Mtoto Devotha Lucanus Nagaikaya, anayeishi na shangazi yake katika mtaa wa Togo, kata ya Mahenge Mjini, wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro ana umri wa miaka minne, lakini muda wote hubaki amelala kitandani.
Mtoto huyu hawezi kukaa, akacheza wala kutembea na shingo yake imelegea, mikono imekakamaa hivyo inawalazimu walezi wake kumlisha siku zote.
Wakati wote mtoto huyo analazimika kuwa na mwangalizi kwani anapojisaidia huhitaji kubadilishiwa nguo na kufuliwa.
Mtoto huyu analelewa na shangazi yake, Emma Nagaikaya baada ya mama wa mtoto huyu, Imelda Maumba, kumkimbia alipojifungua kutokana na kupatwa na ugonjwa wa kichaa.
Shangazi wa mtoto huyu anasema kutokana na ukosefu wa fedha na maisha duni ya familia yake, ameshindwa kumtibu mtoto huyo licha ya ushauri uliotolewa na madaktari wa kumfanyia mazoezi ya muda mrefu.
Imani ni kwamba pale mtoto huyo atakapofanyiwa mazoezi anaweza kujimudu baadhi ya mambo yeye mwenyewe.
“Mimi shangazi yake sina uwezo wa kifedha, nimeshindwa kumhudumia, muda wote ni kulala kitandani, kulishwa. Muda wote na kuwa chini ya uangalizi," anasema Nagaikaya.
Kutokana na hali duni ya kipato, ameshindwa kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam alikoandikiwa kupatiwa mazoezi maalumu ya viungo tangu mwaka 2013 hadi sasa.
Kitendo cha kukosa fedha anasema kimemfanya kubaki mjini Mahenge bila ya kuwa na msaada wowote kwa kuwa Hospitali ya wilaya ya Ulanga haina wataalamu wala vifaa vya mazoezi maalumu ya viungo kwa mtoto huyo.
“Nimelazimika kubaki nyumbani nikihangaika na mtoto huyu na matatizo yake yanazidi kukua siku hadi kutokana na kukosa msaada wa kitabibu,” anasema Nagaikaya.
Nagaikaya anaeleza chanzo cha maradhi hayo akisema, mtoto aliyapata tangu akiwa na umri miezi mitano baada ya kuugua homa kali ambayo madaktari walipomchunguza waligundua aliugua homa ya uti wa mgongo.
“Tulimhangaikia kupata matibabu, lakini alipofikisha umri wa miezi minane alionesha dalili za kushindwa kukaa chini, kuongea, wala kushika kitu yenye mweyewe huku akilala muda wote kitandani,” anasema Nagaikaya.
Kutokana na uduni wa kipato, anasema inamlazimu kutumia takribani Sh 17,000 kwa ajili ya kununulia nepi maalumu zinazotosheleza kwa wiki moja pekee na fedha inapokosekana hana namna ya kufanya.
Nagaikaya, ambaye ni mama anayehudumia familia ya watoto 10 wakiwemo wanne wa mdogo wake, hana msaidizi mwingine isipokuwa kubeba majukumu hayo pekee.
Mama huyu anaishi katika nyumba ndogo na watoto hao wanaomtegemea kwa kila jambo. Anaomba jamii iweze kusaidia katika kumtibu mtoto huyo.
Wanafamilia hiyo, wanakiri mtoto huyo anayeumwa kuwa anapata mateso makubwa kutokana na maradhi hayo. Upendo Nagaikaya, anasema familia yao haina uwezo kifedha kugharimia matibabu na mazoezi ya mara kwa mara.
Anasema, baba wa mtoto huyo, Lucanus Nagaikaya mwenye watoto wanne hana uwezo na ameondoka nyumbani hapo muda mrefu kwenda kuishi katika Kijiji cha Ibuyu kutafuta maisha na kumwachia dadake amlee Devota.
Mama yake Devota, ambaye alipatwa na kichaa baada ya kujifungua mtoto huyo, yuko katika kijiji cha Kisewe ambako wanasikia bado yuko katika hali ya kuchanganyikiwa. Upendo, anasema jamii inayowazunguka imekuwa na mtizamo tofauti wakidai mtoto huyo apelekwe kupatiwa tiba za waganga wa jadi kwa madai kwamba amerogwa; kitendo kinachopingwa na familia yao.
Anasema baadhi ya majirani wengine wanaonesha kuguswa na ugonjwa wa mtoto huku wakimfariji shangazi yake.
Jamii inaombwa kumsaidia mtoto huyo kupitia simu ya mlezi wake, Emma Nakaikaya; 0712 801864 aweze kupata fedha za matibabu na pia kumhudumia.
Kwa mujibu wa wataalamu, ugonjwa unaomsumbua mtoto huyu ni matatizo kwenye ubongo (Cerebral Palsy). Huu ni ugonjwa ambao mtoto anaambukizwa akiwa ama tumboni au mara baada ya kuzaliwa kutokana na maambukizi ya bakteria wa ugonjwa huu.
Mtoto mwenye ugonjwa huu, anaweza kutambuliwa kabla ya kufikia umri wa miezi minne. Shingo yake hushindwa kusimama na hawezi kutembea anapofikia miezi 10 hadi mwaka mmoja.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob, anaelezea ugonjwa huu akisema watoto wenye nao, hutambulika kutokana na dalili za kushindwa kukua kulingana na umri na uwezo wa vitu anavyovifanya, kuchelewa kuongea au kushindwa kabisa kuongea.
Dk Jacob anasema dalili nyingine ni mtoto mwenye ugonjwa huu anapokuwa akishikwa, mikono yake na mwili wake unakuwa umekakamaa mithiri ya kuni.
Watoto wenye kuzaliwa kabla ya umri wao na wanaozaliwa pacha wapo katika athari za kupatwa na ugonjwa huu.
Wengine walio katika uwezekano wa kuupata, ni wale wanaopata homa kali, uti wa mgogo na kurithi katika familia. Dk Jacob anasema ugonjwa huu hauna matibabu kamili isipokuwa, mtoto anaweza kufanyiwa mazoezi maalumu na ya muda mrefu ili aweze kuimarika kimaumbile kumwezesha kuongea ama kutembea.
Ni kweli tatizo la ugonjwa huu wa ulemavu wa ubongo linawapata baadhi ya watoto mara nyingi akiwa tumboni mwa mwama mjamzito, mtoto anaabukizwa wakati wa msukukuko wa kujifungua ama baada ya muda mfupi kupita,” anasema Dk Jacob.
Dk Jacob anasema pamoja na ugonjwa huu kutokuwa matibabu yakuponyesha kabisa, lakini moja ya tiba inayoweza kuwasaidia watoto wenye ugonjwa huu ni kuwafanyia mazoezi maalumu ya viungo na ni kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu.
Anasema kupitia wataalamu maalumu wa mazoezi ya viungo, wanaweza kuboresha upungufu yaliyomo kwa watoto wenye ugonjwa huo na hivyo kuwasaidia kupata unafuu wa kuongea ama kutembea na si kuliondoa kabisa tatizo hili.
“Mazoezi haya yanahitaji vitu vingi na fedha nyingi kwani yanachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu kumwezesha mtoto aliyeathirika na ugonjwa huu kuboreka kiafya,” anasema.
Hivyo anasema, ndugu ama wazazi na walezi wa watoto wenye matatizo haya wengi kipato chao ni kidogo na wanaishi mbali na hospitali ya rufaa kuliko na wataalamu na vifaa vya mazoezi maalumu kwa watoto hao.
Matokeo yake, hushindwa kuwapeleka watoto wao kufanyiwa mazoezi hayo maalumu ya viungo ambayo ni ya muda mrefu.
“Mazoezi haya yanaweza kufanyika hata nyumbani kwa mgonjwa, tatizo ni vifaa na wataalamu wa aina hii, hivyo wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wa ubongo wamekata tamaa kuwahudumia kitabibu,” anasema Dk Jacob.
Pamoja na hayo, anasema lengo la serikali ni kusogeza huduma kama hivyo katika hospitali za wilaya za mkoa huu, lakini bado changamoto ni rasilimali fedha na wataalamu.