Monday, August 29, 2016

YANGA YANG'ARA TENA.

Wachezaji wa Yanga wakifurahia ushindi.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu bara, yanga jana kuanza vizuri kampeni zao kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Afrikan Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam.

Yanga imeanza kutetea taji lake baada ya kutupwa nje ya michuano ya kimataifa ya kombe la shirikisho Afrika kwa kufungwa na TP mazembe ya Congo DR mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya makundi.

Ikicheza  soka safi Yanga ilichukua dakika 19 kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Deus Kaseke baada ya kuunganisha pasi safi ya Simon Msuva.

Afrikan Lyon ambayo ni mechi ya kwanza ilitoka sare 1-1 na mechi ya Azam, jana ilizidiwa karibu kila idara na kuonekana kuchoka hasa katika kipindi cha pili.

Msuva aliiandikia Yanga bao la pili katika dakika ya 59 akiunganisha pasi ya Haruna Niyonzima kabla ya kumpiga chenga kipa wa Lyon na kuujaza mpira wavuni.

Pamoja na kuelemewa huko, Lyon walijitahidi kufanya mashambulizi ambapo katika dakika ya 76 Tito Okello alishindwa kumalizia krosi akiwa amebaki peke yake na kipa.

Yanga iliendeleza mashambulizi na dakika ya 90 Amisi Tambwe alikosa bao baada ya mpira wa kichwa aliopiga kugonga mwamba na mpira kurudi uwanjani.

Zikiwa zimebaki sekunde chache mpira  kumalizika, Juma Mahadhi aliyeingia uwanjani  kuchukua nafasi ya Msuva aliandika bao la tatu kwa Yanga baaa ya kazi nzuri ya Niyonzima.

Yanga itacheza mechi ya pili keshokutwa ambapo itaminyana na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo wa Taifa.

Kutoka kwenye uwanja wa CCM kirumba Mwanza, Alexander Sanga anaripoti kuwa wenyeji Toto Africans wameshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbeya city.

Wageni Mbeya City waliandika bao hilo katika dakika ya tano lililofungwa na Haruna Shamte kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja golini.


No comments: