Thursday, October 6, 2016

WATU SITA WAUAWA NA AL-SHABAB NCHINI KENYA.


Watu sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia eneo lenye nyumba za makazi Bulla usiku wa manane.

Gavana wa jimbo la Mandera, Ali Roba ameandika kwenye twitter kwamba watu sita wameuawa na mmoja kujeruhiwa, amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye plot hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.

kituo kimoja cha redio kinachojihusisha na kundi la Al-shabab kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo. Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu walioshambulia walikuwa watu kutoka maeneo mengine.

Gazeti la Standard nalo linasema kuwa walioshambuliwa walirusha guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.

Roba alisema dalili zote zinaashiria wavamizi hao walikuwa wa kundi la Al-shabab. Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa Al-shabab kutoka Somalia.

Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na umoja wa mataifa.


No comments: