Thursday, September 15, 2016

MWANAMKE AKAMATWA KWA KUIBA MTOTO MWENYE SIKU 10.

Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi wa Kipawa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za wizi wa mtoto Angel Meck mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo Maimuna Mohammed mkazi wa Chamwino katika manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea Septemba 13, saa tano asubuhi katika mtaa wa Kilimahewa manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka kituo cha Afya Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera kisha wagawane.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mama mtoto baada ya kugundua kuwa ameibiwa alienda kutoa taarifa kituo cha polisi. Ndipo polisi walipoanza kufanya msako kwenye mabasi yote ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani akienda mkoani Dar es salaam.

Mtuhumiwa alikiri na kusema hakuwa na nia mbaya bali alitaka kwenda kumlea huyo mtoto.


No comments: