Aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Faraja Nyalandu amemkingia kifua mshindi wa mwaka huu Diana Edward akisema hata yeye aliposhinda alizushiwa mambo mengi, lakini anashukuru kwa kuwa yalimjenga.
Katika waraka wake wenye maneno 223 aliouweka kwenye mtandao wa Instagram, mrembo huyo alisema alikaribishwa katika dunia ya umaarufu kwa kashfa lakini kwa msaada wazazi wake alifanikiwa kusimamia malengo yake.
Alimtaka Miss Tanzania afanye anachokiamini na kupuuzia maneno ya watu kwa sababu yanaweza kumtoa katika njia yake.
“Njia ya mafanikio ni ngumu, kwako Miss Tanzania wetu fanya kile unachokiamini, usikubali maneno haya ya watu yakuondoe katika mstari, kwa Watanzania wenzangu tujitahidi kuyaunga mkono yaliyo mazuri, tusibomoe…Tujenge,” alisema.
Akizungumzia ushindi wake, Diana alisema amejipanga kulitumikia vyema hasa kukomesha vitendo vya ukeketaji katika jamii ya Kimasai.
Tuesday, November 1, 2016
FARAJA NYARANDU AHAMASISHA WATANZANIA KUACHA KUMSEMA VIBAYA MISS TANZANIA 2016.
MWANAFUNZI ALIGONGA GARI LA POLISI KWA SABABU YA KUJIPIGA SELFIE.
TANZANIA KUSHIRIKI MASHINDANO INDIA.
UTAFITI:SUMU YA NYOKA NI DAWA YA KUMALIZA UCHUNGU.
Joka mwenye sumu kali zaidi duniani huenda akawa jibu la kupatikana dawa ya kupunguza uchungu. Hii ni kwa mujibu ya wanasayansi.
Joka anayejulikana kama 'Blue Coral' ndiye mwenye sumu kali zaidi na hupatikana zaizi Kusini Mashariki mwa Bara Asia. Utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida la afya la Toxin umepata joka huyo huwalenga maadui wake ambao husababisha uchungu kwa binadamu.
Wanasayansi wanasema huenda sumu hii ikatumika kutengeneza dawa ya uchungu. Baadhi ya wanyama ambao sumu yao imetumika kutengeneza dawa ni pamoja na konokono wa baharini na bui bui wa sumu.
Wanasayansi sasa wanataka joka huyu kuhifadhiwa hususan baada ya maeneo mengi anakopatikana kugeuzwa kuwa mashamba ya michikichi. Wanasayansi walifanya utafiti wao katika nchi za China, Singapore na Marekani.
Watafiti wanasema japo kwa mwanadamu nyoka huwa adui, lakini wakati huu huenda akawa suluhu la matatizo mengi ya kiafya.
MAGUFULI AMTAJA MPEMBA ANAYEHUSIKA NA UJANGILI HADHARANI.
Si kawaida kwa Rais kutaja jina, japo la utani, la mtuhumiwa.
Lakini ilikuwa hivyo kwa Rais John Magufuli alipomtaja mtu anayeitwa “Mpemba” akishangaa sababu za mamlaka za ulinzi na usalama kushindwa kumkamata kutokana na kudaiwa kuhusika kwake katika ujangili.
“Meno 50 maana yake ni tembo 25 wamekufa. Na zile operesheni nyingine zinazoendelea mpaka sasa, I hope (natumaini) mambo mengi yataonekana,” alisema Rais alipotembelea ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii Jumamosi na kukuta shehena ya meno ya tembo.
“Kwa hiyo kwa sababu operesheni bado inaendelea, nilitaka kujiridhisha tu na kuwaona watuhumiwa wenyewe. Kwa sababu hata hili jina la Mpemba limeshasikika sana na ningeshangaa sana kama mngeshindwa kumshika.”
Katika kuonyesha kuwa kazi nzuri imefanyika ya kumkamata mtu huyo, Rais aliwapongeza akiwahakikishia kuwa Serikali ipo na hivyo wamkamate mtu yeyote bila kujali cheo, utajiri wake wala umaarufu wake.
WAZAZI WA WANAFUNZI WALIOKOSA MIKOPO WALALAMIKA.
Baada ya kutangazwa mchakato wa uhakiki wa wanafunzi wanaonufaika na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliokosa mikopo wameelezea hali zao kiuchumi kwamba siyo nzuri.
Onesmo Mpinamafuja ambaye ni mzazi wa Rehema Onesmo anayesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema bodi inatakiwa kuhakiki wanafunzi wote kwa usahihi ili mwanaye aweze kunufaika na mkopo huo kwa kuwa hali ya kiuchumi nyumbani si nzuri.
“Bajeti ya mtoto tunayomtumia ni Sh10,000 na hapo atumie kwa muda wa mwezi mmoja. Si hela inayotosha ila ni hali halisi ya maisha ilivyo ngumu. Serikali itusaidie wazazi tumesomesha watoto kwa uwezo mdogo tulitegemea chuo majukumu yatapungua ila yameongezeka,” alisema Mpinamafuja.
Mpinamafuja alisema mahitaji ya binti yake ni makubwa tofauti na hali ya bajeti, hivyo aliitaka Serikali kuona namna ya kuwasaidia upya wanafunzi hao
MTIHANI WA KIDATO CHA NNE KUANZA LEO.
Watahiniwa 408,442 wamesajiliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne unaotarajia kuanza leo hadi Novemba 18, mwaka huu.
Akizungumzia maandalizi ya mtihani huo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wa shule ni 355,995 na wa kujitegemea ni 52,447. Mwaka 2015, waliosajiliwa kufanya mtihani ni 448,382, hivyo kuwapo na upungufu wa watahiniwa 39,940.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 355,447 waliosajiliwa, wavulana ni 173,423 ambao ni asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa na asilimia 51.28. Watahiniwa 59 ni wasioona na wenye uoni hafifu ni 283.
Alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447 waliosajiliwa, wanaume ni 25,529 sawa na asilimia 48.68 na wanawake ni 26,918 sawa na asilimia 51.32.
Pia watahiniwa wa kujitegemea wasioona wako saba, wanawake watatu na wanaume ni wanne. Mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa ni 54,317.
Kuhusu watahiniwa waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde alisema baraza limesajili 20,634 ambao wanaume ni 7,819 sawa na asilimia 37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11. Mwaka jana, idadi ya watahiniwa wa QT walikuwa 19,547.
“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” alieleza Dk Msonde.
Aidha, baraza limewaasa wanafunzi, walimu kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo yote.
Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi 238 kutoka shule sita walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu wa mtihani.
Dk Msonde alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. Pia Dk Msonde alitoa mwito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa Mitihani ya Taifa,” alieleza.
MCHINA ATAPELIWA MIL.22 NA KIJANA ALIYEJITAMBULISHA KWA JINA LA RC MAKONDA.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema Mkurugenzi wa Kampuni ya Group Six International, raia wa China, Jensen Hung (39) ametapeliwa zaidi ya Sh milioni 22 na mtu aliyejiita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Wakazi wa jijini humo na wageni wametahadharishwa kuwa makini.
Kwa mujibu wa Polisi, kumeibuka wimbi la wahalifu wanaotumia mbinu hususan majina ya viongozi wa serikali au watu mashuhuri na kujipatia fedha kwa njia ya kitapeli kinyume cha sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia zaidi majina ya viongozi haswa jina la Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kujipatia fedha.
“Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa raia wa kigeni kwamba kuna baadhi ya wahalifu wanaotumia vibaya jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa watoe kiasi cha fedha za kigeni na fedha za kitanzania kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo huko nchi za nje kama Ufilipino,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema katika tukio la kwanza lilitokea Oktoba mosi, raia wa China, Marco Li (24) ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Group Six International mkazi wa Mikocheni B alipigiwa simu na mtu asiyefahamika kwa namba 0719340914 akijitambulisha kuwa yeye ni Makonda akimtaka atoe kiasi cha Dola za Marekani 3,500.
Alisema fedha hizo alidai kwamba ni kwa ajili ya msaada wa kusomesha mwanafunzi, aliyechaguliwa Chuo Kikuu cha Manila kilichopo nchini Ufilipino, ambapo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Jensen Hung (39) pia mkazi wa Mikocheni B alikubali ombi hilo na kumtuma msaidizi wake aende kwa Makonda kwa ajili ya kujiridhisha.
"Alipofika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa hakuweza kuonana naye badala yake alipiga simu kwa namba tajwa hapo juu, ambapo mkuu wa mkoa feki alipokea simu na kumweleza kuwa yeye ana shughuli nyingi hivyo Oktoba 4, Marco Li alituma Sh 7, 595,000 kupitia benki,” alieleza Kamanda Sirro.
Alisema Oktoba 6, Jensen alitumia fursa hiyo kumuomba mkuu huyo wa mkoa bandia kwamba amsaidie kuongezwa muda wake wa kuishi nchini ambao ulikuwa umeisha na ndipo mtuhumiwa huyo akamtaka atoe kiasi Dola za Marekani 7,000 ambapo mlalamikaji alitoa kiasi cha Sh 15,260,000 kupitia akaunti ya Benki ya ECO.
Alisema Oktoba 25, mwaka huu mkuu huyo wa mkoa feki alimpigia simu mkurugenzi wa kampuni hiyo akimweleza kwamba suala lake la Uhamiaji limekamilika hivyo atoe Dola za Marekani 5,000 na ndipo walipogundua wametapeliwa baada ya kupiga simu kituo cha Polisi kuhakiki namba ya simu inayotumika kama ni ya Makonda na kujibiwa kuwa hiyo si namba yake.
Sirro alisema Agosti mosi mtu huyo alijaribu kumtapeli Kelvin Stander (54) raia wa Afrika Kusini akitumia namba 0719 340914, akijitambulisha kwamba ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiomba msaada wa Dola za Marekani 1,500 kama mchango wa kumpeleka mwanafunzi masomoni Chuo Kikuu cha Manila kilichopo Ufilipino.
Alisema tapeli huyo alitaka fedha hizo zitumwe kupitia akaunti namba 002345401590701 ya ECO benki ya Nairobi ikiwa na 'swift code' ECOTZTZ ,ndipo mlalamikaji akagundua haikuwa sahihi na kupiga simu iliyopo kwenye nyaraka iliyotumwa.
Alisema baada ya kupiga kupitia namba ya simu +25-257 56 04 iliyopo Ubalozi wa Ufilipino Nairobi na baada ya ufuatiliaji, waligundua kuwa taarifa zilizopo kwenye hati hiyo siyo sahihi.
“Agosti 4, mwaka huu mtuhumiwa alipigiwa simu na mlalamikaji kuwa taarifa zilizopo kwenye hati siyo sahihi lakini mtuhumiwa alisisitiza kwamba taarifa zipo sahihi na wao watume dola 1,500 na atatangaza kwenye vyombo vya habari siku itakayofuata kuwasifia kwa msaada waliojitolea,” alisema.
Aidha, alisema baada ya mlalamikaji kuwa na mashaka na watu hao, alipiga simu Polisi Kanda Maalumu na kuelezwa kwamba namba hiyo ya simu siyo ya mkuu wa mkoa halisi ndipo alipojiridhisha mtu huyo ni mdanganyifu.
“Wakazi wote wa Dar es Salaam wanapaswa kuwa makini na matapeli hao na wakiona dalili kama hizo wapige simu Polisi kwa msaada zaidi ili sheria ichukue mkondo wake,” alieleza Kamanda Sirro.
SCHWEINSTEIGER AREJEA KIKOSI CHA KWANZA MAN U.
Mshindi wa kombe la dunia 2014, Bastian Schweinsteiger amerudi katika mazoezi na kikosi cha kwanza cha Manchester united.
Kiungo huyo mwenye miaka 32 amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha wachezaji wa chini ya umri wa miaka 23 tangu Jose Mourinho alipoteuliwa kuwa kocha msimu huu.
Nahodha huyo wa zamani wa Ujerumani kwa mara ya mwisho aliichezea Man U mwezi Machi wakati Louis van Gaal alipokuwa kocha wa mashetani hao wekundu.
Alisema mwezi August kuwa hana tatizo binafsi na Mourinho na Man U itakuwa klabu yake ya mwisho kucheza barani Ulaya.