Majibizano ya risasi baina ya polisi na majambazi yaliyodumu kwa takribani saa saba kuanzia saa 8:20 usiku wa kuamkia jana mtaa wa Vikindu Mashariki, Mkuranga mkoani pwani, yamesababisha vifo vya watu wawili akiwemo askari polisi na mtu mwingine anayedhaniwa kuwa ni miongoni mwa majambazi.
Mbali ya milio ya risasi, mtaa huo pia ulitanda moshi kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa mfululizo na kuibua taharuki kubwa kwa wakazi wake. Mmoja wa majirani katika nyumba iliyozingiwa waliyoishi watuhumiwa, Mjenge Faki alisema walishtuka usingizini na kuanza kusikia milipuko ya risasi na ghafla wakaanza kutokwa na machozi kufuatia hewa hiyo ya machozi kuanza kusambaa.
Katika majibizano hayo, askari aliyekuwa katika majibizano na mtuhumiwa walikufa hapo hapo. Hata hivyo kamanda wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi, licha la kuwepo eneo la tukio, hakuwa tayari kuzungumzia lolote, akisema mwenye jukumu la kuzungumzia tukio hilo ni Kamanda wa polisi kanda ya Dar es salaam, Simon Sirro.
Naye Kamanda Sirro akizungumzia hilo alisema, taarifa rasmi ya tukio hilo zitatokewa leo kwani bado wanakusanya taarifa kuhusiana na tukio hilo. Lakini Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema katika mapambano hayo, Jeshi la polisi limepoteza askari mmoja, lakini bado lipo imara na litaendelea kuwasaka wahalifu popote watakapokuwepo.
"Askari wetu katika shughuri zake za kupambana na majambazi ameuawa hapa leo (Jana) usiku, ni tukio baya katika mkoa wetu, wilaya yetu na nchi yetu kwa ujumla. Hawa ni wahalifu, lakini mbaya zaidi hata watoto na familia zao zinaaminika wana mafunzo maalumu ya kulinda wazazi wao ambao ni wahalifu" alisema Ndikilo.
Aliongeza kuwa, kama waalifu hao walidhani kwa kuua askari watakuwa wametimiza malengo yao, basi wamechelewa kwani watawawinda popote pale watakapokwenda. Kwa mujibu wa Faki milio ya risasi na mabomu ilisikika katika nyumba inayosadikiwa kumilikiwa na mkazi wa Temeke, aliyetajwa kuwa ni Salum Kingungo.
"Tulianza kusikia kama watu wanakimbizana kutoka eneo la juu barabarani na kelele hizo zikaja kuishia ndani ya nyumba hii walianza kusikia majibizano baina ya watu waliokuwa nje na mingine kutoka ndani, lakini hatukuweza kujua kinachoendelea kwani tulijawa na hofu kubwa", alisema Faki.
Alisema alishindwa kutoka nje na hata walipobaini kuwa ni askari, hawakuruhusiwa kutoka nje hadi ilipohitimu saa tano asubuhi.
Katika majibizano hayo ya risasi na mabomu, nyumba inayodaiwa yalikuwa makazi ya watuhumiwa hao, iliharibiwa vibaya. Baada ya hali kutulia, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo akiwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, alipata fursa ya kuzungumza na wananchi.
Baada ya kutembelea nyumba hiyo na kujionea hali halisi, waliwataka wananchi wa Mkulanga na mkoa wa Pwani kwa ujumla kuwa watulivu kwani serikali imejipanga na kupambana na watu wachache ambao sio waaminifu.
Saturday, August 27, 2016
POLISI NA MAJAMBAZI WAJIBISHANA KWA RISASI HUKO MKURANGA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment