Friday, September 2, 2016

CHRIS BROWN ATOA NYIMBO MPYA MASAA MACHACHE BAADA YA KUACHIWA NA KUWA HURU.

Msanii wa Marekani, Chris Brown ambaye alikuwa anashitakiwa kwa kosa la kumtishia mwanamitindo bunduki, amemaliza kesi yake na sasa yupo huru.

Ni habari njema kwa mashabiki wa Chris Brown kuwa masaa machache baada ya kutoka jera na kuwa huru aliachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la WHAT WOULD YOU DO?

Sikiliza na download hapa:  What Would You Do? 


NHC WAVAMIA OFISI ZA FREEMAN MBOWE NA KUTOA VITU NJE.

Madalali wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Foster Auctionare wamevamia ofisi za kampuni ya Free Media, wachapishaji wa gazeti la Tanzania Daima na ukumbi wa Disco wa Billicanas na kutoa nje samani na vifaa mbalimbali.

Hatua hiyo inatokana na madai kuwa, mpangaji wa jengo hilo lililopo katika mtaa wa Mkwepu na Indira Gandhi jijini Dar es salaam, Freeman Mbowe anadaiwa Sh bilioni 1.172 na Shirika la Nyumba la Taifa.

Tukio la kutoa vifaa lilianza mapema jana asubuhi katika eneo la tukio, madalali wa NHC walionekana wakitoa nje samani katika ofisi zilizopo katika jengo hilo, ikiwemo ya gazeti hilo na vifaa vingine katika eneo la ukumbi wa disco la Billicanas.

Akizungumza wakati madalali wakiendelea kutoa vitu nje, Meneja wa kitengo cha madeni wa NHC Japhet Mwanasenga, akisema mpangaji wa jengo hilo anadaiwa kiwango hicho cha fedha na hajalipa kuanzia miaka ya 90.

Alisema kutokana na kutokulipa fedha hizo, licha ya kupewa notisi, ndio maana shirika limeamua kuingia na kutoa vitu nje ili aweze kulipa. Alisema mpangaji huyo aliambiwa na alipewa na notisi na NHC ya siku 30 pamoja na notisi ya dalali lakini hakulipa deni ndani ya muda huo.

"Sasa hakuna namna usipolipa deni lazima uondolewe katika jengo ni fedha za miaka mingi kuanzia miaka ya 90" alisema Mwanasenga. Alisema baada ya kumhamisha kwa lazima, wataendelea kufanya utaratibu wa kumdai.

Kuhusu vifaa alisema, vinaenda kwa dalali ambaye ataomba kibali NHC juu ya kuviuza vifaa hivyo baada ya siku 14 kama deni halitalipwa. Kuhusu ubia katika upangaji katika jengo hilo, Mwanasenga alisema hakuna suala kama hilo na NHC inamhesabia kama mpangaji wa kawaida.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa kampuni ya udalali, Joshua Mwaituka alisema wao watahifadhi vifaa hivyo katika ghala lililopo Buguruni jijini humo na ndani ya siku 14 wakipata idhini kutoka NHC wataviuza.

Kwa muda wote kazi ya kuhamisha vitu ilipokuwa inaendelea mpaka mchana saa 8, lakini mpangaji wa jengo hilo hakufika kuzungumzia suala hilo.


MDUKUZI WA WATU MAARUFU MITANDAONI AKAMATWA NCHINI MAREKANI.

Mahakama moja nchini Marekani imemfunga jera raia mmoja mwenye asili ya nchi ya Romania kwa kosa la udukuzi mtandaoni kwa watu maarufu nchini humo ikiwemo familia ya Bush.

Marcel Lazar, alikuwa akitumia mfumo wa "Guccifer" kutekeleza udukuzi huo, amefungwa jela kwa muda wa miezi hamsini na mbili .

Mwendesha mashtaka alisema Marcel alidukua akaunti ya barua pepe ya familia ya Bush nakubaini picha binafsi zenye kushikamana na maraisi wa zamani George H.W Bush na George W Bush.

Wakati wa mahojiano na mtuhumiwa huyo, alisema alivunja mfumo wa kompyuta binafsi, uliokuwa ukitumiwa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokratiki Hilary Clinton wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, hata hivyo kitengo cha usalama wa kimtandao nchini humo umepinga madai hayo.

Marcel alifikishwa nchini Marekani mwezi Aprili na kukutwa na hatia ya kuingilia mifumo binafsi ya watu ya kompyuta zilizokuwa na ulinzi binafsi.


UN YAWATAKA WANANCHI WA GABON KUWA NA UTULIVU.

Rais Bingo na mpinzani wake Ping

Umoja wa Mataifa umehimiza kuwepo kwa utulivu nchini Gabon baada ya fujo kuzuka kuhusiana na utata kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais.

Baraza la usalama la umoja huo limetoa wito kwa wagombea wakuu na wafuasi wake kujizuia kufanya uchochezi na kutatua mzozo wa sasa kupitia njia za kisheria.

Maafisa wa usalama kufikia sasa wamewakamata watu zaidi ya elfu moja baada ya siku ya pili ya maandamano ya wafuasi wa upinzani.

Upinzani unadai Rais Ali Bongo aliiba kura wakati wa uchaguzi huo uliofanyika jumamosi.

Rais Bongo amesisitiza kwamba ameshinda kwa njia halali na kuutaja ushindi wake kuwa ushindi wa watu wa Gabon.

Amesema kuna kundi dogo la watu wachache waliotaka kutwaa madaraka na ambao wameshindwa.

Matokeo ya uchaguzi yametangazwa jumatano alasiri na kumpatia Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na Ping aliyepata 48.2% ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5.594.

Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na hakuna ajuaye hasa nani alishinda.

Upande wa Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonyesha 99% ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zilizotolewa wazi.

Bongo aliingia madarakani mwaka wa 2009, baada ya kifo cha babake aliyekuwa ameongoza taifa hilo tangu 1967.

Kabla ya kuingia kwenye siasa Ping aliwahi kuhudumia kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.


MARK ZUCKERBERG AONESHA UTOFAUTI WAKE AFRIKA.

Mark Zuckerberg akila Ugali na Samaki nchini Kenya.

Mwanzilishi wa kampuni ya Facebook Mark Zuckerberg amezuru nchini Kenya katika ziara yake ya mataifa ya Bara la Afrika.

Zuckerberg aliwasili siku ya jumatano akitokea  nchini Nigeria, alifanya kikao na Waziri wa habari nchini Kenya, Joseph Mucheru ambapo walizungumza kuhusu mtandao na mipango ya serikali kuhakikisha kila kijiji kimeunganishwa na mtandao.

Baadae Zuckerberg alielekea katika hoteli ya Mama Oliech katika chakula cha mchana ambapo kwa mara ya kwanza alikula ugali na samaki.

"Swala muhimu ninapozuru taifa lolote jipya ni kujaribu kula chakula chao, nilipenda sana Ugali na samaki mzima wa Tilapia" alisema Zuckerberg.


MELANIA TRUMP ALISHITAKI GAZETI LA DAILY MAIL LA UINGEREZA.

Melania Trump

Melania Trump amelishitaki gazeti la Daily Mail la Uingereza pamoja na mwanablogu wa Marekani akitaka alipwe $150m (£114m) kuhusiana na tuhuma kwamba alikuwa kahaba miaka ya 1990, wakili wake amesema.

Gazeti la Daily Mail lilidokeza kwamba huenda Trump alifanya kazi ya muda kama kahaba New York, na kwamba alikutana na mumewe Donald Trump ambaye kwa sasa anawania uraisi mapema kuliko inavyodhaniwa.

Mwanablogu Webster Tarpley aliandika kwamba Bi Trump anahofia sana maisha yake ya awali yasifichuliwe kwa umma.

Madai hayo ni uongo mtupu, wakili wake Charles Harder amesema.

"Washtakiwa walitoa tuhuma kadhaa kuhusu Bi Trump ambazo ni za uongo 100% na kumharibia sana sifa" Bwana Harder alisema.

Bi Trump 46 alizaliwa Slovenia na akahamia Marekani kufanya kazi kama mwanamitindo miaka ya 1990. Aliolewa na Trump 2005.

Gazeti la Daily Maily lilinukuu madai yaliyokuwa yamechapishwa na jarida moja la Slovenia kwa jina Suzy kwamba wakala wa uanamitindo ambaye Bi Trump alikuwa akifanyia kazi wakati huo pia alihudumia kama wakala wa kutafutia kazi makahaba, nyaraka za mahakama zinaonesha.

Gazeti hilo pia lilimnukuu mwanahabari wa Slovenia Bojan Pozar, ambaye aliandika kitabu kuhusu maisha ya Bi Trump ambacho hakijaidhinishwa, ambaye alidai kwamba Melania alipigwa picha za utupu New York mwaka 1995 na akadai kwamba mwanamke huyo alikutana na Trump miaka mitatu kabla ya wakati ambao inadaiwa walikutana, ambayo ni mwaka 1998.

Wakili wake anasema alihamia Marekani mwaka 1996.

Tarpley alidai kuwa Melania ana wasiwasi sana huenda wateja wake matajiri wa wakati huo wakafichua siri yake na kwamba alikuwa na mfadhaiko.