Saturday, September 3, 2016

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMTUSI RAIS MAGUFULI KWENYE MTANDAO WA WHATSAPP.

Mhasibu wa shule ya Sekondari ya Mtakatifu Josefu, Elizabeth Asenga (40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kumkashifu Rais John Magufuli kwenye mtandao wa Whatsapp.

Elizabeth alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa serikali Leonard Chalo, mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili Chalo alidai kuwa, Agosti 6 mwaka huu, huku akijua Elizabeth alituma ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya WhatsApp kwenye kundi la kijamii liitwalo STJ Staff Social Group. Inadaiwa aliandika ujumbe unaosema;

"Good morning humu, hakuna rais kilaza kama  huyu wetu duniani, angalia anavyompa Lissu umashuhuri fala lile, picha yake ukiiweka ofisini ni nuksi tupu, ukiamka asubuhi, ukikutana na picha yake kwanza, siku inakuwa mkosi mwanzo mwisho".

Baada ya mshitakiwa kusomewa mashtaka alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kesi hiyo ihairishwe hadi tarehe nyingine.

Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaotakiwa kusaini dhamana ya shilingi milioni mbili. Kesi itatajwa tena Septemba 22.

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara Juma Shabani (31) amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kesi Sita likiwemo la kutakatisha dola za Marekani 340,000 sawa na shilingi milioni 680.


No comments: