Sunday, August 28, 2016

ACHORA TATOO KWENYE TITI LENYE SARATANI.

Wakati alipokuwa akiugua saratani ya titi, Alison Habbal alikuwa akihisi kisunzi na kuchoka.

Akiwa miaka 36 wakati alipoanza kuugua ugonjwa huo, Alison ambaye ni raia wa Sydney alijua kwamba atapoteza nywele zake na titi lake.

Mpango wa kutengeneza titi jingine kutumia upasuaji wa kutumia plastiki haukumvutia.

"Sikutaka kuwekwa titi bandia kutoka kwa ngozi ya watu wengine, niliona niweke tatoo" alisema.

Wakati wote nilipokuwa mgonjwa niliwatafuta wachoraji tatoo katika mitandao, aliongezea. Na baada ya majadiliano marefu niliamua kumpa kazi ya uchoraji huo msanii kutoka New Zealand, Makkala Rose, mwenye umri wa miaka 23.

Tatoo hiyo ilichorwa mjini Melbourne kwa saa 13 mnamo tarehe mosi mwezi Julai.

Alison alifurahia kazi hiyo na akaamua kuchapisha picha yake katika mitandao ya Instagram na Facebook.

Hatua ambayo ilimpatia umaarufu mkubwa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo wengi walisifu wazo lake.


JOAO MARIO ASAJILIWA INTER MILAN.

Joao Mario

Joao Mario amejiunga na klabu ya Inter Milan kutoka Sporting Lisbon kwa kitita cha pauni milioni 38.4 na kuwa mchezaji ghali zaidi wa Ureno na kuwahi kuuzwa na klabu ya Ureno.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliyashinda mauzo ya Cristiano Ronaldo ya pauni milion 12.24 na nani aliyeuzwa kwa kitita cha pauni milioni 25 kuelekea Manchester United.

Inter bado inaendelea na mazungumzo ya kumsajiri Gabriel Barbosa kutoka Santos.

Kiungo wa katiu Mario aliichezea Sporting mara 171 na kushinda Euro 2016 na Ureno


MCHEZAJI AGOMA KUHESHIMU WIMBO WA TAIFA WA MAREKANI.

Colin Kaepernick

Mchezaji wa soka ya Marekani NFL amekataa kusimama ili kutoa heshima wakati ambapo wimbo wa taifa unapoimbwa akipinga mile anachotaja ni ubaguzi wa rangi.

Colin Kaepernick anayeichezea timu ya San Fransisco 49ers alisalia akiwa ameketi wakati wimbo wa taifa ulipoimbwa.

"Sitasimama kujivunia bendera ya taifa linalokandamiza watu weusi na watu wengine wa rangi" alisema.

Mashabiki wengine walimzomea mchezaji huyo wakati anaingia uwanjani.

Lakini timu yake ilisema kuwa inaheshimu haki yake ya kugoma wakati timu ya 49ers ilipokuwa ikikabiliana na Green Bay Packers katika mechi ya kirafiki.

"Tunatambua uhuru wa mtu binafsi kujichagulia na kushiriki katika sherehe za wimbo wa taifa" alisema msemaji wa timu, akipinga kile anachosema ni ubaguzi wa rangi.


TRUMP ASISITIZA KUJENGA UKUTA KUWAZUIA WAHAMIAJI.

Mgombea wa Urais chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amesema kuwa atabumi mfumo ambao utasaidia serikali kudhibiti uhamiaji.

Akizungumza wakati wa kampeni katika jimbo la Lowa bwana Trump alisema kuwa mfumo huo utasaidia kuwatimua watu ambao wanaishi nchini Marekani licha ya muda wa viza zao kumalizika.

Pia alirejea wito wake wa kujenga ukuta kati ya mpaka wake na Mexico kuwazuia wahamiaji.


RIHANNA AFURAHISHWA NA KITENDO ALICHOFANYA DRAKE.

Bango aliloandikiwa Rihanna na Drake.

Siku mbili zilizopita Drake alimuandikia ujumbe Rihanna kwenye Bango kubwa lililopo nchini Marekani akimpongeza Rihanna kuchaguliwa kwenye MTV Video Music Awards.

Rihanna amefurahishwa kwa kitendo hicho alichofanya Drake na kusema kwamba "ni kitu kizuri ambacho hakuna mwanaume mwingine aliyewahi kunifanyia".

Drake ameonyesha upendo mkubwa sana kwa mrembo Rihanna. Tazama hapo juu picha ya bango aliloweka Drake.


IDADI KUBWA YA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI HAWAJUI KUSOMA.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya ufundi Mhe. Joyce Ndalichako.

Ukaguzi uliofanyika katika shule za msingi 6,831 zilizokaguliwa 2015/16 umebaini kuwa wanafunzi 10273, katika shule 515 nchini hawajui kusoma wala kuandika.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi uthibiti ubora wa shule katika Wizara ya Elimu, Sayansi,  Teknolojia na mafunzo ya ufundi Marystella Wasena jana jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumzia mikakati ya kukagua na kusimamia utekelezaji na ufundishaji wa kusoma, kuandika na kuongea KKK kwenye shule za awali na msingi.

Alisema miongoni mwa wanafunzi hao 10,273 wasichana ni 5,263 na wavulana ni 5,010 huku tathmini ikibainisha kuwa sababu mojawapo ya tatizo hilo ni wanafunzi wenyewe kushindwa kumudu kujifunza. Pia zipo sababu zilizotokana na watekelezaji wa mtaala wakiwemo walimu wenyewe kukosa umahili wa kufundisha KKK.

Kutokana na hali hiyo alisema idara inaendelea na mipango ya kuwajengea uwezo wathibiti ubora wa shule ili wapate umahiri huo shuleni.

Alisema katika awamu ya kwanza idara katika mradi wa kukuza Stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu LANES imeshawewezesha wathibiti ubora wa shule 1,469 kupitia mafunzo elekezi yaliyofanyika Mei mwaka huu katika vyuo vya ualimu vya Patandi (Arusha), Butimba (Mwanza), Mtwara, Morogoro na Kleruu (Iringa).

Alisema kupitia mafunzo hayo yaliyofanyika Mei, idara iliazimia kuanzisha uthibiti ubora wa ndani ya shule kwa kuhakikisha kila kanda na wilaya inateua shule mbili za mfano zikiwemo shule za sekondari na binafsi ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa.

Naye mthibiti ubora wa shule elimu ya awali na msingi Hawa Selemani alisema shule binafsi zinafanikiwa katika eneo hilo kwa sababu zinachukua wanafunzi wachache kwa kila darasa tofauti na za serikali ambazo zinalenga kutoa huduma.


WATAKAO TUMBUIZA KATIKA TUZO ZA VMAs 2016.

Wasanii wakubwa wametajwa kuwa watatumbuiza katika tuzo za VMAs jumapili leo usiku. Angalia majina ya watakao tumbuiza katika tuzo hizo za MTV Video Music Awards hapo chini:

Rihanna atafungua tuzo hizo huko Madison Square Garden.
Britney Spears atafata kutumbuiza huku akiungana na G-Eazy.
Ariana Grande na Nick Minaj watatumbuiza wimbo wao mpya unaoitwa Side To Side.
Nick Jonas na Ty Dolla $ign watakuwepo pia kuburudisha tuzo hizo.
Halsey na Chainsmokers watatumbuiza pia siku ya leo.
Future naye bila kukosa atakuwepo leo kwenye hizo tuzo.

Kuna uwezekano wa Kanye West pia kuwepo lakini bado haijathibitishwa. Na kuma uvumi kuwa Beyonce atafanya surprise kwenye tuzo hizo ingawa hayupo kwenye list ya watakaotumbuiza.


ASKARI AFYATUA RISASI WODINI.

Kamanda wa polisi George Kyando

Kitendo cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba 9 ya wanawake na watoto, ambapo wakina mama walipiga mayowe kwa hofu huku wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha watoto zao vitandani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio na kueleza kuwa lilitokea jana alfajiri.

"Chanzo ni ulevi wa kupindukia, tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha kipimo ni alama kati ya 70 na 40....katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10", alisema.

Kamanda Kyando alisema siku ya tukio askari huyo akiwa na wenzake alikuwa katika lindo akilinda makazi ya Kamanda wa magereza wa mkoa, lakini alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba 9, ambako mkewe alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.

Mke wa mtuhumiwa huyo Theresia Kalonga ambaye ni askari magereza, alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi.

"Mtuhumiwa huyo tunamshikiria huku taratibu  za kumkabidhi kwa kamanda wa magereza mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao, kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea", alisema kamanda Kyando.

Akizungumza hospitalini hapo, Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dk.John Gurisha alisema, askari huyo baada ya kuingia wodini aliweka siraha yake chini, akafunua chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje kafyatua risasi hewani na kutoboa paa.

"Mtuhumiwa huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa", alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa wodini hapo na mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa, lakini alisababisha taharuki kubwa wodini.

"Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU waliwahi kufika hospitalini hapo na kumtia nguvuni na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa na risasi kumi" alisema.

Muuguzi wa zamu wodini humo, Rose Katabi, alisema askari huyo alipofyatua risasi akina mama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha muuguzi ili kusalimisha maisha yao.

Waliingia walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza kusema atarudi tena, akatoka nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua risasi hewani kisha akaondoka na kutokomea gizani" alisema muuguzi.


MAGUFULI: BINADAMU INAPASWA TUPENDANE.

RAIS John Magufuli amesema kwamba binadamu wanapaswa kuwa wamoja hata kama wanatofauti mbalimbali zikiwemo za kimadhehebu ya kidini, siasa na kanda, huku akiwaomba viongozi wa dini kuendeleza juhudi zao za kuliombea taifa na kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizonazo.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo jana baada ya kumalizika kwa misa takatifu ya kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe.Benjamini Mkapa na Mkewe Anna iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es salaam.

Hafla ya jubilei hiyo ilifanyika nyakati za mchana kwenye ukumbi wa Kardinali Rugambwa uliopo kando ya kanisa la Mtakatifu Petro-Oysterbay na ilitanguliwa na misa ya shukrani.

Rais Magufuli alisema miaka 50 ya ndoa ya Mkapa ambaye ni muumini wa kanisa katoliki na mkewe Anna ambaye ni muumini wa kanisa la Kilutheri, inawafundisha watanzania wote hususani wanasiasa kuishi kwa upendo na kulinda amani waliyonayo.

Kwa upande wake, Rais mstaafu Mkapa pamoja na kuwashukuru viongozi wote, ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria misa ya shukrani na jubilei hiyo ya miaka 50 ya ndoa yake, alimshukuru mwenyezi Mungu kwa kuijalia ndoa yake umri mrefu.

Aidha alitoa mwito wa watanzania wote kupenda na kushirikiana huku akibainisha mafunzo aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa kidini kuwa "kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake".