Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limetuma salamu za shukrani kwa Gavana wa Jimbo la Akwa Ibom, Gabriel Emmanuel kwa zawadi ya dola 10,000 za kimarekani ( sawa na sh. 21.5 milioni) kwa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars).
Hiyo ni baada ya kuonesha mchezo mzuri na wapinzani dhidi ya wenyeji Super Eagles ya Nigeria uliofanyika uwanja wa kimataifa wa Godswill Akpabo mjini humo.
Taifa Stars ilicheza mechi hiyo Jumamosi Septemba 3 2016, katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure Taifa stars ilifungwa bao 1-0 mara baada ya kuibana Super Eagles hivyo kumsukuma Gavana huyo kuandaa hafla ya chakula cha jioni ambako mbali ya kuizawadia stars, aliizawadia pia Super Eagles dola 35,000 za Marekani.
Taifa Stars ilitua Dar es salaam usiku wa kuamkia leo Septemba 5 ambako baadhi ya wachezaji walipelekwa katika hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya jiji la Dar es salaam, wakati wengine hususani wale wa timu ya Azam FC walichukuliwa na viongozi wao kwa ajili ya safari ya kwenda Mbeya ambako Jumatano wanatarajiwa kucheza na Tanzania Prison kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara utakaofanyika uwanja wa Sokoine mjini humo.
Wakati nyota 18 wakitua Dar es salaam, Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta aliishia Nairobi, Kenya ambako aliunganisha ndege ya kwenda Brussels, Belgium.
Thursday, September 8, 2016
TAIFA STARS YAZAWADIWA MILIONI 21.5 NA GAVANA WA NIGERIA.
MFAHAMU BINADAMU MWENYE UMRI MKUBWA DUNIANI.
Mzee huyu kwa jina la Mbah Ghoto kutoka Indonesia anayetokea kisiwa cha Java anaamini ndiye binadamu mzee kuwahi kuishi.
Amesema ameishi muda zaidi kushinda wake zake wanne, ndugu zake 10 na watoto wake wote.
Huwa najaribu kuwa mvumilivu na kuamini kuwa kuna watu watakaonitunza.
Nimeishi mda mrefu kwa sababu nina watu wanaonipenda na kunitunza. Mimi bado navuta sigara.
Mjukuu wake Suryanto anasema kuwa kwa mujibu wa stakabathi za serikali, Mbah Ghoto ana miaka 145 alizaliwa 31 Disemba 1870.
"Tunaamini stakabathi hizi ni halali kwa mujibu wa nyaraka rasmi za serikali. Tunaamini tarehe yake ya kuzaliwa ni sahihi" anasema Afisa wa serikali Wahyu.
"Siku ya Uhuru alikuwa akialikwa kusimulia yaliyokuwa yakitokea wakati wa vita. Anaweza kusimulia kuhusu vita dhidi ya wakoloni kutoka Japan na Waholanzi" anasema afisa huyo.
Mjukuu wake anasema Mzee huyo huwa hana masharti mengi na huwa haitishi chakula maalum.
"Kitu pekee alitutaka tufanye ni kumnunulia jiwe la kaburi lake" alisema mjukuu.
Mzee huyo anasema kwa sasa anaishiwa na nguvu na hawezi kutarajia aishi muda mrefu zaidi.
Sina nguvu kama zamani, hata kutembea ni shida. Nilikuwa mkulima na nilivua samaki mtoni, sitaki kuendelea kuishi sana ndio maana nimeandaa kaburi, ili nikifariki kila kitu kiwe tayari, alisema.
Mtu ambae aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka Ufaransa aliisha miaka 122 na siku 164. Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.
VOLKSWAGEN KUANZA KUTENGENEZA MAGARI YAO KENYA.
Kenya imetia saini ya makubaliano na kampuni ya Volkswagen ya Afrika kusini ili kuanza kutengeneza magari hayo katika taifa la Afrika Mashariki kulingana na taarifa ya serikali.
Volkswagen imeingia katika mkataba huo kwa kutumia kampuni ya kutengeneza magari nchini Kenya KVM mjini Thika kuunganisha sehemu za magari hayo ikianza na gari yake maarufu la Volkswagen Vivo.
Thika ni mji wa viwanda uliopo kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi na serikali ya Kenya inamiliki hisa katika kampuni hiyo.
Gari la kwanza la Volkswagen Vivo linatarajiwa kuunganishwa katika kiwanda hicho kufikia mwezi Disemba.
Kampuni hiyo ya Ujerumani ilikuwa ikifanya operesheni zake Kenya katika miaka ya 60 hadi mwaka 1977, ikiunganisha mabasi ya Volkswagen, mabasi madogo na matatu ya kombi iliokuwa maarufu sana wakati huo.
TAYLOR SWIFT AACHANA NA MPENZI WAKE TOM.
Taylor Swift na Tom Huddleston wameachana baada ya kuwa na uhusiano wa miezi mitatu.
Uvumi ulianza kwamba wapenzi hao ambao walipewa jina la utani HiddleSwift walikuwa pamoja baada ya kuonekana wakitaniana katika tamasha la Met Gala mnamo mwezi Mei.
Tangu wakati huo wamekuwa pamoja katika kila pembe ya dunia ikiwemo ziara ya Uingereza kuonana na familia ya Tom.
Lakini imeripotiwa kwamba wameshindwa kuendeleza penzi lao.
Hakuna tamko lolote rasmi kutoka kwa Tom wala Taylor lakini watu wanaowafahamu wapenzi hao wameongea.
BINTI ANAYEANDIKA KWA KUTUMIA ULIMI WAKONTA KAPUNDA APATA VIFAA.
Unamkumbuka Wakonta Kapunda? Binti mtanzania mwandishi wa miswada ya filamu anayeandika kwa kutumia ulimi?
Wakonta alipata ajali siku ya mahafali yake ya kidato cha sita miaka minne iliyopita. Ajali hiyo ilimuacha akiwa amepooza kuanzia shingoni na kushuka chini na kumfanya kutoweza kutumia mikono yake kuandika.
Wiki kadhaa zilizopita, BBC iliporusha habari yake msamaria mwema mmoja aliguswa na kumsaidia.
Kupitia kipindi cha Televisheni Focus on Africa katika BBC World Service mwanadada Olivia Soko kutoka Afrika ya Kusini aliguswa kufanya kitu kumsaidia Wakonta.
Akiwa mkurugenzi wa kampuni ya WhirlMarket Technologies, Olivia alijitolea kutoa msaada wa programu ya kompyuta iitwayo Nuance Dragon Naturally Speaking.
Jinsi programu hii inavyofanya kazi ni kwamba mtumiaji yeye anazungumza anachotaka kukiandika kupitia kipaza sauti chake halafu programu hiyo inaandika yenyewe katika kompyuta ya mtumiaji.
Wakonta alijaribu kuitumia jana akaifurahia, lakini bila shaka atahitaji muda zaidi ili aizoee vizuri.
WAPINZANI NCHINI ZIMBABWE WANYIMWA CHAKULA.
Tume ya haki za binadamu nchini Zimbabwe imesema kuwa watu wanaounga mkono wapinzani, walio kwenye maeneo ya ukame wamenyimwa misaada ya chakula na chama tawala cha ZANU-PF.
Mwenyekiti ya bodi maalum Elasto Mugwadi amesema kuwa kwa sasa uchunguzi umebainisha kuwa watu wanaounga mkono upande wa upinzani wanaambiwa waziwazi kuwa hawatopewa msaada wowote wa chakula na inaarifiwa kuwa watu wengi wameathirika kutokana na hali hiyo.
Taarifa ya serikali inaonyesha kuwa nusu ya wakazi wa vijijini wamekumbwa na njaa, jambo linalochochea kupingwa kwa utawala wa Rais Mugabe.
Wakati huo huo mahakama kuu nchini humo imebatilisha marufuku ya maandamano yaliyokatazwa na polisi kwenye mji mkuu wa Harare. Ambapo marufuku hiyo ilidumu kwa muda wa wiki mbili.
Wanaharakati wanne wanaopinga utawala wa Rais Mugabe ndio waliwasilisha pingamizi mahakamani kupinga uamuzi wa polisi kupiga marufuku maandamano.
Hakimu wa mahakama kuu wa nchini humo, amesema kuwa marufuku hiyo ilikuwa batili. Siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wimbi la maandamano nchini Zimbabwe.
MICHUANO YA OLIMPIKI YA WALEMAVU KUANZA LEO BRAZIL.
Michuano ya Olimpiki kwa watu walemavu inatarajiwa kuanza leo mjini Rio de Janeiro nchini Brazil. Waandaaji wa michuano hiyo wameahidi kuwepo kwa shamra shamra za kila namna katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo ambayo lengo lake ni kuleta changamoto kwa watu wenye mitizamo tofauti kwa walemavu na hivyo kupitia michuano hiyo dhana hiyo itatupiliwa mbali kutokana na uwezo utakaooneshwa na wachezaji wa jamii ya walemavu.
Moja ya changamoto kubwa katika michuano hiyo ya Olimpiki ni kubugikwa na mgogoro wa kifedha pamoja na mauzo ya tiketi ya ufunguzi wa michuano hiyo kwenda mwendo wa Kobe.
Michuano hiyo inatarajiwa kushirikisha wanariadha zaidi ya elfu nne kutoka mataifa mia moja na sitini ulimwenguni watakaokuwa katika gwaride la ufunguzi, ingawa miongoni mwa hao wanariadha wa kutoka nchini Urusi hawamo.
Wanamichezo wa Urusi wamepigwa marufuku kushiriki michuano hiyo kutokana na wasiwasi wa utumizi wa dawa za kusisimua misuli ambazo zilipigwa marufuku michezoni, inaelezwa kuwa sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo zitashuhudiwa na mamilioni ya watu ulimwenguni kote.
MGANGA ACHOMWA MOTO BAADA YA KUMUUA MJUKUU WAKE.
Wananchi katika kijiji cha Kalundi Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kisha kumteketeza kwa moto mganga wa kienyeji, Patrick Mwandaliwa (44) wakimtuhumu kumuua mjukuu wake, Silvia Mwanakatwe mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema tukio hilo lilitokea Septemba 4, saa mbili usiku, kijijini Kalundi wilayani Nkasi mkoano humo.
Akisimulia mkasa huo kamanda Nkasi alidai usiku wa tukio Mwandaliwa alikutana na mpwa wake Maria Kapele (21) dukani kijijini humo akiwa amembeba mtoto wake wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Mwandaliwa alimuomba mpwa wake huyo mjukuu wake huyo kisha akaondoka naye mpaka nyumbani kwake, mpwa wake hakuwa na wasiwasi wowote kwakuwa aliyemchukua mwanae ni mjomba ake.
Maria alihisi ni mda mrefu umepita tangu mjomba ake amchukue mtoto wake ndipo alipomtuma mtoto wa jirani yake kwenda kumchukua, lakini alipofika kwa Mwandaliwa alikuta mlango umefungwa akarudi na kumtaarifu mama wa mtoto.
Inadaiwa kuwa mama mtoto alipofika kwa mjomba ake ampe mtoto, alikana na kusema yeye hana mtoto wake. Ndipo Mwandaliwa alipomsukuma mpwa wake na kuingia ndani na kufunga mlango.
Mwandaliwa alipanga magunia ya mahindi mlangoni akizuia mtu yoyote yule asiweze kufungua mlango, ndipo mama mtoto alipopiga mayowe kuomba msaada kwa watu.
Watu walikusanyika katika eneo hilo la tukio, kwa kuwa walikuwa wengi waliweza kuvunja mlango na kuingia ndani na kumkuta Mwandaliwa akiwa ameshika ndoo ya plastiki mkononi akiwa na mwili wa mtoto, tayari akiwa amekufa, akiwa amemtoboa shingoni kwa kitu cha ncha Kali.
Ndipo wananchi wakiwa na silaha za jadi walimvamia Mwandaliwa na kumpiga sana kisha kumchoma.
Mwili wa Mwandaliwa ulizikwa chini ya uangalizi wa askari kwa sababu wananchi waligoma kumzika.
APPLE YAZINDUA IPHONE 7.
Kampuni ya Apple imezindua simu zaidi ya iPhone Jumatano. Uzinduzi huo ulifanyika siku chache baada ya washindani wao wakubwa wa Samsung kulazimika kusitisha kuuza simu zake za Note 7 kutokana na matatizo ya betri.
Wachanganuzi wa masuala ya teknologia wanaendelea kujadili kuhusu sifa na vifaa vipya ambavyo huenda vikawepo kwenye simu hiyo mpya.
Wengi walitarajia Apple itupilie mbali suala la tundu la kuwekea headphone jack, na badala yake kuwa na tundu moja pekee.
Hili litawafanya watumiaji wa simu hizo kutumia headphone za teknolojia ya Bluetooth au zile zinazoweza kutumia tundu la lightning la kampuni ya Apple ambalo pia hutumiwa kuwekwa chaji.
Hata hivyo vifaa vya awali havitaacha kutumika kabisa na Apple inatarajiwa kuzindua kifaa ambacho kitamuwezesha mtu kutumia kuunganisha headphone na simu na kuendelea kuitumia.
Uzinduzi wa iPhone ulifanyika siku ya jana mjini San Francisco, Califonia.
Na imetoa aina mpya ya earphone zinazojulikana kama Airpods.
Sifa nyingine za simu hiyo;
Kitufe cha nyumbani sasa kinaweza kutofautisha uzito kinavyobonyezwa na kutoa mtikisiko. Kitufe hicho sasa hakiingii ndani ya simu.
Simu hizo zinaweza kuingizwa ndani ya maji ya kina cha 1m (3.2ft) kwa dakika 30 wakati mmoja bila kuharibika.
Aina kubwa ya iPhone 7 plus ina lensi mbili za kamera sehemu ya nyuma, ambayo inaimarisha uwezo wa kupiga picha.
Airpods zitagharimu £159. Pia zina uwezo wa kugundua zinapoingizwa masikioni. Hii inaziwezesha kusitisha uchezaji mziki zinapochomolewa maskioni.
Simu hizo zitaanza kuuzwa Septemba 16.