Wednesday, August 31, 2016

KODI ZA SIMU ZAONGEZA KIPATO NCHINI.

Sheria ya fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji wa ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato yaliyotolewa na kampuni za simu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na kamati ya kudumu ya Miundombinu, imeonesha kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumiwa kwa wastani wa Sh.milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria Julai pekee mwaka huu imelipa Sh.bilioni 1.9.

Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa kampuni ya Tigo walikuwa wanatoa wastani wa sh.milioni 250 kwa mwezi lakini sasa wametoa jumla ya sh.bilioni 1.48.

Barongo ambaye ni Meneja msaidizi kitengo cha walipa kodi wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna mtambo maalumu wa kusimamia mawasiliano na udhibiti wa mapato yatokanayo na simu (TTMS) unaosimamiwa na mamlaka ya mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.

"Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwenzi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa. Baada ya hiyo tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua" alisema Barongo.

Aliendelea kusema "kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia". Makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.


No comments: