Monday, September 19, 2016

TANZIA: NGULI WA MUZIKI AFRIKA KUSINI MANDOZA AFARIKI DUNIA.

Mandoza

Nguli wa muziki nchini Afrika kusini Mduduzi Tshabalala maarufu kama Mandoza amefariki baada ya kuugua saratani kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amefariki dunia akiwa na miaka 38.

Mandoza alisifika kwa album kadhaa za mziki aina ya kwaito, aina ya mziki wa Afrika kusini ambao hukaribiana sana na Hip hop.

Nyimbo zake nyingi zilivuma zikiwemo nyimbo kutoka albamu yake ya kwanza Nkalkatha. Familia ya Mandoza imesema kuwa mwanamziki huyo aligundulika kuwa ana saratani baada ya kuanza kuumwa na kichwa sana pamoja na kutatizwa na macho mwaka mmoja uliopita.


RADI YAUA WATU NA WENGINE KUJERUHIWA SHINYANGA.

Kamanda Mkuu wa polisi mkoani Shinyanga Muliro Jumanne.

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa wamejikinga na mvua chini ya mti kando ya malambo ya kunyweshea mifugo katika kijiji cha Ntundu kata ya Busangi katika halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne alisema ajali hiyo ilitokea juzi 8:30 mchana katika kijiji hicho wakati mvua ilipokuwa ikinyesha, ndipo watu hao wakaamua kujikinga kwenye mti na radi ikapiga na kusababisha vifo vyao.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Fikiri Paschal (35) na Maneno Luzalia (16), wakati waliojeruhiwa na kupata mshituko baada ya radi kupiga ni watano ambao ni Mhoja Pasiani (32), Abel Feleshi (12), Nhungwa Jeremiah (22), Juma Mussa (16) na Paschal Mabula (11) ambaye ni mwanafunzi wa Ntundu.

Aliwataka wananchi kutokaa karibu na miti hasa kipindi hiki cha mvua za masika zinapokaribia kunyesha kwa wingi ili kuepuka tukio kama hilo ambalo limepoteza maisha ya watu, huku akifafanua kuwa katika mfumo wa umeme pia kuna madhara.


WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASISITIZA KUWA HALI YA UCHUMI KWA SASA NI SHWARI.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Serikali imesema hali ya uchumi kwa sasa ni shwari kabisa na inaendelea kuimarika, si mbaya kama inavyodhaniwa na kupotoshwa na baadhi ya watu.

Aidha imesema imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu, usimamizi thabiti wa raslimali za umma na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa pili wa maendeleo ya miaka mitano.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu alipokuwa akielezea mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini wakati akihairisha vikao vya bunge vya mkutano wa nne wa bunge la 11 lililoketi kwa wiki mbili kuanzia Septemba 6.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchumi, hususani mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa taifa, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wabunge na watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika.

Aliongeza kuwa tathimini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha inaonesha kuwa benki nchini zipo salama, zina mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha.