Wednesday, August 31, 2016

CHRIS BROWN MATATANI KWA KUMTISHIA MWANAMKE BUNDUKI.

Chrus Brown

Polisi nchini Marekani wamemkamata na kumzuilia mwanamziki mashuhuri Chris Brown kwa tuhuma za kumtishia mwanamke bastora.

Polisi waliitwa kwenye makazi ya Chris Brown na mwanamke aliyewapigia simu na kuomba msaada saa tisa usiku wa kuamkia Jana.

Malkia wa urembo, Baylee Curran ameliambia gazeti la LA Times, kwamba mwanamziki huyo alimwelekezea mtutu wa bunduki.

Hata hivyo walizuiwa kuingia na ilibidi wasubiri hadi wapate idhini ya jaji kabla ya kufanya msako wa kutafuta bunduki katika maeneo hayo.

Mwanamke huyo aliyewaita mapolisi, baadae aliwaambia vyombo vya habari kwamba walitofautiana na Chris kuhusu majohari.

Alisema aliingia kwa Chris akiwa na rafiki yake na mshirika wa kibiashara na alikuwa akiangalia mkufu wa thamani uliokuwa umevaliwa na mwanaume mmoja, pale mwanamziki huyo alipomkaripia na kumtaka aondoke mara moja akiwa amemwelekezia bunduki.

Alifanikiwa kuondoka makazi hayo bila madhara.

Chris Brown ameandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kwa kujitetea na kuwalaumu polisi kwa kumuhangaisha.

Wakili wake alifika kwenye makazi hayo na kumtaka aandamane na polisi hao. Mwanamziki huyo anatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya uvamizi.

Chris amewahi kujitia matatani awali, hususani alipomshambulia aliyekuwa mpenzi wake na mwanamziki Rihanna 2009.


NAULI MPYA YA TRENI KUTOKA STESHENI KWENDA PUGU Tsh 600/-.

Abiria wanaotumia usafiri wa treni inayofanya safari kati ya stesheni, Dar es salaam na Pugu wataanza kulipa nauli ya sh.600 baada ya nauli hiyo kupitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA).

Awali treni hiyo ya kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilikuwa ikitoza sh 400 kwa mtu mzima na sh 200 kwa mwanafunzi wakati treni hiyo ilipokuwa kwenye majaribio.

Wanafunzi watalipa sh.100 kutoka kituo kimoja kwenda kingine.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRL Ng'hwani Rashid amesema, kampuni hiyo ilikuwa ikitoza  sh.400 wakati ikisubiri kukamilika kwa mchakato wa ukokotoaji nauli ambayo imesimamiwa na Sumatra.


MKULIMA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUMNAJISI MTOTO WA MIAKA 6.

Mkazi wa wilayani Igunga mkoa wa Tabora, Simba Kanyala (54) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi wa Wilaya hiyo akidaiwa kunajisi.

Mwananchi huyo anakabiliwa na mashtaka ya kumnajusi mtoto mwenye umri wa miaka 6. Kanyala ni mkulima wa kijiji cha Nkinga, tarafa ya Simbo.

Mwendesha mashtaka wa Jeshi la polisi Wilaya ya Igunga, Frank Matiku, ameeleza Mahakama kuwa Agosti 23 mwaka huu saa kumi jioni katika kijiji cha Nkinga, mshtakiwa alimnajisi mtoto na kumsababishia maumivu sehemu za siri.

Habari kamili itaendelea badae.


UVCCM KUSITISHA MAANDAMANO YA AMANI WALIYOPANGA KUFANYA SEPTEMBA MOSI.

Shaka Hamdu Shaka

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umetangaza kusitisha maandamano waliyokuwa wamepanga kufanya ili kuunga mkono juhudi na kazi inayofanywa na Rais Magufuli, ikielezwa ni kutokana na kutii katazo la jeshi la polisi nchini.

Umesema kuwa umepokea majibu ya barua yao kutoka kwa mkuu wa jeshi la polisi (IGP) Ernest Mangu inayowataka kuacha kufanya maandamano yao kwa sababu polisi wamezuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na maandamano nchi nzima.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu mkuu wake Shaka Hamdu Shaka, alisema mbali na barua hiyo pia wamefikia uamuzi huo unatokana na utii, nidhamu na kizingatia utaratibu wa mamlaka za juu ndani ya chama.


Tuesday, August 30, 2016

MAANDAMANO YA UKUTA MARUFUKU KUFANYIKA DODOMA.

Jeshi la polisi mkoani Dodoma limepiga marufuku na kuwataka wananchi wasishiriki katika maandamano yatakayofanyika Septemba mosi.

Limesema maandamano hayo ya ukuta ambayo yameandaliwa na Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA si halali na yana nia ya kupotosha na kuvuruga amani ya nchi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa  amesema kwa muda mrefu kumekuwa na makundi ya wafuasi wa Chadema kuhamasishana ili kufanya vurugu kupitia hoja ya maandamano waliyoyapa jina la UKUTA.

"Wapo watu wanaosambaza machapisho mbalimbali yenye kauli za uchochezi katika fulana, mabango na katika mitandao ya kijamii na pia wapo wanaofanya kampeni zisizo halali nyumba kwa nyumba kuwashawishi watu kufanya uhalifu huo" alisema kamanda.


WALIOJIHUSISHA NA WATUMISHI HEWA MATATANI.

Serikali imeanza kuwashughulikia wale wote waliojihusisha na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa na polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

Sambamba na hilo, serikali unatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kuwaondoa wafanyakazi hewa.

Waziri wa nchi, ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora), Angellah Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya Wizara yake katika kipindi cha "tunatekeleza" kinachorushwa na televisheni ya TBC1.

"Kwa sasa wapo watumishi wanahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua za kisheria" alisema.


LEMA AWAGOMEA POLISI.

Godbless Lema

Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema, amezua tafrani kwenye mahakama ya hakimu mkazi Arusha baada ya askari polisi waliomleta awali kutaka apande gari kwenda mahabusu kwa sababu ya kutokidhi masharti ya dhamana. Awali Lema, alisomewa makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Desdery Kamugisha na Wakili wa serikali Innocent Njau. Katika mashtaka ya kwanza ni la kutuma ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwake kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Mashtaka ya pili kutumia Whatsapp kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wa jiji la Arusha kuandamana Septemba Mosi. Baada ya Lema kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Kamugisha alimuuliza kama ni kweli au la, na Lema alikana baada ya kukana Wakili Njau aliomba Lema asipewe dhamana kwa sababu wana taarifa za kiintelijensia kuwa, endapo atapewa dhamana maisha yake yatakuwa matatani. Hoja ya Wakili huyo wa serikali, ilipingwa na wakili wa utetezi John Mallya. Baada ya mabishano hayo Hakimu Kamugisha alitupilia mbali pingamizi la Wakili Njau la Lema kunyimwa dhamana. Baada ya sharti la dhamana kutolewa, wadhamini wawili walijitokeza ambao ni madiwani wa jiji la Arusha, lakini hali tofauti ilijitokeza baada ya wakili wa serikali Njau kukagua barua ya kumdhamini Lema na kugundua kuna kasoro za matumizi ya majina. Kutokana na sintofahamu hiyo wakili alikubaliana na hoja ya Njau na kusema kuwa Lema atafute wadhamini wengine na kuahirisha kesi hiyo kwa muda hadi Septemba 19 mwaka huu. Baada ya kusomewa kesi hiyo, ikasomwa kesi ya pili ambayo inadaiwa ya kutoa lugha ya uchochezi kati ya Agosti mosi hadi 26 mwaka huu kwa njia ya kurekodi kwa sauti "audio clip" na kurusha kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuhamasisha maandamano Septemba mosi mwaka huu. Saa 8:20 mchana mapolisi walimtoa mahabusu na kumpandisha kwenye gari wakitaka kumpeleka mahabusu Kisongo. Kutokana na sintofahamu hiyo Lema alibishana na polisi hao huku akiwa na Mawakili wake, Mallya na James Lyatuu walihoji kuwa wanampeleka wapi wakati muda wa mahakama haujafika. "Muda wa mahakama haujafika mnanipeleka wapi, nasema nitafia hapa mahakamani muda huu ni saa nane, muda wa mahakama haujaisha mnanipeleka wapi, siendi, mniue, siendi popote mniue hapahapa, muda wa mahakama haujaisha bro, mnanipeleka wapi na kwanini mnanifanyia hivyo, nasema siendi kokote bora kufa, sikubali" alisema Lema.