BABY MADAHA. |
Mwigizaji wa filamu za bongo, Baby Joseph Madaha ‘Baby Madaha’, amejikuta akishikwa na butwaa baada ya kuporwa pochi yake na vibaka wawili waliokuwa katika pikipiki eneo la Makonde, Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Mwigizaji huyo alipatwa na mkasa huo usiku wa juzi, wakati akielekea kununua chipsi karibu na kituo cha daladala cha Makonde. Ghafla pikipiki iliyokuwa na vibaka wawili waliopakizana ilipita kwa kasi karibu yake na kumpora simu mbili aina ya Samsung na mkoba uliokuwa na vipodozi, fedha na hati ya kusafiria.
“Yaani hata sikuamini nilipokutana na mkasa ule, nilikuwa nikitokea Uwanja wa Ndege nikielekea kwangu Makonde, lakini nikiwa kituo cha daladala Makonde nilihisi njaa, nikaelekea kwenye banda linalouza Chipsi, ndipo nielekee nyumbani, lakini kabla sijafika katika banda wakaja watu wawili wakiwa wamepakizana katika pikipiki iliyokuja kwa kasi wakanipora mkoba wangu na kukimbia kwa kasi.
“Katika pochi yangu kulikuwa na simu mbili aina ya Samsung, dola 100 ambazo ni zaidi ya laki mbili, vipodozi na hati yangu ya kusafiria, lakini kwa bahati nzuri nilishika sura za wale vibaka na baada ya kutoa taarifa polisi ulifanyika msako mkali wakakamatwa wengi na nilipoitwa nilifanikiwa kuwatambua walionipora,’’ alieleza Baby Madaha.
Alisema baada ya utambuzi huo ulifanyika ukaguza katika nyumba wanazoishi vibaka na baadhi ya vitu, ikiwemo simu moja, vipodozi na dola 100 zikapatikana, upelelezi unaendelea kusaka vitu vilivyobaki, ikiwemo hati ya kusafiria, watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi.
Kwa sasa Baby Madaha na wasanii wenzake wawili, Isabella Mpanda na Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’ wapo mbioni kuzindua wimbo wao mpya wa ‘Mario’ kupitia kundi lao la Scorpion Girl.
No comments:
Post a Comment