Wednesday, November 2, 2016
MSHINDI WA MAISHA PLUS ATATUMIA FEDHA ALIZOSHINDA KUSOMEA FILAMU NA KUSAIDIA WATOTO YATIMA NCHINI KENYA.
Mshindi wa Shindano la Maisha Plus msimu wa tano kutoka nchini Kenya, Olive Kiarie, amesema atatumia fedha alizoshinda kujifunza taaluma ya uandaaji wa filamu.
Akizungumza jana, Olive alisema mbali na kutumia fedha hizo kujifunza filamu, nyingine atazipeleka katika kituo cha kulelea watoto yatima nchini Kenya.
Olive alisema anashukuru kuibuka na ushindi, hivyo ni vema akarudisha shukrani kwa wale waliofanikisha mafaniko yake.
“Nashukuru, kuwa mshindi ni kitu kikubwa, hivyo nimekuja kutoa cheti, kuonyesha jinsi gani nimethamini mchango ulioonyeshwa na gazeti hili.
“Nilipanga kutoa fungu la 10 la fedha nitakazoshinda kwa watoto yatima nyumbani kwetu, hilo lazima nilitimize,” alisema Olive.
Olive alieleza kuwa Tanzania ni nchi yenye watu wakarimu wenye upendo, kupitia shindano hilo ameweza kujifunza mambo mengi.
TAIFA STARS KUKUTANA NA ZIMBAMBWE NOVEMBA 13.
Timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imepata mwaliko kutoka Chama cha Soka cha Zimbabwe (Zifa) wa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe Warriors utakaopigwa Novemba 13, mwaka huu jijini Harare.
Kikosi cha Taifa Stars kinachonolewa na kocha, Charles Mkwasa, hakijafanikiwa kucheza mechi ya kujipima nguvu tangu kilipochuana na Nigeria Agosti 3, mwaka huu katika mchezo wa mwisho wa Kundi G wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alithibitisha kupokea mwaliko huo na kudai kuwa mwishoni mwa wiki hii Mkwasa atatangaza kikosi kitakachoingia kambini kujiandaa na mchezo huo.
“Tumeukubali mwaliko wa kucheza nchini Zimbabwe Novemba 13, mwaka huu, hivyo kikosi kitakachotangazwa kitaingia kambini kuanza maandalizi kabla ya kwenda jijini Harare,” alisema.
Mchezo huo ni muhimu kwa Tanzania ambayo mwezi uliopita ilizidi kushuka katika ubora wa viwango vya Shirikisho la Kimataifa (Fifa) na kushika nafasi ya 114, huku Zimbabwe ikiwa nafasi ya 110.
Taifa Stars inakutana na Zimbabwe baada ya kushindwa kujipima nguvu na Ethiopia mwezi uliopita katika mchezo uliopangwa kwa mujibu wa kalenda ya Fifa kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea nchini humo.
Katika hatua nyingine, timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imeingia kambini jana kuanza mazoezi ya siku saba kabla ya kwenda Korea Kusini Novemba 8, mwaka huu kushiriki mashindano ya timu za vijana.
BUGANDO WAGUNDUA UGONJWA HATARI KWA WATOTO.
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (CUHAS), kimegundua kuwapo maambukizi ya bakteria mpya aina ya enterobacter bugandesis ambao huwaathiri watoto njiti na walio na umri chini ya mwezi mmoja.
CUHAS wanasema matibabu ya maambukizi hayo hugharimu Sh milioni 4.5.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Makamu Mkuu, Taaluma na Utafiti wa CUHAS, Profesa Stephen Mshana, alisema bakteria hao husababisha maambukizi ya ugonjwa (Neonatal Sepsis) ambao dalili zake ni kupata homa kali, degedege, kupumua kwa taabu na kushindwa kunyonya.
Alisema katika utafiti wao wamebaini asilimia tano ya watoto walio na umri chini ya mwezi mmoja ambao hutibiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) wameathiriwa na enterobacter bugandesis.
Alisema bakteria huyo husababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa muda sahihi na matumizi ya dawa yasiyoidhinishwa na daktari.
Profesa Mshana alisema bakteria hao ni sugu lakini hutibika ila matibabu yake ni ghali ambapo chupa moja ya dawa huuzwa kwa Sh 300,000 na mgonjwa huhitaji chupa 10 hadi 15 kwa matibabu ya siku saba.
“Dawa zinazotibu ugonjwa unaosababishwa na bakteria enterobacter bugandesis ni ghali na Watanzania wengi hawawezi kumudu. Chupa moja ya dawa inafika hadi Sh 300,000, mtoto akipatwa na tatizo hili kwa wiki moja anaweza kuhitaji chupa 10 hadi 15,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), Lucy Mogele, alisema katika kipindi cha mwaka 2015 walipokea watoto 240 walio na umri chini ya miezi miwili ambapo kati yao watoto 12 waligundulika kuwa na bakteria hao, mwaka huu tangu Januari hadi Oktoba wamepokea watoto 180 na watoto tisa wamebainika kuwa na maambukizi.
Akizungumzia mafanikio ya chuo hicho, Makamu Mkuu wa CUHAS, Profesa Paschalis Rugarabamu, alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003 kimetoa madaktari bingwa 111 kati yao wamo wa magonjwa ya akina mama, afya ya watoto, utabibu na upasuaji ingawa idadi hiyo haikidhi mahitaji ya taifa.
TANZANIA KATIKA NAFASI YA PILI AFRIKA MASHARIKI KWA KUTOA HUDUMA ZA KIFEDHA.
Tanzania imetajwa kuwa nchi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa huduma za kifedha kwa wateja wenye kipato cha kati na cha chini.
Taarifa zilizotolewa na Shirikisho la Asasi za Huduma za kifedha Tanzania (Tamfi) zinaeleza kuwa kwa Tanzania huduma za kifedha zinawafikia wananchi 3,800,000.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari leo, Mwenyekiti wa Tamfi, Joel Mwakitalu alisema Tanzania imeshika nafasi ya pili kati ya nchi tano za Umoja wa Afrika Mashariki.
Nchi ambazo zilikusanywa taarifa ni kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.
Nchi ya kwanza imetajwa kuwa ni Kenya ambayo inawafikia watu milioni nne kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa mwaka 2014 katika nchi zote za EAC huku Tanzania zikisimamiwa na Shirikisho la Asasi za Huduma za kifedha Tanzania (Tamfi).
Nchi ya kwanza imetajwa kuwa ni Kenya ambayo inawafikia watu milioni nne kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa mwaka 2014 katika nchi zote za EAC huku Tanzania zikisimamiwa na Shirikisho la Asasi za Huduma za kifedha Tanzania (Tamfi).
Mwakitalu alisema kinachosababisha huduma za kifedha kutowafikia wateja wengi ni miundombinu kushindwa kuwafikia walio vijijini.
"Tumekutana na wenzetu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India kujadili ni namna gani huduma za kifedha zitawafikia wananchi wengi kupitia vikundi vidogovidogo kama Vicoba na vinginevyo kwakuwa vinawagusa sana wananchi wenye kipato kidogo," amesema Mwakitalu
BONDIA MASHALI APUMZISHWA KATIKA MAKAO YAKE YA MILELE (MAKABURI YA KINONDONI).
Pumzika kwa amani Thomas Mashali.
MBOGA YA MCHICHA YAGUNDUA BOMU.
Wanasayansi wameweza kuifanya mboga ya aina ya Mchicha au 'Spinach' kugundua bomu.
Imearifiwa kwamba majani ya mchicha yanaweza kuhifadhi kemikali aina ya 'nitro-aromatics' ambazo hupatikana kwenye mabomu ya kutegwa arthini na silaha zinazozikwa arthini.
Siyo lazima mboga hii iwekwe nyaya yeyote ili kuweza kugundua bomu, bali mmoja anaweza kufahamu kwa kutizama au kwa taarifa maalum za simu.Utafiti huu umefanikishwa na Chuo Ki Kuu cha Massachusetts Institute of Technology-MIT.
