Tafiti zinaonyesha kuwa madaktari wa nchi za kusini mwa Afrika, wanatoa dawa nyingi zaidi ya zilizoagizwa na Shirika la Afya duniani WHO.
Utafiti huo uliofanywa na chuo kikuu cha London kwa ushirikiano na kituo cha kutoa ushauri wa Afya cha nchini Ghana ikihusisha nchi 11 za kusini mwa jangwa la Sahara zinaonyesha kuwa wagonjwa wanapewa takribani dawa tatu kila wanapotembelea hospitali zaidi ya maelekezo ya WHO.
Inasemekana tatizo ni baya zaidi kwenye taasisi zinazotengeneza faida na kuchochea kuuza dawa.
Tafiti zimeonyesha kuwa matumizi makubwa ya madawa yanasababishwa na kulazimisha kutumia madawa, kuzidisha dozi na kuleta athari mbaya kwa mchanganyiko unaosababishwa na kuchanganya dawa mbalimbali.
Pia wamegundua wagonjwa wengi wamekuwa wakipewa dawa za kutuliza maumivu pasipo kufanyiwa vipimo na kuongeza hatari ya maambukizo yanayosababisha na kupambana na dawa.
Monday, August 22, 2016
UTAFITI:MADAKTARI AFRIKA WAZIDISHA MADAWA.
ALIYEDANGANYA KUWA NI MZEE AKAMATWA MAREKANI.
Polisi nchini Marekani wamemkamata mtoro mmoja baada ya kugundua kuwa alikuwa akidanganya yeye ni mtu mzee.
Polisi walizingira nyumba moja huko Massachusetts na kumuamrisha Shaun "Shizz" Miller atoke nje.
Kisha akatoka nje akiwa amejibadirisha na kuwa kama mtu mzee, lakini wakati polisi waligundua kuwa alikuwa ni yule aliyekuwa wakimtafuta mwenye umri wa miaka 31 wakamkamata.
Amekuwa mafichoni tangu ashitakiwe kwa kuhusika kwenye ulanguzi wa madawa ya kulevya April mwaka huu.
Wakati polisi wakisaka nyumba hiyo, walipata bunduki mbili na karibu dola 30,000 pesa taslimu.
DARAJA REFU ZAIDI LA KIOO KUFUNGULIWA CHINA.
Daraja refu zaidi duniani ambalo sakafu yake ni ya kioo limefunguliwa katika mji wa Zhangjiajie katika mkoa wa Hunan nchini China.
Daraja hilo ndilo la juu zaidi lenye sakafu ya kioo duniani na linaunganisha milima miwili ambayo hufahamika kama milima ya Avatar. Filamu ya Avatar iliandaliwa katika milima hiyo.
Ujenzi ulikamilika Desembq mwaka jana. Urefu wa daraja hilo ni 430m na liligharimu $3.4m (£2.6m).
Daraja hilo limewekwa 300m juu ya ardhi, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Xinhua.
Sakafu yake imeundwa kwa vipande 90 vya vioo ambavyo vina tabaka tatu.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, daraja hilo lenye upana wa mita 6, ambalo mchoro wake uliandaliwa na msanifu majengo kutoka Israel Haim Dotan, tayari limeweka rekodi kadha za dunia katika usanifu mijengo na ujenzi.
Maafisa waliandaa hafla ya kuthibitisha uthabiti wake, walituma watu wenye nyundo kujaribu kuvunja vioo. Pia magari yaliyojaa abiria yalipita juu yake.
Maafisa wamesema watu 8000 wataruhusiwa kutumia daraja hilo kila siku.
WAZIRI MKUU ATOA TAHADHARI HII KWA WATENDAJI KATAVI.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka watendaji halmashauri mkoani katavi kuwa makini na matumizi ya fedha za maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao na atakayethubutu kuzichezea zitamuunguza.
"Fedha hii tafadhari ni ya moto, msicheze na hii ya halmashauri tunayoileta hapa kwa ajili ya wananchi itawaunguza vidole, tunaileta kwa madhumuni tunataka wananchi wahudumiwe". Alisema waziri mkuu.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo jana jioni wakati akihutubia umati mkubwa wa wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Azimio wilayani Mpanda.
Alisema ni lazima wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha viwango vya ubora wa miradi inayojengwa katika maeneo yao kuwa inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.
UVCCM KUFANYA MAANDAMANO AGOSTI 31.
Umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi (UVCCM) wanatarajia kufanya maandamano ya amani Agosti 31 kwa ajili ya kueleza utendaji kazi wa Rais Mhe. John Pombe Magufuli kwa watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, kaimu katibu mkuu wa umoja huo Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa maandamano hayo wameshamwandikia barua mkuu wa jeshi la polisi kwa ajili ya kupata ulinzi siku hiyo.
Amesema kuwa wasipopata ulinzi watafanya kwa kujilinda wenyewe ikiwa ni lengo la kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya utendaji kazi wa Rais Magufuli.