Monday, August 29, 2016

KAMPUNI YA MBOWE IMEBAKIZA SIKU MOJA KULIPA BIL.1.3/-NHC.

Freeman Mbowe

Kampuni ya Mbowe Hotels Limited (MHL) imebakiza siku ya leo tu, kuwa tayari imelipa deni la shilingi Bilioni 1.3 ya kodi ambayo inadaiwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC) ili kujinasua katika hatari ya kuondolewa katika jengo la shirika hilo lililopo katika makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Ghadhi Makunganya jijini Dar es salaam.

Jengo hilo ni maarufu kutokana na kuendesha shughuli mbalimbali za starehe na burudani kutokana na kuwepo kwa Club maarufu ya Billcanas.

Hatua hiyo inatokana na notisi mbili zilizotolewa; Moja na shirika la nyumba la Taifa Juni 24, mwaka huu ikitishia kuvunja makubaliano ya mkataba wa ukodishaji wa jengo hilo na kufuatia na notisi ya kampuni ya udalali ya mahakama ya fosters, ambazo zote zinakamilisha muda wake leo.

Kampuni hiyo inamilikiwa na mwenyekiti wa taifa wa Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

Mbowe alinukuliwa na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki akilihusisha deni hilo na masuala ya kisiasa, kwa madai kuwa suala hilo linakuzwa na kupotoshwa ili kumnyamazisha katika harakati za kisiasa, bila kukiri uwepo wa shauri baina ya pande hizo mbili juu ya deni hilo.

Mkurugenzi mkuu wa NHC Nehemiah Mchechu, alithibitisha kuwepo kwa mpango wa kuiondoa kwa nguvu kampuni ya Mbowe katika jengo hilo.

"Ni kweli kuwa tumempa mpangaji wetu huyo Mbowe notisi ya kumuondoa. Kampuni ya Hoteli za Mbowe ni miongoni mwa wateja wetu watatu ambao ni wadaiwa sugu wa kodi ya pango kwa wateja binafsi nchini" alisema.

Mchechu alisema suala hilo ni la kibiashara na halina mahusiano na masuala ya siasa, kama ilivyodaiwa na Mbowe hivi karibuni alipoongea na vyombo vya habari.

"NHC haina uhusiano na masuala ya kisiasa wala kujihusisha nayo, hatuna uhusiano wowote na masuala ya umoja wa kupambana na udikteta (UKUTA), namuomba Mbowe atambue kuwa hili ni suala la kibiashara na si vinginevyo" alisema Mchechu.

Hatua ya NHC ya kuandika notisi ya kuvunja mkataba, ilitokana na kampuni ya Mbowe kushindwa kujibu na kusaini hati mpya ya makubaliano ya namna ya ukodishaji wa jengo hilo uliowasilishwa kwa kampuni hiyo January 18, 2015.


No comments: