Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amewataka wananchi wa Pemba wasibabaishwe na wanasiasa waliofilisika, wanaowadanganya watu na kusisitiza kuwa uchaguzi mkuu umekwisha na hautafanyika mwingine hadi 2020 na Ali Mohammed Shein ndio Rais halali wa Zanzibar.
Amewakemea wanasiasa wanaopita kila kona na wakitembea Ulaya, amesema safari zao hizo zitaishia vichochoroni kwani Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk.Shein.
"Nataka niwaambie hao wanaokwenda nje kwa kujitangaza na kujitapa, kwamba Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk. Shein...uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo 2020" alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema hayo wakati akihutubia wananchi wa mikoa miwili, kisiwa cha Pemba ya kaskazini na kusini katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Gombani ya kale, uliokuwa na lengo la kutoa shukrani kwa wananchi wa Pemba kwa kumpigia kura katika uchaguzi wa Oktoba mwaka Jana.
Alisema anakerwa na matukio ya vitendo vya chuki na uhasama ikiwemo watu kuchomeana mali zao ikiwemo mikarafuu, neema ambayo wananchi wamepewa na Mungu.
Alisema matukio hayo yanafanywa kwa lengo la kujenga chuki na uhasama huku baadhi ya watu wakiathirika vibaya baada ya kuharibiwa mazao yao.
Aliongeza kuwa, wakati akila kiapo cha utii na uaminifu aliahidi kulinda Muungano pamoja na amani na utulivu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwaonya viongozi wanaopandikiza chuki na uhasama kwamba atapambana nao kwa nguvu zote.
Aliviagiza vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinawasaka watu wote wanaofanya vurugu kiasi kuhatarisha amani na utulivu.
"Mimi nawashangaa sana watu wa Pemba, mmepata Rais mpole sana ambaye anatoka Pemba, sasa sijui mnataka nini jamani" alihoji Magufuli.
Dk.Magufuli alisema tangu kumalizika kwa marudio ya uchaguzi mkuu Machi mwaka huu, viongozi wa vyama vya upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) waliosusia uchaguzi huo ambao Dk. Shein alishinda kwa kishindo kwa asilimia 91.4 wamekuwa wakipita ndani na nje ya nchi wakidai uchaguzi huo haukua halali.
Saturday, September 3, 2016
RAIS MAGUFULI ASISITIZA KUWA SHEIN NDIO RAIS HALALI WA ZANZIBAR.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment