Madalali wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Foster Auctionare wamevamia ofisi za kampuni ya Free Media, wachapishaji wa gazeti la Tanzania Daima na ukumbi wa Disco wa Billicanas na kutoa nje samani na vifaa mbalimbali.
Hatua hiyo inatokana na madai kuwa, mpangaji wa jengo hilo lililopo katika mtaa wa Mkwepu na Indira Gandhi jijini Dar es salaam, Freeman Mbowe anadaiwa Sh bilioni 1.172 na Shirika la Nyumba la Taifa.
Tukio la kutoa vifaa lilianza mapema jana asubuhi katika eneo la tukio, madalali wa NHC walionekana wakitoa nje samani katika ofisi zilizopo katika jengo hilo, ikiwemo ya gazeti hilo na vifaa vingine katika eneo la ukumbi wa disco la Billicanas.
Akizungumza wakati madalali wakiendelea kutoa vitu nje, Meneja wa kitengo cha madeni wa NHC Japhet Mwanasenga, akisema mpangaji wa jengo hilo anadaiwa kiwango hicho cha fedha na hajalipa kuanzia miaka ya 90.
Alisema kutokana na kutokulipa fedha hizo, licha ya kupewa notisi, ndio maana shirika limeamua kuingia na kutoa vitu nje ili aweze kulipa. Alisema mpangaji huyo aliambiwa na alipewa na notisi na NHC ya siku 30 pamoja na notisi ya dalali lakini hakulipa deni ndani ya muda huo.
"Sasa hakuna namna usipolipa deni lazima uondolewe katika jengo ni fedha za miaka mingi kuanzia miaka ya 90" alisema Mwanasenga. Alisema baada ya kumhamisha kwa lazima, wataendelea kufanya utaratibu wa kumdai.
Kuhusu vifaa alisema, vinaenda kwa dalali ambaye ataomba kibali NHC juu ya kuviuza vifaa hivyo baada ya siku 14 kama deni halitalipwa. Kuhusu ubia katika upangaji katika jengo hilo, Mwanasenga alisema hakuna suala kama hilo na NHC inamhesabia kama mpangaji wa kawaida.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa kampuni ya udalali, Joshua Mwaituka alisema wao watahifadhi vifaa hivyo katika ghala lililopo Buguruni jijini humo na ndani ya siku 14 wakipata idhini kutoka NHC wataviuza.
Kwa muda wote kazi ya kuhamisha vitu ilipokuwa inaendelea mpaka mchana saa 8, lakini mpangaji wa jengo hilo hakufika kuzungumzia suala hilo.
Friday, September 2, 2016
NHC WAVAMIA OFISI ZA FREEMAN MBOWE NA KUTOA VITU NJE.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment