Friday, October 7, 2016

SIMBA YAMUOMBA RADHI RAIS MAGUFULI KWA VURUGU NA UHARIBIFU WA UWANJA TAIFA.

                                         OFISA HABARI WA SIMBA, HAJI MANARA.
Rais wa Simba, Evans Aveva na Kamati yake ya Utendaji kwa niaba ya benchi la ufundi, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wameomba radhi kwa Rais John Magufuli kutokana na vurugu za Uwanja Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba ilicheza mechi ya Ligi Kuu na Yanga, lakini mashabiki wake walifanya vurugu na kung’oa viti vya uwanja huo wakipinga bao la kuongoza la Amisi Tambwe baada ya mchezaji huyo kushika mpira kwa mkono kabla ya kufunga. Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa iliyosababisha polisi kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya mashabiki.

Serikali imetangaza kuufungia uwanja huo kwa timu hizo.

Akizungumza na wandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Simba Haji Manara alisema kwa moyo wa dhati na unyenyekevu mkubwa wameona umuhimu wa kuomba radhi kwa kitendo cha mashabiki wachache kuharibu rasilimali ambazo zimejengwa na kodi za Watanzania wote.

“Rais ndiye msimamizi wa rasilimali za nchi hii hivyo tumemwandikia barua Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye tukamwomba atuombee radhi kwa Rais kwa kitendo cha mashabiki wetu kung’oa vitu kwenye mchezo uliochezwa Oktoba mosi dhidi yetu na Yanga,” alisema Manara.

Manara alisema wakati wao wakiwa wamekaa jukwaa kuu na kuona tukio lile likitendeka walitamani kuruka kwenda kuwasihi mashabiki wasing’oe viti na kuahidi kuwa halitatokea tena kwani limeshusha thamani ya klabu.

Pia Manara aliiomba serikali kupitia kwa Meneja wa Uwanja wa Taifa kufunga kamera ili kusaidia kubaini waharibifu kwani endapo kamera zingekuwa zinafanya kazi wangewabaini mashabiki hao na kuwachukulia hatua.

Manara alifika mbali na kuomba polisi wanaolinda usalama wakati mechi zikichezwa wawe wanatazama mashabiki kuliko ilivyo sasa wanatazama mechi na kusahau majukumu yao.
Katika hatua nyingine, Simba imeilalamikia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Bodi ya Ligi kwa kutokuwa makini katika kupanga waamuzi wenye weledi wa sheria 17 za soka hasa kwenye mechi kubwa ya Simba na Yanga.

“Haiwezekani mwamuzi (Martin Saanya) anatoka kufungiwa mwaka mmoja na anapewa kuchezesha mechi kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, huko ni kukosekana kwa umakini kwa vyombo vinavyosimamia soka nchi hii,” alisema Manara.


“Mwamuzi alishindwa kumudu mchezo alikuwa anatoa maamuzi ambayo yalionekana dhahiri kuwa na faida upande wa pili hili ni suala ambalo linatakiwa kutazamwa kwa makini,” alisema Manara.

No comments: