MSAJILI wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Projest Kahyoza amejitoa katika shauri la Mkurugenzi wa Kampuni ya Tiptop Connections, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ anayetakiwa aieleze Mahakama ni kwa nini asifungwe jela baada ya kushindwa kulipa Sh milioni 250.
Babu Tale ambaye ni Meneja wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul‘ Diamond’, anatakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kutii hukumu ya Mahakama iliyomtaka amlipe Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Shehe Hashimu Mbonde fedha hizo baada ya kuuza kanda za mahubiri yake bila ridhaa yake.
Msajili Kahyoza alijitoa katika shauri hilo baada ya Shehe Mbonde kuandika barua kumtaka ajitoe kwa sababu hana imani naye.
Akiahirisha kesi hiyo, Msajili Kahyoza alisema, anajitoa kwa sababu kuna barua imemfikia kutaka ajiondoe katika shauri hilo, lakini aliongeza kuwa aliyeandika barua hiyo aelezwe ukweli kuhusu yeye kukutana na wakili wa wadaiwa kabla ya kesi kutajwa.
Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameomba msajili ajitoe kwa sababu hajaridhishwa na jinsi anavyoshughulikia shauri hilo tangu alipokee, pia kesi inavyoendelea anahisi haki aliyopewa na mahakama hiyo haitatendeka au itacheleweshwa.
Aliorodhesha baadhi ya mienendo inayomtia mashaka ikiwemo kesi hiyo kuahirishwa zaidi ya mara nane kwa sababu tofauti tofauti ikiwemo ya mawakili wa wadaiwa kutokufika mahakamani, pamoja na sababu nyingine bila kuwataka wahusika kueleza jinsi watakavyolipa fedha hizo.
Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameeleza kutiwa shaka na ukaribu kati ya msajili na wakili wa wadaiwa kwa kuwa amekuwa akishuhudia wakili huyo akiingia katika Ofisi ya Msajili kabla kesi haijatajwa mahakamani, jambo linalomfanya ahisi wanapanga jinsi kesi inavyokwenda.
Msajili Kahyoza aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 8, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa Msajili mwingine wa kusikiliza.
Sunday, October 30, 2016
MSAJILI WA MAHAKAMA AJITOA KATIKA KESI YA BABU TALE.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment