Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itawapoka mikopo baadhi ya wanafunzi ambao uhakiki utawabaini kuwa hawakuwa wanastahili kupewa mikopo waliyokopeshwa. Utaratibu huo utawagusa wanafunzi wapya na wale wanaoendelea na masomo baada ya bodi kufanya uhakiki na uchunguzi wa taarifa za wanufaika wote wa mikopo. Uchunguzi huo unaanza kesho.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru alisema wanafunzi watakaokutwa na hadhi zisizostahili wataondokewa na sifa za kuendelea kupata mikopo na kulazimika kurejesha kiasi cha fedha watakachokuwa wamepokea tayari. Alifafanua kuwa kiasi cha fedha ambacho watalazimika kurejesha wanafunzi ambao watakutwa hawana uhitaji ni fedha walizochukua kuanzia Novemba mwaka huu.
“Kwa kweli tukikuta mtu ambaye anapata mkopo na hana uhitaji kwa kweli tutamnyang’anya mkopo ili apate mtu mwingine mwenye uhitaji,” alisema Badru.
Uamuzi huo wa bodi wa kutangaza kuwapoka mikopo baadhi ya wanafunzi ni wa kwanza kufanywa na chombo hicho ambacho mara kwa mara kimekuwa kinatoa mikopo kwa kufuata sera za serikali.
Miaka ya nyuma wanufaika wa mikopo hiyo walikuwa ni wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili bila kujali familia wanazotoka. Lakini mwaka huu, serikali imetangaza kuwa sera ya mikopo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya vipaumbele vya taifa na uyatima, ulemavu, ualimu wa sayansi na hisabati, sayansi ya tiba na afya, sayansi asilia, sayansi ya ardhi, usanifu majengo na miundombinu na uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo na gesi asilia na mabadiliko ya tabianchi.
Badru katika maelezo yake, alifafanua kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wote wanahakikiwa, bodi hiyo imeandaa dodoso ambalo litawekwa kwenye tovuti ya bodi hiyo na wanafunzi wote ambao wananufaika na mkopo wa bodi ni lazima wajaze taarifa za kiuchumi za wazazi na walezi wao.
Alipoulizwa kwa nini wanafunzi wanaoendelea na masomo wapokwe mikopo wakati waliomba kwa kutumia masharti yaliyowekwa kwa wakati huo, Badru alisema kwamba bodi yake haileti masharti wala mwongozo mpya, bali umekuwepo miaka yote.
“Mwongozo tunaoutumia ni sawa na ule uliotumika mwaka jana, ila kama bodi ni lazima tufanye uhakiki ili kuboresha taarifa zetu ili iwe rahisi kuwadumia,” alisema mkurugenzi huyo mtendaji na kusititiza kuwa wanafunzi wasio na uhitaji wa mikopo lazima waondolewe mikopo hiyo.
Mikopo ni kwa watoto wa maskini Akizungumzia vigezo ambavyo bodi yao imevifuata mwaka huu katika utoaji wa mikopo, Badru alisema kwamba walengwa zaidi ni watoto wenye uhitaji mkubwa hasa watoto wa wakulima ambao wengi wao ni maskini. Alifafanua kuwa katika kuwabaini hao, bodi hiyo imepitia wanufaika wote wa mikopo na shule za sekondari walizosoma pamoja na ada ya mwisho aliyolipa mwanafunzi huyo wakati akiwa kidato cha sita.
“Tuna orodha ya shule zote na ada zao, sasa ili kubaini wahitaji tunaangalia alikosoma mwanafunzi huyo na ada aliyokuwa analipa, hii inatusaidia kuwapata watoto wa wakulima na maskini ili waweze kunufaika na mikopo hii ya serikali,” alisema Badru.
Alifafanua kuwa kuna wanafunzi ambao walikuwa wanasoma kwa ufadhili wa mashirika ya dini au ya mtu binafsi hao nao watawafikiria katika kuwapatia mikopo kwa kuwa taarifa zao wamezijaza kwenye fomu kuonesha aliyekuwa anamlipia ada.
Alisema pia kwamba watoto yatima ambao wamefiwa na wazazi wao nao ni walengwa wengine katika mikopo waliyoitoa.
Alisema wanufaika wengine ni wale ambao wanasoma masomo ya kipaumbele cha taifa. Waliopangiwa mikopo Badru alisema baada ya uchambuzi wanafunzi 20,183 wamepatiwa mikopo ambao wanasoma mwaka wa kwanza na wanafunzi 93,295 ambao wana sifa mbalimbali.
Alisema wanafunzi wengine wenye sifa ambao maombi yao yana kasoro bado wanaendelea kupokea maombi yao yenye marekebisho na watawapatia mkopo.
Mtendaji huyo wa Bodi alisema wanafunzi ambao hawakuridhika na uamuzi wa bodi wanaruhusiwa kukata rufaa ndani ya siku 90.
Alisema bodi yake itashughulikia rufaa hizo ndani ya muda huo ili mwombaji ajue hatima yake. Badru alisema asilimia 90 ya wanafunzi waliomba mkopo wameshapatiwa mkopo na majina yao yamewekwa kwenye tovuti ya bodi hiyo. Kuhusu kiasi ambacho mwanafunzi amepata, alisema wanafunzi watafahamu asilimia waliyopata baada ya kwenda chuoni na kuletewa stakabadhi ya malipo iliyofanywa na bodi kwa chuo husika.
“Kwenye ile orodha hatujaonesha kiwango cha asilimia, ila kiasi hicho kimeoneshwa kwenye pay list tuliyotuma chuoni. Tunapeleka orodha hiyo kwa awamu,” alisema Badru. Pia alisema kwamba wanafunzi ambao hawakujumuishwa katika uchujaji wa mikopo ni wanafunzi 27,053.
Katika orodha hiyo kuna wadahiliwa 6,581 hawakuomba, wadahiliwa 8,781 ni wahitimu binafsi, wadahiliwa 9,940 wamefuzu kwa vigezo ainishi, wadahiliwa 1,416 ni wale ambao waliomba mkopo wakashindwa kurekebisha taarifa zao licha ya kupewa fursa ya kufanya hivyo.
Kwenye orodha hiyo wamo wadahiliwa walioomba mkopo lakini wamehitimu kidato cha sita miaka mitatu iliyopita idadi yao ni 245 na waliomba mkopo wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 30 ni 27,053.