Wanasayansi waliweka kemikali za carboni kwenye maji na kisha kufanya mizizi ya mboga kupitisha maji yale hadi kwenye matawi ya mchicha. Kisha wanasayansi wakapapasa majani ya mchicha na vyuma maalum.Majani yale yalianza kutoa chembechembe za moto ambazo zinaweza kuonekana kwa kopyuta.
Pia chembechembe hizo zinaweza kuonekana kwa simu ya mkononi. Wanasayansi sasa wanasema mboga ya mchicha pia inaweza kutumika kufahamu uwepo wa visima vya maji arthini, kemikali zilizovuja kutoka kwa silaha na madini ya nitro-aromatics. kwa sasa wananuia kuwezesha mboga hiyo kuweza kugundua bomu iliyotegwaa arthini kwa kwa mbali.
CHRISTIAN BELLA ATOA YA MOYONI.
King of the Best Melodies CHRISTIAN BELLA amefunguka kuwa hana shobo na collabo za kimataifa. "Kuna idea ambazo nazifanyia process, lakini bado zijaanza process yoyote kuhusu collabo ya kimataifa. Na mimi kila siku huwaga sina haraka, najua kila kitu kina wakati wake na kama nikiamua kufanya collabo nitatangaza. Na sina presha pia ya collabo yoyote ya nje. Nachokuwa na presha nacho ni kutengeneza ngoma zinazokubalika nyumbani namaanisha Tanzania, East Africa kwa ujumla na Kongo," amesikika Bella katika kipengele cha PIGIA MSTARI kinachosikika kupitia Kipindi cha THE SPLASH kinachorushwa na Ebony FM ya Iringa.
Katika hatua nyingine Christian Bella amezungumzia siri kubwa ya yeye kuwa na mashabiki wengi na ambao wanaongezeka kila siku. "Kikubwa msanii unatakiwa kuwa mtu wa watu," anasema. "Unatakiwa kuwa na discipline ya kazi. Pia unatakiwa kuwa mbunifu na mimi kinachonifanya niwe karibu na mashabiki wangu na kuongeza mashabiki wapya kila siku ni uwezo wangu wa kazi na kikubwa Mungu anampa kila mtu nyota kwahiyo hiyo nyota niliyopewa ina mchango mkubwa wa mimi kupendwa na watu," ameeleza Bella.
Kuhusu Malaika Band, muimbaji huyo anasema, "Ujue Amerudi nimetoa mwaka jana. Unajua kitu ambacho kinawafelisha wasanii wa bendi nikuunganisha nyimbo ambazo hazifanyi vizuri lakini unaunganisha tu. Unajua kama umetoa wimbo wa bendi inabidi uiachie time ili ufanye vizuri. Wimbo kama amerudi bado una nafasi kubwa sana na bado mkubwa sana, sina haraka ya kutoa wimbo na bendi labda mwaka kesho, sisi hatufanyi mashindano."
MKE WA LEMA AFIKISHWA MAHAKAMANI.
Mke wa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema, amefikishwa mahakamani leo kwa tuhuma za kumtusi Mkuu wa Mkoa kwa kumtumia ujumbe wa simu wenye neno ‘shoga’. Mke wa Mbunge huyo amekana kumtusi Mkuu huyo wa Mkoa, amedai neno ‘shoga’ sio tusi bali ni neno ambalo hulitumia kuwaita marafiki zake.
KESI YA SCORPION YASOGEZWA MBELE.
Kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili Salum Njwete ‘Scorpion’ imeahirishwa hadi Novemba 16, mwaka huu itakapotajwa tena.
Kesi hiyo iliyopo Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeahirishwa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Flora Haule baada ya upande wa mashtaka kudai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
“Mheshimiwa Hakimu, mshtakiwa yupo mbele ya mahakama yako ila tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa sababu upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika"alidai Wakili wa Serikali Chesensi Gavyole.
Kutokana na maombi hayo, Hakimu Haule alikubaliana na kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
MOYES APIGWA MARUFUKU KUCHEZA MECHI MOJA.
Meneja wa Sunderland David Moyes amepigwa marufuku mechi moja na chama cha soka cha England kwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya mwamuzi wa mechi.
Aidha, amepigwa faini ya £8,000.
Kisa hicho kilitokea baada ya refa kunyima Sunderland mkwaju wa penalti dakika ya 90 mechi ya Jumatano wiki iliyopita ambapo klabu hiyo ilishindwa 1-0 na Southamptn Kombe la FA.
Baada ya mechi hiyo, Moyes alisema: "Tatizo lilitokea aliponiandama hadi pahala nilipokuwa nimesimama. Nilitumia lugha ya matusi na sikufaa kufanya hivyo."
Sunderland watacheza na Bournemouth Ligi ya Premia Jumamosi.
Moyes aliteuliwa meneja wa Sunderland Julai na ameshinda alama mbili pekee kutoka kwa mechi 10 ligini.
MADINI MAPYA YAMEGUNDULIWA NCHINI.
Madini mapya yamegunduliwa nchini, katika eneo lenye madini ya kipekee la Manyara, na kupewa jina Merelaniite.
Jina hilo limetokana na eneo ambalo madini hayo yalipatikana, Merelani (Mererani) katika milima ya Lelatema katika wilaya ya Simanjiro katika eneo la Manyara.
Eneo hilo linafahamika sana kwa madini ya Tanzanite.
Madini hayo yaligunduliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Michigan cha Marekani, makavazi ya historia asilia ya London, chuo kikuu cha Di Firenze cha Italia na makavazi ya historia asilia ya Smithsonian ya Washington.
Wataalamu sita waliofanya uchunguzi, kwenye makala iliyochapishwa kwenye jarida la Minerals (Madini) wanasema madini hayo yana vipande vinavyofanana na sharubu vya rangi ya kijivu vya urefu wa milimita moja hivi, ingawa kuna baadhi vyenye urefu wa hadi mililita 12.
Kipenyo cha vipande hivyo ni mikrometa kadha.
Madini hayo yanakaribiana na madini ya zoisite (aina ya tanzanite), prehnite, stilbite, chabazite, tremolite, diopside, quartz, calcite, graphite, alabandite na wurtzite.
"Madini haya mapya yametambuliwa na taasisi inayoyapa majina madini, IMA CNMNC (2016-042), na kupewa jina linalotokana na eneo yalipogunduliwa kwa heshima ya wachimba migodi wa eneo hilo wa zamani, wanaoishi na wanaofanya kazi," makala ya wataalamu hayo inasema.
"Wilaya ya Merelani imekuwa maarufu tangu mwishoni mwa miaka ya 1960 kutokana na aina ya madini ya thamani ya rangi ya samawati kwa jina zoisite yafahamikayo kama tanzanite, lakini ni eneo muhimu sana kwa wanaotafuta madini ya kipekee na ni eneo la kusisimua sana kutafuta madini mapya," John Jaszczak, mwanafizikia katika Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Michigan, na aliyeongoza katika kuandika makala kuhusu ugunduzi wa madini hayo anasema.
Madini hayo yalitambuliwa mara ya kwanza mwaka 2012 na Simon Harrison na Michael Wise, bila wataalamu hao kuyafahamu vyema, pale walipogundua vitu vilivyoonekana kama nyaya ndogo zilizokuwa zimedunga na kuingia ndani ya vipande vya madini ya chabazite.
Baadaye uchunguzi zaidi ulifanywa na ikagunduliwa kwamba yalikuwa madini tofauti.
CHUO CHA MAKERERE CHAFUNGWA KUTOKANA NA MGOMO.
Wanafunzi wameanza kuondoka kutoka Chuo Kikuu cha Makerere baada ya Rais Yoweri Museveni kutangaza kifungwe mara moja Jumanne jioni.
Rais alisema amechukua hatua hiyo "kuhakikisha usalama wa watu na mali."
Chuo kikuu hicho kilikuwa kimekumbwa na vurugu kutokana na mgomo wa wahadhiri na wanafunzi.
Chama cha wahadhiri Jumatatu kiliamua kuendelea na mgomo hadi wahadhiri walipwe marupurupu ya miezi minane ambayo yamefikia Sh32bn (dola 9.2 milioni za Marekani).
Wanafunzi walijiunga na mgomo Jumanne, na walitaka kukutana na Rais Museveni badala ya mwenyekiti wa baraza simamizi ya chuo chini ya uenyekiti wa Dkt Charles Wana-Etym.
Naibu chansela wa chuo hicho Prof Ddumba Ssentamu wiki iliyopita alikuwa amewasihi wahadhiri wakubali kurejea kazini huku suluhu ya kudumu ikiendelea kutafutwa.
IDADI YA WATUMISHI HEWA KUFIKIA 19,629.
ANGELINA KAIRUKI.
Watumishi hewa 19,629 wamebainika kuwapo nchini tangu uhakiki ufanyike; na kama wangelipwa, serikali ingepoteza Sh bilioni 19.7 kwa mwezi.
Aidha, kutokana na hali hiyo, serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi 1,663 kutoka katika taasisi zake kwa watumishi waliohusika na kuwepo kwa watumishi hewa na kati ya hizo, watumishi 638 wamefunguliwa mashtaka polisi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema bungeni mjini hapa jana kuwa serikali ingepata hasara hiyo, endapo watumishi hao hewa wangelipwa kwa mwezi.
Akitoa mfano wa halmashauri mbili, Kairuki alisema Kinondoni imekutwa na watumishi hewa 107 na kama wangelipwa ingepoteza Sh bilioni 1.279 na kwa Halmashauri ya Kishapu waligundulika 73 na wangelipwa Sh milioni 543.
Kairuki alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Maida Hamad Abdallah (CCM) aliyetaka kujua hasara serikali imeipata kwa kuwalipa watumishi hewa na adhabu kwa waliohusika na suala hilo.
Alisema, “Hadi sasa watumishi hewa 19,629 wamebainika na kama wangelipwa, kwa mwezi wangeingiza hasara ya Sh 19,749,737,180. Kuhusu adhabu na kurejesha fedha, Kairuki alisema mahakama imekuwa ikitekeleza majukumu yake na kuwatoza faini na wengine kutakiwa kurejesha fedha.
Awali, akijibu swali la msingi la Abdallah aliyetaka kujua serikali inasema nini juu ya wale wote waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo ya watumishi hewa, huku waliohusika wengi wakiwa ni maofisa na watumishi wa serikali, Kairuki alisema hadi Oktoba 25 mwaka huu serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi 1,663.
Kairuki alisema watumishi hao ni kutoka katika wizara, idara zinazojitegemea, wakala wa serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ambao walibainika kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa na 638 kati yao wamefunguliwa mashitaka polisi.
Akitoa mchanganuo, Kairuki alisema idadi ya watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu katika wizara ni 16, idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali ni tisa, Sekretarieti za mikoa sita na Mamlaka ya Serikali za Mitaa 1,632 wanaofanya idadi ya watumishi 1,663 waliochukuliwa hatua.
“Hatua hii inajumuisha kuwasilishwa kwa masuala yanayowahusu baadhi ya watumishi hawa katika vyombo na ulinzi na usalama na hadi kufikia tarehe 25.10.2016, watumishi 638 mashitaka yako polisi, 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na watumishi 975 mashtaka yao yamefikishwa kwenye mamlaka zao za kinidhamu,” alisema Kairuki.
Alisema sambamba na hatua hiyo, serikali inaendesha ukaguzi wa mara kwa mara wa Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (HCMIS) na maofisa wanaobainika kuhusika au kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika taasisi na mamlaka zao, huchukuliwa hatua za kinidhamu, kama vile kuwafungia dhamana na uwezo wa kuingia na kufanya kazi katika mfumo huo.
NAPE AWAPA MAKAVU YANGA.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO, NAPE NNAUYE.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kuwa Yanga haikufuata taratibu katika mchakato wake wa kubadili umiliki kwani hata Mkutano Mkuu wa wanachama uliendeshwa kienyeji.
Mbali na hilo, Nape pia alisema kuwa kabla ya kuhitimisha mkutano huo wa wanachama, uongozi wa Yanga ulitakiwa kutoa notisi ya siku 60 kwa wanachama wake kama Katiba yao inavyoagiza.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma katika kipindi cha radio moja, Nape alisema kuwa Serikali inajua kuwa Manji hafanyi kazi na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Alisema pamoja na kupitwa na wakati kwa sera ya michezo, lakini wadau wamekuwa wakisuasua kutoa mapendekezo ya marekebisho yake ili iweze kuendana na wakati.
“Mkutano ulioitishwa kwanza hakufuata taratibu, walitakiwa kutoa notisi ya siku 60 kwa wanachama wake, lakini hawakufanya hivyo, Serikali tunajua Manji hafanyi kazi na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji,”alisema.
Alisema kuwa sera ya michezo ina mapungufu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuondoa manung’uniko kwa washika dau, ambao ni klabu za michezo na wanamichezo ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilalamikia sera ya michezo kupitwa na wakati.
Wadau hao hususani wa soka wamekuwa wakilitupia lawama Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuwa ni mzigo kwani imekuwa ikipata mgao kwa kila mchezo wa ligi wa asilimia tano ya mapato, huku likiwa halitoi msaada kwa timu za taifa zaidi ya kukabidhi bendera pindi zinapoenda kwenye michuano ya kimataifa.
Hatahivyo, akizungumzia hilo, Nape alisema, “Mapungufu kwenye baraza yapo lakini hayaondoi umuhimu wa baraza kuwepo kwa sasa kwa vile ndio wanaosajili na kusimamia masuala yote ya michezo, kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa na baraza na si kweli kuwa halifai kwa kile kitu.” “BMT imekuwa ikifanya mambo mazuri, inawezekana mtu ambaye hajahitaji huduma ya baraza hawezi kujua umuhimu wake, dunia inabadilika sioni shida kufanya mabadiliko lakini sio kulitupia mawe baraza,”alisema.
Kauli ya Nape imekuwa ikiwa ni siku chache baada ya BMT kuzuia klabu za Simba na Yanga kuendelea na mchakato wake wa mabadiliko ya umiliki hadi pale zitakapobadili katiba zake.
Kwa upande wa katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema sera ya baraza ya mwaka 71 haliendani kwa matakwa ya sasa kwa yanayoendelea ndani ya klabu za michezo.
“Soka letu la kulipwa, ngumi za kulipwa, mpira wa miguu Fifa imetoa maelekezo na katiba za mfano kwa wanachama wake na haitambui baraza kama chombo cha maamuzi ya juu. Licha ya Fifa kuitambua serikali lakini haipi kipaumbele kwenye maamuzi baraza likae chini liangalie nafasi yake kama litaendelea na majukmu yale yale au yabadilishwe,”alisema Osiah.
Hata hivyo, aliwataka watendaji wa Baraza kukaa chini na kujitafakari iwapo nguvu wanayotumia kwa wakati huu bado wanastahili kwani kuzuia mchakato wa mabadiliko kwenye klabu za Simba na Yanga si sahihi.
Wakati Osiah akisema hayo, Mwenyekiti wa zamani wa Simba na ambaye ia amewahi kuwa katibu mkuu wa FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage alisema “BMT ipo sahihi na ina umuhimu mkubwa na kuzitaka klabu za michezo hususani Simba na Yanga kuheshimu maamuzi ya baraza hilo.
“Kusipokuwa na chombo cha juu kama BMT kusimamia michezo itakuwa vurugu mechi kwenye nchi yetu na inaweza kutugawa, mfano mtu anaweza kuanzisha timu yake ya Wanyamwezi Football klabu akasema wanaocheza ni Wanyamwezi tu, hiyo ni hatari lakini baraza halina udini hivyo bado lina umuhimu mkubwa,”alisema.
VYUO VIKUU 15 MATATANI.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi |
Serikali imetoa siku mbili kwa vyuo vikuu 15, kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ya wanafunzi wanufaika na mikopo wanaoendelea na masomo ili kupangiwa mikopo kwa mwaka wa 2016/2017.
Vyuo hivyo vilivyokuwa viwasilishe matokeo hayo siku 30 kabla ya kufunguliwa, vimepewa siku hizo kuanzia jana, kabla serikali haijachukua hatua zozote.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi alisema hayo jana, alipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Alisema serikali iko katika hatua za mwisho za upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Tarishi alisema baadhi ya vyuo vimeshindwa kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wanaoendelea ili wapangiwe mikopo kwa mwaka unaoendelea, kwani utaratibu lazima vyuo kuwasilisha matokeo kuonesha wanafunzi wangapi wana sifa za kuendelea kupewa mikopo.
“Mikopo haiwezi kutolewa tu kwa kila mwanafunzi, hata kama ameamua kuacha masomo, hivyo vyuo vina wajibu wa kuthibitisha kuwa wanafunzi wanaowaleta bado ni wanafunzi sahihi na wanaendelea na masomo,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Alivitaja vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo hayo kuwa ni Vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha St. John Kituo cha St Mark Dar es Salaam (SJUTDSM), Chuo cha St. John Tanzania (SJUT) na Chuo Kikuu cha Tumaini Mbeya (TUMAMBEYA).
Vingine ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI), Chuo cha United African University of Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Tiba ya Sayansi (STJCAHS), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Kituo cha Makambako na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).
Katibu Mkuu huyo pia alitaka vyuo hivyo kuimarisha mifumo yao ya kuandaa na kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wakati na kwa ukamilifu katika siku zijazo ili kuondoa usumbufu. Akizungumzia hatua watakazochukua wasipotimiza agizo hilo, alisema wanawaagiza kutekeleza maagizo hayo kwa siku walizopewa.
Alisema ana uhakika kauli hiyo inawatosha waungwana hao, kutimiza wajibu wao.
Awali vyuo vyote vya elimu ya juu, vilikumbushwa umuhimu wa kuwasilisha matokeo, kabla havijafunguliwa, ikiwemo serikali kufanya mkutano na Makamu Wakuu wa vyuo vyote vya elimu ya juu mkoani Dodoma na kusisitiza umuhimu wa vyuo kuwasilisha matokeo na nyaraka nyingine muhimu, kabla ya vyuo kufunguliwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kikamilifu na imetenga fedha za kutosha na tayari imetoa Sh bilioni 80.89 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, wanaonufaika na mikopo hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka.
Alisema kati ya kiasi hicho, tayari Sh bilioni 45.2 zimekwishalipwa na kiasi kilichosalia, kitalipwa kwa vyuo baada ya kupokea matokeo kikamilifu. Pia aliwatoa wasiwasi wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokosa mikopo, kupeleka malalamiko katika dirisha maalum la malalamiko, lililofunguliwa na Bodi ya Mikopo kuanzia juzi na serikali ni sikivu, itafanyia kazi.
Katika siku za hivi karibuni, wanafunzi wa elimu ya juu katika vyuo mbalimbali wanaoendelea na masomo, wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kwa mikopo ya elimu ya juu ; huku wanaoanza mwaka wa kwanza, wakilalamikia kukosa mikopo hiyo.
