaka 26 aliingia Marekani akiwa na ndoto ya kuwa mwanamitindo. Jana, akiwa ni Melania Trump, alishika Biblia aliyotumia kuapa Rais wa 45 wa Marekani, Rais Donald Trump.
Ukiniuliza kama alidhani kuna siku angesimama Capitol Hill kwenye uapisho wa Rais kama Mke wa Rais wa Marekani, nitakwambia hapana. Lakini ndivyo Mungu alivyo. Leo hii huhitaji kumheshimu Melania Trump, ila utaheshimu mamlaka yake, na kwakuwa amekalia hicho kiti chenye mamlaka, utajikuta unamheshimu tu.
Unaweza kudhihaki historia yake, lafudhi yake au hata kazi aliyokuwa anafanya. Ila Mungu keshampa kibali cha kuwa hapo. Hata huyo Askari ukute alimpigia kura Hillary ila anajikuta akitii mamlaka ya Melania.
Kiongozi anaweza akatoka sehemu chakavu isiyo na tumaini. Chini, mwisho kabisa. Kumbuka hata Bwana Yesu alizaliwa katika zizi la ng'ombe. Mungu anaweza kumuinua mtu usiyemtarajia na kumfanya mtawala wako.
Mungu anaweza kukuinua wewe usiyejidhania na kukuweka mahali pa juu. Mipango Yake si kama yetu. Usidharau mtu yeyote na muhimu Usijidharau. Njia Zake si kama zetu.