Tuesday, September 13, 2016

KIBAHA KUKUMBWA NA BOMOABOMOA NOVEMBA.

Wakazi wa Kiluvya Mailimoja hadi Tamko Kibaha waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro wametakiwa kubomoa majengo yao kabla ya bomoabomoa kuanza Novemba 24.

Bomoabomoa hiyo itawahusu wakazi ambao majengo yao yapo ndani ya mita 60 kila upande wa barabara na ambao tayari nyumba zao zimeekewa alama ya X kuwataarifu kuwa wamejenga sehemu sio sahihi.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema katika kikao cha bodi ya barabara kuwa wananchi watambue kuwa taarifa walizopewa za kubomolewa nyumba zao ni za kweli na itahusisha nyumba zote zilizo ndani ya mita 60 kila upande na sio 120 kama ilivyosemwa awali.

Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Asumta Mshama alisema "mimi bado naona tunawasumbua hawa wananchi wakati hawana tabu ya kuondoka. Wote waliowekewa X wanajua siku yoyote wanatakiwa kuondoka".


VITAMBULISHO VYA TAIFA KUBADILISHWA.

Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani ambavyo havina saini, huku ikitarajia kutoa vitambulisho vipya vyenye saini kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi kwa kuchukuliwa alama ya kibayologia ikiwemo alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.

Aidha inatarajia kutoa vitambulisho vipya kuanzia Septemba 14 katika ofisi zote za NIDA za wilaya. Taarifa iliyotolewa jana Dar es salaam na Kaimu mkurugenzi mkuu wa NIDA Andrew Massawe alisema kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika pamoja na vipya huku taratibu za kubadilisha zikiendelea.