Imeelezwa kuwa baada ya kufanyika uchambuzi, wanafunzi 20,183 wanaoanza mwaka wa kwanza katika vyuo mbalimbali wamepatiwa mikopo; huku wakitarajia kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema serikali kwa sasa inaandaa taarifa kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na ikishakamilika itawasilisha bungeni, kama walivyoomba wabunge.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kujibu mwongozo uliotolewa na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola (CCM) kuomba mwongozo bungeni, akitaka leo serikali ilete taarifa kuhusu mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo, kwa kile alichoeleza kuwa wanafunzi wengi walioomba mikopo wakiwa na vigezo, hawajapata. Jenista alisema kwa sasa serikali inaandaa taarifa hiyo na ikikamilika, italetwa bungeni kama wabunge walivyoomba.
Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali pamoja na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itadhibiti utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo pekee, ndio wananufaika kwa mikopo hiyo.
Awali, Mhagama alisema serikali haifanyi kazi kwa miujiza, bali kwa kutumia mgangilio wa bajeti iliyowekwa na uthibitisho kwamba serikali inafanya kazi kwa mipango, imeweza kutekeleza kutoa elimu bure ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mhagama alitoa kauli hiyo baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Free Mbowe (Chadema) kuuliza swali la nyongeza lililotokana na swali la msingi la Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (CCM) kutaka kujua Serikali itaanza kutekeleza lini ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na akina mama.
Akifafanua zaidi, alisema kamwe serikali haijiendeshi kwa miujiza bali kwa kutumia mipango iliyojiwekea katika bajeti zake.
“Kuthibitisha jambo hili linatekelezeka, Serikali ya CCM kupitia Ilani yake tumeweza kutoa elimu bure, kuwashangaza Watanzania miradi mikubwa mbalimbali imetekelezwa ikiwemo kununua ndege (mbili za Dash 8, Q400 zilizotengenezwa na Bombardier), Ilani inatekelezwa kwa mambo mengi mbalimbali,” alisema akimjibu swali la nyongeza Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) kuhusu Sh milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji nchini.
Jenista alisema fedha zote zinazoahidiwa na serikali zikiwemo Sh milioni 50, zitatolewa na Watanzania watazipata.
Imeandikwa na Gloria Tesha, Dodoma na Theopista Nsanzugwanko, Dar.
ARSENAL WAPANDA KWENYE CHATI.
Mesut Ozil alifunga bao la dakika za mwisho na kuwawezesha Arsenal kutoka nyuma 2-0 na kulaza Ludogorets Razgrad ya Bulgaria na kuwafikisha hatua ya mondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Ozil alionekana kutulia alipokimbia langoni, akampiga chenga kipa na mabeki wawili na kisha akatumbukiza mpira kimiani.
Awali, matumaini ya Arsenal kurudia ushindi wao mkubwa wa 6-0 mechi ya kwanza yalizimwa Jonathan Cafu alipowaweka Ludogorets mbele baada ya frikiki ya Wanderson.
Cafu alisaidia ufungaji wa pili alipomzidi ujanja Kieran Gibbs na kumpa mpira Claudiu Keseru aliyefunga na kuwashangaza Arsenal.
Granit Xhaka aliokoa jahazi upande wa Arsenal kwa kombora la kutoka hatua 15 kutoka kwa goli baada ya kupokea krosi kutoka Ozil na kufufua matumaini ya Arsenal kwa bao moja.
Olivier Giroud naye alifunga kwa kichwa kutoka kwa mpira uliotoka kwa Aaron Ramsey na kusawazisha.
Kipa wa Arsenal David Ospina alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira mara mbili kutoka kwa Wanderson kabla ya Ozil kufunga.
Arsenal sasa wamefika hatua ya 16 bora na wameendeleza msururu wao wa kutoshindwa hadi mechi 15.
MATOKEO Kamili: Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya
KUNDI A
Basel 1-2 Paris Saint Germain
Ludo Razgd 2-3 Arsenal
KUNDI B
Besiktas 1-1 Napoli
Benfica 1-0 Dynamo Kiev
KUNDI C
Bor Monchengladbach 1-1 Celtic
Manchester City 3-1 Barcelona
KUNDI D
Atletico Madrid 2-1 FC Rostov
PSV Eindhoven 1-2 Bayern Munich
Subscribe to:
Posts (Atom)